Search This Blog

Sunday, February 26, 2023

MAPENZI YA FACEBOOK - 1

   

IMEANDIKWA NA: JUMA HIZA

*******************************************************

Chombezo :  Mapenzi Ya Facebook 

Sehemu Ya Kwanza (1)


Phidelis anasimulia;


Nakumbuka nilifahamiana naye kupitia Facebook, alikuwa ni rafiki yangu, nilipenda sana kulike pamoja na kukomenti picha zake. Alikuwa ni msichana mrembo sana, alijaaliwa kila sifa zinazoweza kumshawishi mwanaume yoyote rijali atamani kuwa naye. Alikuwa akijulikana kwa jina la Cleopatra Mushi ila kwa facebook alikuwa akitumia jina la Precious Girl, sijui kwanini aliamua kutumia jina hili ila pengine ni kutoka na uzuri aliyokuwa nao.

Alikuwa akipenda sana maisha ya starehe, picha zake alizokuwa akipost katika akaunti yake ziliweza kuakisi maisha halisi ambayo alikuwa akipendelea kuishi. Alionekana kuwa msichana wa maisha ya kitajiri sana.

Nilitamani sana kuwa naye kimapenzi ila sikuwa na maisha kama aliyokuwa nayo hivyo niliona sikustahili kufanya hivyo, niliogopa kumwambia.

Picha zake alizokuwa akizipost akiwa na mwanaume zilizidi kuniweka katika wakati wa maumivu sana, nilikuwa nikiumia kwasababu nilikuwa nikimpenda sana. Nilitamani siku moja afahamu ni kwa jinsi gani nilivyokuwa nikimpenda lakini muda haukuweza kuruhusu hilo.

“Nampenda sana huyu demu ila tatizo ana mtu wake,” niliamua kumueleza ukweli rafiki yangu Juma juu ya Cleopatra alivyokuwa ameniteka akili yangu.

“Sasa unachoogopa hapo ni nini?” aliniuliza Juma huku akionekana kutojali lolote.

“Tatizo ana mtu wake.”

“Mbona mimi sioni tatizo hapo kama unampenda mwambie ukweli halafu akikataa basi unakula kona,” aliniambia Juma.

Kwa kweli kila nilipokuwa nikizitazama picha za Cleopatra zilizidi kuniweka katika wakati mgumu, nilikuwa nikimpenda sana. Nilitamani afahamu ukweli wa moyo wangu. Ulikuwa ukimpenda japo mpaka kufikia wakati ule sikuwa nafahamu historia ya maisha yake.

“Umependeza mdada,” niliamua kukomenti picha yake moja aliyokuwa ameipost muda mfupi. Alikuwa amevalia sketi fupi iliyoyaacha vyema mapaja yake wazi yaliyoonekana kunona huku juu akiwa amevaa kishati kilichokuwa kimembana kisawasawa, kilimkaa vyema na kuzidi kuonekana msichana wa kisasa. Alipendeza sana tena na kwa weupe aliyokuwa amejaaliwa ndiyo kwanza alizidi kunoga.

“Asante mkaka,” alinijibu kitendo ambacho kilinishangaza sana, sikutegemea kama angeweza kunijibu kwa wakati ule.

Ngoja nikuambie kitu ndugu yangu, nilikuwa nikipenda sana kulike na kukomenti picha zake, nilikuwa nikijaribu kujiweka karibu naye ili japo niweze kupata nafasi ya kuzungumza naye lakini mara zote alikuwa ni mtu wa kunitolea nje, hakuwa akinijibu lolote.

Siku ile nilipoamua kukomenti picha yake na yeye kunijibu hakika nilikiona kuwa nikitendo cha kipekee. Niliitazama kwa muda wa dakika tatu lile jibu lake huku nikitabasamu. Nilikuwa nahisi furaha isiyokuwa na kifani.

Sikutaka kupoteza muda nikaamua kumfuata inbox.

“Mambo mrembo,” nilimtumia ujumbe mfupi lakini alikuwa kimya hakuweza kunijibu lolote. Sikukata tamaa, niliamua kumtumia tena ujumbe mwingine lakini hakuweza kujibu kitu. Tukio hili lilizidi kuniumiza sana, alikuwa akionekana kuwa online lakini hakuwa akizijibu meseji zangu jambo ambalo lilizidi kunifanya nianze kumuona alikuwa akijisikia.

Kila nilipokuwa nikiziona picha zake pamoja na mwanaume aliyekuwa akimpost katika akaunti yake nilikuwa nikijisikia vibaya sana, kuna kipindi sikutaka kabisa kumuona Cleopatra katika macho yangu. Niliamua kutoka facebook na kufanya mambo mengine lakini ajabu haikupita siku nilijikuta nikitamani kumuona msichana huyo hivyo niliingia facebook na kumuangalia. Nilijikuta nikifurahi mara baada ya kumuona. Alikuwa akivutia sana machoni mwangu.

“With my baby!” haya yalikuwa ni moja kati ya maelezo yaliyoambatana na picha aliyokuwa amepiga yeye pamoja na mwanaume mmoja aliyekuwa na asili ya kiarabu. Walikuwa wakionekana kuwa wenye furaha sana.

Nilizidi kuumia sana kila nilipokuwa nikimuona mwanaume huyo, nilimchukia sana katika maisha yangu japo sikuwahi kuonana naye.

Sikuchoka kumtumia ujumbe mfupi kila nilipopata nafasi niliamua kumtumia huku nikiamini kuna siku angeweza kunijibu jambo ambalo lingeweza kuufurahisha moyo wangu.

Baada ya kupita siku kadhaa aliweza kunijibu.

“Poa Phidelis, mzima wewe? Samahani nilikuwa bize ndiyo maana ukaona kimya.”

“Usijali, mimi niko salama kabisa sijui wewe mrembo.”

“I’m oky.”

“Nafurahi kusikia hivyo mrembo.”

“K,” alinijibu kwa kifupi kwa kuandika herufi “K” akimaanisha neno Ok.

Kwa kweli nilijisikia vibaya sana, niliona kama alikuwa amenidharau. Nilijaribu kumtumia ujumbe mwingine lakini hakuweza kunijibu lolote japo nilimuona kuwa online. Hilo lilizidi kuniumiza sana moyoni mwangu.


Hakika mapenzi yalikuwa yakiniendesha sana wala siwezi kulipinga hilo. Kabla sijamfahamu huyu Cleopatra au Precious Girl katika mtandao wa facebook kipindi cha nyuma niliwahi kuwa katika mahusiano na msichana mmoja ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la Ester. Alikuwa ni msichana mrembo sana, alitokea kuuteka moyo wangu.

Niliamua kufunga pingu za maisha na yeye ni kwasababu nilikuwa nikimpenda sana, alikuwa akinipenda na kunionyesha mapenzi ya dhati yaliyozidi kunifanya nimuone yeye tu katika sayari ya mapenzi.

Uwepo wake katika maisha yangu ulikuwa ni wa thamani sana. Mapenzi yetu yalikuwa yametawaliwa na furaha sana, nilikuwa nikimpenda sana lakini naweza kusema ndoa yetu ilikuja kuingiliwa na mdudu. Mdudu ambaye amefanya mpaka leo hii nimeamua walau kuwasimulia kile kilichowahi kutokea katika maisha yangu hasahasa maisha ya kimahusiano.

Facebook! Ndiyo mdudu aliyekuwa akiitafuna ndoa yangu na Ester. Licha ya mapenzi niliyokuwa nayo kwa mke wangu lakini bado Facebook ilizidi kuidhulumu nafsi yangu ya upendo.

Nakumbuka siku ya kwanza Ester kujiunga na Facebook ilikuwa ni pale ambapo niliamua kumnunulia simu. Hii ilikuwa ni moja kati ya ahadi ambayo nilimuahidi kwa muda mrefu. Nilimuambia mambo mengi sana ambayo yanaweza kutokea katika mtandao huu. Nilimuambia juu ya maisha feki wanayoishi watu facebook. Sikutaka kumficha kitu ni kwasababu na mimi nilikuwa ni mtumiaji wa mtandao huu.

“Jamani mume wangu inamaana huniamini au?” aliniuliza Ester kwa sauti ya kudeka.

“Hapana sio kama sikuamini ila najaribu kukuambia tu,” nilimjibu huku nikimsogelea, wakati huo tulikuwa tupo chumbani.

“Mimi sipendi jinsi unavyonihisi vibaya.”

“Najua hupendi mke wangu ila nayasema haya ili kulilinda penzi langu.”

“Hata kama mume wangu lakini unajua fika kuwa nakupenda wewe na siwezi kuwa na mwanaume mwingine zaidi yako.” aliniambia huku akiwa amejilaza kifuani mwagu, maneno yake yalipenya vyema masikioni mwangu na kunifanya nijihisi mwenye bahati hasa kwa kumpata mwanamke ambaye alikuwa akinipenda sana na hakuwa tayari kunipoteza katika maisha yake.

“Chunga Facebook isije ikavuruga ndoa yetu,” nilimuambia huku nikimpapasa taratibu mgongoni.

“Usijali Mume wangu nakupenda sana,” aliniambia kwa sauti ya kitoto.

“Nakupenda pia,” nilimjibu katika namna ya utulivu sana.

Niliwahi kushuhudia jinsi Facebook ilivyovuruga mahusiano ya watu. Facebook ndiyo ilikuwa chanzo cha migongano na mikanganyiko ya ndoa nyingi ambazo ziliwahi kuvunjika. Mimi ni shahidi katika hilo, nakumbuka Facebook ndiyo ilikuwa chanzo cha kuvunjika kwa ndoa ya kaka yangu ambaye alikuwa akimpenda sana mkewe ambaye nilikuwa nikimuita shemeji.

Kwa kweli sikutaka yale yaliyowahi kutokea katika maisha ya kaka yangu yaweze kunitokea. Nilijifunza mambo mengi sana hivyo nilikuwa makini sana hasa kwa kulilinda penzi langu, kuilinda ndoa yangu, roho yangu.

Baada ya kupita wiki moja tangu mke wangu Ester ajiunge na Facebook nilianza kupatwa na wasiwasi mkubwa sana. Sikujua wasiwasi ule ulikuwa ukitokea wapi hasa kwani tayari Ester alikuwa ameshakuwa mke wangu, mke halali kidini.

Simu yake ilikuwa ikipigwa kila wakati na namba ngeni. Niliamua kumuuliza kuwa namba zile zilikuwa ni za watu gani ila mara zote alikuwa akinijibu kuwa walikuwa ni watu wa Facebook ambao walikuwa wakimsumbua.

Wivu ulianza kunisumbua Phidelis mimi ambaye nilizama katika dimbwi la mapenzi, ulianza kunitafuna taratibu na kuniacha na maumivu ambayo sikuyatarajia kwa kipindi kile. Kuna kipindi nilikuwa nikijilaumu ni kwanini niliamua kumnunulia simu ambayo iliweza kumuunganisha na mtandao huu wa Facebook.


Angalizo: Mnaosoma msipite kimya kimya bila kusema lolote. Ukimaliza kusoma toa maoni yako, Like pamoja na Share ili simulizi hii isomwe na wengi.


Unajua nini kilitokea?

Hebu bashiri, niambie nini kitatokea?




Nilizidi kuwa katika wasiwasi mkubwa sana hasa baada ya kuona mke wangu Ester akianza kusumbuliwa na watu aliyodai kuwa walikuwa ni wa Facebook.

“Huyu anayekupigia simu usiku huu ni nani?” nilimuuliza usiku mmoja, yalikuwa ni majira ya saa tano za usiku.

“Simfahamu mume wangu halafu si unaona ni namba ngeni?” alinijibu huku akionekana kuipuuzia simu iliyokuwa ikipigwa.

Mpigaji wa simu ile hakuchoka, alizidi kupiga kila wakati jambo lililozidi kunichukiza sana. Nilijiuliza maswali mengi sana, kila nililokuwa najiuliza lilikosa jibu kwa wakati ule.

“Pokea simu,” nilimuambia baada ya kuona mpigaji wa simu hakuonekana kukata tamaa, alizidi kupiga tu!.

“Hapana mume wangu huu ni usiku halafu sio vizuri kupokea simu za watu tusiowafahamu,” aliniambia.

“Tusipokee au usipokee mbona unanihusisha.”

“Mume wangu tusigombane kisa simu tuachane nayo,” aliniambia kisha akakata simu.

Kitendo hicho kiliniumiza sana, sikutaka kuamini kama mke wangu Ester alikuwa na kiburi kiasi hicho. Ni hapa ambapo tuliingia katika mzozo na sababu kubwa ikiwa ni simu.

“Kwanini umekata simu?” nilimuuliza.

“Amna.”

“Amna?”

“Mume wangu embu tuyaache hayo.”

“Kwanini unapenda kucheza na akili yangu?”

“Kivipi?”

“Nimekuuliza huyu aliyekuwa akikupigia simu ni nani?”

“Simjui.”

“Ester!”

“Kweli mume wangu,” alinijibu katika namna ya kuielegeza sauti yake huku akinisogelea halafu akanikumbatia.

“Mume wangu niamini, nimekuambia mara ngapi kuwa simfahamu huyu mtu halafu naomba mitandao isiharibu ndoa yangu nakupenda sana baba wa wanangu,” aliniambia huku akinipapasapapasa mgongoni.

Nilizidi kuwa katika hali ya sintofahamu. Maneno ya Ester yalinifanya nimuone kama alikuwa akizungumza ukweli mtupu wala hakuwa akiniongopea lakini katika upande mwingine nilimuona kuwa alikuwa akitafuta njia za kutaka kunizunguka kiakili ili nisiweze kufahamu kile kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia. Hilo lilizidi kuniweka katika wakati mgumu sana. Nilianza kuiona ndoa yangu ikiingia dosari. Nilimpenda sana mke wangu, alikuwa ndiyo sababu ya furaha yangu, wakati mwingine nilikuwa nikijaribu kukumbuka yale yaliyowahi kutokea katika maisha yetu kipindi cha mahusiano yetu.

Yale yote yaliyotokea sikutaka yaendelee kubaki moyoni mwangu, niliamua kuyasamehe na kufungua ukurasa mpya.

Siku iliyofuata asubuhi na mapema niliamua kumueleza ukweli mke wangu juu ya jambo lile pamoja na maamuzi yangu niliyokuwa nimeyaamua. Hakika alionekana kufurahishwa sana. Pengine niseme ni katika siku ambayo ilikuwa ni ya aina yake kwani sikuwahi kumuona mke wangu akiwa katika furaha hiyo hapo kabla tangu ilipopita harusi yetu.

“Asante mume wangu yani sikutegemea kama ungeamua hivyo,” aliniambia huku akinikumbatia kwa furaha.

“Kwanini unasema hivyo?” nilimuuliza.

“Unajua binafsi sikupendezewa na kile kilichotokea usiku ule, nakupenda eti mume wangu halafu Facebook inataka kuaribu ndoa yangu hivihivi,” aliniambia katika mtindo wa sauti ya kitoto.

“Usijali ila kuna kitu nataka nikuambie,” nilimwambia.

“Kitu gani hicho tena hubby?” aliniuliza kisha akajitoa katika lile kumbato.

“Ni kuhusu Facebook.”

“Imefanyaje?”

“Nisingependa kuona tena usumbufu katika simu yako.”

“Usijali Phidelis wangu, mwanaume wa maisha yangu,” aliniambia kisha akanibusu shavuni, busu ambalo lilizidi kuamsha hisia za dhati za kimapenzi.

Niliamini Ester ndiye alikuwa kila kitu katika maisha yangu, nilimpenda kwa dhati ya moyo wangu. Niliamua kusahau yale yote yaliyopita na kuamua kuendelea na maisha yetu kama kawaida lakini ilikuwa ni kama vile najaribu kuigiza upofu wakati macho yangu yalikuwa ni mazima. Ester alizidi kunifanyia visa na chanzo kilikuwa ni mtandao wa facebook.




Baada ya kupita siku kadhaa niliyaona mabadiliko makubwa sana kwa mke wangu, hakuwa mtu wa kusumbuliwa tena na namba ngeni. Kwa kweli hali hiyo ilinifurahisha sana, niliona maneno yangu yalisaidia sana hasa kwa kumbadilisha mke wangu. Sikuacha kumsifia katika hilo, alionyesha kunipenda sana na kila kitu kilichokuwa kikitokea ilikuwa ni lazima aniambie. Ni katika tukio hili nilizidi kumuamini sana kupita kawaida.

“Mume wangu,” aliniita siku moja nilipokuwa nyumbani, ilikuwa ni siku ya jumapili, siku hiyo sikwenda kabisa katika mihangaiko yangu ya kila siku.

“Naam,” niliitika huku nikimtazama, alionekana kuwa na kitu alichokuwa akitaka kuniambia ila alisita kuniambia akawa anatazama chini.

“Kuna nini?” nilimuuliza.

“Hakuna kitu,”alijibu huku akiwa ameinamisha kichwa chake chini.

“Mbona sasa upo hivyo,” nilimwambia huku nikijaribu kumuinua, alizidi kuona aibu kunitazama.

“Kuna kitu nataka kukuambia.”

“Kitu gani?”

“Kuna mtu ananisumbua.”

“Nani?”

“Mimi simjui ila ni wa facebook ila ananisumbua sana,” aliniambia huku akionekana kuchukizwa sana na kitendo hicho cha watu wanaomsumbua. Nilichomuambia ni kuacha mawasiliano na mtu huyo ambaye alikuwa akimsumbua.

“Usimjibu chochote,” nilimuambia.

“Sawa mume wangu,” alinijibu.

Nilizidi kumuamini sana mke wangu, kwa jinsi alivyokuwa akinieleza ukweli wa kile kilichokuwa kikindelea katika maisha yake pamoja na watu waliokuwa wanamsumbua hakika kiliniweka katika wakati wa kujiamini sana. Sasa kwanini nisimuamini wakati alikuwa akinieleza ukweli.

****

Siku moja niliamua kuingia facebook na kuanza kuipitia akaunti ya mke wangu. Nilikuwa mwenye furaha sana kwani mpaka kufikia hapo sikuwa na wasiwasi wowote kabisa kwa mke wangu, Ester wangu, Uaridi la maisha yangu.

Ghafla! nilishangazwa na kile nilichokuwa nikikiona katika akaunti ya mke wangu. Picha za nusu uchi alizokuwa amezipost huku nyingine akiwa amekaa mikao ya ajabu, zilizidi kunishangaza sana. Niliendelea kuipekuwa akaunti yake ambayo iliongoza kwa kufuatiliwa na wanaume wengi. Niliziangalia zile like elfu moja pamoja na komenti mia saba alizokuwa akikomentiwa katika picha zake.

“Mambo dada.”

“Poa Aidan.”

“Umetokelezea sana miss.”

“Asante sana.”


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog