Search This Blog

Monday, October 24, 2022

TATTOO - 5

 





    Chombezo : Tattoo

    Sehemu Ya Tano (5)



    Ilipoishia wiki iliyopita

    “Unamaanisha nini?” aliuliza Annabel, machozi yakaanza kumbubujika.

    “Naomba uniache na maisha yangu,” alisema Jonathan na kuinuka, akaanza kuondoka mahali hapo. Annabel akahisi kuzimiazimia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lilikuwa ni pigo la moyo, Annabel akahisi kupigwa ganzi mwili mzima, mwili wake ukaanza kutetemeka, hakuamini kile alichokuwa amekisikia kutoka kwa Jonathan kwamba hakuwa akimpenda japokuwa alifanya mambo mengi kama kujilazimisha.

    Aliitegemea siku hiyo kuwa miongoni mwa siku zenye furaha maishani mwake lakini ghafla ikabadilika na kuwa siku iliyojaa maumivu makali. Machozi yakaanza kumbubujika, ghafla akainuka na kuanza kumfuata Jonathan aliyekuwa akipiga hatua kuondoka mahali hapo.

    “Jonathan, Jonathan....” aliita Annabel, Jonathan akasimama na kumwangalia.

    “Ninakupenda Jonathan, ninakupenda mpenzi,” alisema Annabel huku akilia kama mtoto mdogo.

    Wapita njia na watu wengine waliokuwa wakiendelea na shughuli zao mahali hapo wakaziacha kwa muda na kuanza kuwaangalia wawili hao. Annabel aliendelea kulia kama mtoto mdogo, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea.

    “Annabel, sitaki kukupotezea muda wako, naomba ufanye mambo yako. Ninapenda kukuona ukiwa na furaha na ndiyo maana nimeamua kukwambia mapema. Nimejitahidi kukupenda lakini moyo wangu umeshindwa kabisa, naomba unielewe Annabel,” alisema Jonathan, kwa wakati huo, kila neno aliloliongea lilikuwa kama msumari wa moto wenye ncha kali moyoni mwa Annabel.

    Kwa usiku huo, kila kitu kilichokuwa kikiendelea, Annabel alijiona yupo ndotoni na muda wowote ule angeamka na kujikuta yupo kitandani. Ukweli ni kwamba hiyo haikuwa ndoto, kilikuwa ni kitu halisi kilichokuwa kikiendelea, mtu aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, aliamua kumwambia ukweli na kumuacha.

    “Nitaishi vipi bila wewe? Nitakwenda wapi kuuficha uso wangu Jonathan? Umeniumiza mpenzi, umeniumiza Jonathan....” alisema Annabel na hapohapo kuanza kukimbia.

    Alionekana kuchanganyikiwa, kile kilichokuwa kimetokea hakuwa amekitegema kabla. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno. Yale maneno aliyokuwa akiyasikia kwamba mapenzi yalichoma na kuuma, huo ndiyo ulikuwa muda wake, alikuwa na maumivu ambayo hayakuwa na dalili ya kupona.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kaka, demu anaweza kujiua huyu, mfuatilie,” alisema jamaa mmoja aliyekuwa akiwaangalia.

    Jonathan hakutaka kupuuzia, alichokifanya ni kuanza kumfuata Annabel aliyekuwa akikimbia. Miguuni hakuwa na viatu, alikimbia pekupeku kuelekea barabarani huku akiendelea kulia.

    “Annabel...” aliita Jonathan, Annabel hakusimama, bado aliendelea kukimbia zaidi.

    Mbio zake zikaishi nje ya Bajaj moja iliyokuwa imeegeshwa nje ya Ukumbi wa Amazon, kwa kasi akaifuata na kuingia ndani. Dereva aliyekuwa amesimama nje, naye akaingia.

    “Wapi dada?” aliuliza dereva.

    “Tuondoke, sitaki huyu mtu anikamate,” alisema Annabel huku akimwangalia Jonathan aliyekuwa akija kasi. Dereva akaiwasha Bajaj hiyo na kuondoka mahali hapo.

    Ndani ya Bajaj, Annabel alionekana kuwa mwingi wa mawazo, hakuacha kulia, bado kilio chake kiliendelea kama kawaida. Maumivu hayakumuisha, kila wakati alikuwa akilia tu huku wakati mwingine akiulaumu moyo wake kumpenda Jonathan. Kilichomuuma zaidi, ni ile tattoo isiyofutika aliyojichora yenye jina la Jonathan.



    Safari nzima Annabel alikuwa akilia tu, machozi yaliendelea kumbubujika mashavuni mwake, moyo wake uliendelea kuwa katika maumivu makali ambayo hakuona kama yalikuwa na dalili zozote zile za kuweza kufutika.

    Saa 6.17 usiku, Bajaj ikasimama nje ya nyumba yao, akateremka, akamlipa dereva kiasi alichokihitaji na kulifuata geti. Mara baada ya kuligonga, mlinzi akatokea na kulifungua.

    Hakuongea kitu chochote, bado moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, kila alipokuwa akikaa, alimfikiria Jonathan tu.

    Mlinzi hakuongea kitu, akamuacha, akaelekea chumbani kwake kwa mwendo wa kunyata, akajifungia chumbani na kukaa kitandani.

    Mawazo yake yakaanza kurudi nyuma kama mkanda wa filamu. Akaanza kumfikiria Jonathan toka siku ya kwanza alipomuona, alipomtuma Fatuma aende kuongea naye na hata siku ile aliyokutana naye, kila alichokuwa akikifikiria mahali hapo, alizidi kuumia.

    Hakuamini kama kweli Jonathan yule aliyekuwa akimpenda na kumthamini ndiye aliyemfanyia hayo, upendo mkubwa aliokuwa nao juu yake ukaendelea kuwepo na hicho ndicho kilichokuwa kitu pekee kilichomuumiza kupita kawaida.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kila alipoiangalia tattoo ile isiyofutika iliyokuwa kifuani mwake, ikiwa na jina la Jonathan, ilimpa maumivu zaidi, akabaki akilia kitandani hapo huku mto wake ukiwa ndicho kitu pekee kilichokuwa kikimfariji, hasa kwa kuukumbatia.

    “Nilijichora tattoo kwa ajili yake, kweli ameamua kuniacha? Kwa nini umenifanya hivi Jonathan? Ina maana haukuuona upendo mwingi niliokuwa nao juu yako?” alijiuliza Annabel kana kwamba Jonathan alikuwa ndani ya chumba hicho.

    Ukweli uliendelea kuwa ukweli tu, Jonathan aliyekuwa akimpenda na kumthamini alikuwa ameondoka mikononi mwake, hakutaka kuwa naye tena. Usiku huo hakulala, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Jonathan na mambo yote ambayo aliwahi kumfanyia mvulana huyo. Kila alichokuwa akikikumbuka, kiliendelea kumuumiza zaidi.

    Kuanzia siku hiyo, Annabel hakutaka kujihusisha na mapenzi, yalikuwa yamemuumiza mno na sasa alitaka kuwa peke yake, aendelee kuyauguza maumivu yake mpaka yatakapopoa kabisa.

    Usiku huo hakulala, kila alipokuwa akijitahidi kujigeuza huku na kule, usingizi haukupatikana kwani kichwa chake kilitawaliwa na mawazo juu ya mwanaume aliyemuumiza, Jonathan.

    Mpaka kunakucha, Annabel alikuwa macho, akajiandaa na kuelekea shuleni. Kila kitu kilichotokea usiku uliopita bado kiliendelea kuwepo kichwani mwake, alimuona mtu mbaya kwa kuwa tu aliuumiza moyo wake.

    “Mbona upo hivyo Annabel?” aliuliza Fatuma, rafiki yake kipenzi.

    “Fatuma, hivi mimi siyo mzuri?” aliuliza Annabel.

    “U mzuri.”

    “Hivi mimi sivutii?”

    “Unavutia. Hebu niambie, tatizo nini?”

    “Jonathan...Jonathan ameuumiza moyo wangu Fatuma.”

    Jonathan! Amefanyaje?” aliuliza Fatuma lakini hata kabla Annabel hajajibu chochote, akaanza kulia.



    Annabel aliendelea kulia, alimhadithia Fatuma kila kitu kilichotokea usiku juu yake na Jonathan. Kila alichokisikia Fatuma hakutaka kukiamini, hakuamini kama Jonathan angeweza kufanya jambo kama hilo kwani alionekana kuwa mwenye mapenzi ya dhati kwa Annabel.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Unafiki mwingi wa Jonathan uliwapiga upofu wote wawili, walimuona mtu mwema mwenye mapenzi ya dhati kumbe alikuwa muongo hata zaidi ya shetani. Kilichofuatia ni Fatuma kuanza kumpa pole Annabel kwani alijua ni kwa namna gani alikuwa ameumia moyoni.



    “Usilie Annabel, utampata mwingine tu,” alimbembeleza Fatuma.

    “Sitaki, sitaki Fatuma, sitaki tena mapenzi,” alisema Annabel huku akijifuta machozi yaliyokuwa yakimbubujika.



    Annabel hakuyatamani tena mapenzi yale aliyokuwa amefanyiwa na Jonathan yalimuoneshea maumivu halisi ya mapenzi jinsi yalivyokuwa, hakutaka kurudi tena kwa kuhofia kuyapata maumivu kama hayo aliyoyapata.



    Masomo yake yaliendelea kama kawaida, kila siku alikuwa mtu wa mawazo tu na hata mwaka huo ulipokwisha na mwaka mwingine kuingia, bado mawazo juu ya Jonathan yalikuwa yakimsumbua kwani kila alipokuwa akiiangalia ile tattoo aliyokuwa amejichora, ilimkumbusha mwanaume huyo.



    Katika mwaka huo akafanya mtihani wa kidato cha nne na matokeo yalipotoka, hakuwa amefanya vizuri. Hayo yalikuwa ni maumivu mengine ambayo alitakiwa kupambana nayo, wazazi wake hawakumlaumu zaidi ya kumtia moyo kwamba kipindi kingine alitakiwa kuwa makini zaidi.



    Annabel hakujiunga na kidato cha tano, akaamua kuanza masomo ya chuo ngazi ya ‘Certificate’ katika Chuo cha Prince And Princess kilichokuwa Posta Mpya akisomea Uhasibu. Tattoo ile haikutoka mwilini mwake, kila alipokuwa akiiangalia iliuumiza moyo wake lakini hakuwa na la kufanya.



    Wakati mwingine alipokuwa akijiangalia kwenye kioo alikuwa akiiziba kwa kipande cha khanga, hakutaka kuiona kwa kuamini kwamba ingeendelea kumkumbusha mbali zaidi. Alitamani kuikimbia lakini hata hilo nalo halikuwezekana, bado iliendelea kuwa kama alama ambayo ingebaki maishani mwake miaka yote.

    Uzuri wake ukawa gumzo chuoni hapo, wanachuo wakaanza mishemishe zao za kumtaka kimapenzi, hasa watoto wa Kiarabu ambao walikuwa wengi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Annabel hakutaka kuwa na mtu yeyote yule, kile kilichokuwa kimetokea maishani mwake kilimpa fundisho, hakutaka kurudi kule alipotoka.“Annabel, msichana pekee wa Kitanzania mwenye sura kama malaika,” alisema Rahim, kijana wa Kiarabu kutoka katika familia ya kitajiri.



    Annabel hakujibu kitu. Rahim akasogea pale alipokuwa amekaa na kutulia pembeni yake, akaanza kumwangalia kuanzia juu mpaka chini, uzuri wa Annabel ukaendelea kumchanganya, yeye ndiye alikuwa mwanaume wa kwanza chuoni hapo kumfuata, hivyo alitaka kuhakikisha anampata hata kabla ya hao wengine wanaoogopa kumuingia.



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog