Search This Blog

Monday, October 24, 2022

JICHO LA KAMORE - 5

 





    Chombezo : Jicho La Kamore

    Sehemu Ya Tano (5)



    Swali la kwanza lilipata pingamizi. Kumpeleka Kisolwa, Polisi moja kwa moja hakuona kuwa ingesaidia. Kule watampokea kama mtuhumiwa 'fulani.' Ataswekwa ndani. Kitakachofuata ni Mzee Kibua kuandikisha maelezo akiwa ni mlalamikaji. Baada ya hapo ni kesi mahakamani. Na hapo ndipo Mzee Kibua atalazimika kwenda mahakamani mara kwa mara kufukuzana na kesi hiyo. Kwake, hiyo ingekuwa ni kero nyingine. Hakuwa tayari kusumbuana na makarani wa mahakama kwa kufuatilia kesi ya ubadhirifu wa kitu kama shilingi milioni mbili au tatu. Akalitupilia mbali wazo hilo.



    La pili, pia aliona kuwa ni wazo baya na litakalomtia matatizoni. Lilikuwa ni jambo rahisi sana kulitekeleza. Muda wote hutembea na bastola aliyoipata kwa taratibu zote za kisheria. Isingekuwa vigumu kwake kuichomoa na kushindilia risasi moja kichwani mwa Kisolwa kabla hajajipeleka polisi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ingewezekana, lakini matokeo ya kufanya hivyo yangemzulia usumbufu mwingine, na labda pia angejikuta akipoteza fedha nyingi kwa kuwapa 'askari njaa' ambao wangemwahidi kumwokoa na kesi ya kuua kwa kukusudia au kutokukusudia. Fedha ambazo angetoa huenda zingezaa mafanikio au angekuwa ni kama vile amezitupa chooni. Lakini hakutaka kubahatisha, hivyo, wazo hilo nalo akaliweka kando. Halikuwa na uzito wowote.



    Wazo la tatu ndilo angalau lilipata uzito kidogo. Lakini alipolitafakari kwa kina akaona kuwa kumfukuza kazi Kisolwa haitakuwa dawa ya kumtibu maradhi hayo yaliyokwishamvaa, maradhi ya kukosa uaminifu kazini. Hivyo aliamua kuondoka naye hadi katika ofisi za MP Brother's Co. Ltd sanjari na risiti hiyo na nyingine za siku zilizopita.



    *****



    “KUNA mteja yeyote uliyemhudumia leo?” lilikuwa ni swali lililotumika kama ukaribisho kwa Kamore wakati alipoingia ofisini kwa Meneja Utumishi, Martin Peka.

    Haikuwa ni ile sauti ya Martin Peka ambaye Kamore alimfahamu. Na ni hapo alipohisi kuwa mambo yameharibika; mpango wake umegundulika, mpango uliomwingizia shilingi milioni tatu za chapchap. Alimtazama kidogo Martin Peka kisha akayahamishia macho kwa Meneja Masoko, Salum Amour aliyekuwa akimtazama kwa namna ya kumsuta.



    “Zungumza,” hatimaye Salum alimshtua.



    Aseme ukweli au awaongopee? Kamore alijiuliza. Aliamini kuwa kuwaongopea itakuwa ni sawa na kujipalia mkaa wa moto. Ni dhahiri kuwa hawa wakuu wake wa kazi wameshang'amua kila kilichofanyika kati yake na Kisolwa. Lakini, pamoja na kuamua kukiri kuwa kuna mteja aliyekwishafika siku hiyo, hata hivyo hakuwa tayari kutoboa ukweli kuwa alimhudumia.



    “Ndio, kuna mteja mmoja alikuja,” alijibu.



    “Ukamhudumia?” Martin Peka alimwuliza.



    “Hapana.”



    “Kwa nini?”



    “Alikuwa na upungufu wa malipo.”



    Salum na Martn walitazamana, wakacheka, vikiwa ni vicheko vilivyomdhihirishia Kamore kuwa ni vya dhihaka.



    “Kamore, umenyea kambi,” Salum alimwambia. “Jitahidi kuzungumza ukweli mtupu. Vinginevyo, endapo tutalazimika kumleta mteja huyo, na akatupa maelezo tofauti na ya kwako, utakuwa umejiweka katika mazingira magumu zaidi. Tafadhali, zungumza kitu kinachoeleweka.”



    Ulikuwa ni mtihani mgumu kwa Kamore. Hawa wakuu wake wa kazi alikuwa akifanya nao mipango hii mara kwa mara na kugawana mapato kwa viwango vilivyolingana. Lakini huu wa leo hakumshirikisha yeyote kati yao. Aliamini kuwa hiyo ni sababu kuu iliyowaudhi. Na tayari pesa zote zilishatua kwa Suzana. Afanye nini? Mbele kulikuwa na simba mwenye njaa, nyuma aliandamwa na nyati aliyejeruhiwa!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    *****



    MZEE Kibua alizima gari lake nje ya ofisi za MP Brother's dakika kumi tu baada ya kutoka ofisini kwake. Kisha akamwamuru Kisolwa kuteremka. Wakafuatana kuingia ndani ya ofisi hizo. Muda mfupi baadaye walikuwa mbele ya Katibu Muhtasi wa Meneja Masoko.



    “Una miadi naye,” Mzee Kibua aliulizwa.



    “Hapana, lakini mimi ni mteja wenu mkubwa,” Mzee Kibua alijibu.



    “Jina?”



    “Bwana Kibua. Mara kwa mara na kodi magari yenu kwa kusafirisha bidhaa mbalimbali mikoani.”



    Yule katibu muhtasi alinyanyua simu na kuzungumza kidogo kisha akaitua na kumwelekeza Mzee Kibua mlango wa Meneja Utumishi huku akiongeza, “Meneja Masoko yuko hukohuko kwa Meneja Utumishi.”



    Mzee Kibua alitoka. Mguu kwa mguu hadi kwenye ofisi hiyo. Ndani humo kulikuwa na Meneja Utumishi Martin Peka, Meneja Masoko Salum Amour na karani wa hesabu, Kamore Bulungutu. Mzee Kibua alipoingia alikaribishwa kiti hali kadhalika, Kisolwa.

    Kilichofuata ni salamu kisha kutambulishana. Wakati huo mapigo ya moyo wa Kamore yalizidisha kasi. Kumwona tena Kisolwa hapo, Kisolwa ambaye usoni alionesha bayana kukumbwa na taharuki, kwake ilikuwa taswira nyingine kuwa mambo yameharibika.



    Hatimaye, baada ya Mzee Kibua kuketi, aliwatazama wengine kwa zamu, kabla hajayatua kwa Meneja Masoko, na kumwambia, “Niliona kuwa itakuwa busara kuja moja kwa moja kuonana ana kwa ana badala ya kuchukua hatua za haraka kuripoti polisi. Kwa bahati nzuri, baada tu ya kukupigia simu huyu kijana wangu alifika ofisini.”



    Ukimya mfupi ukatanda ofisini humo. Wakati huo Mzee Kibua alikuwa akifunua jalada lake alilokuja nalo. Muda mfupi baadaye akaliweka mezani likiwa wazi. “Hizi ndizo risiti zote nilizokwishalipia hapa ofisini kwenu,” alisema huku akiwatazama wote kwa zamu. Akaendelea, “Hizi nne ni za siku za nyuma, na hii hapa ni ya leo. Nashangaa Meneja Masoko unaniambia eti hakuna malipo yoyote yaliyofanyika leo kutoka kwangu. Kwa kweli kauli yako imenishangaza sana.”



    Meneja Masoko, Salum Amour aliguna. Kisha akalitwaa jalada hili la Mzee Kibua na kuzitazama kwa makini nyaraka zilizomo. Kwa mara ya pili akaguna. Akamsogezea Meneja Utumishi jalada hilo. Naye akazitazama lakini hakutoa mguno wowote. Kwa ujumla, hitilafu za risiti zote nne za nyuma hazikuwa ngeni kwao, Salum na Martin. Walihusika! Walishiriki katika kuzitengeneza hitilafu hizo kwa kuchapisha vitabu bandia vya risiti.

    Lakini hii risiti ya mwisho ndiyo iliyozua utata. Hawakuitambua! Siyo tu kutoitambua kama risiti, la hasha. Ilikuwa ni risiti kama risiti hizo nne za siku za nyuma. Kutoitambua kwao ni kwa kutohusishwa katika mgawo. Waliamini kuwa kuna mzunguko haramu uliowapitia. Kamore kawazidi ujanja!



    Mara Salum akamwamuru Kamore alete vitabu vyote vya risiti. Dakika tano baadaye Kamore akawa amevileta. Uchunguzi wa kina ukafanyika. Ndipo tofauti ya nambari za risiti halisi na ile ya bandia ilipobainika. Kosa hili halikuwa kosa wakati Kamore alipokabidhiwa risiti na Samba. Ilivyotokea ni kwamba wale 'wajanja' waliozitayarisha risiti tatu za bandia hawakuona kuwa itakuwa busara kutumia nambari za ile risiti halisi waliyopewa. Walichofanya ni kupachika nambari walizoona kuwa zinafaa. Na ni hilo lililozibua ya kuzibuka ofisini humo.



    Meneja Masoko alimtolea macho Kamore na kumwuliza, “Hii ni risiti ya wapi?”



    Hakukuwa na jibu lolote.



    Bila ya kutarajia, Kamore na Kisolwa wakatazamana, macho ya Kisolwa yakiwa kama vile yanamwuliza Kamore, imekuwaje? na ya Kamore yakimhoji Kisolwa tufanye nini? Walikuwa kwenye wakati mgumu.



    Meneja Masoko, Salum Amour na mwenzie, Meneja Utumishi, Martin Peka waligeuka mbogo. Wakambana vilivyo Kamore kuhusu ile risiti bandia. Nyusoni na katika kauli zao walionekana kuwa walikuwa wakitekeleza majukumu ya kazi lakini kumbe, mioyoni mwao walikuwa na uchungu na hasira kwa kuwa tu Kamore alifanya mpango ule peke yake, bila ya kuwashirikisha, na zaidi, alikula peke yake!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa upande wa pili, Mzee Kibua naye alihamaki baada ya kubaini kuwa risiti aliyopewa na Kisolwa ilikuwa bandia. “Mambo haya yatamalizikia polisi!” alibwata huku akinyanyuka kitini. “Siwezi kukubali kugeuzwa bwege na mtu niliyemlea na kumwamini kama mwanangu! Hapana! Haiwezekani! Sikubali! Ni polisi tu!”



    Salum na Martin walimtazama kidogo Mzee Kibua kisha Martin akamwambia, “Usemayo ni sahihi, mzee. Lakini subiri kidogo.”



    “Nisubiri nini?”



    Hakuna aliyemjibu. Martin alishamgeukia Kamore na kwa sauti kali lakini ya chini, alisema, “Hii nd'o nafasi yako ya mwisho. Una la kutuambia?”



    Kimya!



    Kamore aliinamisha uso chini, fikra zake zikiwa kwa Suzana, mwanamke aliyetokea kuuteka vilivyo moyo wake. Kwa wakati huo, ile asali ambayo aliionja na kuiona tamu kuliko ilivyo, sasa aliiona imebadilika ladha. Ilikuwa na ladha ya shubiri!



    Afanye nini?



    *****



    WAKATI Kamore akijiona kuwa anakabiliana na moto wa jehanamu, Suzana alikuwa nyumbani, chumbani mwake akianza kuuangalia mkanda wa video, mkanda ambao kama hautapishi basi unachefua machoni mwa mstaarabu yeyote. Ulikuwa ni mkanda wa filamu ya ngono, filamu ambayo washiriki wake ni kama vile walikuwa wamepagawa kwa vitendo walivyokuwa wakivifanya.



    Ni majuzi tu Suzana alipoununua mkanda huo. Na aliununua kwa dhamira ya kupata nyongeza ya kile atakachopaswa kumfanyia Kamore pindi atakapolitekeleza hili alilolitekeleza. Zoezi hilo la kuuangalia mkanda alilifanya kwa umakini wa hali ya juu, akifuatilia kila hatua ya kila lililofanyika katika filamu hiyo. Kuna baadhi ya mitindo ambayo aliwahi kuapa kuwa kamwe asingeitumia maishani mwake. Ilikuwa ni mitindo iliyomtisha na kumchefua. Lakini, tangu alipoununua mkanda huu amekuwa makini kuifuatilia, moyoni akiwa ameshadhamiria kuwa jioni ya siku hiyo, pindi Kamore atakapokuja, mitindo hiyo ndiyo ipewe kipaumbele katika starehe yao.



    Ndiyo, alitaka kumdhihirishia Kamore kuwa yeye si kwamba ni mwanamke mrembo hadharani tu bali pia ni bora hata chumbani.



    Walikubaliana kuonana saa 3 usiku, lakini muda huo ulifika na kuzidi dakika 30, Kamore hajatokea.



    “Atakuwa wapi bwege huyu?” alijikuta akinong'ona na kufuatisha msonyo mkali.

    Wakati huo alikuwa ameketi sofani, chupa ya soda ikiwa kando yake, akishusha kooni mafunda mawili, matatu kila baada ya dakika chache. Punde akaachia tabasamu la mbali. Alimkumbuka dada yake, Martha. Ni juzi tu walipomzungumzia Kamore, na Martha akampa wazo la kumkamua pesa za kutakata. Na alimkamua. Pesa zenyewe tayari anazo katika himaya yake. Shilingi milioni tatu!



    Tangu alipokamata pesa hizi, hajawasiliana na Martha. Mara akatwaa simu yake ya mkononi na kulisaka jina la Martha. Alipolipata, akampigia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Vipi dogo langu?” sauti ya Martha ilipenya sikioni mwa Suzana.



    “Shwari tu, mbona kimya?”



    “Ni kawaida tu, dogo langu. Mihangaiko inaniacha hoi.”



    Ukimya wa sekunde chache ukapita kisha Martha akawa tena hewani, “Enhe, inakuwaje na yule bwege wako?”



    “Mbona shwari! Mambo tayari!”



    “Kweli?!” sauti ya Martha ilijaa mshangao. “Una maana kishakujaza mshiko?”



    “Nd'o maana 'ake.”



    “Kiasi gani?”



    “Tatu.”



    “Tatu... una maana...” Martha alisema kwa kusitasita.



    “Em tatu, shosti!”



    “Weee! Yaani milioni tatu!”



    “Sa' kumbe,” Suzana aliilegeza sauti yake na kuweka mikogo ya dharau. “We ulidhani elfu tatu? Nyoo! Mie ni chizi wa kupokea shombo hiyo? Alfu tatu ni za kumpa baba yake au mama yake, s'o mimi, shosti! Nimemkamua!”



    “Usin'tanie Suzy.”



    “Kwa nini nikutanie dada?”



    “Eh, hongera zako basi.”



    “Asante dada,” Suzana alijibu kwa utulivu. Kisha akaongeza, “Sasa kesho uje tupange mambo f'lani f'lani.”



    “Kesho, saa ngapi?”



    “Sema wewe.”



    Martha alifikiri kidogo kisha akajibu, “Saa kumi jioni. Sawa?”



    “Poa tu.”



    “Ok, bye.”



    “Bye.”



    Baada ya hapo Suzana hakutulia. Sasa aliamua kumpigia Kamore. Hakumpata! Ilikuwa ni ama Kamore kazima simu au kaporwa na vibaka. Suzana aliwaza hivyo. Haikuwa kawaida kupita saa nzima bila ya Kamore kumpigia. Mara kwa mara alimpigia au kumtumia ujumbe wa maandishi. Lakini siku hii, tangu walipoachana kule nyumbani kwa Kamore baada ya kukabidhiwa kitita cha pesa, hakukuwa na cha kupigiwa smu au kutumiwa ujumbe wowote. Suzana alishangaa.



    Saa nne ikagota!



    Saa tano!



    Mtoto wa kike akachoka. Akaamua kuzima taa, akalala. Alikuja kuzinduka saa 8, usiku huohuo na kutazama simu aone kama kuna simu yoyote iliyopigwa, na zaidi akitarajia kukuta ni Kamore aliyepiga. Wapi! Ilionyesha kuwa hakuna yeyote aliyempigia. Hata Kamore! Na hadi mapambuzuko hakukuwa na sura ya Kamore iliyoonekana hapo wala mawasiliano yoyote baina yao.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alibaki kitandani akigaragara huku akijiuliza ni kwa nini Kamore awe mkimya tangu alipompatia kitita kile cha pesa? Au alikuwa anamtega? Na kwa nini amtege? Mbona alionekana kuwa na uchu mkubwa kabla ya hapo? Anaumwa? Kapata ajali ya gari? Ka...ka...



    Alijiuliza maswali mengi na yote hayakupata majibu. Akatupa macho kwenye televisheni. Akaupeleka mkono kwenye stuli kisha akaitwaa 'rimoti' na kuiwasha televisheni. Ilikuwa ni saa 12.00 asubuhi. Akaweka stesheni fulani iliyokuwa ikitangaza taarifa ya habari. Hakuifuatilia taarifa hiyo lakini kilipofika kipindi cha kupitia vichwa vya habari vya magazeti ndipo aliposhtuka na kutega sikio vizuri, macho kayatumbua kwenye kioo cha televisheni. Ndipo pia aliposikia kuwa Kamore na mtu mwingine walikamatwa na Polisi kwa tuhuma za kughushi nyaraka za kampuni ya MP Brother's na kujipatia mamilioni ya pesa isivyo halali.



    Ilikuwa ni habari ya kumshtua Suzana. Ilimshtua, ikamshangaza lakini haikumhuzunisha. Kwa nini ahuzunike? Kwa nini ahuzunike ilhali alichokihitaji kwa Kamore ameshakipata? Akifungwa jela hiyo ni shauri yake, akipona katika kesi hiyo, heri yake.

    “Atajiju,” alinong'ona huku akitwaa simu yake na kulisaka jina la dada yake, Martha. Muda mfupi baadaye alikuwa akimtaarifu Martha juu ya habari hiyo.



    “Hee! Yamekuwa hayo tena?” Martha alimwuliza kwa mshangao.



    “Nd'o 'ivo shosti.”



    Mara msonyo mkali ukapenya masikioni mwa Suzana. Martha huyo! “Bwege yule! Achana nae. Mradi wewe nyota ya jaha imeshakushukia, basi mfute akilini mwako. Mwache aubebe msalaba wake. Atakapochoka ataanza kukubembeleza kwa kukuimbia..Nibebe..nibeebe...”



    Wakacheka kwa mkupuo, vicheko vilivyodhihirisha kutokuwa na uchungu wowote kufuatia taarifa ya Kamore kutiwa mbaroni.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog