Chombezo : Jasho La Masumbuko
Sehemu Ya Tano (5)
AKAWAZA kuwa askari polisi wengi huwa hawana mazoezi ya kutosha. Wakishatoka Moshi kwenye mafunzo basi, hujipweteka. Zaidi, hubakia kuwaghasi raia kwa kuwapiga virungu na kula rushwa.
Imani hiyo ilimwongezea ujasiri. Akamvaa yule askari aliyekuwa mbele yake na kumpiga ngwala ya nguvu. Hakubisha; alikwenda juu mzimamzima na alipokuwa akirejea chini alipokelewa na teke zito la kichwani. Dakika iliyofuata alikuwa akijinyoosha chini huku akitoa mkoromo wa kutisha.
Kisha akatulia!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati huo yule askari wa pili aliduwaa, na yale majibwa yakimkodolea macho kama yanayosubiri amri ya nini cha kufanya. Punde akili ikamrudia. Akafyatua risasi mbili kumwelekea Masumbuko. Lakini Masumbuko akiwa ameshahisi kitakachofuata, alijirusha haraka upande wa pili, na badala yake, zile risasi ziliyapata yale majibwa na kufa palepale.
Vifo vya majibwa yale vilimfanya yule askari achanganyikiwe maradufu. Jakamoyo likampata. Akatupa bastola chini na kutoka mkuku! Mbio kama farasi!
Masumbuko hakumwachia, aliokota jiwe na kumwandama.
“Huyooo! Mwizi huyooo!” vijana wengine walioshuhudia tandabelua ile wakaungana na Masumbuko.
“Mkamateni...!”
Mara vijana wengine wawili wakazuka mbele yao. Wakamtinga yule askari. Mmojawao akamkamata yule askari na kubwata, “Majuzi mlinivunjia kibanda changu cha biashara kwa madai kuwa ninaharibu sura ya jiji. Leo wewe ni halali yetu!”
Papohapo akamtwisha gumi la uso. Kofia ya jamhuri ikapaa angani na kutua hatua takriban kumi nyuma yake.
Mara Masumbuko akafika. “Mwachie kwanza!” alisema, kisha yeye akamkwida shingoni na kumtwanga kichwa.
Askari akatema damu!
“Kwa nini mmemuua yule bibi?” alimuuliza kwa hamaki. “Sema kwa nini mmemuua? Nyie ni walinda usalama wa raia au wauaji? Hamwezi kumhoji mtu bila ya kumpiga? Mnapata mishahara mikubwa na posho nono kwa ajili ya kuua?”
Askari alikuwa hajiwezi. Hakuweza hata kujibu. Damu iliendelea kumtoka mdomoni kama beberu.
Umati uliokusanyika pale ukazidi kushangilia na kuporomosha kauli za kejeli dhidi ya askari huyo.
Lakini punde king'ora kikasikika tena. Mara sauti kutoka katika kipaza sauti ikatawala anga: “Wote mlioko hapa mko chini ya ulinzi! Yeyote atakayejaribu kukimbia ajihesabu kuwa tayari ni maiti!”
Askari takriban hamsini hivi kutoka katika kikosi maalumu cha kutuliza ghasia walikwishalizingira eneo hilo. Vijana wengi wakatiwa mbaroni na kutupwa ndani ya karandinga.
Wakapelekwa kituo cha Polisi.
**********
SIKU iliyofuata tukio hilo lilikuwa gumzo vinywani mwa watu. Idadi kubwa ya watu ilifurika kituo cha Polisi. Wengi kati ya hao, sio kwamba walifika hapo kwa madhumuni ya kutafuta njia ya kuwatoa jamaa zao waliosweka ndani, la hasha. Walikuja kwa minajili ya walao kulitupia macho tu yule aliyedaiwa kuwa ni 'jambazi sugu.'
Na isitoshe, magazeti mengi yaliandika, televisheni na redio zikatangaza na kuonyesha.
Gazeti moja lilikuwa na maelezo: LILE JAMBAZI LILILOSABABISHA MAUAJI MAKUBWA JIJINI JUZI, JANA LILIZUA SONGOMBINGO NYINGINE HUKO VINGUNGUTI, JIJINI DAR ES SALAAM. ASKARI MMOJA, AJUZA NA MBWA WAWILI WA POLISI WALIUAWA. ASKARI MWINGINE AKISHIRIKIANA NA KIKOSI MAALUMU WALIFANIKIWA KULITIA MBARONI JAMBAZI HILO NA SASA LIKO KITUO CHA POLISI...
Jambazi hilo halikuwa lingine bali ni Masumbuko Maliyatabu. Ndiyo, Masumbuko alitiwa mbaroni na hatimaye kusimamishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisalata kwa tuhuma ya mauaji.
Mwaka mmoja ulikwisha akiwa rumande tangu kesi ilipofunguliwa. Upelelezi ulikuwa haujakamilika!
Sasa alishayazoea maisha ya rumande. Yale maharage yaliyooza, ugali usioiva, achilia mbali matandiko hafifu na msongamano wa kutisha, kwake yalikuwa ni maisha ya kawaida. Kuna ule usemi wa 'kama hupati unachokipenda, basi penda unachokipata.'
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa jinsi hali ilivyokuwa, Masumbuko alilazimika kufuata usemi huo kwa moyo mkunjufu. Hatimaye ikaja siku. Ilikuwa ni asubuhi, alipolisikia jina lake likitajwa na askari jela. Alikuwa akahitajika mahakamani.
Kama alivyokuwa akifarijika mara kadhaa zilizopita alipopelekwa mahakamani na kurudishwa rumande, safari hii pia alifarijika kupelekwa huko. Faraja hiyo ilitokana na kwamba, kitendo cha kwenda huko kingemfanya na yeye ajisikie yuko 'duniani' kama binadamu wengine.
Angeonana na watu wengine, na labda angepata msaada fulani, msaada ambao hakujua ungetoka kwa na nani na kwa kiasi gani. Kukaa gerezani kutwa, kucha kulimfanya ajione kuwa ni mtu ambaye hatofautiani na wale waishio jehanamu.
Jina lake lilitajwa akiwa ni miongoni mwa watu watakaokwenda mahakamani kwenye mwendelezo wa kesi zao. Na siku hiyo ilikuwa ni siku ya walalamikaji na mashahidi wao kutoa maelezo.
Walipanda katika karandinga la Polisi na baada ya muda wakatinga mahakamani. Siku hiyo watu walikuwa wengi zaidi, labda kwa kutaka kuusikia ushahidi wa upande wa mashtaka.
Mashtaka yake yaliposomwa, baadhi ya watu wakatikisa vichwa kwa masikitiko. Yalikuwa ni mashtaka mazito. Masumbuko akaanza kupoteza matumaini ya kuokoka. Hakuwa na wakili ambaye labda angemsaidia katika utetezi. Na hata hivyo angempataje wakili ilhali hali yake ya kipato ilikuwa duni?
Mawakili wengi hufanya kazi kwa makubaliano ya malipo. Na si vichele vya pesa, la. Ni pesa nyingi. Pesa hizo hakuwa nazo, na hakuwa na uwezo wa kuzipata. Hata laki tano asingezipata!
Akainua mikono.
Yote akamwachia Mungu.
Cha ajabu, katika mashtaka yaliyosomwa, kifo cha yule bibi kizee aliyepigwa na askari na kukata roho palepale hakikutajwa! Vifo vya Aboubakary, Mheshimiwa Kisu Makalikuwili, mbwa wawili na yule askari ndivyo vilivyotajwa.
Masumbuko aliyakana mashtaka yote hayo. Na hapo ndipo jaji aliposema kuwa kesi hiyo ni ya muda mrefu hivyo ingepaswa kuanza kusikilizwa haraka iwezekanavyo.
Upande wa mashtaka nao ukatoa kauli kuwa mashahidi wake muhimu wote walikuwepo.
Ndipo Masumbuko alipomwona msichana mmoja akisimama katikati ya watu walioketi ndani ya chumba cha mahakama. Kisha kwa mwendo wa taratibu, mwendo wa kujidai, akapanda kizimbani tayari kwa kutoa ushahidi wake.
Alikuwa ni Happy!
Akiongozwa na mwendesha mashtaka, Happy alitakiwa kuithibitishia mahakama kwamba, Masumbuko ndiye aliyehusika na vifo vile na pia kusababisha kuvurugika kwa amani.
Kwanza Happy alikula kiapo kama ilivyo kawaida ya mahakama. Akamtazama Masumbuko kwa tabasamu la mbali lakini lililozungumza mengi.
Kisha: “Mheshimiwa jaji,” alianza. “Nitasema kweli tupu kama nilivyoapa muda mfupi uliopita. Na yote nitakayosema, nitayasema kwa hiari yangu; sikulazimishwa na mtu wala kushawishiwa. Nitasema kweli hiyo nikiwa najiamini kuwa nina akili timamu na wala sijatumia kilevi cha aina yoyote.”
Sauti yake haikuwa ile ya yule Happy ambaye Masumbuko alimfahamu hapo kabla. Hii ilikuwa ni sauti thabiti, sauti iliyoashiria ujasiri na ushupavu. Mahakama ilikuwa kimya. Kila mtu alimkodolea macho Happy, shauku ya kukisikia hicho alichotaka kukisema ikiwa imewajaa.
“Mheshimiwa jaji, matukio yote dhidi ya mshtakiwa niliyashuhudia kwa macho yangu haya mawili,” Happy aliendelea. “Katika tukio la kwanza, gumi zito la mkono wa kulia wa mshtakiwa ndilo lililoniletea mapengo haya.”
Kufikia hapo akafunua mdomo na kuonyesha mwanya mkubwa katika meno ya chini. Akamtupia jicho kidogo Masumbuko kisha akaendelea, “Hata hivyo, ukweli ni kwamba mshtakiwa hahusiki hata kidogo na makosa yaliyotajwa.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Miguno ilitawala katika ukumbi wa mahakama.
Baadhi ya watu walibaki midomo wazi kwa mshangao.
Minong'ono ikazuka!
Ghafla jaji akagonga meza kwa nguvu tiii! “Hapa ni mahakamani!” alifoka. “Siyo baa au sokoni! Kimya!”
Utulivu ukarejea kama awali.
“Endelea,” jaji alimwambia Happy.
Naam, Happy akaendelea kutoa maelezo kwa utulivu, akiyaepuka kijanja maswali ya shahidi wa upande wa ulalamikaji aliyekuwa amefura kwa hasira. Shahidi huyo alikuwa ni askari wa Jamhuri ya Muungano aliyeiwakilisha serikali katika kesi hiyo.
Hatimaye, katika hali iliyowashangaza wengi, Happy alihitimisha maelezo yake kwa kusema, “Mheshimiwa jaji, kwa upande wangu naamini kuwa mshtakiwa siyo jambazi wala muuaji!”
Wasikilizaji walishangaa, wakaduwaa!
Mwendesha mashtaka alibaki kinywa wazi!
Jaji aliendelea kuandikaandika kwenye karatasi yake bila ya kumtazama Happy.
Kwa ujumla maelezo ya Happy hayakutegemewa na asilimia kubwa ya watu waliofika hapo mahakamani kuifuatilia kesi hiyo.
Wakati watu wengine wakibaki wameshangazwa na maelezo hayo, Happy aliteremka na kutembea kivivuvivu au tuseme kwa madaha na kwenda kuketi mahala pake.
Masumbuko alishindwa kuyaamini masikio yake kama pia alivyoshindwa kuyaamini macho yake. Kwa mbali akahisi jasho likimtoka, jasho la mlalahoi! Jasho la matumaini! Jasho lililomtoka kifuani kwa Happy kule Nzega, kwa Mwanahawa na kwa Chausiku hapo Dar, halikuwa jasho la bure.
Limelipa!
Happy! Happy yule aliyediriki kumwandikia barua yenye kilo nyingi za matusi na kashfa, leo hii anamtetea mahakamani! Happy ambaye tayari ana dosari kubwa ya mapengo kutokana na kipigo, leo anamkingia kifua!
Alishindwa kuamini. Akatamani kumrukia amkumbatie, hakuweza.
Shahidi wa pili alikuwa ni Mwanahawa. Huyo alipanda kizimbani huku amembeba mtoto mdogo. Masumbuko alimtazama Mwanahawa na kushtuka. Akamtazama yule mtoto kwa makini zaidi na kujiwa na kumbukumbu fulani kichwani mwake. Akashusha pumzi ndefu na kuhisi jasho likimtoka makwapani.
Mwanahawa alizungumza kwa kifupi tu: “Siku ambayo shemeji Kisu Makalikuwili aliuawa nilikuwepo eneo la tukio. Ni mimi niliyekuwa naye garini. Nilichomoka na kukimbia wakati gari lilipotiwa moto.
“Mheshimiwa jaji, naithibitishia mahakama hii tukufu kuwa shemeji Kisu aliuawa na kuchomwa moto na kundi la watu; wengi wao wakiwa ni wauza maji, wasukuma mikokoteni na vijana wa kijiweni.
“Mheshimiwa jaji, huyu mshtakiwa alifanya kazi kwa marehemu zaidi ya mwaka mmoja. Ninamfahamu vizuri. Hana tabia mbaya kama kibaka au ujambazi. Na siku ya tukio sikumwona!”
Yalikuwa ni maelezo mengine yaliyowashangaza watu. Huyu Mwanahawa ambaye ni shemeji wa Kisu Makalikuwili leo anamtetea Masumbuko!
Kesi iliahirishwa, na kila ilipotajwa, mashahidi wa upande wa mashtaka ama walimtetea Masumbuko au walitoa ushahidi wa kujikanganya. Matokeo yake kesi ilipoteza msisimko huku vyombo mbalimbali vya habari vikiuponda upande wa mashtaka.
**********
ZIKIWA zimebaki siku mbili hukumu itolewe, likazuka jambo lililomshangaza Masumbuko. Ilikuwa ni asubuhi alipoitwa na askari wa zamu. “Kuna mgeni wako,” aliambiwa.
“Mgeni wangu?” Masumbuko alishangaa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Fanya haraka,” askari alimhimiza. “Nitawapa dakika mbili tu za kuongea. Sijui ni mkeo au dada'ako yule.”
Masumbuko alinyanyuka huku bado akijiuliza, ni nani huyo atakayekuwa amekuja kumtembelea? Hakuwa na kaka wala dada katika jiji hilo. Hata wale 'chinga' wenzake, wasingeweza kumtembelea leo wakati walikosa nguvu ya kumjulia hali siku chache tu baada ya kutiwa mbaroni.
“Ni nani huyo?” alijiuliza kwa mnong'ono ambao haukuweza kuyafikia hata masikio yake mwenyewe.
Akamfuata yule askari huku swali hilo likijirudia moyoni mara kadhaa.
Hatimaye alifika sehemu aliyopelekwa. Akashtuka. Akashangaa, kinywa kakiachia wazi.
Alikuwa ni Happy!
“Happy!” Masumbuko aliropoka huku akimtazama Happy kwa macho makali na wakati huohuo akizilaani seng'enge zilizomtenganisha na Happy.
Happy alimtazama Masumbuko bila ya kutamka chochote. Lakini tazama yake ilikuwa na mengi aliyoongea na yakiwa ni mazuri. Masumbuko alilibaini hilo macho yao yalipogongana. Mara Happy akayahamisha macho kutoka kwa Masumbuko na kumtazama kidogo yule askari.
Askari yule alijua ni kwa nini ametazamwa. Akasema, “Nawapa dakika mbili mzungumze.” Akasogea umbali wa hatu kumi na kuwaachia uhuru Masumbuko na Happy.
“Askari wote wangekuwa kama huyu...” Masumbuko alisema na kuiacha sentensi hiyo ikielea.
Happy hakutamka chochote kuhusu kauli hiyo ya Masumbuko. Zaidi, alitabasamu kidogo na kumtupia jicho yule askari kabla hajamrudia Masumbuko.
“Unajua Masu,” Happy alianza kusema. “Nimekutesa sana. Najua hivyo, lakini nakuomba sana unisamehe. Na nitakuomba msamaha zaidi keshokutwa wakati utakapokuwa huru...”
“Nini?”
“Nasema hivi...” Happy alisema na kusita kidogo. Akamwangalia tena yule askari, na akafurahi kumwona akijishughulisha na watu wengine. Sasa akamrudia tena Masumbuko.
Akaendelea: “Nasema hivi, nitakuomba msamaha keshokutwa utakapoachiwa huru.”
Masumbuko alizidi kushangaa. “Kwa nini unasema nitakapoachiwa huru?”
Happy alicheka kidogo huku akiendelea kumtazama Masumbuko kwa namna ya mapenzi ya dhati. “Usihofu, Masumbuko,” aliendelea kusema. “Hali halisi inajionyesha. Huoni hata mashahidi wa upande wa mashtaka wameingia mitini, na wengine walikuwa wanajikanganya kanganya wakati wakitoa maelezo?”
Masumbuko aliguna. Akakosa la kusema. Akabaki akimwangalia Hapyy kama vile atazamaye sanamu.
Happy akaendelea: “Masumbuko, Mungu yuko pamoja nawe. Anazijua shida zako. Siku zote nimekuwa nikikuombea upone katika janga hili. Kwa kweli ni wewe uliye moyoni mwangu...” akasita kidogo na kuyaepuka macho ya Masumbuko.
Kwa kiasi kikubwa Happy alijisikia kuona haya wakati akizungumza hayo aliyokuwa akiyazungumza. Ndiyo, ni huyu Masumbuko aliyeivunja ile himaya yake ya usichana enzi zile huko Nzega. Na walikubaliana kufunga pingu za maisha baada ya Happy kurejea kutoka California, Marekani, jambo ambalo halikutekelezeka.
Happy alikumbuka vizuri siku alipodiriki kushika kalamu na karatasi na kumwandikia barua Masumbuko, akimshushia tani kadhaa za kashfa na matusi yasiyomithilika, akithubutu pia kumwambia kuwa sasa kuna Mwarabu aliyekabidhiwa lile tunda ambalo yeye, Masumbuko alilionja kimakosa!
Isitoshe, kile kitendo cha kumwagia maji machafu kule Upanga akiwa ndani ya gari lake, BMW, kwa wakati huu alikichukulia kama kosa lisilosameheka. Kwamba Masumbuko aliamua kuchukua sheria mkononi kwa kumpiga baada ya kumtoa garini, kwa Happy aliona kuwa kilikuwa ni kipigo kilichomstahili.
Haikumwingia akilini kuwa kwa yeyote mwenye akili timamu angeweza kuvumilia baada ya kufanyiwa unyama wa aina ile.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akilini mwake kulikuwa na kitu kikimsuta kwa kumwambia kuwa ulimbukeni umemponza. Kilichojiri baada ya mkasa wa kuuawa kwa mpenzi wake, Aboubakary siku ile ya patashika pale Upanga aliona kuwa ni pigo alilopewa na Mungu. Akajiona yu mkosaji nambari moja.
Na sasa aliamua kuuweka bayana ukweli huo.
“Masumbuko,” aliunyanyua tena usowe na kuendelea, “nakujulisha tu kwamba, baba yake Aboubakary amekamatwa na boti ya kisasa iliyojaa dawa za kulevya, cocaine huko Mauritius. Tayari kishanyongwa. Tumsahau!
“Sasa nakwambia hivi, keshokutwa ndiyo siku ya hukumu yako. Na kwa kuwa nakujali na kukupenda sana, nimefuatilia sana suala lako huko mahakamani hadi nikapata siri ya hukumu hiyo. Utatoka. Utaachiwa huru, na ukishakuwa huru tutakwenda kwangu.”
“Nina nyumba huko Mbezi. Naamini itatutosha. Siyo nyumba kubwa sana, lakini inastahili kuitwa nyumba ya binadamu. Tutakwenda huko ukiwa ni mume wangu halali. Tafadhali nakuomba uniamini. Sasa nitakuwa mwanamke mwema na mwaminifu kwako.
“Kwa kweli dunia imenifunza mengi. Naapa, sitarudi kwenye mkondo ule wa maisha. Masu...Masu...Masumbuko, yakumbuke yale matone ya damu siku ile usiku tulipouzindua ujana wetu chumbani mwako...” hakumalizia chochote alichotaka kuendelea kusema, kilio cha chinichini kilimtia kwikwi na kumzulia kigugumizi kilichomzuia kuendelea kuzungumza.
Masumbuko aliingiwa na huruma. Akasema, “Happy, acha kulia. Acha kulia Happy. Nina imani Mungu alikuumba kwa ajili yangu, Happy. Yaliyotokea nd'o yamekwishatokea; tusiyajali sana. Wakati mwingine binadamu inabidi apitie kwenye mkondo wa ajabu maishani mwake ili tu aweze kuupata ukweli.
“Huenda ilikuwa ni lazima hayo yatokee kwanza ndipo mwafaka kati yetu upatikane. Tuombe Mungu nitoke...”
“Utatoka mpenzi!”
“Tuombe Mung...”
“Nakwambia hivi, Mungu anazijua shida ulizozipata!” ni kama vile Happy alikuwa akifoka.
Mara akasogeza kichwa kwenye zile nondo na kunong'ona, “Us'jali, keshokutwa utafaidi. Utakula kila chakula utakachohitaji, na utakula kwa jinsi unavyotaka.”
Yalikuwa ni maneno mazito masikioni na akilini mwa Masumbuko. Wakatazamana kwa takriban dakika nzima, macho ya kila mmoja yakizungumza mengi.
“Happy...” hatimaye Masumbuko aliipata sauti yake.
“Masu..”
“Happy, nakupenda.”
“Masu mi' nakupenda zaidi.”
Masumbuko alitaka kutamka neno jingine zaidi, hakuweza. Alikumbwa na kigugumizi. Akaishia kushusha pumzi ndefu akimtazama Happy wakati akiondoka huku akijitupa kivivuvivu, mtikisiko wa matako yake makubwa ukimsisimua Masumbuko kwa kiwango kikubwa. Vinyweleo vikamsimama mithili ya mbwa aliyeshtushwa na kitu.
HITIMISHO
Kesi ya Masumbuko iliishia kwa yeye kuachiwa huru baada ya kukosekana kwa uthibitisho wa tuhuma zilizomkaabili. Na hata pale jaji alipotamka rasmi kuwa Masumbuko yu huru, bado Masumbuko mwenyewe hakuyaamini masikio yake.
Ni hadi pale Happy alipomfuata na kumkumbatia huku pia askari wakimtaka aondoke ndipo Masumbuko alipoamini kuwa sasa yuko huru.
“Hivi naota?” alimuuliza Happy wakati wakitoka nje ya ukumbi wa mahakama.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Huoti, Masumbuko,” Happy alimjibu huku akiwa bado amemshika mkono kwa namna ya watu wapendanao. “Huoti. Nilikwambia, Mungu anazijua shida zako. Na anajua kuwa kuna mtu anayeitwa Happy ambaye anakuhitaji katika maisha yake.”
“Ni kweli, Happy. Mungu ashukuriwe.”
Mara wakatazamana. Wakati huo walikuwa nje kabisa ya jengo la mahakama. Wakasogeleana. Wakakumbatiana. Vinywa vyao vikakutana. Busu hilo likadumu kwa takriban dakika nzima, watu wakiwashangaa, na wao wakionyesha kutoujali mshangao wa wanaowashangaa.
Naam, huo ukawa ni mwanzo kamili wa uhusiano wao mpya, uhusiano ambao awali ulitetereka na hatimaye 'kufa' baada ya Happy kukumbwa na jinamizi la maisha.
*****MWISHO *****MWISHO*****MWISHO*****
0 comments:
Post a Comment