Search This Blog

Monday, October 24, 2022

TIMBWILI...TIMBWILI - 1

 





    IMEANDIKWA NA : INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO) 





    *********************************************************************************



    Chombezo : Timbwili .... Timbwili

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    NI jambo la kawaida kwa kitongoji cha Kariakoo jijini Dar kufurika watu tangu asubuhi hadi usiku. Kuna wafanyabiashara wengi, kuna waajiriwa, kuna wakaazi, kuna wazururaji na hata vibaka. Taswira hiyo hujitokeza zaidi siku za Jumatatu hadi Ijumaa huku Jumamosi na Jumapili au zile siku za sikukuu huwa na upungufu kidogo wa watu.



    Saad ni mmoja wa waliofika katika kitongoji cha Kariakoo takriban kila siku. Aliishi Kigogo lakini ajira yake ndiyo iliyomlazimu afike Kariakoo kila kukicha. Alikuwa ameajiriwa katika duka moja kubwa la mauzo ya jumla lililokuwa Mtaa wa Msimbazi.



    Jioni moja, kitu kama saa 11 hivi, alikuwa akielekea kwenye kituo cha daladala kwa ajili ya kupata usafiri wa kurudi nyumbani. Mara mbele yake, kwenye mkusanyiko wa watu waliosubiri usafiri wa Magomeni, Manzese, Ubungo, Kimara na kwingineko, alimwona msichana mrembo ambaye hakuwa mgeni kwake. Walifahamiana siku nyingi.



    Msichana huyo aliitwa Mwajuma. Alikuwa akiishi Magomeni Mwembechai, na hapo Kariakoo alikuwa akifanya kazi ya uhudumu katika kampuni moja iliyohusika na uchapaji wa vitabu na magazeti.



    Walitazamana, wakatabasamu na kusogeleana. Wakasalimiana wakiwa wameshikana mikono. Wakaulizana habari za siku nyingi zilizopita, takriban miaka miwili.



    Hatimaye Saad alitaka kuendelea na safari yake. Akajaribu kuunasua mkono wake kutoka kwa Mwajuma.

    Haikuwezekana. Mwajuma aliendelea kuushika mkono huo. “Haraka ya wapi, Saad?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nyumbani.”



    “Nyumbani?” Mwajuma alimshangaa. “Unawahi kupika? Mkeo ana kazi gani jioni?”



    Saad alikosa jibu. Akamtazama Mwajuma kwa namna ya kumshangaa. Na kabla hajapata lolote lile la kusema, Mwajuma akaongeza, “Bado mapema, Saad. Kwako ni kwako tu. Utakwenda muda wowote. Hebu kanipe bia moja kwanza. Nina kiu ya bia barrriiidi!”



    Saad alimkazia zaidi macho Mwajuma. Kisha akacheka. Akilini wake alijua kuwa huo ni mzaha kama mizaha mingine.



    “Unacheka nini sasa, Saad? Sina masikhara mwenzio.”



    “Nimekuelewa, Mwajuma,” Saad alisema. “Kwa kweli nimekuelewa, lakini kwa leo itakuwa ngumu.”



    “Kwa nini iwe ngumu?” Mwajuma alikuwa king'ang'anizi, mkono wake ukiongeza nguvu ya kukishika kiganja cha Saad.



    “Basi tu. Tufanye siku nyingine.”



    “Acha hizo, Saad,” Mwajuma alisema kwa unyonge huku akiuachia mkono wa Saad taratibu. “Sema tu hutaki, Saad.”



    “Hapana, Mwajuma. Siyo kwamba s'taki. Nina ratiba nyingine kwa leo.”



    “Hakuna cha ratiba wala nini. We' sema hutaki tu.”



    “Basi ndiyo, sitaki!”



    “Ndiyo, hutaki tu,” Mwajuma aliuendeleza unyonge katika sauti yake. “Roho mbaya hiyo. Kwani kuna ubaya gani ukininunulia bia mbili tu, Saad? Yaani umekuwa ka' hunijui vile! Kwani tukiingia katika baa yoyote hapa Kariakoo mkeo atajua? Na hata akijua hatajali!”



    “Nini? Unasema hatajali?” Saad alimtazama Mwajuma kwa mshangao mkubwa. Alionyesha dhahiri kutopendezwa na kauli hiyo. Akaongeza, “Mwajuma, kwa kweli sipendi kumuudhi mke wangu. Nampenda na ninamheshimu sana. Siko tayari kumvunjia heshima.”



    Mwajuma alimtazama Saad kwa makini na kumwona jinsi alivyo thabiti katika kauli yake. Akainamisha kidogo uso kisha akaunyanyua tena, safari hii tabasamu la mbali likimtoka. “Hivi,” hatimaye alisema, “utajisikiaje kama utapata fununu au utakuwa na hakika kuwa Halima anatembea na mwanamume mwingine?”



    Halima ndiye aliyekuwa mke wa Saad.



    “Sijakuelewa,” Saad alisema huku akimkazia macho Mwajuma.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mwajuma alikohoa kidogo. “Tuseme, Halima anatongozwa na mwanamume mwingine, anamkubali, na anatembea naye mara mbili, tatu hivi kwa wiki. Kama utajua utajisikiaje? Utaudhika?”



    Saad alitabasamu kidogo, lakini halikuwa tabasamu halisi bali la kulazimisha. Kisha akacheka kidogo, kicheko ambacho kama lile la tabasamu, hakikuwa kicheko cha furaha. Kitu fulani mithili ya kaa la moto kilipenya moyoni mwake.



    “Saad, nasema hivi, kama mkeo huyo atakuwa na bwana wa pembeni, na wakawa wanafanya kama mimi na wewe tulivyokuwa tukifanya, itakuuma?” sauti ya Mwajuma ilikuwa ya msisitizo mkali, tabasamu la dhihaka likichanua usoni pake.



    “Maswali gani hayo, Mwajuma?” Saad alihoji huku akionyesha kuanza kuondoka.



    “Basi, Saad,” Mwajuma alimzuia. “Ni maneno ya kawaida tu hayo. Usiondoke. Twen'zetu kwangu basi. Bia ninazo nyumbani. Tutakula, tutakunywa na hata ikibidi, tutazikumbushia enzi zetu.”



    Saad alimkazia macho Mwajuma, macho makali, akionyesha kushangazwa zaidi kwa maneno aliyoambiwa. Kisha, kwa sauti ya msisitizo mkali, sauti ambayo kwa namna moja au nyingine ilifurika tani kadhaa za dharau, alisema, “Siyo rahisi. Hilo ni jambo lisilowezekana. Sahau kabisa. Nawahi nyumbani, Mwajuma.”



    “Unamwahi mkeo?”



    “Kumbe nimwahi nani mwingine?”



    Kicheko cha dhihaka kilimtoka Mwajuma. “Acha hizo, Saad,” alisema. “Halima hayupo nyumbani. Amini, usiamini.”



    “Nini?”



    “Hivyo hivyo ulivyosikia,” Mwajuma alijibu, safari hii tabasamu lake likichanua zaidi huku macho yakithibitisha kauli yake. Alipoona Saad haelekei kuyajali maneno hayo, aliongeza, “Halima unayemkimbilia wala hayuko mbali kutoka hapa.”



    “Yuko wapi?” Saad aliuliza kwa kuamini kuwa Mwajuma anazungumza uzushi mtupu.



    “DDC.”



    “DDC?”



    “Nd'o maana'ake,” Mwajuma alijibu kwa nyodo. “Yuko DDC nd'o nakwambia ivo, kwani unadhani yuko wapi?”



    Saad alimtazama Mwajuma kwa makini zaidi. Sasa akaona kuwa kuna kila dalili ya maneno hayo kutawaliwa na ukweli. Akahisi kitu fulani kikimkereketa kooni kiasi cha kushindwa hata kumeza mate.



    “Mwajuma, utani mwingine s'o mzuri.”



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Mwajuma alicheka kwa mara nyingine, kicheko kilekile cha dhihaka. Kisha akasema, “Mwenzio anakandamiza, we' eti unajitia kudai unamwahi nyumbani. Angalia Saad, usije ukawa ni mume bwege.”



    “Masikhara hayo, Mwajuma.”



    “Masikhara yatoke wapi, Saad?”



    Saad hakujisikia vizuri. Akaondoka bila hata ya kumuaga tena Mwajuma. Akamwacha kaduwaa!



    **********



    DUNIANI kuna watu! Duniani kuna mambo! Unaweza kupita barabarani hususan maeneo ya mijini, ukakutana na mtu akicheka au akilia. Sababu, haijulikani. Ama utakuta mtu akikoroga tope kwenye sufuria mithili ya apikaye ugali. Na huenda ukamsikia mtu huyo akizungumza peke yake eti: “Hivi kweli huu ugali utawatosha wanangu?”



    Hao wanaye anaowasema, huwaoni!



    Kwa jumla unaweza kukutana na mtu akifanya mambo ya ajabu-ajabu hadharani, akiwa amevaa nguo au akiwa mtupu kama alivyozaliwa!

    Inaweza kuchukuliwa kuwa siku hiyo Saad alikuwa miongoni mwa watu wa aina hiyo. Yeye, mara tu alipomwacha Mwajuma kaduwaa kando ya barabara, alitembea kwa hatua ndefu huku msururu wa mawazo ukimpitia akilini mwake.



    Kicheko cha vuguto, machozi ya moyoni na matukio ya kutisha vilimjia kichwani wakati akipita Kituo cha Polisi cha Msimbazi. Mara akafumbua mdomo akijaribu kutamka neno, sauti haikutoka.



    Akaendelea kutembea, akikaza mwendo, na sasa akajitia kutamka tena maneno fulani, lakini sauti haikutoka. Hata hivyo, kadri alivyokuwa akiigiza kuzungumza huku sauti ikiwa haitoki, ndivyo alivyojiaminisha kuwa sauti ilitoka.



    Akazidisha mwendo maradufu. Hatimaye akafanikiwa kuropoka: “Ushenzi!”



    Baadhi ya watu walimtazama, wakamshangaa na kujiuliza ni vipi kijana huyo aliyevalia kinadhifu azungumze peke yake barabarani kama chizi? Kalewa? Kafiwa na mtu wa karibu katika familia au marafiki zake? Jibu halikupatikana.



    Saad aliendelea kukaza mwendo, akipigana vikumbo na baadhi ya watu. Hatimaye alijikuta mbele ya lango kuu la Ukumbi wa DDC Kariakoo. Akaingia ukumbini.



    Watu wengi walikuwa ukumbini humo. Baadhi walikuwa wakipata mlo, baadhi walikunywa bia, soda au maji. Alisimama kwa dakika chache akiwatazama watu hao. Mara akainamisha uso, akihisi uzito kichwani, akiamini kuwa kwa kufanya hivyo atajisikia ahueni.



    Akiwa katika hali hiyo, mara wazo likajikita kichwani mwake, wazo lililomtaka aondoke ukumbini humo na kwenda zake nyumbani. Lakini hakukubali, akapingana na wazo hilo kwa nguvu zote. Akavuta hatua ndefu akielekea ndani zaidi, akitafuta sehemu yenye nafasi, ajitwalie kiti na kuketi kabla ya kufuatia kile kilichompeleka hapo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Haikuwa kama alivyotaka. Wakati akipita meza moja hadi nyingine, mara macho yake yakatua katika meza moja. Akashtuka na kushangaa. Baada ya mshtuko na mshangao huo, hasira zikatwaa nafasi nafsini mwake. Na alikuwa na sababu ya kukumbwa na hali hiyo.



    Halima!



    Mbele yake, hatua kama ishirini au thelathini hivi, alimwona mkewe, Halima, akiwa ameketi meza moja na mwanamume ambaye alimtambua fika.



    Ni Nsanzugwanko, mtu ambaye pesa hazikuwa ni kitu kinachoweza kuadimika katika himaya yake. Alikuwa ni mtu aliyekwishausogelea utajiri. Kama ilivyo kawaida ya wakazi wa mijini, hususan wale ambao hawana tabia ya kufuatilia mienendo ya watu, kwa hapo DDC Kariakoo pia watu hawakujua Nsanzugwanko alikuwa amefanikiwa vipi kuwa miongoni mwa wachache ambao 'wanazo.'



    Mara chache, kama wengine, alifika hapo na kunywa bia, na mara chache vilevile alikuwa akiambatana na Halima. Kwamba uwezo wa kiuchumi wa Nsanzugwanko ulitokana na mbinu za kughushi saini mbalimbali za vigogo wa mashirika makubwa, na saini hizo zikamnufaisha kwa kupata pesa, malaki kwa mamilioni, lilikuwa ni jambo gumu kubainika kwa watu wa kawaida, hususan hawa wapenzi wa kukanyaga hapo DDC Kariakoo kila kukicha na kila kukichwa.



    Alifanya mambo yake kwa umakini wa hali ya juu, sanjari na kuhakikisha mbele ya jamii anaonekana ni mtu wa kawaida, mfanyabiashara wa safari za mikoani, ambaye mambo yake yamemnyookea. Na wengi walimchukulia hivyo.



    Ni huyo Nsanzugwanko ambaye alikuwa ameketi na Halima, nyuso zao zikiwa zimejaa bashasha na vinywaji vikishuka matumboni mwao!



    Saad hakuyaamini macho yake baada ya kuwaona. Akahisi anaota. Ni kama vile michirizi ya barafu ilikuwa ikimpitia katika uti wa mgongo wake. Akatetemeka mithili ya aliyekumbwa na shoti ndogo ya umeme.



    Baadhi ya wanywaji na walaji walimwona, na walimtazama kwa makini, sekunde chache kwake na sekunde chache kwa Halima. Watu hao walimjua vizuri Saad, kuwa ni mtoto wa town. Na pia walimjua vizuri Halima, kuwa ni mkewe Saad. Lakini waliishia kuwatazama tu, hakukuwa na yeyote aliyeweza kubashiri ni kipi ambacho kingetokea.

    Hawakuwa hao wanywaji na walaji pekee waliomwona. La. Hata Halima alimwona. Hata Nsanzugwanko alimwona!



    Kila ambaye Saad alimtupia macho alikuta naye akimwangalia. Akasonya kwa hasira. ‘Ni heri nisingekuja’, alijisemea kwa mnong'ono ambao hakuyafikia hata masikio yake mwenyewe.

    Pia, akawaza kuwa, ingekuwa vyema kama asingeyajali maneno aliyoambiwa na Mwajuma; angeenda zake nyumbani ambako asingeigundua siri hii iliyofichuka kiasi cha kuunyong'onyesha moyo wake kwa kiwango kisichokadirika.



    Lakini alikuwa amechelewa. Na macho ya waliomtazama ni kama vile yalikuwa yakimwambia, “Saad we’ ni mwanamume. Usikubali huyo mwanamke akuvunjie heshima. Mshughulikie yeye na mjinga-mjinga wake.”



    Angeweza?



    Ukweli ni kwamba, hasira zilishamtawala. Alitamani kumfuata Halima pale na kumfunza adabu. Amzabe makofi matatu yenye uzito wote nyuma yake. Na iwe ni palepale ukumbini!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hata hivyo papohapo wazo jingine lilimjia akilini. Kwamba, afikiri kwanza na kuyatafakari matokeo ya hatua yoyote aliyotarajia kuichukua wakati huo. Ni hilo lililomtisha.



    Nsanzugwanko alijaaliwa umbo kubwa na alikuwa ni mkorofi. Hapo DDC Kariakoo walikuwa na rekodi yake ya kuwashushia vipigo vya 'mbwa mwizi' wanaume wawili waliompapasa makalio mwanamke mmoja aliyekubaliana naye kustarehe pamoja siku hiyo. Wakware hao walimfanyia vitendo hivyo mwanamke huyo wakati alipoanza kucheza muziki uliopigwa na bendi fulani maarufu jukwaani.



    Alicheza kwa kunengua kiuno kwa umahiri mkubwa na ndipo wakware hao walipomfuata na kuanza kumpapasa. Kilichofuata hakikutofautiana na gharika kwa wale wakware.



    Siku hiyo Saad aliishuhudia songombingo hiyo, na alikiri kuwa Nsanzugwanko ana ubavu wa kupambana na zaidi ya mwanamume mmoja! Ni hilo lililomfanya jioni hii asitishe kufanya chochote kile kitakachomkera Nsanzugwanko. Hakuwa na ulemavu wowote maungoni mwake, na alihitaji kuendelea kuwa hivyo.



    Lakini, je, asipowavaa Nsanzugwanko na Halima hapo walipo, wateja wengine watamchukuliaje? Hawatamchukulia kama 'mume bwege'?

    Akawakazia macho Halima na Nsanzugwanko. Macho yake na ya Halima yakakutana. Aliyaona macho ya Halima kama vile yanayomwambia, 'Acha paniki. Jihadhari. Ukizua sheshe la aina yoyote utakuja juta baadaye.'

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akanywea na kubaki akiwatazama kwa uchungu.

    ITAENDELEA

    0 comments:

    Post a Comment

    Blog