Search This Blog

Monday, October 24, 2022

JICHO LA KAMORE - 4

 





    Chombezo : Jicho La Kamore

    Sehemu Ya Nne (4)



    Mikunjo michache ikiwa bado imejiunda katika paji la uso wake, Samba aliipokea kijikaratasi kile na kukitazama kwa makini. Ilikuwa ni risiti halali ya kampuni ya MP Brother's Co. Ltd. Akashangaa, mshangao uliokuwa bayana hata machoni mwa Kamore.

    Akayatoa macho katika risiti.



    Akaunyanyua uso na kumtazama Kamore usoni sawia. Paji la uso wake likiwa bado na mikunjo huku macho yakitangaza dhiki iliyomwandama kila kukicha, kwa sauti ya kutojiamini alisema, “Sijakuelewa.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unashangaa nini?” Kamore alimwuliza. “Acha kushangaa-shangaa ovyo. Kumbuka Samba, mimi na wewe tumetoka mbali. Usidhani kuwa nimekosa mtu wa kumuunganishia mpango huu. Hapana. Dar hii ni kubwa. Ina mamilioni ya watu. Wapo wasomi wa viwango vya juu, vya kati na vya chini. Lakini Samba hao wote sikutaka kuwashirikisha. Nimekuchagua wewe. Unasemaje?”



    “Hakuna noma mtu wangu,” Samba alijibu. “Tuzungumze tu kwa uzito unaostahili. Si unajua kuwa sina kitu?”



    “Kwa hilo us'konde. Wewe nihakikishie kama unaweza kuzipata risiti hizo.”



    “Kuzipata sio tatizo. Nikikanyaga mtaa wa Samora au Mansfield tu, ninazo. Mshiko tu nd'o unahitajika hapa, mtu wangu.”



    “Ok, kesho amkia kazi hiyo,” Kamore alisema. “Lakini nakuomba sana uwe makini. Ukikamatwa usinitaje.”



    “Usihofu,” Samba alitamka kwa kujiamini. “Mimi ni mtoto wa mjini. Nadhani hunijui vizuri. Mimi sio yule Samba wa enzi za skuli.”



    “Poa. Nakupa siku mbili tu. Kuna elfu ishirini sasa hivi. Ukiniletea risiti mbili au tatu utakutana na ishirini nyingine.”



    Haikuwa kazi ngumu kwa Samba. Siku ya tatu jioni alimfuata Kamore nyumbani na kumkabidhi risiti tatu ambazo hazikutofautiana na zile za kampuni ya MP Brother's. Kamore alishangaa. Akazitazama kwa makini kisha akasema, “Sasa mambo yatatuendea vizuri. Tutatengeneza pesa ya kutakata.”



    *****

    WATEJA waliosafirisha bidhaa zao katika miji mbalimbali ndani na nje ya nchi kupitia kampuni ya MP Brother's walizilipia bidhaa zao katika ofisi ya Mweka Hazina, Kamore. Malipo hayo yalitofautiana kulingana na umbali wa safari na uzito au wingi wa bidhaa husika. Na katika kuwalipisha wateja wake ndipo alipofanya mbinu za kupata pesa za ziada. Kwa mfano, televisheni mia mbili zilizopelekwa Mwanza zikistahili kulipiwa shilingi milioni nne, yeye alitoza milioni mbili tu na kupewa laki tano taslimu kama 'asante' yake.



    Baada ya kupata zile risiti bandia siku iliyofuata mteja alikuja ofisini. Na kwa mara ya kwanza, kwa kutumia moja ya zile risiti bandia alifanikiwa kupata shilingi milioni mbili! Pesa zote zilizotakiwa kuingia kwenye mfuko wa kampuni, ziliingia mfukoni mwake. Akachekea moyoni, kicheko cha furaha. Muda mfupi baadaye akapata laki tano, na alipokuja mteja wa tatu akapata laki tano nyingine. Sasa hatua moja muhimu ilikuwa imekamilika. Kwa nini asifurahi? Aliamini kuwa kila kitu kitakwenda kama alivyopanga, na Suzana atafurahi.



    Ofisini hakukukalika tena. Mara tu mteja wa tatu alipoondoka yeye alizipaki pesa zile kwenye mfuko na kuondoka. Huyooo! Moja kwa moja nyumbani kwake.



    *****



    MZEE Kibua alipomwajiri Kisolwa na kumchunguza kwa muda wa miezi mitatu, hatimaye akawa na imani naye. Na hapo ndipo alipompa majukumu muhimu. Miongoni mwa majukumu hayo ni kulipia bidhaa zilizosafirishwa ndani na nje ya nchi. Hakujali kuziona risiti za malipo, mradi hakuna kilichoharibika, aliridhika na utendaji wa Kisolwa. Hakutambua kuwa Kisolwa naye alikuwa akinufaika kwa mbinu zake akishirikiana na Kamore.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku ambayo Kisolwa alikwenda MP Brother's kulipia marobota mia tatu ya mitumba kwa ajili ya kusafirishwa mkoani Mbeya, Mzee Kibua alikuwa amempa shilingi milioni 5 kiwango ambacho Kisolwa alidai kuwa ndicho kilichostahili. Alimpatia pesa hizo asubuhi, saa 2, na akamhimiza kushughulikia malipo hayo haraka iwezekanavyo.

    Hadi saa 6 mchana Kisolwa alikuwa hajarejea ofisini. Mzee Kisolwa akashangaa. Akasonya kwa hasira.



    Akaitwaa simu na kuishika katika mkono wa kulia. Sekunde mbili za awali alikuwa akiitazama simu hiyo. Sekunde ya tatu aligundua kuwa kile alichokihitaji kisingewezekana. Kisolwa hakuwa na simu! Ni juzi tu alipomtaarifu kuwa aliporwa simu yake na vibaka wakati akirejea nyumbani. Ni kumbukumbu hiyo iliyomfanya asonye kwa hasira, moyoni akijilaumu kwa kutomnunulia simu nyingine mara tu alipompa taarifa. Ni kipi kilichomchelewesha? Na kama kuna tatizo lolote si angetumia hata simu za vibandani? mzee huyo alijiuliza.



    Ilipotimu saa 7 Mzee Kibua alishindwa kuvumilia. Akaamua kupiga simu kwa Meneja Masoko wa MP Brother's Co. Ltd. Akampata. Katika maongezi yao ya awali ikabainika kuwa bado malipo kutoka kwa Mzee Kibua hayajawasilishwa hapo ofisini. Mzee Kibua hakukubali. Akawaka: “Siki'za meneja, unamfahamu vizuri yule kijana wangu?”



    “Namfahamu vizuri, mzee.”



    “Basi ni yeye niliyemtuma huko kwenu,” Mzee Kibua alisema. “Ametoka hapa saa mbili na dakika chache tu, asubuhi. Amekuja huko! Sasa ni saa saba na dakika kumi...!”



    “Lakini mzee,” meneja alizungumza kwa upole. “Ninachokwambia mimi ni kwamba, kumbukumbu za ofisi zinaonyesha kuwa hadi muda huu n'navyoongea na wewe hakuna mteja yeyote aliyetufikia. Huo nd'o ukweli, mzee.”



    “Haiwezekani meneja!” Mzee Kibua alimaka.



    Walizungumza kwa kirefu, na hatimaye Mzee Kibua akajenga hisia za kuibiwa. Na ndipo alipotoboa kila kitu, kwamba alimpa Kisolwa shilingi milioni tano za kulipia marobota mia tatu ya nguo za mitumba kwenda Mbeya. Ni kiwango hicho cha pesa kilichomshangaza meneja. Akaguna. “Kiwango halisi kilichopaswa kulipwa ni shilingi milioni moja na nusu tu!” hatimaye alisema simuni.



    Mzee Kibua alizidi kuchanganyikiwa. Kwa sauti yenye kigugumizi akauliza, “Lakini mbona mie kan'ambia kuwa mmemwambia kuwa ni milioni tano?”



    “Ni mie nd'o mkadiriaji, mzee,” Meneja alijibu. “Na leo sijamkadiria mtu yeyote! Lakini mzee, nakushauri usiwe na wasiwasi. Vuta subira kidogo. Nipe muda nilifuatilie suala hili. Huna haja ya kupaniki, mzee wangu.”



    *****



    MENEJA Utumishi wa MP Brother's Co. Ltd, Martin Peka, alishangaa pale alipomwona Meneja Masoko, Salum Amour akiingia ofisini mwake huku uso ukiwa umekunjamana.



    “Vipi?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kuna tatizo,” lilikuwa ni jibu la Salum.



    “Tatizo gani?”



    Ikafuata hadithi ndefu kuhusu ujio wa Mzee Kibua hapo ofisini sanjari na kile kilichobainika. Martin Peka akashangaa. “Kamore yupo?” aliuliza.



    “Hayupo. Na hajaniaga.”



    Martin Peka aliguna. “Kuna kitu hapa,” alisema na kugonga meza kwa kiganja cha mkono wa kulia. “Mpigie simu, aje haraka. Nahisi kuna mchezo mchafu uliochezwa hapa.”



    Salum alitwaa simu yake ya mkononi, akabonyeza tarakimu kadhaa kisha akaitega sikioni.



    *****



    AKIWA nyumbani kwake, Kamore alihisi mambo yamemwendea kama alivyotaka. Shilingi milioni tatu zilizokuwa kibindoni mwake zilikaribia kumtia wazimu. Sasa ikabakia kazi moja; kumpigia simu Suzana na kumtaarifu juu ya 'mzigo' wake. Na alifanya hivyo. Robo saa baadaye Suzana alifika hapo kwa Kamore na kukabidhiwa kile kitita cha pesa.



    Shilingi milioni tatu zikawa katika himaya ya Suzana!



    Ilikuwa ni aina fulani ya ndoto inayopendeza akilini mwa Suzana. Sasa kwa kiasi fulani akajisikia kumpenda Kamore, pendo la dhati lakini lililochanganyika na huruma.

    Ndiyo, alimhurumia lakini pia alimshangaa.



    Wachunguzi wa mambo hudai kuwa katika karne hii ya ishirini na moja wanaume wengi wamebadilika kitabia. Vichwa vyao vinatawaliwa na fikra za maendeleo ya kimaisha. Siyo rahisi kwa mwanamume kumpatia mwanamke kiasi hicho cha pesa, mwanamke asiye mkewe, maarufu kwa sifa ya 'hawara.' Wanaofanya kama alivyofanya Kamore, wengi wao huwa wameshajenga nyumba zao, wameshawasomesha watoto wao, na au wana miradi mikubwa inayowaingizia pato zuri kila kukicha.



    Wengine wenye utaratibu huo ni wale waliokwishaufukuza umaskini na kujitenga na kundi la 'wenye pesa'. Hao huwa kwenye daraja la utajiri. Wao, huwa tayari wanajiona kuwa wamekwishafanya kila kilichowastahili kukifanya katika kusaka maendeleo, hivyo kilichobaki ni kula raha za dunia. Na miongoni mwa raha hizo ni pamoja na kuchukua wasichana wadogo, kuhonga nyumba, gari na kadhalika na kadhalika.



    Siyo kwamba hawapo watu wa aina ya Kamore, watu ambao bado wamepanga vyumba uswahilini na hawana hata fikra za kujenga au kununua nyumba. Wapo, na hao huziendekeza anasa, wakinywa pombe kwa wingi, wakibadili wanawake kwa fujo huku wakidiriki kuwanunulia hawara zao nyumba au viwanja. Watu wa aina hiyo hujiona kuwa ni wajanja na wanayaweza maisha.



    Katika mtaa alioishi Kamore, wakazi wengi hususan vijana wenzake hawakumwona yu mjanja. Zaidi walimchukulia kuwa ni limbukeni au juha. Hata hivyo waliishia kumshangaa tu na kufumba vinywa vyao mbele yake au mbele ya wale waliomtukuza, huku wakati wakiwa peke yao humcheka na kumsikitikia, baadhi yao wakimhurumia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Miongoni mwa waliomhurumia ndiye huyu Suzana ambaye hata hivyo huruma yake haikudumu sana moyoni mwake, mara ikayeyuka. Kilichochukua nafasi ni kufurahia pato. Hakuiona sababu ya kuendelea kukisumbua kichwa chake kwa kumhurumia, kumshangaa au kumsikitikia Kamore huyu ambaye, zaidi alimchukulia kama 'bwege.'

    Wala hakuona kama ilimpasa kuhoji au kujiuliza ni vipi pesa hizo zimepatikana haraka kiasi hicho.



    Hayo hayakumhusu. Yaliyomhusu ni jinsi ya kumfanya Kamore ajione yu mfalme kwa kulitekeleza hili la kumpatia pesa, na jinsi ya kuzitumia pesa zenyewe. Atazitumia vipi, hilo lilikuwa ni juu yake, halikumhusu Kamore hata chembe.



    “Sijui nikushukuru vipi,” hatimaye Suzana alimwambia Kamore. “Nadhani sina neno la kutosha katika shukrani zangu. Lakini nitakushukuru. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote, kwa akili yangu yote na kwa viungo vyangu vyote. Na ninaamini utazipokea shukrani zangu kwa moyo mkunjufu. Utakuja jioni?”



    “Yeah, nitakuja.”



    “Saa ngapi?”



    “Tatu usiku.”



    “Ok, nitakusubiri,” Suzana alisema. “Utanikuta nikiwa tayari kukupa shukrani zangu za dhati. Na ninaamini utazipokea kwa nguvu zote na mbinu zote.”



    Suzana alinyanyuka, akatoka huku akiachia tabasamu la mbali, akilini mwake akiamini kuwa siri ya mafanikio hayo ni mwili wake, alioutumia kama ngao dhidi ya wanaume bahili na utaalamu alioutegemea kama silaha au sumaku ya kuwanasa 'wenye nazo' na wenye uchu wa wanawake warembo.



    *****



    SIMU ya Kamore ilipoita ndiyo kwanza alikuwa anatoka nyumbani baada ya kumkabidhi Suzana zile pesa. Kichwani mwake alikuwa akimwaza Suzana tu. Na kwa mara ya kwanza alijikuta akiwa na fikra za kumwoa. Awe mkewe wa ndoa na hivyo kumletea heshima mitaani.



    Ni mawazo hayo yaliyomfanya asahau kuitoa simu mfukoni hadi ikakatika. Lakini haukupita muda mrefu mara ikaita tena. Safari hii akaitoa haraka ma kuitazama. Akashtuka. Akawaza, aipokee au aiache iite hadi itakapokatika tena, na ikishakatika aizime kabisa. Hata hivyo wazo la kuizima liliota mbawa ghafla baada ya kutafakari na kuona kuwa kitakuwa ni kitendo kitakachotafsiriwa na mpigaji kuwa ni uhuni. Akabonyeza kitufe cha kupokelea na kuitega sikioni.



    Muda mfupi baadaye aliirudisha mfukoni. Akaifuata teksi huku kakunja uso. Kwa mbali matone ya jasho yalijiunda katika paji la uso wake. Hakuwa timamu kimawazo. Hakutegemea kupigiwa simu kutoka ofisini, tena kupigiwa na Meneja Masoko, Salum Amour. Alihisi kuna jambo zaidi ya jambo, jambo lisilo la heri. Akayatafakari maswali ya Meneja Masoko, maswali aliyoyauliza kwa sauti kali: “Uko wapi? Mbona hukuaga?” Na kisha ikafuata amri: “ Njoo haraka ofisini. Zisizidi dakika kumi hujafika! Vinginevyo...”



    Ulikuwa ni wito ulioonyesha bayana hatari iliyo mbele yake. Lakini afanye nini? Hakuwa na budi kuitekeleza amri hiyo. Na alifanya hivyo.



    *****

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    HII ilikuwa ni Wiki ya Usalama Barabarani. Jiji la Dar es Salaam lilikuwa na patashika zilizowahusu madereva wa vyombo vya moto. Kisolwa alikuwa miongoni mwa waliokumbwa na kashkash hiyo. Wakati alipotoka MP Brother's huku akiendesha gari dogo, jekundu aina ya Toyota Mark 11 mali ya Mzee Kibua, alikumbana na askari kabla hajafika ofisini.



    Alipoombwa leseni yake, 'akajiumauma.' Aliachiwa baada ya saa tatu huku akipewa onyo kali. Alipofika kwa bosi wake hakupata ukaribisho wa kawaida. Mzee Kibua alionyesha dhahiri kukasirika. Hata hivyo alipoulizwa kuhusu kuchelewa kwake alijitetea kwa kisingizio cha 'Wiki ya Usalama Barabarani.' “Trafiki walinikamata, na wamenisumbua sana,” alijitetea. “Wamegundua kuwa indiketa moja ya nyuma, kushoto haifanyi kazi. Isitoshe, bima imekwisha muda wake. Kwa kweli palikuwa hapatoshi. Wameniachia muda si mrefu baada ya kuwabembeleza sana. Na hata hivyo trafiki mmoja amesema baadaye nikamwone.”



    Mzee Kibua alikohoa kidogo. Hakuonyesha kujali alichoambiwa na Kisolwa. Akatupa macho darini kisha akamrudia Kisolwa na kumwambia kwa sauti ya chini, “Nipe risiti.”

    Kisolwa alitoa risiti mfukoni na kumpatia. Mzee Kibua aliitazama stakabadhi ile kwa makini kisha akaachia tabasamu dhaifu, tabasamu ambalo machoni mwa Kisolwa lilidhihirisha kuwa ni la dhihaka. Na tabasamu hilo halikudumu, alilikata ghafla na kumtazama Kisolwa kwa macho makali.



    “Kisolwa,” hatimaye alimwita kwa sauti nzito, ya chini na yenye kijimkwaruzo cha mbali, sauti iliyomfanya Kisolwa ahisi kuwa sentensi itakayofuata haitakuwa ya kawaida wala nzuri kwa upande wake.



    Mzee Kibua hakusubiri kuitikiwa. Aliendelea, “Nilikupa shilingi ngapi?”



    “Milioni tano, mzee,” Kisolwa alijibu kwa ujasiri wa kulazimisha.



    “Umelipa shilingi ngapi?”



    “Milioni tano.”



    “Kwa kusafirisha mizigo kwenda wapi?”



    “Mbeya.”



    “Na tumesafirisha mizigo ya aina hii mara ngapi kwenda Mbeya?”



    “Mara nne, mzee.”



    “Na tumekuwa tukilipia shilingi ngapi kila tunaposafirisha?”



    Kisolwa alikumbwa na kigugumizi, sauti ikagoma kutoka.



    “Ulikuwa ukisema malipo ni shilingi milioni tano. Bisha!”



    Bado Kisolwa alikuwa hana kauli ya kujibu.



    “Haya hii risiti ni ya shilingi ngapi?” Mzee Kibua alizidi kumbana, safari hii akiuinua mkono na kuining'iniza risitii hiyo, akiishika kwa ncha za vidole vya shahada na gumba. “Ni ya shilingi milioni tano au milioni mbili na nusu?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Bado kinywa cha Kisolwa kilikamatwa na gundi. Ajibu nini? Ni kweli kuwa risiti ilionyesha kuwa amelipa fedha taslimu shilingi 2,500,000 tu na siyo 5,000,000 alizopewa na Mzee Kibua. Ndipo upekuzi wa kina ulipofanyika. Mzee Kibua akaamua kuzichunguza nyaraka zote zilizohusiana na malipo yaliyopita. Kila jalada likachunguzwa. Siri ikafichuka!



    Risiti zote zilizopita zikauweka bayana ujanja uliotumiwa na Kisolwa katika kujipatia pesa za ziada kwa njia ya udanganyifu. Mzee Kibua alishindwa kuamini mara moja, na ilipotokea akaamini, kwa mbali alijikuta akitetemeka kwa hasira. Alimtumbulia macho Kisolwa mithili ya atazamaye mzimu au chochote kile kishangazacho na kuogofya. Na wakati huo alijiuliza ni hatua gani iliyostahili kuchukuliwa dhidi ya Kisolwa. Ampeleke kituo cha Polisi? Amtie risasi ya kichwa? Au amfukuze kazi?



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog