Search This Blog

Sunday, February 26, 2023

MAPENZI YA FACEBOOK - 4

    

Chombezo :  Mapenzi Ya Facebook 

Sehemu Ya Nne (4)


Kwa kweli sikutaka kuendelea kuwa katika yale maumivu niliyokuwa nikiyapata kwa wakati ule, ni ukweli usiopingika kuwa nilimpenda sana mke wangu wala hakukuwa na mwanamke mwingine niliyekuwa nikimpenda zaidi yake, naweza kusema ukiotoa upendo niliyokuwa nao kwa mama yangu mzazi, mwanamke aliyekuwa akifuatia ni yeye.

Nilimpenda sana katika maisha yangu, nilimpa nafasi kubwa sana katika moyo wangu wa mapenzi. Aliishi kwa kujiachia sana nadhani hii ndiyo sababu iliyopelekea kuanza kunichanganya.

Tukio la kushuhudia namba ngeni zikiingia katika simu ya mke wangu pamoja na meseji mbalimbali halikuwa la kwanza kutokea, nakumbuka mara ya kwanza nilipolishuhudia niliweza kumkanya na alikiri kutorudia tena, ni kweli ilikuwa ni kama alivyokuwa ameniahidi lakini haikuwa katika maana ya kile alichokuwa akikizungumza. Bado aliendelea na tabia yake ya kisirisiri mpaka pale nilipobahatika kumfumania.

Kwa kweli sikutaka moyo wangu uendelee kupitia katika yale maumivu uliyokuwa ukiyapitia, niliamua kuachana na mke wangu. Niliamua kuachana naye ni kutokana na vituko alivyokuwa akinifanyia. Mapenzi aliyokuwa nayo kwangu yote aliyahamishia katika mtandao wa facebook, aliipenda sana Facebook na ndiyo sababu ambayo naweza kusema iliyosababisha mimi na yeye kutengana.

Yalikuwa ni maamuzi magumu sana ambayo yaliugharimu moyo wangu lakini nilijikaza kiume, sikutaka kuwa mdhaifu katika hilo hasa katika harakati za kupigania amani ya moyo wangu.

“Kwanini umeamua kufanya maamuzi hayo?” lilikuwa ni swali la kwanza kabisa la Juma kuniuliza mara baada ya kukutana naye na kumsimulia kila kitu kilichokuwa kimetokea.

“Juma sikuwa na njia nyingine ya kufanya,” nilimjibu huku nikimtazama, alionekana kuchukizwa sana.

“Phidelis rafiki yangu hivi unajua haupo sawa?”

“Kivipi?”

“Hivi utawezaje kumuacha mke wako kisa facebook.”

“Juma unazungumza kwa kuwa hujaoa, ingia katika ndoa utafahamu ni kwa jinsi gani mke anauma, asikwambie mtu ndoa ni ngumu mno imejaa kila aina ya matatizo.”

“Una maanisha nini?”

“Unaniuliza tena?”

“Ila haukuwa sahihi kuachana na mke wako.”

“Kama kuvumilia nimevumilia mengi tu, acha aende zake,” nilimwambia Juma huku akiendelea kunishangaa.

****

Baada ya kupita mwezi mmoja nilipata habari kuwa Ester anaolea tena, kiukweli sikutaka kuamini habari hizo japo kwa wakati ule nilikuwa nimeachana naye lakini kwa upande mwingine iliniuma hasa baada ya kusikia mke wangu niliyeachana naye alikuwa akiolewa na mwanaume mwingine, hilo lilizidi kunichanganya sana. Nayakumbuka maumivu niliyowahi kuyapata kipindi kile alipokuwa akinifanyia visa lakini haya yalikuwa ni maumivu mengine kabisa, niliumia kwasababu ya wivu. Wivu wa kumshuhudia mke wangu niliyeachana naye akiolewa na mwanaume mwingine.

Niliamua kuchunguza ukweli wa habari zile na hatimaye nikaweza kufahamu. Ester mke wangu alikuwa akiolewa na yule mwanaume aliyejulikana kwa jina la Osmon ambaye mapenzi yao yalianzia Facebook. Kwa kweli sikutaka kuamini kabisa kwa kile nilichokuwa nakishuhudia kwa macho yangu. Sijui ni kwanini nilikuwa katika maumivu makali kiasi hicho, niliamua kulipa kisasi, kisasi cha kumtafuta mwanamke facebook ambaye ningeweza kumuoa. Ama kwa hakika facebook imeficha siri nyingi sana, kama lilivyo jina lake nilikwenda kupenda kitabu nisichokifahamu kabisa.


Angalizo: Mnaosoma msipite kimyakimya bila kusema lolote. Ukimaliza kusoma toa maoni yako, Like na Share ili simulizi hii isomwe na wengi.


Unajua nini kilitokea?

Hebu bashiri, niambie nini kitatokea?





Moyo wangu ulikuwa na kisasi kikubwa sana. Tukio la kushuhudia ndoa ya Ester hakika liliniumiza sana. Nilijitahidi kuvumilia maumivu niliyokuwa nikiyapata lakini nilishindwa kabisa.

Picha zake na mume wake alizokuwa akizipost zilizosindikizwa na maneno yaliyokuwa yakinilenga kwa asilimia mia moja, zilizidi kuniumiza sana moyoni mwangu, nilihisi maumivu yasiyomithilika.

“Ina maana alikuwa hanipendi, sasa kama alikuwa hanipendi si angesema ili nisifunge ndoa naye?” nilijiuliza swali lililokosa jibu kabisa.

Nilizidi kuwa katika wakati mgumu sana katika maisha yangu. Maisha yangu yalibadilika kwa kiasi kikubwa sana, nilikuwa ni mtu wa kuwaza kila wakati, kula, kunywa, kuvaa hata wakati mwingine kulala kwangu ilikuwa ni tabu, sikuwa mtu wa kwenda tena katika mihangaiko yangu, niliishi kwa kuteseka sana.

Kuna kipindi nilitamani kumuomba msamaha Ester na kumuambia kuwa kile kilichokuwa kimetokea kati yetu niliamua kusamehe hivyo tulitakiwa kuishi kama zamani. Hilo lilikuwa jambo gumu sana kulifanya, niliamini sikutakiwa kulifanya hata kidogo.

Niliamua kuingia facebook na kuanza kumtafuta msichana ambaye niliamini ningeweza kumuoa kabisa ikiwa ni katika harakati za kutaka kulipiza kisasi, niliamini kwa kufanya hivyo nilikuwa naenda kuuridhisha moyo wangu, moyo ambao ulisalitiwa, uliumizwa na Ester mwanamke ambaye alinidhihaki katika ulimwengu wa mapenzi.

Nilipoingia katika akaunti yangu ya facebook kazi yangu kubwa ilikuwa ni kuongeza idadi ya marafiki, nilikuwa nikiongeza marafiki huku wengi wao wakiwa ni wasichana. Niliwaomba urafiki wasichana wengine ambao kiukweli nilikuwa siwafahamu kabisa.

Msichana wa kwanza kabisa kunikubalia ombi langu la urafiki alijulikana kwa jina la Juliet Dickson, alionekana kuwa msichana mrembo sana, macho yake ya kurembua, sura ya kitoto iliyosindikizwa na umbo lake matata lilizidi kumfanya aonekane kuwa msichana mrembo sana, alikuwa akivutia kutazama.

Niliingia katika akaunti yake na kuanza kupekuwa baadhi ya picha mbalimbali alizowahi kuzipost. Kwa kweli alinivutia sana na hii ndiyo sababu iliyonifanya nikaamua kumuomba urafiki kitendo ambacho hakikuchukua muda akaweza kunikubalia ombi langu. Nilipomuangalia, alionekana kuwa online kwa wakati huo. Sikutaka kupoteza muda kabisa nikaamua kumtumia ujumbe mfupi.

“Asante kwa kunikubalia ombi langu.”

“Usijali karibu.”

“Asante mrembo?”

“Sawa.”

“Vipi lakini?”

“Safi tu!”

“We ni mrembo sana, unavutia kwa kweli.”

“Asante kaka yangu.”

“Maisha yanasemaje?”

“Yako poa?”

“Uko pande zipi?”

“Dar.”

“Dar kubwa lakini.”

“Nipo Sinza.”

“Sinza ipi?”

“Sinza makaburini.”

“Nashukuru kufahamu.”

“Usijali na wewe?”

“Mimi niko temeke tandika.”

“Ooh! Sawa,” alijibu Juliet na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa urafiki wetu.

Juliet alitokea kuuteka moyo wangu, nilijikuta nikianza kumpenda kwa mara ya kwanza baada ya kuziona picha zake. Sikutaka kuamini licha ya uzuri aliyokuwa nao eti! alikuwa ameolewa, nilijiaminisha kuwa alikuwa bado hajaolewa na hivyo ni mimi pekee ambaye nilitakiwa kumuoa.

“Lazima nimkamate Juliet,” nilijisemea huku nikizitazama picha zake, alikuwa akivutia sana.

Nilichokuwa nakiamini ni mapenzi ya kweli niliyokuwa nikiyatafuta facebook, niliamini kwa muonekano wangu nisingeweza kukosa mwanamke ambaye angeweza kunipenda na kuiziba nafasi aliyoiacha mke wangu.

Niliamini katika mapenzi ya kweli ambayo ningeweza kuyapata ila naweza kusema ilikuwa tofauti na kile nilichokuwa nakitegemea. Ama kwa hakika mapenzi ya facebook yameniacha na funzo kubwa katika maisha yangu.

****


Facebook! Facebook! Kama sio facebook leo nisingeamua kukusimulia simulizi hii ambayo itakwenda kukuacha na funzo kubwa katika maisha yako.

Nilipoanza urafiki na Juliet, hakuonekana kabisa kujali urafiki huo japo mara kwa mara nilikuwa nikilike pamoja na kukomenti picha zake. Niliutumia muda wangu mwingi sana katika kuchat na Juliet huku nikiamini mwisho wa siku nitafanikiwa kuwa naye kimapenzi.

“Umependeza sana.”

“Asante phidelis.”

“Za masiku?”

“Nzuri tu.”

“Hivi ulisema unaishi wapi vile?” niliuliza swali la kinafki huku nikiwa nafahamu vizuri.”

“Jomoni ndiyo umesahau mara hii?”

“Ndiyo sababu nikakuuliza.”

“Sinza makaburini.”

“Unafanya kazi gani?”

“Mbona mapema hivyo jamani.”

“Kwani kuna ubaya wa mimi kufahamu?”

“Hapana hakuna ubaya.”

“Basi niambie.”

“Mimi mwanafunzi.”

“Mwanafunzi wa shule ya msingi, sekondari au?”

“Nipo chuo.”

“Chuo gani?”

“UDSM.”

“Vizuri sana hivi unasomea nini?”

“Kaka naona maswali yamekuwa mengi kama polisi kwaheri,” alinijibu Juliet na huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kujibu jumbe zangu.

Nilijisikia vibaya sana hasa baada ya Juliet kunijibu hivyo , sikutaka kuishia hapo niliamua kumtumia ujumbe mfupi lakini hakuweza kunijibu chochote, alionekana kuwa online kwa wakati huo lakini ni kama vile alikuwa hajali jumbe zangu nilizokuwa namtumia.

“Juliet mbona kimya sasa.”

(Kimya!)

“Juliet!”

(Kimya!)

“Mrembo?”

(Kimya!)

Nilizidi kutuma ujumbe lakini hakuna jibu lolote nililoweza kuambulia. Hakuna siku niliyoweza kujisikia vibaya kama siku hiyo. Nilikuwa nikimpenda sana Juliet japo sikuwahi kukutana naye lakini alionekana kunivutia sana katika maisha yangu. Nilitamani nipate muda wa kuweza kuongea naye ili niweze kumwambia dhamira yangu kwake lakini nilishindwa.

Nilizidi kumsumbua kila siku lakini ni kama vile nilikuwa nikitwanga maji kwenye kinu, hakuna chochote nilichoweza kuambulia zaidi ya ukimya ambayo ulitawala.

Niliichukua moja ya picha ya Juliet na kuisave wallpaper katika simu yangu. Alionekana kuvutia sana. Kila nilipokuwa nikimtazama moyo wangu ulihisi kufarijika sana.

****

Niliamua kumueleza kila kitu rafiki yangu Juma kuhusu Juliet na kwa jinsi nilivyokuwa nikimpenda kutoka moyoni mwangu, nakumbuka jibu kubwa alilonijibu ni kuwa facebook hakuna mapenzi ya kweli. Hilo sikutaka kukubaliana naye kabisa.

“Rafiki yangu facebook hakuna mapenzi,” aliniambia Juma, wakati alikuwa nyumbani kwangu Tandika Azimio majira ya saa kumi jioni.

“Lakini anaonekana kuwa mrembo sana.”

“Kuwa mrembo sio tatizo Phidelis halafu mbona wanawake wako wengi tu kwanini unang’ang’ania huko facebook.”

“Juma wewe unaongea tu hivi kwanza umemuona huyo Juliet mwenyewe?” nilimuuliza.

“Yuko wapi?” aliniuliza huku akionekana kuwa na hamu ya kutaka kumuona, niliamua kumuonyesha picha yake.

“Mtoto huyo hapo,” nilimuambia huku nikimuonyesha.

“Hahaha! Kwahiyo ndiyo umeamua mpaka kumsave kwenye simu yako?”

“Nampenda.”

“Anajua?” aliniuliza swali lililoniweka katika wakati mgumu wa majibu, ni ukweli usopingika kuwa mpaka kufikia wakati ule sikuwa nimeweza kuzungumza na Juliet habari zozote kuhusu mapenzi, nilijivika vazi la mapenzi ili hali muhusika hata hakuwa anafahamu lolote kuhusu mahusiano hayo.

“Ndiyo,” nilimjibu kwa kumdanganya.

“Ila kuwa makini na mapenzi ya facebook wengi wanalia, wengine wanatamani hata kujiua kwasababu ya mapenzi hayohayo ya facebook,” aliniambia Juma maneno ambayo kwa kweli yalinichanganya sana, nilizidi kuwa katika wakati mgumu sana, nilijiuliza maswali mengi ambayo mengi yalikosa majibu.

Sikutaka kusikia lolote lile juu ya mtandao huu ambao uliweza kuniachanisha na mke wangu ambaye aliweza kuolewa tena na mwanaume ambaye alimpatia hukuhuku facebook.

****


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog