Chombezo : Mapenzi Ya Facebook
Sehemu Ya Pili (2)
“Uko pande zipi mrembo.”
“Dar.”
“Nimekupenda ghafla!”
“Huhuhuhu! Asante jomoni.”
“Njoo inbox.”
“Nakuja.”
Ilikuwa ni moja kati ya komenti alizokuwa akijibu mke wangu, nilikuwa nikizisoma huku nikiwa siamini kabisa. Kwa kweli sikutaka kuamini kile nilichokuwa nikikiona kwa macho yangu, nilihisi wenda nilikuwa katika ndoto na muda wowote ningeweza kuamka lakini haikuwa hivyo, nilikuwa katika ukweli mtupu, ukweli wa kuishuhudia akaunti ya mke wangu.
Nilizidi kushangazwa na kile nilichokuwa nikikiona katika akaunti ya mke wangu, kuna muda sikutaka kuamini kabisa lakini kila nilivyokuwa najitahidi kujidanganya ndivyo moyo wangu ulikuwa unaumia. Nilikuwa naumia sana maumivu ambayo naweza kusema Facebook ndiyo chanzo. Laiti kama nisingekubali mke wangu ajiunge na mtandao huu na amini leo hii nisingekuwa katika haya maumivu yanayoendelea kunitafuna mwilini.
Nilichoamua kukifanya ni kuanza kupitia komenti moja baada ya nyingine, kwa kweli ilikuwa ni vigumu sana hasa kwa kuzipitia zote kwani komenti zilikuwa ni nyingi mno ambazo zilikuwa zikiniumiza sana, nilijikaza kiume na kuamua kuyavumilia yote. Komenti ninayoikumbuka mpaka leo hii ninapokusimulia haya ni ya mzungu mmoja ambaye alijulikana kwa jina la Stewart. Aliandika “My Wife.” Kwa kweli nilijisikia vibaya sana, sikutaka kuamini kama mbali na ndoa yetu kuwa mke wangu alianzisha mahusiano mengine Facebook kiasi kwamba wakafikia kuitana mke na mume. Hili lilizidi kuniuma sana. Asikuambie mtu mapenzi yanauma sana, mapenzi yanakosesha amani, mapenzi yanaweza yakakufanya ukaamua maamuzi ambayo haukuwahi kuwaza kuamua hapo kabla.
Wivu niliyokuwa nao kwa mke wangu sikutaka uendelee kubaki katika kilindi cha moyo wangu, kwa niliyobahatika kuyaona yaliniridhisha tosha. Sikutaka kuendelea kujiumiza tena japo machozi ya maumivu ya moyo wangu yalinidondoka lakini nilivumilia. Nilikuwa naililia ndoa yangu, mke wangu, mwanamke ambaye nilikuwa nikimpenda sana.
Niliamua kumsimulia rafiki yangu Juma yale yote yaliyokuwa yametokea.
“Aisee pole sana ndugu yangu, mimi bado niponipo sana sioi leo wala mwakani,” aliniambia Juma maneno yaliyozidi kuniumiza sana, inamaana nimeikurupukia ndoa? Nilijiuliza swali lililoniacha katika wakati wa maumivu.
“Sasa unanishauri nini?” nilimuuliza, wakati huo tulikuwa katika bar moja, nilikuwa nikinywa pombe kwa ajili ya kupunguza mawazo yaliyokuwa yakinisibu.
“Kuna kitu huwa unakosea sana,” aliniambia Juma ambaye alikuwa akinywa maji kwa wakati huo.
“Kitu gani?”
“Binadamu anaishi kwa mazoea.”
“Mazoea, mbona sikuelewi?”
“Najua nivigumu mno kunielewa kwasababu na wewe ni miongoni mwa wakoseaji.”
“Juma nipo hapa kwa ajili ya ushauri wako yani kiukweli akili yangu imechanganyikiwa sana, sitaki hata kumuona Ester.”
“Nikuulize kitu.”
“Ndiyo niulize.”
“Unahisi pombe ndiyo suluhisho la mawazo?”
“Sasa unataka nifanye nini?”
“Mwanaume anasifika kwa kuwa na maamuzi thabiti wala hatishiki na lolote lile linalomsibu. Usiwe mtu wa kupelekeshwa na hisia bali wewe ndiyo unatakiwa uzipelekeshe hisia.”
“Una maanisha nini?”
“Yani na hapo pia bado hujanielewa?”
“Juma nimechanganyikiwa kiukweli.”
“Najua hata nikisema umuache mkeo kisa Facebook kwakweli wapo ambao watanishangaa kwa ushauri wangu ila labda nikuulize kitu hivi bado unampenda mkeo?”
“Ndiyo nampenda sana lakini kwa anayonifanyia kwa kweli yananiumiza sana.”
“Msamehe mkeo.”
“Nimsamehe?”
“Ndiyo sasa ulitaka nikwambie muache, ok basi muache mkeo,” aliniambia Juma katika namna ya utani, sikuwa katika utani hivyo aliamua kuniambia nifanye uchunguzi ndipo niweze kufanya maamuzi. Nakumbuka alichoniambia suluhisho la matatizo ya ndoa yangu bado yalikuwa katika himaya ya mikono yangu.
“Phidelis suluhisho la matatizo yako unayo mikononi mwako, kuwa na maamuzi pia usikurupuke kufanya maamuzi kwani yatakugharimu,” aliniambia Juma maneno yaliyoniingia vyema.
****
Nilirudi nyumbani majira ya usiku, nakumbuka ilikuwa ni majira ya saa tano za usiku. Nilimkuta mke wangu akiwa amekasirika sana, nililigundua hilo baada kumsalimia, hakuitikia salamu yangu jambo ambalo lilizidi kuniumiza. Ina maana hakuisikia salamu yangu? Nilijiuliza kisha nikamsalimia tena.
“Mke wangu umeshidaje?” nilimsalimia.
“Unatoka wapi usiku huu?”
“Mke wangu foleni.”
“Foleni, na mbona usinipigie simu.”
“Nilijua kuwa nitawahi hata hivyo nikaona nisikusumbue.”
“Hee! Yani wewe mwanaume umenishinda na mbona unanukia pombe siku hizi unakunywa?”
“Pombe?”
“Ndiyo.”
“Mimi?”
“Kwani naongea na nani hapa?” aliniuliza huku mikono yake ikiwa kiunoni.
“Mke wangu,” nilimuita kwa sauti ya utulivu sana.
“Sema,” alinijibu huku akiwa ameubetua mdomo wake.
“Wewe ndiyo sababu ya mimi kuwa hivi, mimi sio mlevi lakini nimejikuta nakuwa miongoni mwa walevi, mapenzi niliyonayo kwako sijui kwanini unashindwa kuyaheshimu,” nilimwambia kwa kukurupuka maneno ambayo yalituingiza katika ugomvi mkubwa sana, Ester alizidi kugombana na mimi huku akiwa hajui sababu ya mimi kuyasema yale.
“Kwahiyo mimi sasa hivi ndiyo nakufundisha ulevi?” aliniuliza kwa sauti ya ukali.
“Hapana simaanishi hivyo.”
“Ila?” aliniuliza.
Kuna muda nilitaka kumwambia yale niliyoyaona Facebook lakini niliyakumbuka maneno ya Juma, sikutakiwa kukurupuka katika hilo niliamua kuwa mweye subira. Niliamua kuomba msamaha kwa yale yaliyokuwa yametokea kisha amani ikarejea katika ndoa yetu. Niliishi kwa maumivu makali mno.
Kila nilivyokuwa nikimtazama Ester pamoja na upole aliyokuwa nao kwa kweli sikutaka kuamini kama ni yule ambaye alikuwa akibinua makalio yake Facebook. Nilizidi kuumia mno, mapenzi yalikuwa yakinitesa Phidelis mimi ambaye sikuwa mzungumzaji sana.
****
Sikutaka kukurupuka katika kufanya maamuzi, niliamua kuvuta subira huku nikiendelea kumchunguza mke wangu. Nilikuwa katika mpango mgumu sana, naweza kusema ni katika mpango uliyoshiriki katika kuushambulia moyo wangu kwa mikuki iliyonipa maumivu makali sana. Kuna kipindi nilijitahidi kuyavumilia lakini nilishindwa nilitaka kumwambia lakini pia nilisita kufanya hivyo. Nikabaki naugulia maumivu ya ndani kwa ndani. Moyo wangu ulikuwa ukiuma mithili ya maumivu ya moto wa pasi.
Ama kwa hakika usikubali udhaifu wako kila mtu akaufahamu kwani utaweza kujikaribisha katika wakati wa maumivu kila siku, utakuwa ni mtu wa kukosa furaha. Hili ndilo lilikuwa kosa langu kubwa ambalo nililifanya kwa mke wangu. Aliufahamu udhaifu wangu, udhaifu ambao aliutumia katika kuuvunja moyo wangu wa mapenzi.
Tukio lile la kushuhudia komenti za wanaume ambao alikuwa akiwajibu pamoja na picha zake za nusu uchi zilizidi kuniumiza sana, kila wakati tukio hilo lilikuwa likinijia katika akili yangu, nilijitahidi kusahau lakini sikuweza kabisa badala ya kusahau ndiyo kwanza nilikuwa nikiziona zile komenti za wale wanaume waliyokuwa wakimsifia, sifa ambazo nyingine sikuwahi hata kumsifia.
Nilizama katika dimbwi la mawazo, nilikuwa nikiifikiria ndoa yangu, nilikuwa nikimfikiria Ester wangu. Kuna kipindi nilihisi ndoa ilikuwa ikienda kunishinda kabisa nikawaza kumuacha lakini nilipoyafikiria maswali ya ndugu na marafiki watakayoniuliza juu ya ndoa yetu kuvunjika huku sababu ikiwa ni Facebook niliacha kuwaza hivyo, nilihisi kumpenda sana mke wangu.
“Kuna nini?” aliniuliza mke wangu wakati huo alikuwa bize akiperuzi simu yake.
“Hakuna kitu,” nilijibu huku nikijitahidi kuigiza tabasamu, hakika iliniwia vigumu sana.
“Mbona sasa huendi kazini?”
“Sijisikii vizuri.”
“Unaumwa?”
“Hapana sipo sawa tu!”
“Mmh! Mwenzetu vipi au umeshagombana huko maana,” aliniambia huku akiangua kicheko kikubwa sana.
“Unacheka nini?” nilimuuliza.
“Amna nimeona kituko huku Facebook,” alinijibu huku akionekana kuitazama kwa umakini wa hali ya juu simu yake.
Nilizidi kujisikia vibaya sana hasa baada ya kumuona mke wangu akizidi kuwa bize na simu yake. Nilijiuliza ni nini kilichokuwa kinamuweka muda mrefu huko Facebook kiasi kwamba akawa anasahau majukumu yake mengine. Sikuweza kupata jibu kabisa.
Nilichokuwa nimepanga kwa wakati huo ni kumnyang’anya simu ili niweze kuona ni kitu gani hicho kilichokuwa kikimfurahisha kiasi kwamba hata ule uwepo wangu mahali pale akawa hauthamini.
Niliinuka na kumnyang’anya simu kitendo ambacho kilizua mtafaruku mkubwa sana. Sikutegemea kama kingeweza kuleta mtafaruku huo. Kwa kweli sikutaka tena kuendelea kuwa katika upole wa kiasi hicho. Moyo wangu ulivumilia matukio mengi sana ambayo kiukweli yalinitesa sana katika maisha yangu.
“Naomba simu yangu tafadhali,” aliniambia huku akionekana kuchikizwa sana na kitendo nilichokifanya.
“Sikupi,” nilimjibu huku nikimtazama usoni. Alioneka kuwa na wasiwasi mkubwa sana.
“Mume wangu ni nini lakini?”
“Nimesema sikupi.”
“Kila siku ugomvi mimi nimechoka sasa,” aliniambia huku akijifanya kulia, kilio cha kinafki.
Sikutaka kuyajali machozi yake, nilichokuwa nataka ni kukishuhudia hicho kituko kilichokuwa kikimchekesha mke wangu.
Lahaula!
Sikuamini kile nilichokuwa nakiona katika simu ya mke wangu. Alikuwa akichat na mwanaume aliyejulikana kwa jina la Osman Ismail, huyu alioneka kumfahamu kabisa, nililifahamu hilo kupitia chatting zao.
Osmon:Baby nimekumis sana.
Ester:Nimekumis pia honey.
Osmon:Uko wapi?
Ester:Home.
Osmon:Unafanyaje?
Ester:Nipo na baba yangu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment