Chombezo : Tattoo
Sehemu Ya Pili (2)
“Kuna mvulana nilimuona.”
“Mvulana yupi?”
“Sijui ni mvulana yupi.”
“Sawa. Amefanya nini?”
SASA ENDELEA...
“NIMETOKEA kumpenda mno,” alisema Annabel.
Fatuma akashtuka, hakuamini kile alichokuwa amekisikia, akamwangalia Annabel vizuri ili kupata uhakika juu ya kile alichokuwa amemwambia, msichana huyo alionekana kumaanisha kwa kila alichokuwa amekiongea mahali hapo. Fatuma akavuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu kabisa.
“Unasemaje?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Najua umenisikia. Naomba unisaidie kumfikishia hii taarifa,” alisema Annabel.
“Unamfahamu?”
“Hapana. Nilimuona siku hiyo tu, hata jina lake simfahamu.”
“Kwa hiyo umemuona siku moja na siku hiyohiyo ukatokea kumpenda?” aliuliza Fatuma.
“Ndiyo.”
“Kweli makubwa.”
“Naomba unisaidie Fatuma. Moyo wangu upo kwenye mapenzi ya dhati juu ya mvulana huyo,” alisema Annabel, machozi yalikuwa yakimlenga.
“Nitakusaidiaje?”
“Kumpa taarifa.”
“Nitamjuaje?”
“Sijui. Naomba unisaidie Fatuma.”
“Mbona inakuwa ngumu sana, mimi nitamjuaje?”
“Ni mweusi, siku ile alikuwa ameshika penseli na karatasi pale uwanjani,” alisema Annabel.
“Mmmh! Huo mtihani.”
“Naomba unisaidie, nitakupa zawadi yoyote uitakayo,” alisema Annabel.
Huo ulikuwa mtihani mzito kwa Fatuma, ni kweli alitamani sana kumsaidia rafiki yake kumpata mvulana huyo lakini hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kufanikisha kile kilichokuwa kikihitajika.
Alikumbuka vema maelezo ya Annabel kwamba mvulana huyo alikuwa ameshika karatasi na kalamu pale uwanjani, alikuwa mweusi lakini hakujua ni namna gani angeweza kumpata.
Kwa sababu hakutaka kumuona rafiki yake akiwa kwenye hali ya majonzi, akaamua kumsaidia. Kuhusu fedha halikuwa tatizo, akakabidhiwa kiasi cha shilingi elfu thelathini ya kumsaidia kwenda Mbezi High School kwa ajili ya kumtafuta mvulana huyo na kisha kumwambia kile alichokuwa ameagizwa.
Ndivyo alivyofanya, alipanga siku ya kwenda kisha akafika hadi shuleni hapo. Alikutana na wanafunzi watano wamesimama, akawasalimia kisha akamwuliza mmoja wao:
“Kuna kaka namuulizia,” Fatuma aliuliza.
“Anaitwa nani?” akarudishiwa swali.
“Simfahamu ila wiki iliyopita tulipokuwa tumekuja kucheza mechi, alikuwa ameshika karatasi na karatasi, bila shaka kuna kitu alikuwa akichora,” alisema Fatuma, alifuatisha maelezo ya Annabel.
“Mmmh! Huyo atakuwa Jonathan ma’nake yeye ndiye hupenda kuchorachora,” alisema kijana mwingine.
“Hapana. Hawezi kuwa yeye, Jonathan hawezi kuuliziwa na demu mkali kama huyu,” alisema mwanafunzi mwingine.
Uzuri wa Fatuma ulionekana kuwachanganya. Hata Fatuma mwenyewe alijikuta akianza kujishtukia kutokana na namna walivyoonekana kuvutika naye.
“Mnasema anaitwa Jonathan?” Fatuma akauliza akionekana kuwa na shauku ya kujua.
“Ndiyo ila hatuna uhakika kama ndiye huyo unayemuulizia kwa sababu hadhi yake na yako, dizaini kama hamuendani hivi,” alisema mwanafunzi mwingine.
“Naomba nimuone, nataka kuongea naye,” alisema Fatuma.
Kijana mmoja akatoka mbio kwenda kumtafuta Jonathan mgeni wa Fatuma ambaye alitumwa na Annabel, jambo ambalo vijana wale hawakujua kabisa.
Fatuma alikuwa amekaa kwa presha, uzuri wa rafiki yake, Annabel ulikuwa umemchanganya sana, kuona kijana ambaye alikuwa ameuliziwa na Annabel angekuwa mzuri ambaye alistahili kuwa na rafiki yake.
Baada ya dakika tano, kijana yule alirudi huku akiwa ameongozana na Jonathan. Kwa kumwangalia tu, alionekana kama mtu aliyetoka kuchunga ng’ombe; alikuwa mchafu mno, nywele zake zilikuwa timtim. Bila shaka, alikuwa akiongoza kwa uchafu shuleni hapo.
“Ndiye huyu?” aliuliza Fatuma huku akionekana kushtuka.
“Ndiye mwenyewe,” alijibu kijana yule aliyekuja na Jonathan, Fatuma alikaribia kuzimia kwa presha.
Moyoni alikiri Jonathan hakuwa na hadhi hata robo ya kuwa na rafiki yake Annabel ambaye urembo wake ulikuwa tishio. Alibaki amekodoa macho asijue la kufanya!
Kwa muonekano wake tu, Jonathan hakustahili kuwa na msichana kama Annabel. Jonathan alikuwa mvulana mchafu, alionekana kutokuwa na uwezo kifedha hata kidogo. Kwa muonekano ambao alikuwa nao ulimfanya Fatuma kuona Annabel alikuwa amepotea njia.
“Nani ananiita?” aliuliza Jonathan, wote wakayageuza macho yao na kumwangalia Fatuma.
“Huyu ndiye Jonathan?” aliuliza Fatuma kwa mara ya pili, alionekana kutokuamini kabisa.
“Ndiye yeye, ila tulikwambia,” alisema kijana mmoja.
Fatuma akaomba kusogea pembeni kwa lengo la kumpigia simu Annabel na kumwambia kuhusiana na Jonathan. Kila mmoja alikuwa kimya, bado uzuri wa Fatuma ulikuwa ukiwachanganya vijana wale, hawakuamini kama kweli alifika shuleni hapo kumuulizia mtu kama Jonathan.
“Hivi wewe Annabel una akili kweli?” aliuliza Fatuma mara baada ya simu kupokelewa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Umekutana naye?”
“Kwanza nijibu swali langu, una akili kweli?”
“Kwa nini unauliza hivyo?”
“Hivi huyu Jonathan uliyeniambia ndiye huyu niliyeonana naye au kuna mwingine?”
“Wewe umeonana na yupi?”
“Mvulana mmoja mchafuchafu hivi, nilipoulizia Jonathan, wameniletea huyu kijana mchafumchafu,” alisema Fatuma.
“Upo naye hapo?”
“Ndiyo. Ila nafikiri siyo yeye.”
“Hebu mpige picha nitumie kwenye whatsapp,” alisema Annabel.
Hilo lilikuwa zoezi dogo kwa Fatuma, alichokifanya ni kumpiga picha Jonathan na kisha kumtumia Annabel kama alivyotaka.
Bado Fatuma alikuwa akiendelea kumshangaa Jonathan, muonekano wake ulikuwa ukimshangaza mno kwani bado hakufanana kuwa na msichana kama Annabel.
Annabel alikuwa msichana mrembo mno, mbali na urembo, msichana huyo alitoka katika familia iliyokuwa na fedha. Wazazi wake walikuwa wafanyabiashara wakubwa ambao walikuwa wakiheshimika kutokana na utajiri wao.
“Ndiye yeye,” alisema Annabel mara baada ya kuangalia picha ya Jonathan.
“Kwa hiyo huyu ndiye uliyempenda?”
“Ndiyo.”
“Hebu kuwa siriasi Annabel.”
“Kweli tena. Malizana naye,” alisema Annabel na kukata simu.
Fatuma akashusha pumzi ndefu, hakuamini kama kweli rafiki yake alikuwa ameangukia katika mapenzi ya kijana huyo ambaye hakufanana kuwa na Annabel kwa kila kitu.
“Kuna nini jamani, mbona mmeniita halafu hakuna kitu kinachoendelea?” aliuliza Jonathan.
“Naomba kuongea nawe pembeni,” Fatuma alimwambia Jonathan, wakasogea pembeni huku wavulana wale wengine wakiondoka mahali hapo.
“Kuna nini?”
“Wewe ndiye Jonathan?”
“Ndiyo.”
“Ooopsss..Unamfahamu Annabel?”
“Hapana.”
“Humfahamu msichana fulani mrembo wa shule ya Kisutu?”
“Hapana.”
“Kumsikiasikia je?”
“Kumsikia nimemsikia lakini sikutaka kumtilia maanani kwa sababu hanihusu,” alisema Jonathan.
“Sawa. Msichana huyo anataka kuonana na wewe.”
“Anataka kuonana na mimi? Kuna nini?”
“Amesema kwamba ametokea kukupenda.”
“Ametokea kunipenda! Mimi?”
“Ndiyo.”
“Hapana. Nadhani si Jonathan mimi.”
“Ni wewe jamani. Naomba upange siku ya kuonana naye.”
“Sina muda kabisa dada yangu.”
“Naomba upange siku, aonane na wewe tu.”
“Sawa. Mwambie aje nyumbani.”
“Nyumbani kwenu?”
“Ndiyo.”
“Ni wapi?”
“Manzese Midizini.”
“Mmmh!”aliguna Fatuma.
Mguno alioutoa Fatuma ulionyesha dhahiri alikuwa akiendelea kudharau sababu iliyomfanya Annabel kutaka kuwa na mvulana aliyesimama mbele yake, Jonathan.
Alifahamu fika kwamba Annabel alikuwa msichana mrembo aliyependwa na kila aliyemwangalia, hivyo alitakiwa kuwa na mvulana aliyekuwa na hadhi kubwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kukaa Manzese Midizini kilikuwa kitu kingine kilichojenga picha fulani kichwani mwake. Manzese alipachukulia kama sehemu nyingine za uswahilini hivyo hakutegemea kwamba uzuri aliokuwa nao Annabel,
utajiri waliokuwa nao wazazi wake leo hii alikuwa ameangukia katika mapenzi ya mvulana aliyekuwa akitokea Manzese Midizini, moja ya sehemu walizokuwa wakiishi watu maskini.
“Una simu?” Fatuma alimuuliza Jonathan huku akiwa na uhakika kwamba mvulana huyo hakuwa na simu kabisa.
“Hapana,” alijibu Jonathan.
Hali aliyokuwa nayo Jonathan iliendelea kueleza kila kitu kilichoendelea maishani mwake. Umaskini wake ulionekana kupitia mavazi yake na hata ngozi yake. Alikuwa amepauka, nguo zake alizozivaa zilikuwa chafu huku zikiwa zimechakaa.
“Anabel hastahili kuwa na huyu Jonathan,” alijisemea Fatuma.
Fatuma hakutaka kuendelea kukaa zaidi, akaondoka huku akiwa na dukuduku la kukutana na Annabel na kumwambia ukweli juu ya muonekano aliokuwa nao Jonathan, alitaka kumwambia ana kwa ana kwamba Jonathan hakuwa na hadhi ya kutembea naye, alitakiwa kutafuta mwanaume mwingine.
***
Annabel alikuwa amesimama mbele ya kioo chumbani kwake, katika kipindi kirefu alikuwa akijitazama huku akiwa na nguo yake ya ndani tu iliyokuwa na rangi ya zambarau.
Kila alipokuwa akijitazama, alijiona kuwa msichana mrembo mwenye umbo la kuvutia kuliko msichana yeyote aliyesimama mbele yake. Hapo ndipo alipogundua kwamba wavulana walistahili kumfuata na kumtaka kimapenzi kwani urembo wake ulimvutia hata yeye mwenyewe.
Hakujitoa thamani, alijiona kukamilika kwa asilimia mia moja, kila alipokuwa akijaribu kutoa tabasamu, uzuri wake uliongezeka zaidi, japokuwa hakuwahi kumuona malkia wa Misri aliyesifika kwa uzuri, Cleopatra, alikiri kwamba alimzidi kwa kiasi kikubwa.
“Jonathan, huu mwili nimekupa wewe, ufanye utakavyo lakini nakuomba usiniache,” alijisemea Annabel huku akiendelea kujitazama kwenye kioo, kila alivyoendelea kujitazama, alizidi kumpa sifa Mungu kwa kumpa uzuri uliopitiliza.
Bado honi zilikuwa zikisikika kutoka nje, muda huo ulikuwa ni asubuhi na kama kawaida dereva alikuwa amefika nyumbani hapo kwa ajili ya kumchukua Annabel na kumpeleka shuleni. Honi alizisikia lakini hakujali.
Uzuri wake ulimchanganya hata yeye mwenyewe, hakutaka kutoka mbele ya kioo, aliendelea kusimama mpaka aliposikia mama yake akigonga.
“Unafanya nini muda wote?” aliuliza mama yake, bi Maria baada ya kuona mlango haufunguliwi.
“Nakuja mama,” alijibu Annabel, kwa harakaharaka akachukua nguo zake, akazivaa na kutoka chumbani.
Macho yake yakagongana na ya mama yake, alionekana kuchukizwa.
“Samahani mama,” alisema Annabel, alijua fika mama yake alikuwa amekasirika.
“Sawa. Nenda shule,” alisema bi Maria, Annabel akatoka akaingia ndani ya gari ya kifahari aina ya Jeep SUVs na kuondoka nyumbani hapo.
Garini, mawazo yake yalikuwa juu ya Jonathan, mvulana huyo ambaye alimuona siku moja tu aliuteka moyo wake kupita kawaida, hakutoka kichwani, kila alipokuwa akikaa, akilala na hata kutembea alikuwa akimuwaza.
Mbali na Jonathan, akaanza kumfikiria rafiki yake, Fatuma aliyempa kazi ya kumfuatilia Jonathan. Alipokumbuka kwamba siku iliyopita Fatuma alikuwa amemtumia picha ya Jonathan, akachukua simu yake aina ya Huawei p6 na kuufungua mtandao wa kijamii wa WhatsApp na kuanza kuiangalia picha ya Jonathan.
Annabel akashindwa kujizuia, kila alipokuwa akiiangalia picha ile, mapigo ya moyo yalikuwa yakidunda kwa kasi kupita kawaida. Mapenzi juu ya Jonathan yalimchanganya, japokuwa alijiahidi kutokupenda, mvulana huyo aliivunja ahadi yake hiyo.
Kama kupenda, Annabel aliyahisi mapenzi mazito moyoni mwake, moyo wake uliburuzwa vilivyo na Jonathan, alimpenda mvulana huyo kuliko mtu yeyote katika maisha yake.
Gari likasimama katika sehemu ya maegesho, Annabel akaufungua mlango na kutoka, akaagana na dereva na kuanza kuelekea darasani. Kiu yake kwa wakati huo ilikuwa ni kutaka kuonana na Fatuma, alitaka kusikia mengi kuhusiana na Jonathan kwani aliamini kwamba hicho ndicho kingekuwa kitu pekee ambacho kingempa furaha zaidi moyoni mwake.
“Umemuonaje?” aliuliza Annabel mara baada ya kukutana na Fatuma.
“Annabel.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Najua unachotaka kusema. Fatuma, ninampenda mno Jonathan, najua ni mtu maskini ila nimetokea kumpenda, naomba usiongee kitu chochote kibaya juu ya Jonathan, utaniumiza,” alisema Annabel, kwa mbali machozi yalikuwa yakimlenga.
Fatuma akashusha pumzi ndefu, ni kweli alitaka kumwambia Annabel kwamba hakustahili kuwa na mvulana kama Jonathan lakini maneno yake yalimfanya kumuonea huruma rafiki yake huyo.
“Ni mzuri,” alisema Fatuma, muonekano wake tu ulionesha dhahiri kwamba alikuwa amejilazimisha kusema maneno hayo.
Japokuwa Annabel alilitambua hilo lakini maneno yale yakampa furaha na kuufanya moyo wake kufarijika. Akamsogelea Fatuma na kumkumbatia kwa furaha.
“Nisaidie kumpata,” alisema Annabel.
“Nitakusaidia, anataka kuonana na wewe leo,” alisema Fatuma.
“Mmmh! Nitaweza kuonana naye kweli?”
“Kwa nini usiweze?”
“Ninaogopa Fatuma, ninamuogopa Jonathan,” alisema Annabel.
“Jikaze, wala hatishi, jikaze tu Annabel,” alisema Fatuma.
Siku hiyo ilikuwa ni siku ya furaha kwa Annabel lakini pia ilikuwa ni siku ilioufanya moyo wake kuwa katika hali ya hofu.
Alitamani kuonana na Jonathan lakini moyoni alikuwa na hofu kubwa.
Darasani hakusoma vizuri, kila mwalimu aliyekuwa akiingia alimuona kama akimpotezea muda kwani kitu alichokuwa akikitaka ni kutoka darasani kisha kumfuata Jonathan tu.
Mshale wa dakika aliuona unakwenda taratibu kuliko siku nyingine, kutoka saa moja mpaka saa jingine kwake aliona kuwa mwaka mzima.
Saa 8:30 mchana kengele ikagongwa na wanafunzi walitakiwa kuondoka shuleni hapo. Kwa haraka sana Annabel akachukua simu yake na kumpigia dereva na kumdanganya kwamba siku hiyo walikuwa na kazi ya ziada hivyo wangeruhusiwa kutoka saa kumi na moja jioni, dereva akakubaliana naye.
“Tuondoke,” alisema Annabel.
“Dereva wako akija?”
“Nimekwishaongea naye, twende, nataka kwenda kumuona Jonathan,” alisema Annabel huku akionekana kuwa na haraka.
Hawakutaka kuendelea kubaki shuleni hapo, wakatoka na kisha kuchukua Bajaj iliyowapeleka mpaka katika Shule ya Sekondari Mbezi kwa ajili ya kumuona mvulana aliyetokea kumpenda kwa mapenzi yote, Jonathan.
Ndani ya Bajaj, kila wakati Annabel alikuwa akimsumbua Fatuma aendelee kumwambia mambo mengi kuhusiana na Jonathan. Kila wakati masikio yake yalikuwa yakiwasha na mkuno pekee ulikuwa ni kulisikia jina la Jonathan tu.
“Nampenda Jonathan, natamani awe wangu peke yangu, tupeane mapenzi na kuwa pamoja milele, kama akinikubali, sina budi kujichora Tattoo yenye jina lake, nitajichora katika upande wa moyo wangu,” alijisemea Annabel, kadiri walivyozidi kwenda mbele na ndivyo mapigo yake ya moyo yalivyozidi kumdunda.
Walichukua zaidi ya dakika 30, wakafika shuleni hapo na kushuka kutoka kwenye Bajaj, wakamlipa dereva kiasi cha fedha alichohitaji na kuanza kupiga hatua kulifuata geti.
Wanafunzi walibaki wachache, wengi walikuwa wamekwishaondoka. Walipolifikia geti, wakaingia ndani na kuelekea kwa mlinzi na kisha kumuulizia Jonathan.
Wanafunzi wengine waliokuwa pembeni walibaki wakimwangalia Annabel, kwa wale waliokuwa wakisikia juu ya uzuri wa msichana huyo siku hiyo walimuona laivu.
“Mmmh! Yule msichana mzuri,” alisema mwanafunzi mmoja akiwa na wenzake.
“Yule anaitwa Annabel,” alisema mwanafunzi mwingine.
“Kumbe ndiye yule?”
“Yeah! Ni mzuri mno, wewe unamuonaje?”
“Yeah! Anavutia kupita maelezo.”
Annabel hakuwa muongeaji, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakimdunda kupita kawaida, kila alipokuwa akifikiria kwamba Jonathan angefika hapo muda mchache ujao, hakuwa akijisikia amani moyoni mwake.
Mapigo ya moyo yaliongezeka zaidi mpaka kumfanya kutokwa na kijasho chembamba huku akihisi joto mwilini mwake. Kila alipokuwa akiwaangalia wanafunzi waliokuwa wakimwangalia, uso wake ulionekana kuwa na hofu moyoni mwake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mnamuulizia mchoraji wa shule?” aliuliza mlinzi huyo, alikuwa akimfahamu Jonathan.
“Ndiyo, tunaweza kumuona?”
“Bila shaka, ila mnatakiwa kusubiri nje ya eneo la shule,” yule mlinzi aliwaambia.
Hilo wala halikuwa tatizo hata kidogo, walichokifanya ni kutoka nje ya eneo la shule na kusimama chini ya mti. Annabel aliendelea kuwa na hofu, kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele ndivyo ambavyo mapigo yake ya moyo yalizidi kudunda zaidi.
Hakuongea kitu, alionekana kuwa kama mtu aliyekaririshwa kitu cha kuongea kwamba endapo angeufumbua mdomo wake na kuongea basi angeweza kusahau.
Mlinzi akamuita mwanafunzi mmoja na kumuagiza kwenda kumuita Jonathan. Mwanafunzi yule akaondoka, baada ya dakika tatu, akarudi akiwa ameongozana na Jonathan na kumwambia kuhusu wageni wake waliokuwa wakimsubiri nje.
Jonathan hakushtuka kwani siku iliyopita aliambiwa na Fatuma kwamba msichana huyo angeweza kurudi shuleni hapo na kukutana na msichana aliyesifika kwa uzuri, msichana ambaye alikuwa amekufa kimapenzi juu yake, Annabel.
Jonathan alipotoka nje ya geti la shule, macho ya Annabel yakatua kwa mvulana huyo, mapigo yake ya moyo yakazidi kudunda zaidi. Miguu yake ikaanza kutetemeka na kijasho chembamba kumtoka.
Japokuwa alitoka katika familia iliyokuwa na fedha lakini kijana wa kimaskini alimtetemesha vilivyo na kumfanya kutokwa na kijasho cha woga.
“Habari zenu?” Jonathan aliwasalimia.
Moyo wa Annabel ukamlipuka, akauhisi mwili ukizidi kutetemeka, kitendo cha kuisikia sauti ya Jonathan kilimfanya kujisikia vizuri kuliko kipindi chote cha maisha yake.
Uwepo wa Jonathan mahali hapo ukampa furaha lakini kitu cha ajabu hakuweza kuonyesha tabasamu, bado hofu ilimjaa moyoni.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment