Search This Blog

Monday, October 24, 2022

TIMBWILI...TIMBWILI - 3

 





    Chombezo : Timbwili .... Timbwili

    Sehemu Ya Tatu (3)



    “NASEMA, toka!”



    “Siondoki!” Halima aling'aka. “Siondoki mpaka un'ambie kosa langu!”



    “Nasema, ondoka!”



    “Siondoki! Labda uniue!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sitaki kukugusa, Halima,” sauti ya Saad ilikuwa ya upole. “Kumbuka mtoto wetu yuko kwa bibi yake. Anahitaji matunzo ya baba na mama. Nikikuua nitakuwa nimemwathiri sana mwanetu. Nakuomba tu, uondoke.”



    Halima alimtazama Saad kwa sekunde chache na kuibaini hasira iliyojikita moyoni mwake. Hivyo hakuhitaji kuuendeleza mjadala usiokuwa na matunda mema. Kwa upole alitwaa vitu vyake na kuondoka.



    **********



    SIKU tatu za awali baada ya Halima kuondoka, chumba kilitawaliwa na upweke. Na kwa ujumla kilipwaya. Saad alilibaini hilo, lakini alipiga moyo konde na kujipa matumaini kuwa hali hiyo haitofautiani na mtu kukumbwa na msiba. Utafiwa, marehemu atazikwa na hatimaye yale majonzi yataanza kupotea taratibu. Kisha hali itarudi kuwa ya kawaida. Utazoea na kusahau.



    Ni hilo lililomwondolea fadhaa Saad. Sasa fikra mpya zikamwingia kichwani. Alimkumbuka Mwajuma, yule mwanamke aliyekutana naye mtaa wa Msimbazi na akamwambia juu ya Halima kuwepo ndani ya ukumbi wa DDC Kariakoo.



    Mwajuma aliwahi kuwa mpenzi wake na hata kilifikia kipindi akatangaza uchumba. Na kama isingetokea akazuka Halima, ni Mwajuma ambaye angeolewa.



    Kuhusu sababu iliyopelekea hadi akamweka kando Mwajuma, na Halima kutwaa nafasi, halikuwa jambo alilotaka kulitia akilini tena. Cha muhimu ilikuwa ni kuurejesha uhusiano wake na Mwajuma tu.



    Wazo hilo lilimtia faraja kwa kiwango kikubwa. Sasa akajisikia kurejewa na nguvu zake. Angeweza kwenda mjini, angeweza kufanya kazi kama kawaida na angezungumza na watu kwa kujiamini, akiwa na hakika kuwa utu na heshima yake havijatoweka. Hata kula, angekula kama kawaida, akaisikia ladha ya chakula na kuifurahia shibe.



    Aliamini kuwa, kwa kuwa mwili wake haukupasuka wakati wa raha, basi haungedondoka katika kipindi hiki cha upweke na karaha. Hata hivyo bado alikiri kuwa, kwa kiasi fulani maisha yake yameathirika, na asubuhi ya ujana wake imetoweka.



    Asubuhi ya siku ya nne, siku aliyopata wazo lililomtia faraja, alijikuta akinong'ona, “Halima! Lazima nikutoe akilini. Lazima nikusahau. Nikuue moyoni na fikrani mwangu. Lazima...! Ndiyo! Lazima nikufungie nje ya maisha yangu!”



    **********



    NI katika mtaa uleule wa Msimbazi, na pia ni jioni, hii ikiwa ni siku nyingine baada ya ile siku ambayo Mwajuma na Saad walikutana. Ilishapita wiki nzima tangu walipoonana, na jioni hii, kama kawaida yake Mwajuma alikuwa akielekea katika kituo cha daladala.

    Mara akasikia akiitwa, “Mwajuma!”



    Akageuka. Akamwona Saad akimjia, tabasamu la mbali likichanua usoni pake. “Haa! Saad!”



    “Mwajuma!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/





    Wakapeana mikono na kuchukua kitambo kifupi wakijuliana hali. Kisha Mwajuma akaonyesha kutaka kuendelea na safari yake ya kituoni. Lakini jioni hii ni Saad aliyemzuia Mwajuma.



    “Mwajuma, tafadhali usiondoke.”



    Mwajuma aliguna na kumtazama Saad kwa mshangao. “Kwani vipi, Saad?” hatimaye alimuuliza.



    “Nataka tuzungumze kidogo. Tutafute sehemu tuzungumze huku tukipata kinywaji.”



    “Saad, leo yamekuwa hayo tena?” mshangao ulizidi kujiweka bayana usoni na katika sauti ya Mwajuma.



    “Ndiyo, Mwajuma,” kwa unyonge Saad alijibu.



    “Nashukuru sana,” Mwajuma alisema. “Lakini kwa kweli itakuwa ngumu kwa leo. Ninakwenda nyumbani...ah...no. Tuseme ninakwenda saluni kuseti nywele.”



    Saad alimshika mkono Mwajuma. Akamtazama kwa huruma, kisha kwa sauti ya chini akasema, “Mwajuma una taarifa kuwa mimi na Halima tu'shaachana?”



    Mwajuma hakujibu. Wala hakuonyesha kushtushwa na swali hilo. Akabaki akimtazama Saad kwa macho ya kawaida, hali ambayo akilini mwa Saad ilimjengea hisia kuwa tayari Mwajuma ana taarifa.

    Kama vile ibilisi kapita katikati yao, ukimya wa muda mfupi ulitawala.



    Kisha Mwajuma alishusha pumzi ndefu, akatoa mguno wa masikitiko.



    Saad akapata nguvu ya kuendelea. “Siko tena na Halima. Tumeachana!”





    “Nimekusikia, Saad. Lakini kwa kweli hukufanya vizuri,” Mwajuma alisema huku akimwangalia Saad usoni sawia, sauti yake ikiwa dhaifu, akionyesha bayana kukumbwa na huzuni.



    “Sikufanya vizuri?” Saad alimkazia macho.

    “Ndiyo, ulifanya makosa,” Mwajuma alisisitiza.



    Mikunjo ya mbali ilijiunda usoni pa Saad. “Kwa nini unasema ivo?” alimuuliza. “Kwa nini un'ambie ivo wakati unajua fika kuwa Halima alikuwa anatembea ovyo na wanaume? Mwanamke hata hajui kama Ukimwi upo!”



    “Pamoja na hayo, Saad,” Mwajuma alikuwa mpole. “Kubali-ukatae, uliamua kumwacha baada ya siku ile mimi kukwambia kuwa yuko DDC 'anakandamiza'. Uongo?”



    “Hilo ni mojawapo. Lakini Mwajuma, ya nini kuendelea kuzungumza kuhusu huyo hayawani, chizi aliyechizika? Achana nae. Tuzungumzie yetu. Yetu, mimi na wewe.”



    “Yetu mimi na wewe?!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo.”



    “Yapi tena hayo?”



    Ukimya mwingine ulipita. Kisha, kwa sauti ya unyonge zaidi, macho yakiutangaza zaidi unyonge huo, Saad alijibu, “Ni ya kawaida tu, Mwajuma. Naomba utambue jambo moja; kwamba, tangu niachane na Halima sijala chakula bora. Yaani labda niseme sijala chakula cha nyumbani. Nadhani hadi hapo umenielewa.”



    “Saad,” Mwajuma alimkazia macho. “Saad, ya kweli hayo?”





    “Sina sababu ya kukudanganya, Mwajuma. Huo ndio ukweli wenyewe. Tafadhali, naomba basi unipe hata kampani tu, tutafute mgahawa wenye chakula kizuri, nile. Au, twende kwako unisongee ugali.”



    Yalikuwa ni maneno yaliyomwingia vilivyo Mwajuma. Kwake, yalikuwa ni maneno aliyoyahitaji, na aliyoyapenda. Lakini alihitaji kuilinda heshima yake, hivyo hakuwa mwepesi wa kukubaliana na pendekezo lolote haraka haraka, pendekezo apewalo na yeyote.



    Alimtazama kidogo Saad, kisha kwa sauti ya kujiamini, lakini sauti hiyo ikiwa na uzito mkubwa wa mtiririko wa kusihi, alisema, “Lakini Saad, kumbuka nimekwambia kuwa nakwenda saluni. Isitoshe, sipendi kukuficha, kwa sasa nina mtu wangu. Itakuwa vigumu kuyakumbusha yetu ya kale...”



    “Yaani...” Saad alimkata kauli. Akamtazama kwa macho makali zaidi, kisha akaendelea, “Nadhani sijakuelewa. Umesema una mtu?”



    “Nd'o maana'ake,” Mwajuma alijibu. “Kwani ulitegemea nini baada ya wewe kunitelekeza? Kwa kweli, Saad, nimevumilia sana. Kwa mwanamke mwingine isingekuwa vigumu kuchanganyikiwa na kuchukua hatua ya kukufuatilia kwa kukughasi kiasi cha kuihatarisha ndoa yako.



    “Mimi sikufanya hivyo. Nilitulia, nikamwomba mola anipatie mtu wa kunipoza machungu ya kutelekezwa. Na nilimpata.”



    Saad alihisi kizunguzungu. Akili yake haikufanya tena kazi vizuri. Bila hata ya kutamka neno jingine, aliuacha mkono wa Mwajuma na kuanza kuondoka. Akavuta hatua takriban kumi, huzuni ikiwa imeuvaa moyo wake. Kisha aligeuka na kumtazama Mwajuma, macho yake yakitoa taswira ileile ya majonzi makubwa.



    Macho yao yakakutana, safari hii Saad akiyaona macho ya Mwajuma yakiwa tofauti na awali, yakimtazama kwa namna ya kubembeleza. Hilo halikuwa jambo lililomchanganya hata kidogo, na angeweza hata kuendelea na safari yake. Lakini, zaidi ya ile tazama ya Mwajuma, jambo jingine lilitokea. Mwajuma alimpungia mkono akimwashiria arudi.



    Kama aliyeendeshwa na mitambo maalumu, Saad alimrudia Mwajuma, safari hii akitembea mithili ya askari wa gwaride aliyeamriwa kutembea kwa mwendo wa haraka. Akamfikia na kumtazama sawia. Akavuta pumzi ndefu na kuzishusha.



    “Vipi, umechukia?” Mwajuma alimuuliza huku akiachia tabasamu la mbali, tabasamu ambalo hata hivyo halikufichika machoni pa Saad.

    Kwanza Saad alitikisa kichwa akionyesha kukataa. Kisha, kwa sauti alijibu, “Hataa. Sijachukia. Na hata nikichukia itanisaidia nini? Mtu mwenyewe wala siujui wivu una sura gani...”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ok, kama hujachukia, unisindikize saluni basi,” Mwajuma alimwambia, safari hii yeye akiwa amemshika mkono.



    “Sawa tu,” Saad aliafiki, kwa kiwango kikubwa faraja ikiwa imemjia moyoni.



    Hawakwenda kwenye kituo cha daladala, Mwajuma alikodi teksi iliyowapeleka hadi Magomeni Mwembechai ambako iliwaacha kwenye saluni. Ni saluni hiyo ambayo Mwajuma alizoea kuitumia kwa kuzirembesha nywele zake.



    Kabla ya kuingia ndani ya saluni hiyo, Mwajuma alimwambia Saad, “Itabidi ukanisubiri mahali fulani. Nikishatoka tunaweza kwenda kwangu nikakusongea ugali kwa samaki wa kwenu, Migebuka. Pia nadhani tutaongea kwa utulivu hayo unayotaka tuongee.”



    Kufikia hapo Mwajuma akaliachia tena tabasamu lake kwa uwazi zaidi, meno yake meupe na yaliyopangika vizuri kinywani yakiongezea uzuri wa sura yake. Akamtazama Saad kwa makini usoni, macho yake yakizungumza mengi, na mengi hayo yakiashiria faraja zaidi na burdani moyoni mwa Saad muda mfupi ujao.



    Kisha akaongeza, “Saad, nadhani pia tunaweza kukumbushia ya zamani kama bado unanipenda.”



    “Bado nakupenda, Mwajuma.”



    “Siku nyingi, Saad.”



    “Ndiyo, siku nyingi, Mwajuma.”



    ***********



    NYUMBA ya nne kutoka kwenye saluni aliyoingia Mwajuma kulikuwa na kijigrosari. Baadhi ya wateja waliketi ndani, baadhi waliketi nje. Saad naye aliamua kuketi nje ili aweze kumwona Mwajuma pindi atakapotoka saluni.



    Akaagiza soda na kuinywa taratibu, macho yake yakitalii kwa wateja wengine. Mara macho yakatua katika meza moja iliyokuwa na watu wawili. Watu hao nao wakamtazama. Wakatabasamu.



    Saad akasimama na kuwafuata. Wakaunganika katika meza hiyo. Wakasalimiana na kuongea hili na lile huku vinywaji vikiendelea kunyweka.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wale watu wawili ambao Saad aliwakuta, walikuwa ni mwanamume na mwanamke; Salum na Hadija. Wao walikuwa wakinywa bia. Katikati ya maongezi yao, Hadija aliuliza, “Vipi shem, mama Sauda ameshaanza yale mafunzo ya ushonaji nguo?”



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog