Search This Blog

Sunday, February 26, 2023

MAPENZI YA FACEBOOK - 3

    

Chombezo :  Mapenzi Ya Facebook 

Sehemu Ya Tatu (3)


Osmon:Ok baadae basi love you.

Ester:Love too Hubby.

Nilizidi kupagawa kwa nilichokuwa nikikisoma kwa wakati ule, nilimtazama mke wangu, alikuwa akitetemeka sana, niliamua kumuuliza kuwa Osmon alikuwa ni nani yake kwa kweli alikosa jibu la kunipa zaidi ya yote alibaki akilia kama mtoto mdogo huku akiniomba nimsamehe kwa kile kilichokuwa kimetokea.


Angalizo: Mnaosoma msipite kimya kimya bila kusema lolote. Ukimaliza kusoma toa maoni yako, Like pamoja na Share ili simulizi hii isomwe na wengi.


Unajua nini kilitokea?

Hebu bashiri, niambie nini kitatokea?





Nilikuwa katika maumivu makali sana moyoni mwangu, kila nilivyokuwa nikimuangalia Ester na kwa jinsi alivyokuwa akilia, nilihisi kumchukia sana. Moyo wangu ulikuwa umeshachoka kwa vile vituko alivyokuwa akivifanya.

“Nisamehe mume wangu,” aliniambia huku akilia machozi, machozi ambayo kiukweli niliyafananisha na yale machozi ya waigizaji wa bongo muvi.

“Nikusamehe?” nilijikuta nikimuuliza swali ambalo liliniropoka, sikuwa sawa kabisa.

“Mume wangu naomba unisamehe,” alizidi kuniomba msamaha.

“Nimekuuliza huyu Osmon ni nani?” nilimuuliza huku nikiendelea kuyatazama yale machozi yake, sikutaka moyo wangu ulainike kirahisi kwa kuyaonea huruma machozi yale.

“Ni…ni…ni,’ alisema kwa kigugumizi kilichozidi kuniweka katika hasira kubwa sana.

“Ni nani?”

“Ni rafiki yangu wa facebook.”

“Rafiki?”

“Ndiyo mume wangu.”

“Rafiki ndiyo muitane baby.”

“Hapana mume wangu.”

“Halafu unakataa?”

“Ni rafiki yangu ila….”

“Ila nini, halafu mimi ni baba yako?”

“Hapana wewe ni mume wangu,” alinijibu huku akiwa amepiga magoti, alizidi kunisihi nimsamehe kwa kile kilichokuwa kimetokea.

Nilizidi kujisikia vibaya sana, nilikumbuka jinsi alivyokuwa akichat na yule mwanaume. Roho yangu ilizidi kuniuma sio siri. Maumivu niliyokuwa nikiyapata kiukweli siwezi kuyafananisha na kidonda nilichowahi kukipata katika mwili wangu. Niliyakumbuka maneno ya wahenga waliyosema kuhusu ndoa pamoja uvumilivu wake. Kwa kweli akili yangu haikutaka kuyakubali kabisa maneno yao. Nilihisi walikuwa wakidanganya, yani Phidelis mimi ninayeumizwa na ndoa yangu, mke wangu halafu eti! Niendelee kuvumilia? Hapana haiwezekani!

Asikuambie mtu ndugu yangu, mke anauma, ndoa inauma. Mapenzi ni mazuri endapo utapata ambaye anakupenda kwa dhati lakini mapenzi ni mabaya endapo utampata mtu ambaye hakupendi kwa dhati, anaishi kwa kukudhihaki.

Hilo ndilo lililonitokea katika maisha yangu, maisha ya ndoa yangu. Sikutaka kuamini kabisa kwa kile kilichokuwa kimetokea, niliyakumbuka maneno ya Juma aliyoniambia kuwa suluhisho la matatizo yanaiyokuwa yakiikabili ndoa yangu yalikuwa mikononi mwangu. Nilizidi kupagawa sio siri na ni hapa ambapo nikajikuta natokwa na maneno ambayo siyo siri yalikwenda kuugharimu moyo wangu, moyo wa mapenzi uliyokuwa umemuhifadhi Ester mwanamke niliyeamini aliumbwa maalumu kwa ajili ya maisha yangu. Sikutakiwa kuwa mpole katika hili, niliamua kusema kile nilichoamini kiliuridhisha moyo wangu.

“Kwanini lakini niendelee kuteseka kiasi hiki, kwanini uendelee kuwa msumari unayeupigilia moyo wangu bila kujali maumivu yangu unanidhihaki. Nakupenda sana lakini wakati mwingine inanibidi niamini kuwa hakuna mapenzi yasiyokuwa na maumivu. Umekuwa sababu ya maumivu ninayoyapata katika moyo wangu. Najitahidi kuvumilia lakini imefikia kikomo, nakiona kifo changu katika macho yangu na chanzo ni wewe, unashiriki katika kuuvunja moyo wangu lakini ni kwanini unayafanya haya? Unasahau kuwa mimi ni mume wako, unasahau kuwa mimi ndiye mwanaume wako, unasahau kuwa mimi ndiye kila kitu kwako, sasa kwanini unasahau yote hayo lakini? Facebook amekuwa adui anayekufanya uniumize kila siku. Nakupa kila kitu lakini huridhiki.

Mwanzo nilipoziona komenti za wanaume waliyokuwa wakikomenti katika picha zako nilihisi wenda hakukuwa na chochote kilichokuwa kikiendelea, nilijipa moyo na kuamini kuwa labda walikuwa ni marafiki tu ambao hata ulikuwa hauwafahamu lakini kumbe nilikuwa najidanganya. Umeona urafiki haautoshi sasa umeamua kujenga uhusiano nao, umekubali kuwa katika mapenzi na mwanaume wa facebook halafu bado unasahau kuwa wewe ni mke wa mtu, Kwanini Ester kwanini lakini unanifanyia haya?” nilimuuliza swali lililosindikizwa na maneno yaliyotoka katika kitako cha moyo wangu, nilikuwa katika maumivu makali sana. Nilijitahidi kuvumilia machozi yasinidondoke lakini nilishindwa kabisa mwisho machozi yalichukua hatamu yake, yalinitiririka mashavuni mwangu.

***

Nilimtazama mke wangu ambaye kwa wakati huo alionekana kuwa na wasiwasi mkubwa sana, hakuweza kujibu lolote, alizidi kulia huku akinisihi nimsamehe.

“Nisamehe bure mume wangu sirudii tena,” aliniambia.

“Sitaki kusikia sentensi hii moja kila wakati kwanini lakini umeamua kunifanyia hivi?”

“Sio akili yangu ni ibilisi alinipitia?”

“Ibilisi?”

“Mume wangu niamini kweli sirudii tena.”

“Osmon ni nani yako?”

“Alikuwa rafiki yangu wa facebook.”

“Halafu.”

“Ila mume wangu alikuwa akinisumbua sana kila siku alikuwa akinitongoza, kiukweli ilikuwa ni usumbufu ikabidi nimkubalie japo sijawahi kukutana naye wala kufanya naye chochote,” aliniambia Ester maneno yalizidi kuumiza moyo wangu mithili ya kisu butu anachochinjiwa kuku.

“Anaishi wapi?”

“Yupo Mwanza,” alinijibu jibu ambalo lilinishangaza sana, nilijaribu kuulinganisha ule umbali kutokea Daresalaam mpaka Mwanza lakini sikutaka kuamini kabisa. Yani mtu unakubali kuanzisha mahusiano na mtu ambaye hata hukuwahi kuonana nae mmekutana Facebook halafu unakubali awe mpenzi wako wakati huohuo ni mke wa mtu. Hilo lilizidi kunishangaza sana. Kuna kipindi nilihisi wenda nilikuwa katika jumba la sanaa ya maigizo ambapo nilikuwa nikishuhudia visa na mikasa iliyokuwa ikiendelea katika jumba hilo jambo ambalo lilikuwa si kweli, mke wangu alikuwa akivifanya vitu hivi kwa akili zake timamu.

“Kwahiyo ni mpenzi wako?” nilimuuliza.

“Hapana,” alinijibu kwa kukataa jibu ambalo lilinishangaza tena.

“Wewe siumeniambia huyu ni mpenzi wako halafu unakataa tena?”

“Laki…” kabla hajamaliza kunijibu ghafla! Simu yake ikaita, nilipoitazama katika kioo chake ilikuwa ni namba ngeni. Sikutaka kupoteza muda nikapokea.

“Ester tangu juzi hupokei simu yangu ni nini kimetokea au kuna kosa nimekufanyia basi nisamehe mpenzi wangu,” ilisikika sauti ikisema kwa kulalamika kwa upande wa pili, kwa kweli sikutaka kuamini kabisa masikio yangu kwa kile nilichokuwa nakisikia. Nilipomtazama Mke wangu bado alionekana kuwa katika wasiwasi sana, machozi yalizidi kumdondoka tu.

Sikutaka kujibu jibu lolote lile, nilichoamua kukifanya ni kuikata simu kwa wakati ule. Sijui ni nini kilitokea ila ninachokumbuka nilijikuta nikishikwa na hasira kisha nikaipigiza simu ukutani, ikapasuka vipande vipande.

“Ester! Ester! Ester mke wangu,” nilimuita kwa sauti iliyochanganyika na hasira.

“Abee mume wangu,” aliitika huku akitetemeka.

“Ni nini hiki unafanya, unakosa nini kwangu, ni nini ambacho sikupi mpaka unahadaika na hawa wanaume?” nilimuuliza huku nikivikunja viganja vyangu, nilikuwa katika hasira isiyokuwa na kifani.

Wazo la haraka lililonijia kichwani mwangu ni kumpiga mke wangu kiasi cha kumvunja moja ya kiungo muhimu katika mwili wake, wazo hilo nililipitisha lakini lilipokuja suala la utekelezaji nilisita, moyo wangu haukutaka kufanya hivyo.

Machozi ya Ester aliyokuwa akiyadondosha huku akizidi kuniomba msamaha sikutaka kuyajali kabisa kwa wakati ule, ni hapa ambapo niliamini katika ule usemi usemao umdhaniaye ndiye kumbe siye. Kwa kweli nilimuamini sana mke wangu, ni mwanamke ambaye aliichukua sehemu kubwa sana katika maisha yangu. Nilimfanya kuwa kama malkia wa ngome ya mapenzi yangu aliyoitawala kiasi kwamba sikutaka kabisa kuchanganya falme. Maisha bila furaha yalikuwa si chochote, furaha hiyo alikuwa nayo Ester, kila kitu alichokuwa akikifanya katika maisha yangu kilizidi kunipa furaha ambayo ilizidi kuyaweka maisha yangu katika usalama wa hali ya juu.

“Kama ni kupenda nilikupenda sana mke wangu ila katika hili inabidi nikubali kupoteza kimoja katika maisha yangu ili nibaki na amani ya moyo,” nilimwambia huku nikimtazama.

“Tafadhali mume wangu usiniache,” aliniambia huku akiwa amepiga magoti.

Nakumbuka ndoa yangu mpaka kufikia wakati ule ilikuwa imetimiza mwaka mmoja, mwaka ambao sikubahatika kupata mtoto kabisa. Kwa kweli sikutaka kuendelea kuishi katika ndoa iliyokuwa ikininyima furaha. Japo nilikuwa nikimpenda sana mke wangu ila ni kama vile kulikuwa na sauti iliyokuja nafsini na kuniambia kuwa sitakiwa kuendelea kuishi katika ndoa iliyokuwa ikinitesa angali bado nilikuwa kijana.

“Naomba huu ndiyo uwe mwisho wetu chukua kila kilichokuwa chako uondoke zako, sikutaki tena katika maisha yangu,” nilimuambia maneno yaliyoniumiza kwa kiasi fulani lakini niliamua kujikaza kiume.

****

Kwanini mapenzi yaendelee kunitesa, kwanini niendelee kuishi maisha ya kuwa kama mkimbizi katika dunia hii ya mapenzi. Mapenzi yaliyowaacha watu wengi katika maumivu makali sana. Kila mtu analia na maumivu yake, wengine wanayachukia mapenzi huku wengine wakitamani kujiua sababu kubwa ikiwa ni mapenzi. Kuna muda huwa najiuliza hivi ni nini kipya katika mapenzi lakini sipati jibu kabisa.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog