Chombezo : Bwana Mihamala
Sehemu Ya Tano (5)
Mr Shamte akapata hasira, akanyanyuka na kuchukua hati ya nyumba ambapo aliandika jina la Judy kama ndiye mmiliki wa nyumba hiyo lakini aliificha sehemu ambayo haikuonekana kirahisi na alimdanganya Judy kuwa nyumba hiyo amempangia. Lengo lake alitaka siku moja amuoneshe mali zake zote ambazo alimnunulia.
Ingawa Mr Shamte alikuwa na tabia ya kuwa na wanawake wengi wengi lakini alipokutana na Judy aliwekeza nguvu zake zote kwa Judy. Pamoja na uzee wake wote, alimweka moyoni Judy , kiufupi alimpenda sana ndio maana hakuna jambo ambalo aliliomba Judy alafu yeye akashindwa kulitimiza. Moyo wake ulitekwa sana Judy ndio maana huko nyuma kabla hajakutana na Judy hakuwahi kuitelekeza familia yake japo alikuwa anashiriki mapenzi na wanawake tofauti tofauti.
Mambo haya yote akiyafikilia ndiyo yaliyomtia hasira Mr Shamte hadi akaamua kuyafanya yote aliyoyafanya kwa kina Shaibu.
Mr Shamte akaiangalia ile hati ya nyumba kwa hasira sana, akarudi tena ile sehemu akachukua nyaraka zote alizomwandika Judy, gari alimwandika jina lake kama mmiliki pia kuna shamba alimnunulia Judy nalo alimwandika jina lake..
Mr Shamte aliyafanya hayo yote huku akidhamiria siku moja atamuoa Judy moja kwa moja na kuwa mke wake wa pili wa kihalali kabisa, lakini ndoto zikaishia njiani mara baada ya Judy kukutana Shaibu.
Baada ya kuzichukua nyaraka zote , akaona bora azichome moto na kuzipoteza kabisa. Alitafuta kibiriti lakini hakukiona. Akaamua kuzirudisha tena pale pale alipozitoa na kuzificha tena.
Akaweka vitu vizuri kisha akaamua kurudi kwa mke wake kwenda kupumzika maana kichwa chake kilijaa mawenge wenge, hakikutulia hata kidogo, kilikuwa na mzunguko wa mawazo mengi.
Hata aliporudi kwa mkewe bado hali ilikuwa ileile, mawazo hayakumuisha japo alijaribu kujionesha yuko sawa kwa mkewe. Mke wake aligundua hali ya mumewe lakini hakumpa kampani yeyote kwani alijua ndio kama desturi yake kila anapotoka kwa wanawake zake hivyo alichoamini yeye ni wanawake wake wamemchanganya. Mke wa Mr Shamte hakuwahi kujua kama kuna mtu anaitwa Judy ambaye ndiko anakolala mara kadhaa mume wake.
Mr Shamte alijigaragaza mwenyewe hadi akapata usingizi wa kimazabe.
Asubuhi ikapambazuka, kila mmoja akiwa ana pilika pilika zake za maisha.
*****
Maeneo fulani nje kidogo ya mji wa Dar es salaam, kulionekana watu watatu wakiwa wanaongea ongea,
"Mzee hili shamba ni kubwa sana, hapa unaweza ukalima mihogo....upande wa kule unaweka hata mahindi...., nunua shamba hili mzee...urithi wa kweli ni ardhi , ardhi inapanda thamani kila siku na wala haijawahi kushuka alafu bei yenyewe ni bure kabisa......"
Kijana mmoja mfupi hivi akiwa amevalia baraghashia aliongea huku akimuonesha mzee shamba ambalo lilikuwepo mbeleni mwao. Kijana huyo alionekana wazi kuwa yu dalali alikuwa anataka kumuuzia shamba mzee huyo ambaye alipanda hewani kwelikweli (alikuwa mrefu ) ila bado alionekana yupo ngangari pengine mazoezi alikuwa mtu wa kufanya mazoezi maana mwili wake ulikuwa umekakamaa.
Mzee alivutiwa na shamba hilo, wakakubaliana waanze kulizunguka na kulikagua. Waliingia ndani zaidi, walifika sehemu ambayo waliona kuna michirizi chirizi hivi, alafu nyasi zimepondeka pondeka, wakasimama, wakajiuliza uliza baadae wakaona kuna sehemu ambapo nyasi zimelala sana. Wakasogea karibu, wakashangaa baada ya kuona kuna watu watatu ambao walionekana kama wamekufa vile.
"Jamani eeh hatari hii hapa jumba bovu linaweza kutuangukia, hebu tuondokeni bora hata hela zenyewe nikose kuliko niende jera sasa hivi na corona hii....."
Yule kijana dalali aliongea huku akiwa amejaa hofu. Mwenye shamba naye akakubaliana na dalali wake, walitaka waondoke huku hofu ikimjia ya yeye kubebeshwa zigo la kinyesi yaani kuonekana yeye ndiye aliyefanya hayo kwani shamba ni lake.
Yule mzee mnunuzi aliwatuliza hofu ,
"Hebu tulieni, nchi yetu inaongozwa kwa sheria hivyo hakuna jambo lolote litakalowapata ikiwa serikali itachunguza na kubaini wahusika wa tukio hili ni nani hasa.Wahusika ndio watakaoshughulikiwa na si nyinyi... Mimi hapa ni askari , ngoja nipige simu polisi na watakuja hapa haraka tu wala msiogope...."
Mzee baada ya kusema hivyo akavua koti lake na kumfunika Judy, na kwa sababu koti lilikuwa lefu , liliweza kufunika sehemu kubwa ya mwili wa Judy. Baada ya hapo akapiga simu polisi na kuwapa taarifa hizo.
"Mmmh asee Sijui kimetokea nini hapa...watu ubinadamu umewaisha kabisa...."
Yule mzee alijisemea moyoni huku akishika mikono kiunoni huku wakiendelea kuwasubiri polisi waje eneo la tukio.
*Itaendelea*
Judy na Shaibu wamekata pumzi moja kwa moja au wamezimia tu?
Polisi wakija watafanya nini?
Nini hatma ya Mr Shamte na mambo aliyoyafanya?
Usikose kufuatilia sehemu ijayo.....
_Mungu hachelewi wala hawahi, hufanya pale anapoamua kufanya na wakati ambao yeye anataka_
Shaibu anapigwa vibaya sana na kusababisha kukata moto, Mr Shamte na watu wake wanaamini kuwa Shaibu amefariki na Judy pia amefariki, wanawachukua na kuwatupa porini kisha wanaondoka huku wakiamini wamemaliza kila kitu.
Mr Shamte baada ya kurudi nyumbani anatoa nyaraka zote ambazo zilikuwa na majina ya Judy kama mmiliki, anataka kuzichoma ila anakosa kiberiti na kuamua kuzirudisha alipozitoa.
Watu watatu wanaonekana wanaoneshana shamba , wakati wanalizunguka wanakutana na watu ambao wametupwa, ndio hao akina Shibu na wenzake. Mmoja wapo anapiga simu polisi ili waje eneo la tukio.
Endelea hapa....
Haikuchukua muda sana, polisi waliingia eneo la tukio na ukizingatia aliyepiga simu ni polisi mwenzao tena ana cheo kikubwa huko kazini.Maana siku za nyuma polisi walikuwa na kasumba ya kuchelewa kufika kwenye matukio kama hayo.
Polisi walishuka na kuelekea hadi ilipo miili ya watu hao waliolala. Walifika na daktari, daktari akaanza kuwachunguza wakati huo huo polisi nao wakikagua maeneo hayo ya tukio na kuyaandika mambo fulani fulani katika daftari .
Baada ya muda mfupi tu wakachukuliwa na kupakizwa kwenye gari kisha haraka wakaondoka eneo la tukio watu wote.
Daktari aligundua kuwa Shaibu na Judy bado mishipa yao ya fahamu ilikuwa inafanya kazi hivyo wakapelekwa moja kwa moja kwenye chumba cha wagonjwa mahututi kisha wakaanza kupatiwa huduma.
Muki yeye teyari alikuwa ameshakufa, alipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti.
Polisi waliwasubiri akina Shaibu wapate angalau nafuu kidogo ili waanze kufuatilia kwa kina suala hilo, maana mpaka muda huo hakuna aliyejua kiliwapata nini hadi wakafikia hatua hiyo , ingawa kwa uchunguzi wa awali wa daktari ulionesha Judy ameingiliwa kwa nguvu (amebakwa) na Muki pamoja na Shaibu walipigwa.
Taarifa ya habari ya saa saba mchana ya siku hiyo ilitangaza habari za tukio hilo.
Kupitia taarifa ya habari hiyo, kuna ndugu zake Muki walipata kuzisikia , walienda hosptalini na kuuchukua mwili wa ndugu yao kisha wakaenda kuuhifadhi katika makazi yake ya kudumu jioni ya siku hiyohiyo , hawakutaka kumsubirisha zaidi.
Ndugu zake Muki waliumia sana kumkosa ndugu yao huku angali bado kijana mdogo kabisa lakini ndio hivyo tena kama asemavyo marehemu Remmy Ongala, mwanamuziki mashuhuri nchini Tanzania wa zamani ambaye kwa sasa ni marehemu kwamba "kifo hakina huruma" na hata maneno ya kezilahabu yanasadifu haya "maisha hayana maana, binadamu anazaliwa ili afe", .
Ndugu hao waliahidi kushirikiana na jeshi la polisi mpaka muarifu apatikane kwa njia yeyote ile. Ndugu zake Shaibu nao walipopata habari hizo walienda hospitalini kujua kinachoendelea.
Siku ya pili yake mchana ndipo macho ya Shaibu yakaanza kufunguka kwa mbaali. Yalikuwa yanaona ukungu ukungu tu. Hayakutambua kitu chochote mbeleni mwake. Judy bado alikuwa amezima. Jioni ya siku ya hiyohiyo , Judy naye akayafumbua macho kwa tabu sana.
Siku mbili mbele , afya zao zilianza kuimarika na wakatolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi na kuwekwa katika chumba cha kawaida ambapo hapo sasa ndugu waliruhusiwa kuwaona. Judy yeye hakuwa na ndugu waishio Dar es salaam hivyo ndugu zake Shaibu waliofika kumuona Shaibu ndio haohao waliomuona na yeye na kuwafanya kama ndugu zake. Siku ya tatu , walianza kuzungumza japo kwa shida.
Polisi walichukua maelezo kutoka kwao wote wawili. Maelezo yao kwa pamoja yakamtaja Mr Shamte.
Polisi walienda moja kwa moja ofisini kwa Mr Shamte, wakamchukua maelezo kisha wakamtaka waende hadi katika nyumba ambayo Judy alifanyiwa unyama.
Walipofika pale walikagua kila sehemu lakini nyumba haikukutwa na kitu chochote ambacho kiliweza kumtia hatiani moja kwa moja Mr Shamte.
Kwa sababu yeye ndiye mtuhumiwa ,polisi wakaondoka naye hadi kituoni na kumweka ndani huku uchunguzi ukiendelea.
Kesi ilifunguliwa mahakamani na kupangiwa tarehe ya kusikilizwa. Wakati huo teyari Judy na Shaibu walipata nafuu kabisa, waliweza kuongea vizuri na hata kutembea. Waliruhusiwa kutoka hospitali na walienda kukaa kwa mjomba wake Shaibu.
Siku ya kesi walienda kusikiliza , hata ndugu zake Muki nao walienda siku hiyo. Mashahidi ambao ni Shaibu na Judy wakaanza kutoa maelezo ya tukio zima jinsi lilivyokuwa. Hawakuficha ukweli wowote na hawakuacha hata nukta ya tukio , walieleza kama ilivyo.
Hakimu alipomuuliza Mr Shamte kama anakubaliana na walichosema akina Shaibu , alikataa kila kitu.
Katika utetezi wake , alisema Shaibu na Muki hawakuwa wafanyakazi wake. Hata ile nyumba aliikana , hakuitambua kabisa.
Hakimu alipoona hivyo ikabidi apeleke mbele tena ili uchunguzi uendelee kufanyika.
Mr Shamte aliongea na wakili wake kila kitu na mipango yao ikasukwa. Alimpa maelezo ya kuondoa kila aina ya ushahidi ambao upo ofisini kwao wa kuonesha kuwa hao akina Shaibu waliwahi kufanya kazi hapo ofisini kwake.
Hata wafanyakazi wake wote wakapewa pesa ili kama wataitwa kuthibitisha kama wanawajua Shaibu na Muki basi wakakatae kuwa hawajulikani kabisa hapo ofisini.
Kila kitu kilipangwa kama ilivyotakiwa mpaka ile siku ya kusomwa kesi tena , Mr Shamte alikuwa na amani sana moyoni mwake kwani teyari pesa yake iliongea na kutamka inachotaka. Pesa ilibatilisha kila aina ya ukweli uliohusu kesi hiyo.
Siku hiyo ya kesi, mwendesha mashtaka alisema walienda kufanya upekuzi katika ofisi ya Mr Shamte lakini hakuna ushahidi wowote waliouona kama Shaibu na Muki pamoja na Judy walikuwa wafanyakazi wa Mr Shamte.
Shaibu na Judy waliachwa mdomo wazi baada ya kusikia hilo likisomwa na mahakamani hapo.
Hata ilipofika zamu ya wafanyakazi wenzao nao wakakandamiza msumali wa moto kuwa hawajawahi kuwaona akina Shaibu katika kampuni yao hivyo hawawatambui kabisa.
Mr Shamte akaulizwa swali na mwendesha mashtaka kwamba kwanini alikubali kuonyesa nyumba kama hawajui na alikubali vipi kwenda kwenye nyumba ambayo haijui.
Kwa sababu hapo ndipo mahakamani, Mr Shamte aliikana tena nyumba hiyo kuwa hahusiki nayo na akawaambia kuwa wakatafute mmiliki halali wa nyumba hiyo yeye ndiye anaweza kujua kujua kilichoendelea.
Kesi ikasimama kwa muda, ikabidi polisi waende hadi kwenye ile nyumba ambayo ilisadikiwa kufanyika unyama huku kukiwa na Judy pamoja na Shaibu na Mr Shamte mwenyewe pamoja na wahusika wengine.
Walifika katika ile nyumba, nyumba haikuwa imefungwa na hapakuwa na mtu. Walianza ukaguzi tena. Hadi wakafika katika lile kabati ambalo lilikuwa na nyaraka. Nyaraka zilionesha mmiliki wa nyumba ni Judy pamoja na mali zote zilizomo ndani ni za Judy (pia hata gari).
Mr Shamte akadakia na kusema kuwa bila shaka wamemjua mmiliki wa nyumba kinyume na walivyosema akina Judy kuwa nyumba ilipangishwa na Mr Shamte. Matukio yote yakaandikwa, kisha wakarudi kwa Hakimu na vielelezo vyote.
Hakimu akavisoma vithibitisho vyote kisha akatulia kwa muda wa dakika kama mbili hivi huku akipitia mafaili mengine yaliyopo mezani kwake.
Baada ya dakika tatu kupita , hakimu akasema,
" sasa ni wakati wa kusikiliza hukumu wa kesi hii"
Watu wote wakaongeza ukimya na kumwangalia hakimu atasema nini kuhusiana na kesi hiyo. Mtu pekee aliyeonekana kuwa na furaha ni Mr Shamte kwani alikuwa na uhakika wa kushinda kesi na kurudi zake uraiani.
*Itaendelea*
Kwa jinsi alivyojichanganya changanya na maelezo yake ya kutonyooka , unadhani Mr Shamte atabaki salama?
Nani atapewa zigo la lawama kwamba ndiye aliyemuua Muki?
Nyaraka zinaonesha nyumba ni Ya Judy, Je mwenye nyumba ndiye atakayehukumiwa?
Usikose sehemu ijayo kujua hatma ya hayo yote.
Chukua tahadhari, corona haijaisha.
Baada ya Shaibu na Judy kuokolewa , madaktari wanafanikiwa kuwarejesha katika afya zao za kawaida, kesi ya jinai inafunguliwa mahakamani. Mashahidi mbalimbali wanatoa ushaidi wao juu ya tukio lililotokea.
Ushaidi unakamilika na kilichobaki ni kwa hakimu tu kutoa hukumu. Watu wote wanakaa kimya kumsikiliza hakimu.......
Endelea sasa....
Hukumu ikaanza kusomwa, hakimu akasoma,
"Mahakama imefuatilia maelezo ya mlalamikaji, mlalamikiwa na Mashahidi wa pande zote mbilli"
Hakimu akatulia, kisha akaendelea....
"Katika kesi hii ya jinai namba 345 KT 2020 , upande wa Jamhuri ambao ndio washtaki, wametoa maelezo ambayo yalisindikizwa na maelezo ya mashahidi ambao ndio waliotendewa, mashaidi walisema kuwa Mr Shamte ndiye aliyehusika kuwateka wote watatu na kusababisha kifo kwa Muki, shahidi mmoja ambaye ni Judy alisema kuwa tukio la yeye kubakwa lilitokea katika nyumba ya Mr Shamte huku Mr Shamte mwenye nyumba mwenyewe akishuhudia, mahakama iliifuatilia hiyo nyumba na kubaini kuwa si kweli kama alivyosema shahidi na nyumba hiyo inaonesha ni nyumba ya Shahidi huyohuyo mwenyewe na wala haikuwa ya Mr Shamte.....Mashaidi wakaeleza tena kuwa kilichosababisha haya yote ni wivu wa kimapenzi ambapo Shaibu alihusika moja kwa moja kumchukua mke wa Mr Shamte, hata hivyo mahakama imefuatilia kwa kina na kubaini kuwa Judy hakuwa mke wa Mr Shamte na watu hao hawajuani kabisa kwani Mr Shamte anaye mke wake halali wa ndoa na vyeti vimeonekana...."
Mr Shamte alikuwa anatabasamu tu kwa kile kilichoendelea katika mahakama hiyo.
Hakimu akaendelea kusoma hukumu,
"Mashahidi ambao ndio wahusika wa tukio, walisema kuwa walikuwa wafanyakazi wa Mr Shamte, pia mahakama ilifuatilia kwa karibu na kufanya upekuzi kila mahala, huku ikiwahoji wafanyakazi wake wengine ambao nao walithibitisha kutowafahamu Shaibu na wenzake, na mahakama imejiridhisha kuwa hao wote hawakuwa wafanyakazi katika kampuni ya Mr Shamte........"
"Mahakama imebaini kuwa hata siku hiyo ya tukio , Mr Shamte hakuwepo nchini, alikuwa yupo Kenya katika mambo yake binafsi......
Kwa hiyo ukiangalia ushahidi wa mashahidi wa pande zote mbili, Mahakama inamwachia huru Mr Shamte na tunamfutia tuhuma zote alizopewa juu ya shtaka hili, kuanzia sasa Mr Shamte upo huru! na jalada hili nalifunga rasmi kuanzia sasa"
Hakimu alimaliza kusoma hukumu na kugonga muhuri katika zile karatasi alizokuwa anasoma. Baada ya hapo , watu wakasimama na kupisha hakimu ambaye alikuwa anatoka ndani ya chumba hicho.
Mr Shamte alitabasamu sana na kutoka nje huku akiwa na wapambe wake. Shaibu na ndugu zake , pamoja na ndugu zake Muki na Judy wao walionekana kutoridhika na maamuzi lakini hawakuwa na la kufanya maana mahakamani ndiko inakotolewa haki, na teyari mahakama imetoa hukumu. Walitoka nje kinyonge sana, wakiwa wapo nje ya mahakama, Mr Shamte alimfuata Shaibu na kumshika bega kisha akamwambia,
"Bwana mdogo, kila siku nilikuwa nakuambia; pesa inaweza kuhamisha hata milima , kwa akili yako ndogo ulidhani mimi naweza kufungwa? Cha muhimu wewe shukuru tu haukwenda kuzimu kama mwezio, usijaribu kukata rufaa wala kufanya lolote maana utapoteza muda na hapo sasa nitakupoteza moja kwa moja sitafanya makosa kama yale ya mwanzo , nakukumbusha kijana kamwe usijaribu kushindana kama hauna kitu cha kipekee cha ushindani, kaa mbali sana na watu wenye pesa....dunia haina huruma kabisa , siku likikuta hakuna atakayekuhurumia, take your time, fanya yako......"
Wakati Mr Shamte anasema hivyo kuna ndugu mmoja wa Muki alikuwa yupo karibu yao na alikuwa anasikia, na yeye pia akamshika bega Mr Shamte na kumwambia,
"Tumepoteza mpendwa wetu ambaye sisi tulimsomesha ili aje kuwasaidia ndugu zake, wewe umekatisha ndoto zake na zetu, hatukati rufaa wala hatuendi tena kudai haki popote pale , kwa sababu hapa duniani ni ngumu sana kuipata haki kama ukiwa u mnyonge kama ilivyo kwetu sisi, ila naomba uyakumbuke maneno haya .....Hautakaa kwa amani katika dunia hii, na unyama wako kuna siku utaulipia....nakuhakikishia kabla Corona haijaisha wewe utakuwa teyari umeisha, hauwezi kubaki salama"
Mr Shamte alicheka sana mpaka baadhi ya watu wa karibu yao wakageuka na kuwatazama, Mr Shamte alicheka kwa dharau , yaani alimuona mtu huyo kama mtu aliyeishiwa mipango tu.
Mr Shamte akaondoka na watu wake huku Shaibu naye akiondoka na watu wake.
Kwa sababu mahakama ilimtambua Judy kama mmiliki wa nyumba na uzuri nyaraka zote halali walikabidhiwa wao palepale mahakamani, wakaamua kwenda moja kwa moja katika nyumba hiyo.
Ndugu zake Muki wakachukua nguo na vyeti vyake ambavyo viliwekwa katika chumba cha nje na wakaondoka navyo. Baadae hata ndugu wa Shaibu waliondoka na kuwaacha ndani Shaibu na Judy kwani kama ujuavyo mji wa Dar es salaam hakuna shamba linalotoa mazao kwa hiyo ni lazima watu wafanye kazi ndipo mkono uende kinywani , ndio maana ndugu zao hao hawakutaka hata kusubiri kila mmoja alienda kwenye pilika pilika zake za kutafuta ugali.
Judy na Shaibu wakaanza kuizunguka nyumba na kukagua kila kitu kilichopo ndani humo. Wakiwa wanaendelea na uchunguzi , ghafla aliingia Mr Shamte.
"Haahaa nilijua tu mtakuja hapa na ndio maana nimewafuata hapahapa....Ninawapa wiki moja ya kuhama katika nyumba hii tena hapo nimewahurumia tu, ilitakiwa sasa hivi naifunga nyumba yangu na nyinyi muondoke....Hii nyumba ni yangu kila mmoja wenu analijua hilo..."
Judy akamwangalia Mr Shamte kisha akamwambia,
"Nina nyaraka zote zinazoonesha nyumba hii ni yangu, siami na siendi kokote kule....nitakuitia mwizi sasa hivi naomba utoke nje...."
Mr Shamte akacheka kidogo kwa dharau kisha akamgeukia Shaibu na kumwambia,
"Kijana hivi haukumwambia huyu kahaba mwenzako nilichokuambia pale nje ya mahakama? Narudia tena kwa faida ya wote .....Usijaribu kushindana kama hauna kitu chochote cha ushindani, mimi nina pesa , hamuwezi kunishinda kwa lolote labda tu elimu yenu mliyobaki nayo kichwani na hata hivyo bado mimi ndio kila kitu si mnakumbuka niliwaajiri nyinyi? Kifo kiliwanusuru ila mkiwa wabishi safari hii wote mtakwenda na maji"
Judy alitaka aseme kitu kingine ila Mr Shamte akamkatiza tena kwa kusema yeye.;
"Inaonekana mnataka kushindana, mimi sikuja kwa ajili ya hilo, nimekuja kuwapa maelekezo, kuweni makini na nyumba yangu msiharibu chochote...."
Baada ya kusema hivyo Mr Shamte akaondoka na kuwaacha midomo wazi Judy na Shaibu ambao walishaanza kuipigia hesabu nyumba hiyo wakiamini ni yao na wataishi hapo pamoja.
Judy hakuwa na pa kwenda zaidi zaidi kama atatoka hapo ni kwenda kwao kabisa yaani nje ya Dar es salaam , Shaibu naye pamoja na kuwa ndugu zake lakini hakuwa na uwezo wa kwenda kukaa kwani walikuwa wamepanga chumba kimoja kimoja na ndimo walimokuwa wanaishi na familia zao.
*ITAENDELEA*
_Haki inaposhindikana kupatikana kinachofuatia ni ubaya_
Shaibu na Judy wataenda wapi? Na Je mapenzi yatarudi kama zamani? Judy alibakwa na wanaume watatu, je yupo salama?
Ndugu zake Muki wamehaidi kumfanya Mr Shamte akose amani, je watafanya nini?
Mr Shamte mwisho wake utakuwaje?
Wema ni akiba ila ubaya ni jeneza , dunia huzunguka , hata mambo ya duniani pia huzunguka, hakuna baya lililozaa jema hata siku moja, ukifanya baya tegemea baya zaidi.
Hukumu imetolewa na ile inayoitwa haki imepatikana kwa mujibu wa mahakama, Mr Shamte ambaye ndiye mshukiwa wa tukio anaachiwa huru baada kufanya kazi kubwa ya kuhonga pesa kwa wafuatiliaji wa kesi hiyo.
Masononeko yanatokea kwa ndugu wa Muki na Shaibu baada ya kuona haki ikipindishwa kwa sababu ya pesa.
Judy na Shaibu wanaamua kurudi kwenye nyumba ambayo Mr Shamte aliikana, lakini Mr Shamte bado anawaandama akina Shaibu na kuwaambia waiache nyumba hiyo mara moja. Vinginevyo balaa kubwa litawakumba kama wakienda kinyume na maagizo yake.
Sasa endelea hapa....
Judy na Shaibu walirudi sebuleni na kuangalia namna ya kufanya maana hapo walipo teyari mambo yameharibika.
"Sikiliza nikuambie kitu Shaibu, mimi naamini maneno ya waandishi wa riwaya mbalimbali kama akina Kezilahabi kwamba maisha ya mwanadamu ni kama maji tu yateremkayo kutoka kilimani kwenda bondeni, binadamu hana uwezo wowote wa kubadiri hatma yake, binadamu yupo duniani kwa lengo la kukamilisha tu yale aliyoandikiwa....hata ufanyeje hauwezi kubadili hatma yako, mimi ninachokiona hapa tuendelee kukaa hapa lakini tukatoe taarifa polisi kuwa Mr Shamte bado anatufuatilia, hana uwezo wa kututoa hapa kwa sababu nyaraka zote tunazo sisi"
Judy aliongea huku akiketi katika moja ya sofa lililopo sebuleni hapo. Shaibu naye katia neno,
"Haahaaa Judy bana (huku akitingisha kichwa kuashiria hakubaliani na alichosema Judy) , sitaki kupinga hayo maneno yako na hao waandishi wako akina Kezilahabi lakini nakuuliza swali , hivi kwa mfano wewe ni dereva wa basi la abiria, ukaamua kunywa pombe kwa makusudi alafu ukalewa kisha ukaendesha gari likiwa na abiria, kwa sababu macho hayaoni vizuri ,huku pombe ikiongoza ubongo wako, gari linaacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya watu. Hebu nambie hapo ajali hiyo ni kweli binadamu hakuwa na uwezo wa kuiepuka? .....mimi nadhani mambo mengine tunayapanga wenyewe sisi binadamu na kuna baadhi ya mambo tunayo uwezo wa kuyaepuka, hebu fikiria haya yote si yametokana na wewe mpango wako wa kunileta hapa pengine kama nisingekuwa nakaa hapa haya yasingetokea na wala nisingempoteza rafiki yangu Muki"
Judy akadakia haraka haraka,
"Hivi ni nani aliyeanza kumtafuta mwenzake kama sio wewe? Bila wewe mimi nisingekujua..."
Shaibu akadakia,
"Sio mimi kabisa , bila wewe kuja kufanya muamala siku ile unadhani mimi ningekuona wapi? Ni wewe ndiye uliyenifanya nikujue"
Judy naye akaingilia kati,
"Mimi nilikuja kufanya muamala kama mteja tu lakini wewe ukachukua namba yangu kwa mapenzi yako na kunitafuta, hapo maana yake ni wewe ndiye uliyeanza....na hata wewe kuja hapa ni kwa sababu ya bomoabomoa wala sio mimi, kama isingekuwa bomoa bomoa basi nyinyi hadi leo mngekuwa mnakaa palepale..."
Shaibu na yeye akaketi katika sofa maana alikuwa amesimama muda wote huku akionekana kama maneno ya Judy yamemuangia hivi.
Baadae Judy akakazia maneno yake...
"Kwa hiyo nadhani sasa hivi umeanza kunielewa, hebu unganisha matukio yote yaliyopita utakuja kuona kama hakuna jambo ambalo tungeweza kuliepuka, kwa sababu kila nikifikiria kwakweli pale mwanzoni nilijikuta tu nimelala kwako bila hata kujua na sikupanga kabisa nifanye kitu kama kile...."
Shaibu akashika kidevu na kumuuliza Judy,
"Kwa hiyo maana yako ni kwamba sisi tukae hapa hadi aje kutuua Mr Shamte alafu ndio tuseme hiyo ndiyo hatma yetu na kwamba hatukuwa na uwezo wa kuepukana naye?"
Judy akatulia kidogo kisha akasema,
"Mimi nakuambia wewe huwezi jua tulichoandikiwa, unaweza ukakaa hapa na usije kumuona tena Mr Shamte, pengine kapata ajali alivyotoka hapa! Shaibu nakuambia hauwezi kuijua hatma yake na kamwe huwezi kuibadili hatma yako, wewe si unamkumbuka yule msanii maarufu wa kule Marekani , Michael Jackson? Sasa yule aliajiri madaktari zaidi ya 20 ili waangalie afya yake kila siku kwa lengo la kutaka kuishi miaka 150 hapa duniani ila si unajua kilichompata? Je alifikisha? Amini kwamba huwezi kuipekuka hatma yako, tubaki hapa hapa lililopangwa ndilo litakalotokea...."
Mjadala ulionekana kutofika mwisho kwa sababu kila mmoja alikuwa anaamini lake, wakaufunga mjadala kwa kuanza kuzungumza mada zingine.
Usiku wa siku hiyohiyo , Judy alianza kuhisi maumivu makali sana kwenye tumbo lake. Hakuweza kulala wala kukaa, ilikuwa ni ghafla tu kama kuna kitu kilikuwa kinamchoma kwa ndani hivi.
Hali ilikuwa mbaya, ikabidi Shaibu afanye mpango wa kumpeleka hospitali, akatafuta bajaji na kuweza kumwawisha hosptali.
Madaktari walimpokea na kuanza kumpatia matibabu huku Shaibu akisubiri hatma yake.
Shaibu alikesha hospitali siku hiyo kusubiri Judy apate ahueni, hadi inafika asubuhi Judy alikuwa bado amelala maana alichomwa sindano ya usingizi kwa sababu alikuwa anahisi maumivu makali sana.
Zilipita siku mbili , Judy akiwa bado yupo hospitali, lakini alikuwa anaendelea vizuri.
Siku hiyo hiyo ya pili tangu Judy awe hospitali, mida ya saa saba mchana hivi wakati Shaibu akifanya maandalizi ya mwisho ya kuondoka na Judy ili warudi nyumbani, kuna gari la ofisi ya Mr Shamte liliingia , Shaibu aliwaona baadhi ya wafanyakazi wa Mr Shamte wakimshusha mtu na kumuweka kwenye wheelchair kisha wakaanza kumkimbiza kumpeleka kwa daktari. Shaibu alipoangalia vizuri alimuona Mr Shamte ndiye alikuwa anakimbizwa.
Shaibu akasogea karibu na kumvuta mfanyakazi mmoja ambaye baada ya kumuona Shaibu tu aliona aibu kwani alikumbuka ushahidi wake wa uongo ambao aliutoa akiwa mahakamani,
Shaibu wala hakukumbuka hilo, cha kwanza yeye aliuliza kinaendelea kitu gani.
Mfanyakazi huyo alisema,
" Mr Shamte wakati anakaribia kufika kazini kwenye ile kona aligongana na lile gari linaloleta maziwa pale ofisini, kwa bahati mbaya sana kioo cha gari yake kilivunjika sana na chenga chenga zake zimemwingia machoni, yaani mpaka muda huu haoni kabisa na sijui kama ataona tena asee...."
*Itaendelea*
Baya huzaa baya , wema huzaa matunda.
Vinavyoenda kwa kujizungusha hurudi kwa kujizungusha pia.
Shaibu na Judy wanaingia katika mgongano mkali wa kimawazo wa nini cha kufanya kwa wakati huo baada ya kuanbiwa kuwa wanatakiwa waondoke kwa Mr Shamte, Judy anaonesha msimamo wa kutaka kubaki palepale huku Shaibu akipata hofu ya kubaki hapo hapo.
Judy anaugua tumbo la ghafla na Shaibu anamkimbiza hospitali, Wakiwa hospitali , Shaibu anawaona wafanyakazi wa Mr Shamte wakimleta Mr Shamte akiwa kama mgonjwa mara baada ya kupata ajali. Mfanyakazi mmoja anamwambia kuwa chenga chenga za vioo vimeingia katika macho ya Mr Shamte ambapo vimesababisha kutoona vizuri......
Sasa endelea hapa....
Baada ya mfanyakazi huyo kumweleza hivyo Shaibu, Shaibu alistaajabu sana, aliona ni kama muujiza. Shaibu ilimjia huruma moyoni mwake, roho ya kisasi hakuwa nayo kabisa, alimuombea kwa Mungu ili apate nafuu na aweze kupona.
Mfanyakazi huyo akasema,
"Kaka ngoja tuendelee kupambania afya ya bosi wetu, ila nakuomba unisamehe mimi na wafanyakazi wenzangu wote ambao tulitoa ushahidi wa uongo, mimi najua uliumia sana ila kaka hatukua na jinsi, ilitulazimu tufanye vile kwani kama tusingefanya vile kazi tungekosa na kama ujuavyo mimi nina familia inanitegemea, unadhani kwa jinsi hali ilivyo ngumu sasa hivi bila kazi hapa Dar utaishi vipi? Nisamehe kaka, haya yote ni maisha na teyari limeshapita hilo....."
Shaibu huku akionesha tabasamu lisilo la kinafiki akasema,
"Aaaah ! Mimi niliyaacha palepale mahakamani, mimi nilijua hamkufanya vile kwa makusudi , nilijua ni shinikizo la Mr Shamte na kwa sababu nyinyi mlikuwa mnatetea tonge lenu, vile mlivyofanya ndiyo hivyo hivyo ila yote kwa yote mimi sina kinyongo chochote na nyinyi ni ndugu zangu......
Mimi nimekuja hapa kumleta Judy, unajua Judy tukio ambalo alifanyiwa hadi sasa bado hajakaa vizuri, ingawa anaonekana yu mwenye afya lakini tumbo linamsumbua mara kwa mara, daktari hapa katuambia inabidi tuende muhimbili akafanyiwe uchunguzi wa kina"
Wakati wakiendelea kuongea daktari alimwita Shaibu na kumwambia teyari wameruhusiwa na wanaweza kuondoka.
Shaibu akaagana na mfanyakazi huyo kisha akamfuata Judy na kuondoka naye.
Walirudi kwenye nyumba ileile, lakini Judy hakuonekana kuwe mwenye furaha , alionekana yu mchovu kutokana hitilafu ambayo imetokea kwenye mwili wake.
Shaibu akamwambia Judy juu ya habari za Mr Shamte. Chuki alizonazo Judy juu ya Mr Shamte hazikuweza kuelezeka. Taarifa za kuugua kwake zikamfanya Judy apate nguvu na hata akasahau kabisa kama alikuwa mgonjwa .
Judy aliinuka na kuruka juu kama tai, kisha akatua chini kama ndenge za Air tanzania almaarufu kwa jina la bombadier, huku mikono ikiwa kiunoni, kisha akasema,
"Be serious Shaibu, Really??"
"Yes..... really, why nikudanganye? "
"If it is...afe kabisaa"
"Mmmh Judy acha hizo, Kusamehe ndio njia ya kuifungua minyororo ya chuki iliyofungwa katika moyo wenye maumivu, kama ujuavyo chuki siku zote inamdhuru yule ambaye anaihifadhi ndani ya moyo wake, chuki na kinyongo ni adui wa afya, afya njema hutokana na moyo safi ambao hauna kinyongo wala chuki....Hauko sahihi kabisa kusema bora afe tu, ni kweli kafanya mabaya kwako ila unatakiwa uyaache hayo yote, hebu chukulia mfano, kwa sasa hivi wewe umeshatambua kuwa Mr Shamte ana mke, je yule mke wake akikijua wewe utasemaje? Au na yeye awe na chuki na wewe? "
" Mmmh! We naye ushaanza falsafa zako ambazo hazihusiani hapa, sasa mke wa mr Shamte anaanzaje kuwa na kinyongo na mimi? Mimi nimekuwa na yeye Mr Shamte ila sikujua kama ana mke, kosa la nani hapo? Mimi au mumewe? ....chuki huelekezwa kwa mkosaji, Siwezi kumchekea mtu muovu na hilo lishamte likafie mbali huko...."
"Eeeh basi...ngoja tuachane na masuala ya Mr Shamte, dokta amesema inabidi tuende Muhimbili ili ukaangaliwe upya maana amesema tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi kama ikiwa litachelewa kutafutiwa ufumbuzi, kwa hiyo kesho tutaenda Muhimbili ili ukaangaliwe upya"
Shaibu baada ya kusema hivyo ,Judy akaketi kwenye sofa alafu akamuuliza swali Shaibu,
"Hivi Shaibu baada ya haya yaliyonitokea bado unataka kuendelea kuwa na mimi?"
Shaibu akajiweka vizuri huku akimwangalia usoni Judy na kumuuliza ,
"Una maana gani? Bado sijakupata vizuri...."
"Maana yangu hii, si unajua unyama niliofanyiwa? Nimebakwa hovyo hovyo, sasa nakuuliza kuwa hayo yote bado moyo wako upo kwangu?"
Shaibu hakujibu , alisita kidogo, Judy alibaki akimwangalia tu Shaibu huku akimsubiri aseme neno.
"Vipi? mbona kimya?"
Judy aliuliza.
"Aaah maswali mengine bana ....sioni kama yana umuhimu, hebu achana nalo hilo swali"
Shaibu alijibu na akajifanya hataki maongezi hayo yaendelee. Judy akasema,
"Shaibu swali langu lina maana kubwa sana, nilipanga nikuulize tangu nipo hospitali kulekule ila nikavuta subra hadi leo ndio nimeona nikuulize tu, wewe nijibu tu chochote kilichopo kichwani mwako..."
Huku akitabasamu, Shaibu akasema,
"Why not...?!!! Kwani lile limetokea umepanga wewe? Is not your fault ...bado nakupenda and nitakuwa na wewe..."
Judy akamwangalia Shaibu kisha akamuuliza tena,
"Wale watu hawakutumia kinga yeyote , nina hofu na afya yangu ila ni lazima hapo kesho nitakapoenda hospitali, nikapime na HIV nione itakuwaje, alafu nimekumbuka jambo , wakati ule unaumwa ulisema nimekuua kwanini ulisema vile?"
"......aaah tuachane na hayo yashapita ...."
"Ok anyway
......one more question, sasa ndo tuseme kesho napewa majibu after HIV tested, which kind of answer do you prefer? "
Shaibu baada ya kuulizwa swali hilo na hapo akasita tena, akatulia hakujibu ila baadae akajitoa kimasokimaso, akasema,
"Judy si unakumbuka ulisema binadamu hawezi kuijua wala kubadiri hatma yake? Sasa mimi sioni sababu ya kujadili mambo ya mbele ambayo pengine hatuwezi kuyabadirisha , ngoja tusubiri tuone majibu yatakuwaje ..."
"Kwa hiyo nikikutwa positive? Utafanyaje?"
"Heeeee!! Wewe naye king'ang'anizi kama kupe vile...hebu tuachane na haya mambo , ngoja nikaangalie chips hapo nje ule kwanza..."
Judy akacheka kidogo kisha akaachia tabasamu huku akiamini Shaibu amekwepa kujibu maswali yake labda pengine majibu yake yangemkwaza.
Siku ikapita na asubuhi yake, walienda hospitali ya taifa Muhimbili. Walienda hadi kwa daktari bingwa , wakamfanyia chek up ya mwili mzima Judy.
Wakabaki nje , kusubiri majibu, Shaibu naye siku hiyo alipima HIV.
Wakati bado wanaendelea kusubiri, alifika mama mmoja hivi , akawasalimia akina Shaibu na kuwauliza kama wanaijua wodi ya wagonjwa wa macho. Shaibu na Judy hawakuijua, yule mama kaamua kukaa karibu na akina Shaibu kisha akawa anapiga simu.
"Haya mambo mengine ni laana , nakuambia shoga yangu yaani bora hata life tu ,yaani sijawahi ona raha ya mume hata siku moja, lile limwanaume bora life tu, hapa nimefika ila bado sijaonana nao ndio naulizia ulizia hapa...."
Kwa sababu mama huyo alikuwa karibu sana na Shaibu, Shaibu akaweza kusikia vyema maneno yanayotoka upande wa pili, upande wa pili ukasema,
"Shoga mimi nilikuambia wewe vumilia tu sio unaona eeh, yaogope sana machozi ya binadamu ambayo hayana hatia...mara nyingi machozi yao hulipwa na Mungu mwenyewe! Basi baadae utanipa mrejesho"
Mama huyo akakata simu, alafu akasimama na kuanza kuendelea kuuliza. Wakati huohuo , Shaibu alimuona mmoja wa wafanyakazi wa Mr Shamte akiwa anatoka kwa ndani na kuja upande wa nje ambao wapo wao.
*ITAENDELEA*
Kamwe usiruhusu chozi la binadamu asiye na hatia likulilie na kisha kukaukia katika mashavu yake, ipo siku utayalipia machozi hayo.
Tuishi huku tukijua kila jambo linapita tu hapa duniani kwani vyeo, pesa, au mali ni za muda tu, hakuna jambo la kudumu hivyo kila binadamu mchukulie ana umuhimu fulani katika hii dunia na yupo wa kusudi maalumu.
Tuendelee kuzingatia ushauri wa wataalamu kuhusu Corona.
Mr Shamte yamemkuta yakumkuta, macho yake hayaoni, Judy anafurahia habari za Mr Shamte, Shaibu na Judy wanaenda hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kwenda kuangaliwa mwili wote , wote wanachuliwa vipimo vya damu na kusubili majibu, wakiwa wanaendelea kusubiri kuna mama mwingine naye anaingia hapo hapo.....
Tuendelee......
Shaibu alipomuona mfanyakazi wa Mr Shamte akiwa anaelekea upande walipokaa yeye na Judy akabaini kuwa Mr Shamte atakuwa ameletwa hospitalini baada ya kuhamishwa hospitali ya mwanzo.
Yule mfanyakazi kabla hata hajawafikia akina Shaibu, alimuona mama ambaye alikuwa anaulizia wodi ya wagonjwa wa macho, alimfuata na wakasalimiana, kisha akawa anamwelekeza kitu, mda mchache tu, wakaachana , alafu mfanyakazi huyo akaendelea na safari yake. Mbele akakutana na Shaibu.
Mfanyakazi huyo akamweleza Shaibu kuwa ile hospitali ya mwanzo ilishindikana kabisa hivyo akapewa uhamisho wa kufika hapa jana ileile. Shaibu alipomuuliza kuhusu yule mama , aliambiwa kuwa ni mke wa Mr Shamte.
Mfanyakazi huyo akaendelea kueleza,
"Hata hivyo kaka ninachokuambia Mr Shamte hawezi kuona tena , wamesema mboni imeharibika kabisa na hawana namna yeyote ya kumfanya aweze kuona tena, hapo sasa hivi wanamfanyia upasuaji tu na macho yote yatatolewa kisha atawekewa macho ya bandia, daaah inatia huruma kaka ila ndio hivo tena mipango yake Mungu...."
Shaibu akasikitika sana baada ya kupokea taarifa hizo, Judy alipozipata tu akawaambia waache kumuonea huruma Mr Shamte kwani hayo ameyataka mwenyewe.
Maongezi hayakuendelea tena, yule mfanyakazi aliendelea na safari zake na wakati huohuo Judy na Shaibu waliitwa na daktari kwenda kupewa majibu yao.
Safari hiyo Shaibu wala hakuwa na hofu kama ile ya mwanzo, Daktari aliyasoma majibu na wote kwa pamoja wakawa teyari kuyasikia.
Majibu ya damu kwa wote yalikuwa negative, damu haikuonekana na vijidudu vyovyote. Tatizo lilionekana kwa Judy ambapo mfuko wake wa uzazi ndio ulikuwa na hitilafu. Kuna dawa waliandikiwa wakazitafute na aanze kuzitumia baada ya muda fulani anaweza kukaa sawa na shida hiyo ya kusumbuliwa na tumbo itaisha.
Shaibu na Judy wakarudi nyumbani kwao , nyumba ambayo imepatiakana kama zawadi vile kwa ujinga wa Mr Shamte.
Zilipita siku tatu, Judy akiwa anaendelea kutumia dawa , Shaibu akapata shauku ya kutaka kujua hatma ya Mr Shamte ilikuwaje. Kwa sababu hakuwa na simu kwa wakati huo, aliamua kwenda moja kwa moja hadi Muhimbili.
Kwa bahati nzuri akiwa pale Muhimbili, akiwa anahangaika ngaika kuitafuta wodi wanayolaza wagonjwa wa macho, alikutana na daktari ambaye siku tatu nyuma ndiye aliyewahudumia yeye pamoja na Judy.
"Vipi bwana Shaibu mbona himahima hivi?"
"Aah bwana daktari kwanza habari yako ? Habari za tangu juzi?..."
"Salama tu, vipi mbona hivi....?"
"Aaah kuna mgonjwa fulani hivi wa macho aliletwa hapa tangu yale majuzi ndio nimekuja kumwangalia , sasa hapa hata wodi yenyewe siijui...."
"....Ni ndugu yako?"
"Hapana , aliwahi kuwa bosi wangu...."
"...oooh hebu subiri kwanza..... (daktari anachukua simu na kumpigia mtu)"
Daktari huyo alimpigia simu daktari mwenzake kisha akamuulizia mgonjwa huyo , maana wakati wanaendelea kuongea Shaibu alimtajia na jina la mgonjwa kabisa, majibu ya daktari hayakuwa mazuri sana, Mr Shamte umauti ulimkuta wakati akifanyiwa operesheni ya macho na hii ilitokana na BP (blooad pressure ) ambayo ilipanda ghafla wakati akifanyiwa huwa operesheni. Daktari alisema kuwa baada ya Mr Shamte kupewa taarifa kwamba hataona tena ndio sababu iliyomfanya BP ipande. Daktari akaeleza kuwa teyari ndugu zake wamechukua mwili wake na wameondoka nao.
Baada ya kumaliza akakata simu kisha akamwelezea Shaibu alichoambiwa. Shaibu akayapokea maelezo kisha wakaagana na kila mmoja akaendelea na safari zake.
Baada ya kutoka hapo, Shaibu alienda moja kwa moja ofisini kwa Mr Shamte ili angalau akapate maelezo juu ya kifo chake.
Ofisi kwake hakukuwa na mtu zaidi ya mlinzi na wafanyakazi wa usafi. Lakini kwa sababu Shaibu alikuwa anajulikana aliulizia habari za Mr Shamte kwa mlinzi huyo.
"Kijana wangu kama ulivyosikia ndivyo hivyo hivyo wala hakuna mabadiriko, hivi tunavyoongea teyari ameshazikwa huko kwao Tanga, na hapa kama unavyoona wafanyakazi tumebaki sisi tu, wengine wote wameenda kwenye maziko huko Tanga"
Shaibu akatulia kidogo kisha akauliza swali la kiudadisi,
"Hivi ajali ilikuwaje ? Ni kweli hawakuweza kuonana mpaka wakagongana na kusababisha haya yote?"
"Aaah mdogo wangu , dunia ina mambo yake bwana! Yaani haya mambo yametokea kimaajabu ajabu tu, huwezi amini lakini ndio hivyo tena ishatokea, mimi nakuambia yule kapigwa kipaipai (amerogwa) , unajua hawa watu wenye pesa wana maadui wengi na wana mambo mengi tusiyoyajua lakini tubaki kuamini tu kuwa siku zake zimetimia..."
Shaibu na mlinzi huyo ambaye kwa umri ni wazi kuwa alikuwa mzee, waliongea mambo mengi sana na baadae Shaibu akarudi zake kwa Judy na kumuhadithia kila kitu alichosikia kuhusu Mr Shamte.
Ingawa mwanzoni alimchukia sana Mr Shamte, nafsi ya Judy ilisononeka habari za kifo cha Mr Shamte, alimuombea msamaha kwa Mungu.
".....hii ndio kazi ya Mungu, huwa hainaga kasoro, mtenda maovu hulipwa maovu na mema hulipwa mema, nimeamini usijivunie vitu ambavyo haviwezi kuokoa uhai wako, kwa sababu kuna muda ukifika havitakuwa na msaada kwako....Rest in peace Mr Shamte...."
Judy aliongea hivyo na akaelekea zake jikoni kuangalia chakula chake ambacho kilikuwa kinaendelea kuiva.
Shaibu naye akaunga safari, wote wakaingia jikoni huku Shaibu akimpigisha stori Judy , nini wafanye ili waweze kupata pesa na waendelee na maisha.
Shaibu akatoa wazo wauze gari la Judy alilonunuliwa na Mr Shamte kisha baadhi ya pesa zitakazopatikana waziingize kwenye biashara ya Shaibu ya zamani ambayo ndiyo alianza nayo, biashara ya miamala.
Wazo la Shaibu likaonekana bora maana waliona kuanza kutafuta ajira tena ni kama kujichosha tu kwa sababu kila ofisi nafasi za ajira zimekuwa chache sana, hivyo kujiajiri wao wenyewe ndio njia pekee ya kuwafanya wapate kipato.
Walimtafuta dalali, kwa sababu gari halikuchakaa sana ndani ya siku mbili tu walishampata mteja na wakaliuza.
Walitafuta flemu kubwa maeneo ya rangi 3 (mbagala) kisha wakatafuta laini za uwakala , pia walinunua na mshine za uwakala wa benki. Pia ndani ya flemu hiyo waliweka na Stationary. Mambo yalianza vibaya lakini baadae wateja wakazoea na wakawa wanafanya biashara sana.
Waliamua kutambulishana rasmi kila mmoja kwa ndugu zake, mipango ya harusi pia ilifanyika, ndoa ikafungwa na maisha mengine yakaendelea.
Mke wa Mr Shamte naye baada ya kukamilisha taratibu za mazishi zote, aliamua kuiuza kampuni maana yeye aliona atashindwa kuisimamia kikamilifu.
*MWISHO*
Maisha ya mwanadamu ni ya mapito, hakuna sababu ya kuwadharau wengine.
Ukitaka kuruka agana na nyonga (Kila jambo angalia matokeo kwanza, kisha uone kama linafaa au halifai alafu fanya au acha.
Yote kwa yote wema ni akiba, ubaya ni jeneza!
*MWISHO*
0 comments:
Post a Comment