Search This Blog

Monday, October 24, 2022

TATTOO - 3

 





    Chombezo : Tattoo

    Sehemu Ya Tatu (3)



    ILIPOISHIA

    Moyo wa Annabel ukamlipuka, akauhisi mwili ukizidi kutetemeka, kitendo cha kuisikia sauti ya Jonathan kilimfanya kujisikia vizuri kuliko vipindi vyote katika maisha yake. Uwepo wa Jonathan mahali hapo ukampa furaha lakini kitu cha ajabu hakuweza kuonyesha tabasamu, bado hofu ilimjaa moyoni.



    Annabel aliendelea kutetemeka kwa hofu huku kijasho chembamba kikimtoka. Mtu ambaye kila siku alikuwa akimfikiria na kuuendesha moyo wake vilivyo, Jonathan, kwa wakati huo alikuwa amesimama mbele yake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakuwa muongeaji, alibaki kimya huku akisubiri Fatuma amalize kila kitu kama alivyokuwa ameanza. Wanafunzi wengine waliokuwa wakipita karibu na eneo hilo walikuwa wakimwangalia Annabel tu, uzuri wake bado uliendelea kumvutia kila mtu.



    “Huyu ni rafiki yangu anaitwa Annabel,” alitambulisha Fatuma mara baada ya salamu.

    “Ninamfahamu,” alisema Jonathan.



    “Kama nilivyokwambia jana, ametokea kukupenda sana,” alisema Fatuma, katika kipindi chote hicho Annabel alionekana kuwa na hofu, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakimwenda mbio.

    Jonathan hakuongea kitu, akaanza kumwangalia Annabel kwa umakini. Ni kweli kwamba Annabel alisifika kwa uzuri wa sura lakini kwa Jonathan msichana huyo alionekana wa kawaida mno.



    Hakuonekana kujali sana, kwa sababu sura yake ilikuwa ikionyesha uhitaji mkubwa wa kuwa naye, siku hiyo akamkubalia ombi la kuwa mpenzi wake na hivyo uhusiano wa kimapenzi baina ya watu hao wawili kuanza rasmi.



    Mara baada ya kukubaliwa, wawili hao wakaondoka na Annabel kumuachia Jonathan namba yake ya simu na kiasi cha shilingi laki mbili kwa ajili ya kununua simu itakayowaweka karibu kimawasiliano.



    Siku hiyo ilikuwa ni siku ya furaha kuliko siku zote ambazo Annabel aliwahi kupitia katika maisha yake. Kila wakati alionekana kuwa na furaha, hakuamini kama katika kipindi hicho tayari kile alichokuwa akikihitaji alikipata tena kwa urahisi tofauti na alivyofikiria.



    Njiani, Fatuma alipata shida, kila wakati alikuwa akisumbuliwa na Annabel ambaye alitaka safari nzima azungumziwe Jonathan tu, tena kwa mazuri. Fatuma alikwishalifahamu hilo, kazi yake kwa wakati huo ilikuwa ni kumsifia Jonathan tu kitu kilichomfurahisha mno Annabel.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Furaha ya Annabel iliongezeka siku iliyofuata mara baada ya Jonathan kununua simu na kisha kumpigia. Wakati mwingine Annabel alijihisi kuwa ndani ya usingizi mzito, kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwake kilionekana kuwa kama ndoto moja nzuri na ya kusisimua.



    “Nakupenda Jonathan,” alisema Annabel simuni huku akionekana kuwa na furaha.

    “Nakupenda pia,” alisikika Jonathan.



    Mwanzo wa uhusiano huo ndiyo ukawa mwanzo wa kuwa karibu zaidi. Mara kwa mara Annabel alimtaka Jonathan kufika nyumbani kwao na kumuona mama yake. Hilo halikuwa tatizo kwa Jonathan, mara kwa mara alikuwa akimfuata mpenzi wake nyumbani na kuongea pamoja.



    Maisha ya Jonathan yakaanza kubadilika, kwa wakati huu hakuwa mwanafunzi mchafu kama alivyojulikana bali alikuwa miongoni mwa wanafunzi wasafi shuleni hapo. Annabel alishughulika na kila kitu, kuanzia mavazi mpaka fedha za matumizi shuleni.



    Kama yalivyo mapenzi, hayakuweza kuwa siri, baada ya siku chache wanafunzi wote wa Shule ya Sekondari ya Mbezi High wakafahamu kilichokuwa kikiendelea. Jonathan akaonekana kuwa mtu mwenye bahati kubwa, kitendo cha kuwa na msichana mrembo kama Annabel kilimuweka nafasi ya juu shuleni hapo.



    Mapenzi ya Jonathan yalizidi kumteka Annabel mpaka kufikia kipindi hakuwa akitaka kwenda shuleni bali alikuwa akimfuata Jonathan nyumbani na kuanza kufanya mambo mengi wayafanyayo wapenzi wawapo faragha.

    Annabel hakutaka kusikia kitu chochote kuhusu Jonathan, alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati na alikuwa tayari kufanya kitu chochote kwa ajili ya mvulana huyo. Wazazi wake hawakugundua kitu, kila kilichokuwa kikifanyika kilikuwa siri kubwa kwake.

    Mahudhurio yake shuleni yakawa mabovu, hakuwa mtu wa kujisomea kama ilivyokuwa zamani, muda mwingi alikuwa akiongea au kuchati na Jonathan. Mabadiliko yake yakawashangaza walimu, nao, kama walivyo wazazi wake, hawakujua kitu chochote kilichokuwa kikiendelea.

    Mwalimu mkuu aliposikia kuhusu uhudhuriaji mbovu wa Annabel darasani, akamuita na kumuuliza lakini msichana huyo alijitetea kwamba katika kipindi hicho alikuwa katika matatizo binafsi.

    Mwalimu mkuu hakutaka kuongea kitu kwani alijua kwamba alikuwa akidanganywa, alichokifanya ni kuanza upelelezi wake wa siri kwa kuwatumia wanafunzi waliokuwa wakisoma na Annabel.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Annabel hakugundua kitu chochote kile, kila siku alikuwa akiwasiliana na Jonathan bila kufahamu kwamba kulikuwa na wanafunzi waliokuwa wakimfuatilia.

    Siku zikaendelea kukatika huku akimhudumia Jonathan kwa kila kitu alichokuwa akikihitaji kwa kumpa kiasi kikubwa cha fedha kila mwisho wa wiki.

    “Nataka nijichore tattoo ya jina lako mpenzi,” alisema Annabel, kipindi hicho walikuwa katika ufukwe wa Coco asubuhi, siku hiyo hata shuleni hawakwenda japokuwa walikuwa na sare za shule.

    “Tattoo yenye jina langu?”

    “Ndiyo mpenzi. Ninakupenda sana, ninatamani niwe na jina lako kila wakati,” alisema Annabel huku akiwa kifuani mwa Jonathan.

    “Utajichora wapi?”

    Nitajichora kifuani, upande wa kushoto wenye moyo wangu uliojaza mapenzi yako,” alijibu Annabel.

    “Hakuna tatizo, ila itakuwaje wazazi wako wakiiona?”

    “Usijali, hakuna atakayeiona,” alijibu Annabel.

    Moyoni alikuwa amepania kufanya kile alichokuwa akitaka, alimpenda mno Jonathan mpaka kusababisha kutaka kujichora tattoo iliyokuwa na jina lake.

    Siku iliyofuata, asubuhi na mapema, huku akiongozana na Jonathan, wakaenda sehemu iliyokuwa maalum kwa ajili ya kuchorwa tattoo, alichokitaka mahali hapo ni kuchora tattoo tu, hakujua ni kitu gani kingeendelea maishani mwake, alifikiria kumfurahisha zaidi Jonathan.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA





0 comments:

Post a Comment

Blog