Search This Blog

Sunday, February 26, 2023

MAPENZI YA FACEBOOK - 5

    

Chombezo :  Mapenzi Ya Facebook 

Sehemu Ya Tano (5)


Niliendelea kumsumbua Juliet mpaka pale siku moja alipoweza kunijibu.

“Juliet.”

“Niambie.”

“Mbona upo kimya hivyo?”

“Nilikuwa bize.”

“Vipi lakini?”

“Safi tu.”

“Naweza kukuomba kitu?”

“Kitu gani?”

“Naomba namba zako ili tuwe kunawasiliana kwenye simu kwasababu huku najua sio kila siku tutakuwa tunawasiliana.”

“Ok nitumie namba zako,” alinijibu kisha nikamtumia namba zangu na huo mwisho wa chatting zetu.

Nilikuwa katika furaha isiyokuwa na kifani, kitendo cha kumuomba Juliet na mba kisha na yeye kuniambia nimtumie namba zangu hakika kiliniweka katika furaha isiyomithilika.Niliamini ule ndiyo ulikuwa mwanzo wa mahusiano yetu ambayo baadae ningeweza kumuoa kabisa, nilikuwa radhi kwa lolote kutoka kwa msichana huyo ambaye nilimpata facebook.

Kila siku nilikuwa nikiiangalia simu yangu huku nikitegemea kupokea simu kutoka kwa Juliet lakini hakuna simu wala ujumbe wowote uliyoingia kwenye simu yangu, tukio hilo lilizidi kuniumiza sana. Nilihisi Juliet alikuwa amenidanganya na hivyo asingeweza kunitafuta kabisa.

Baada ya kupita wiki mbili ndipo hapo ambapo niliweza kutumiwa ujumbe na namba ngeni. Sikutaka kupoteza muda niliamua kuchat nayo.

“Mambo.”

“Poa vipi.”

“Safi.”

“Nani mwenzangu?”

“Umenisahau jamani?”

“Hujajibu swali lakini?”

“Mimi Juliet,” alinijubu.

Kwa kweli sikutaka kuamini kama nilikuwa nachat na Juliet, haraka nikaisave namba yake, nilikuwa katika furaha isiyokuwa na kifani.

“Juliet jamani ni wewe?”

“Ndiyo.”

“Mbona sasa umekaa hivyo muda mrefu hata kunitafuta?”

“Nilipoteza simu.”

“Jamani pole sana sasa namba yangu uliipata wapi tena.”

“Siulinitumia facebook, niliingia nikaichukua.”

“Nimefurahi sana.”

“Usijali.”

“Uko wapi?”

“Niko nyumbani.”

“Hujaenda chuo?”

“Hapana.”

“Kwanini?”

“Nimefukuzwa ada.”

“Jamani pole sana.”

“Asante sana.”

“Kwahiyo utafanyaje?”

“Sijui na hapa nilipo nimepanga na mwenye nyumba ananidai kodi yake.”

“Kwani huna wazazi?”

“Sina walifariki miaka mingi sana iliyopita,” alinijibu Juliet jibu ambalo kiukweli liliniumiza sana. Nilitokea kumpenda sana kwa moyo wangu wote na sikutaka kumuona akiwa katika hali hiyo.

***

Sikutaka kukurupuka katika kufanya maamuzi, niliamua kutumia akili katika suala hilo. Niliamini facebook matapeli walikuwa ni wengi sana hivyo sikutakiwa kumuamini Juliet kupitiliza.

Kitu nilichoamua kukifanya ni kumpigia simu na kutaka kuisikia sauti yake, nilitamani sana kumsikia alifananaje sauti. Nilipiga simu yake lakini ajabu haikuwa ikipokelewa kabisa jambo lililonishangaza sana.

“Itawezekanaje?” nilijiuliza mara baada ya kupiga simu zaidi ya mara tatu bila kupokelewa.

Niliamua kumtumia ujumbe mfupi lakini alionekana kuwa kimya.

“Mbona hupokei simu?”

(Kimya!)

“Juliet!”

(Kimya!)

Nilizidi kuwa katika wasiwasi mkubwa sana, sikujua ni nini kilichokuwa kimetokea mpaka Juliet akashindwa kuipokea simu yangu.

Ama kweli jambo usilolijua ni sawa sawa na usiku wa kiza kinene, nilikuwa katika kiza ambacho sikuwa nikifahamu ukweli wa kile kilichokuwa kinaendelea katika maisha yangu.

Mbali na kumfahamu Juliet facebook na kuweza kupata namba zake lakini kiukweli hakukuwahi kutokea siku nikaweza kuzungumza naye kwenye simu, kila nilipokuwa nikimpigia simu alikuwa akiikata na kudai kuwa ilikuwa mbovu hivyo alinitaka tuchat jambo ambalo kiukweli lilikuwa likiniweka katika wakati mgumu sana.

“Kwanini hutaki kupokea simu yangu?”

“Simu yangu mbovu tuchat tu!”

“Kwahiyo hatuwezi kuongea?”

“Ndiyo mpenzi,” alinijibu jibu ambalo kiukweli lilinifanya nishangae kwa kiasi fulani, yani sikuwa nimemtongoza wala kumtamkia neno lolote la kimapenzi sasa ilikuwaje nikawa mpenzi wake. Hilo lilizidi kunishangaza sana.

Nikayakumbuka maneno ya Juma kuwa facebook hakukuwa na mapenzi ya kweli zaidi ya uwongo mwisho wa siku kuumiza. Sikutaka kukubaliana naye kabisa yani kwa jinsi Juliet alivyokuwa akionekana kuwa msichana mrembo sikutaka kukubaliana na maneno yake kabisa, nilihisi alikuwa akiniongopea.

Niliamua kumuambia ukweli wa hisia zangu Juliet, sikutaka kumficha chochote kile nilichokuwa nikikihisi. Nilidhamiria kuwa naye katika maisha yangu.

“Nakupenda Juliet.”

“Unanipenda?”

“Ndiyo.”

“Unanipendea nini?”

“Nakosa jibu la kukujibu ila nimetokea kukupenda tu!”

“Siunajua mimi ni mwanamke ambaye ninahitaji matunzo.”

“Ndiyo nafahamu.”

“Utaweza kunihudumia, kunisomesha pamoja na kunilipia pango la chumba?”

“Ndiyo nitaweza ondoa shaka mrembo.”

“Sawa nimekukubalia ombi lako.”

“Nimefurahi sana kwa kunikubalia ombi langu, nakupenda sana.”

“Nakupenda pia Phidelis wangu.”

Kwa kipindi chote hicho sikuwahi kuongea na Juliet na mara zote nilipokuwa nikitaka kuzumgumza naye alikuwa akiweka vipingamizi vingi, sikujua ni kwanini alikuwa akiweka vipingamizi hivyo hata pale nilipotaka kukutana naye aliweza kunikatalia na kuniambia kuwa nipange siku maamulu ambayo nitaweza kwenda kuonana naye.

Urafiki wetu ulianzia facebook, urafiki ambao ulikuja kuzaa mapenzi ambayo kiukweli nilijikuta nikiwa katika mahusiano ilihali sikuwahi kuonana naye kabisa, yalikuwa ni mapenzi ya facebook tu! kutumiana picha pamoja na kusifiana.

Hata pale lilipokuja suala la kumtumia pesa, nilimtumia bila kusita, niliamini alikuwa ni mwanamke ambaye alikuwa akinipenda sana kuliko kitu chochote kile. Niliamua kumtumia pesa ya pango ya chumba aliyokuwa akidaiwa pamoja na ada ya chuo.

Mapenzi yetu yalibakia kuwa ya facebook tu! mpaka pale siku moja nilipokuja kupata habari iliyokuwa ikitangazwa na kuchapishwa katika magazeti mbalimbali kuhusiana na taarifa za shoga ambaye alikuwa akitumia jina la Juliet mitandaoni kutapeli wanaume.

Kwa kweli sikutaka kuamini kile nilichokuwa nikikiona katika magazeti ya siku hiyo.

***


“SHOGA ANAYETUMIA JINA LA JULIET AZIDI KULIZA WENGI FACEBOOK!” Kilikuwa ni kichwa cha habari cha gazeti moja ambalo nilikuwa nikilisoma. Katika gazeti hilo ilikuwepo picha ya mwanaume mmoja mwenye asili ya shombeshombe pamoja na picha ya mwanamke. Niliitazama kwa umakini wa hali ya juu ile picha ya yule mwanamke. Naam! Hakuwa mgeni machoni mwangu. Alikuwa ni Juliet mwanamke aliyetokea kunichanganya katika mapenzi kiasi kwamba nikawa sioni wala sisikii lolote juu yake.

“Juliet!” nilijikuta nikiita kwa kushtuka.

Sikutaka kuamini kile nilichokuwa nikikisoma katika gazeti, Juliet hakuwa ni mwanamke kama nilivyokuwa nikidhani. Alikuwa ni yule shoga ambaye alikuwa akitumia picha ya mwanamke Facebook ili aweze kuwatapeli wanaume. Naam! Ni kweli alifanikiwa katika mpango huo, aliweza kuwaliza wanaume wengi sana kutokana na uzuri aliyokuwa nao mwanamke yule. Miongoni mwa wanaume waliyolizwa siwezi kupinga nilikuwa ni miongoni mwao.

“Siamini kwa kweli kumbe Juliet si mwanamke ni shoga?”nilijiuliza swali lililonifanya nisiamini kabisa habari ile niliyokuwa nikiisoma katika gazeti.

Nilichoamua kukifanya ni kuichukua simu yangu kisha nikaingia Facebook ili niweze kukiaminisha kile nilichokuwa nikikisoma. Nilipoingia kitu cha kwanza niliingia upande wa kutafuta majina. Nililiandiika jina la Juliet kisha nikaanza kutazama picha ya yule mwanamke ambayo ilikuwa imewekwa katika akaunti hiyo.

Kitu kilichonishangaza hakukuwa na picha katika akaunti ya Juliet, ilikuwa imetolewa. Sikutaka kuamini nikaamua kumtumia ujumbe mfupi lakini nilipotaka kufanya hivyo nilishindwa, alikuwa ameniblock.

Kwa kweli nilihisi kuchanganyikiwa ndugu yangu, kuna kipindi nilihisi nilikuwa nikiyaona mapichapicha tu, sikutaka kuamini kabisa kama nilikuwa nimetapeliwa tena na shoga wa Facebook.

Niliyakumbuka maneno ya rafiki yangu Juma aliyowahi kuniambia kuhusu Facebook, hakika yalionekana kuniingia vyema. Nilitamani kuzirudisha siku nyuma ili niweze kujitoa katika penzi la na Juliet lakini lilikuwa ni jambo gumu kutokea.

Majuto yalikuwa kwangu, nilizidi kujiona mjinga sana hasa baada ya kusalitiwa na mke wangu kisha na mimi kuamua kulipiza kisasi katika mtandao huu ambapo nilijikuta nikiangukia kwa shoga ambaye nilikuwa nikimuhudumia kama mke wangu wa ndoa. Tukio hilo lilizidi kuniumiza sana, kumbukumbu hiyo ilinitesa sana katika maisha yangu.

Niliamua kumuambia Juma ukweli wa kile kilichokuwa kimetokea.

“Umeona umeona?” aliniambia baada ya kumuelezea ukweli wa kile kilichokuwa kimetokea.

“Yani ndugu yangu we acha tu!”

“Lakini nilikuambia mimi.”

“Juma yani siamini.”

“Huamini nini sasa, we endelea kuhudumia,” aliniambia huku akinicheka, kicheko ambacho kilinifanya nijisikie vibaya.

“Sasa unanicheka.”

“Tatizo lako wewe husikii.”

“Nimekoma.”

“Sasa ndiyo ujifunze,” aliniambia huku akionekana kufurahishwa na tukio lile.

Facebook ilinipa funzo katika maisha yangu, sikutakiwa kumuamini mtu bila sababu za msingi katika mtandao huu, ni hapa ambapo niliamini kuwa kuna baadhi ya watumiaji wa facebook walikuwa wakipenda kutumia picha ambazo zilikuwa si zao. Unakuta mtu anaitwa Revocatius Kisoka lakini facebook kaweka picha ya Chris Brown au msichana unakuta kaweka picha ambayo si yake halisi. Hili ndilo lililowahi kunitokea, mapenzi ya facebook yalinipa funzo kubwa mno.

Kuna kipindi nilimuona msichana mwingine facebook, huyu alikuwa akiitwa Cleopatra Mushi lakini kwa facebook alikuwa akitumia jina la Precious Girl, kwa kweli alinivutia sana lakini kila nilipokuwa nikiyakumbuka yale yaliyowahi kunitokea katika maisha yangu ya facebook, niliogopa kumtongoza japo tulikwishaanza kuchat lakini niliamua kumpotezea.

Nimeamua kuishi maisha yangu mpaka pale siku nitakapopata mwanamke ambaye atakuja kunipenda kwa dhati. Aweze kuliziba pengo aliloliacha mke wangu.”


Alimaliza kusimulia Phidelis.


MWISHO.


Mnaosoma kimya kimya bila kusema lolote. Leo ningependa kuona maoni yenu.


Natumaini wote mmejifunza mengi katika simulizi hii, kwa yale ambayo ni mafunzo kwenu yachukueni lakini yale ambayo yataonekana kuwa mabaya yaacheni humuhumu.


Ninashukuru kwa kunifuatilia mwanzo mpaka mwisho wa mkasa huu. Ninachopenda kusema ni kuwashukuru kwa kuniunga mkono kwenye kazi hii kubwa.


Kumbuka mwisho wa simulizi hii ndiyo mwanzo wa simulizi nyingine.


Ahsanteni.


0 comments:

Post a Comment

Blog