Chombezo : Facebook Chatting
Sehemu Ya Tatu
(3)
Ilipoishia
nikaamka
na kisha kuangalia kioo cha simu ile, namba haikuwa imehifadhiwa simuni lakini
kwa kuiangalia tu, nilikuwa nikiijua, ilikuwa ni namba ya Juliet. Huku
nikionekana kuwa katika uchofu, nikabonyeza kitufe cha kijani na kisha kuipeleka
sikioni.
Songa nayo
sasa....
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
JULIET:
Mambo Nyemo!
MIMI: Poa. Mzima wewe?
JULIET: Mimi mzima. Upo
wapi?
MIMI: Nyumbani.
JULIET: Njoo basi hapa uwanja wa
ndege. Nimekwishafika, nataka unipeleke hotelini.
MIMI: (Kitu cha
kwanza, usingizi wote pamoja na uchovu nilio nao vikatoweka, Juliet alikuwa
amefika mkoani Kagera kwa ajili ya kuja kuonana nami, nilishtuka, nikaanza
kujihukumu kwa kujiona kwamba nilikuwa nimemdanganya kwamba naishi Kagera kumbe
ukweli ni kwamba nilikuwa naishi Dar es Salaam alipokuwa akiishi. Katika kipindi
hicho, sikujua nimjibu nini zaidi ya kukaa kimya huku mwili nikiuhisi umepigwa
na ganzi)
JULIET:
Haloooow......!
Bado nilionekana kuchanganyikiwa
kupita kawaida, kitendo cha Juliet kufika ndani ya mkoa wa Kagera ndicho
kilikuwa kitu ambacho kilinichanganya sana. Nilibaki kimya huku nikikipa kichwa
changu nafasi zaidi ya kufikiria juu ya kile ambacho nilitakiwa kumwambia kwa
wakati huo. Juliet aliendelea kuita zaidi na zaidi huku nami nikijifanya kama
kutokusikia, tayari nilikuwa sipo sawa
kichwani.
JULIET: Mbona haunijibu chochote
Nyemo?
MIMI: Ninaogopa kukukasirisha.
JULIET:
Kivipi?
MIMI: Nilikudanganya.
JULIET: Ulinidanganya?
Kunidanganya nini?
MIMI: Kwamba nilikuwa nikiishi Kagera, ila ukweli
ni kwamba siishi huko.
JULIET: Thats too bad Nyemo. Kwa nini
umenidanganya hivi mpaka kuharibu fedha na kuja huku? Kwa nini umenidanganya
Nyemo?
MIMI: Samahani.
JULIET: Unafikiri itasaidia chochote
kile Nyemo?
MIMI: Hapana. Ila naomba unisamehe.
JULIET:
Nikusamehe kwa hili ulilonifanyia Nyemo? Kupoteza zaidi ya laki sita na nusu kwa
hili ulilonifanyia Nyemo?
MIMI: (Kimyaa)
JULIET: Sawa mkali
wangu, nimekuelewa. Naomba uniambie ukweli sasa. Upo wapi?
MIMI: Nipo
Dar es Salaam.
JULIET: Unaishi wapi?
MIMI: Naishi
Tandale.
JULIET: Nitapanda ndege leo jioni kuja huko, nitataka kuonana
na wewe.
MIMI: Sawa (Simu
ikakatwa)
Kwanza nikashusha pumzi ndefu na kisha
kuanza kujutia kile ambacho nilikuwa nimekifanya. Nilijua dhahiri kwamba Juliet
alikuwa akinipenda sana lakini sikuwa na jinsi, kwa wakati huo moyo wangu
ulikuwa kwenye majonzi mazito na nilidhani labda katika kipindi ambacho
ningemuona Juliet katika macho yangu na kisha kumuomba msamaha face to face
ndicho kingekuwa kitu ambacho kingenifanya kuwa na amani moyoni
mwangu.
Saa kumi na moja jioni, simu yangu ikaanza kuita,
nilipoangalia namba, ilikuwa ni ya Juliet. Mapigo yangu ya moyo yakaanza kudunda
kwa kasi, nilikuwa na maswali mengi kichwani mwangu juu ya Juliet huyu, nikapiga
moyo konde na kisha kuipokea.
MIMI:
Hallooow
JULIET: Hallow.
MIMI: U mzima?
JULIET:
Mzima tu. Upo wapi?
MIMI; Nipo nyumbani. Umeshafika
Dar?
JULIET: Tayari nimekwishafika. Nataka kuja kwenu sasa hivi.
Nitafikaje hapo?
MIMI: Upo wapi?
JULIET:
Nyumbani.
MIMI: Wapi?
JULIET: Osterbay.
MIMI:
Sawa. Cha msingi nenda kituoni na kisha upande daladala inayokwenda Ubungo
kutoka Msasani au Masaki.
JULIET: Hapana Nyemo. Nakuja na gari langu
binafsi.
MIMI: Okey! Kama ni hivyo njoo hapa Morocco ya Magomeni, si
unapajua?
JULIET: Ndio.
MIMI: Ukifika hapo si kuna barabara
inaelekea Sinza?
JULIET: Ndio.
MIMI: Njoo na hiyo
barabara.
JULIET: Sawa. Nipe dakika ishirini (Simu
ikakatwa)
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikabaki nikiwa na
presha kubwa. Katika presha ambayo nilikuwa nayo kwa wakati huo ni sawa na
shabiki wa mpira wa miguu ambaye alikuwa akienda kuiangalia timu yake
inayotarajia kucheza na timu ambayo ina uwezo mkubwa zaidi ya timu yake.
Nilibaki nikiwa sijui nifanye nini. Kitu cha kwanza ambacho nilikuwa
nimekifikiria ni kuanza kufanya usafi wa kizushi chumbani
kwangu.
Kwa wavulana watakuwa wanaelewa uharaka
ambao anakuwa nao mvulana wa kufanya usafi mara msichana anaposema nipo njiani
nakuja kwenu. Kila shuka ambalo nilikuwa nikilitandika kitandani nilikuwa
naliona chafu, yaani hata shuka ambalo nilikuwa nimelifua jana yake nalo
lilikuwa likionekana chafu.
Nilichokifanya ni
kuchukua shuka jingine ambalo kwa kidogo sana lilikuwa likipendeza machoni
mwangu na kisha kulitandika. Nikafagia chumba haraka haraka, nikafuta vumbi,
nikachukua air freshner na kisha kuipulizia chumba kizima na kufunga pazia ili
kuifanya harufu ile isitokea nje na kuisha. Nilipoona kila kitu kipo poa,
kandambili zangu za kuendea chooni na bafuni nikazitupia uvunguni pamoja na
ufagio wangu wa chelewa.
Baada ya kila kitu,
nikaanza kukiangalia chumba kile, bado sikuridhika kabisa. Nikaelekea chumbani
kwa kaka yangu na kisha kuchukua mito na kuipeleka kitandani kwangu, viatu
ambavyo vilikuwa vimekaa ovyo ovyo nikavitupia chini ya uvungu wa
kitanda.
Kwa maandalizi ambayo nilikuwa
nimeyafanya, Juliet kwangu akaonekana kama malkia ambaye alikuwa akija
kunitembelea siku hiyo. Nilipoona kila kitu kimekaa sawa, nikatulia nikiwa
nimekaa sakafuni kwani kama ningekaa kitandani, ningeweza kulivuruga shuka lile
na kujikunja jikunja. Wala hazikupita dakika nyingi, simu yangu ikaanza kuita,
nilichokifanya ni kuipokea.
JULIET: Nimefika hapa
wanapaita Kwa Tumbo.
MIMI: Okey, Pandisha hicho kilima cha juu mpaka
huku mwisho.
Bado nilikuwa nikiendelea kumpa
maelekezo Juliet mpaka pale ambapo macho yangu yakaanza kuiona gari aina ya X
Trail fulani ya Bluu ambayo ilikuwa ikija kwa mwendo wa taratibu. Kwa sababu
alikuwa amekwishaniambia kwamba angekuwa ndani ya gari hilo, nilipoona
limekaribia, nikalisimamisha kwa kupunga mkono na kisha Juliet kufungua kioo cha
mlango wa mbele.
Naomba nieleweke jamani....kwa
hapa ningependa nieleweke na watu wote mnielewe kwa umakini kabisa.
Yaani....yaani....yaani.....Mmmh! Kiukweli ni kwamba kwa miaka ishirini na tatu
na nusu ambayo nimeishi katika dunia hii nimekutana na wasichana wengi warembo
ila kwa huyu Juliet ambaye nilikuwa nikimwangalia, alionekana kuwa
zaidi.
Juliet alikuwa mrembo, tena mrembo zaidi ya
warembo ambao niliwahi kukutana nao katika maisha yangu yote. Nilibaki
nikimwangalia Juliet, Mungu wangu! Alikuwa mrembo hasa tena zaidi ya mrembo.
Kama watu wanavyosema kwamba Malkia wa Misri, Cleopatra alikuwa mrembo zaidi ya
wanawake wote wa duniani mpaka sasa, ila nafikiri mtu ambaye aliyesema hayo
hakuwa amemuona Juliet, msichana huyu alikuwa mrembo sana kiasi ambacho sikuwa
nikiishiwa kumsifia.
JULIET: Vipi! Mbona
unanishangaa hivyo?
MIMI: Wewe ndiye Juliet?
JULIET: Ndiye
mimi.
MIMI: Ndiye ambaye ulikuwa umesafiri kuelekea Kagera
kunifuata?
JULIET: Ndiye mimi.
MIMI: Hapana. Wewe ndiye
ambaye nilikuwa nimekuficha kwamba sikai Dar es Salaam?
JULIET: Ndiye
mimi.
MIMI: Kweli wakati mwingine unaweza kujiona una akili kumbe ni
mburula kabisa.
JULIET: Kivipi?
MIMI: Mimi ni Mburula...tena
kiongozi wa mamburula wote duniani. Haiwezekani nikudanganye mtu kama
wewe.
JULIET: Kwa nini?
MIMI: Dah! Twende nyumbani
kwanza.
Juliet akateremka kutoka garini. Kwanza
watu wote ambao walikuwa pembeni na mahali pale wakaonekana kushangaa kupita
kawaida, uzuri wa Juliet haukuonekana kuwa wa kawaida hata mara moja. Najua
kwamba Mungu alikuwa akiwaumba duniani katika matumbo ya mama zao lakini kwa
Juliet akili yangu ilikuwa ikikataa kabisa kwamba hakuwa ameumbwa tumboni mwa
mama yake bali alikuwa ameshushwa moja kwa moja kutoka huko kwa Mungu na kuletwa
duniani kwa lengo moja tu, kunijaribu mimi
tu.
Vipi kuhusu umbo, utazumzungumzia vipi Juliet.
Alikuwa mrembo sana tofauti na picha za uongo ambazo alikuwa ameziweka facebook.
Tulitembea huku tukipiga stori, akili yangu kwa wakati huo ilikuwa ikikifikiria
chumba changu tu, sikujiamini kama chumba kile nilikuwa nimekiacha katika hali
ya usafi. Tulitembea huku tukipiga stori huku yeye akiwa amebeba begi dogo
mgongoni, tulipofika nyumbani, tukaingia chumbani.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tulipofika
chumbani, nikapigwa na mshangao mkubwa sana, na si mimi peke yangu ambaye
nilitakiwa kupigwa na mshangao huo bali hata kama ungekuwa wewe ni lazima
ungepigwa na mshangao pia. Chumba nilikiacha katika mazingira ya usafi wa hali
ya juu ambao sikuwahi kuufanya ila nilipoingia sasa hivi pamoja na Juliet,
chumba kilikuwa shaghalabaghala.
Shuka lilikuwa
lipo ovyo ovyo, viatu na kandambili ambavyo nilikuwa nimeviweka uvunguni
vilikuwa vimetolewa, harufu ya air freshner ambayo nilikuwa nimeipulizia wala
haikuwa ikisikika, vumbi lilikuwa likionekana, mito ambayo niliichukua kwa broo
wala haikuonekana kitandani, yaani kama chumba kilivyokuwa kabla ya kufanya
usafi ndivyo kilivyokuwa kwa wakati huu, mbaya zaidi, hata sufuria niliyopikia
ugali ambayo niliitoa nje na kuiweka kwenye karo, eti nayo ilikuwa chumbani huku
maji na mwiko vikiwa ndani ya sufuria hiyo niliyoiloweka ili ukoko uliokuwa
umeganda utoke.
JULIET: Chumba
kizuri.
Mwili wangu ulikuwa
umenyong’onyea kupita kawaida, nilikuwa nikikiangalia chumba kile huku
nikionekana kupigwa na mshangao mkubwa kupita kawaida. Macho yangu sikutaka
kuyapeleka usoni mwa Juliet kwani nilikuwa najisikia noma kupita kawaida. Muda
wote Juliet alikuwa akikiangalia chumba kile huku akitabasamu kupita kawaida,
hali ambayo aliikuta chumbani mle dizaini ikaonekana
kumfurahisha.
MIMI: Dah!
JULIET: Kuna
nini tena.
MIMI: Kuna jamaa nilimwachia chumba toka juzi mimi
nilikwenda kulala msibani, kanipa funguo kumbe hata chumba hajakifanyia usafi.
Siku nikimnyima ataanza kulalamika (Nilidanganya)
JULIET: Sasa kwa
nini ulimpa ufunguo mtu ambaye unajua si msafi?
MIMI: Huwa ninampa
kila siku hasa ninapoona kwamba silali chumbani. Sasa sijui kwa nini kafanya
hivi. (Niliongea kimajonzi kana kwamba ilikuwa kweli)
JULIET: Pole
sana.
MIMI: Usijali. Ngoja
nikisafishe.
Hapo hapo nikaanza kukisafisha chumba
hicho huku kichwa changu kikiendelea kufikiria juu ya namna ambavyo chumba kile
kilivyokuwa kimechafuliwa namna ile. Kiukweli ni kwamba nilichanganyikiwa, kitu
ambacho kilitokea kilionekana kunichanganya kupita kawaida. Juliet hakutaka
kuniachia mimi tu nifanye usafi wa chumba kile, nae akaanza
kunisaidia.
Tulianza kwa kufanya usafi wa chumba
kile na kisha kuosha vyombo. Nilishangaa sana kwani kwa akili yangu nilikuwa
nikiwaza kwamba Juliet alikuwa mtoto wa ushuwani, msichana ambaye toka
alipozaliwa alimkuta mfanyakazi wa ndani ambaye alikuwa akifanya kazi zote, kwa
hiyo niliamini kwamba asingeweza kufanya usafi kama kuosha
vyombo.
Mawazo yangu na kile nilichokiona vilikuwa
vitu viwili tofauti, Juliet alikuwa akiosha vyombo vizuri kabisa kiasi ambacho
mpaka nilishangaa. Tuliendelea na usafi mpaka pale ambapo tulimaliza na ndipo
tukakaa chini na kupumzika huku chumba kikionekana kung’aa zaidi ya mara ya
kwanza.
MIMI: Asante kwa msaada
wako.
JULIET: Usijali. Karibu.
MIMI: Poa.
JULIET:
Kuna kitu naomba nikugawie kama zawadi.
MIMI: Kitu gani na zawadi ya
kwa ajili ya nini?
JULIET: Huwa unaandika hadithi na kutuwekea
facebook kwa kutumia kompyuta ipi?
MIMI: Ile pale.
JULIET:
Huwa unapenda kuitumia hiyo?
MIMI: Si sana kwani ina uwezo
mdogo.
Hapo hapo Juliet akalifungua begi ambalo
alikuja nalo na kisha kutoa kompyuta moja ya mapajani (laptop) na kisha
kunigawia. Kwanza sikuamini kama kompyuta ile nilikuwa napewa mimi, nikaifungua
na kisha kuangalia ni ya aina gani, ilikuwa ni APPLE ya kisasa, toleo jipya
kabisa ambayo dukani katika kipindi hicho ilikuwa si chini ya milioni mbili na
nusu.
JULIET: Zawadi yako hii kama shukrani zangu
kwa kunifurahisha na hadithi zako facebook.
MIMI: Asante sana
(Nilijibu huku macho yangu yakiendelea kuiangalia laptop ile)
JULIET:
Kuna kingine unachokihitaji?
MIMI: Hapana. Nafikiri hapa umenisaidia
vya kutosha ila nina wasiwasi.
JULIET: Wasiwasi wa
nini?
MIMI: Na hawa matanesco. Kwa tabia zao za kukata umeme na
kurudisha mara kwa mara wanaweza kuiunguza hata hii laptop
yenyewe.
JULIET: Usijali. Hii ina chombo chake maalumu cha kupoza
umeme ambacho kimewekwa humo humo ndani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MIMI: Asante sana
Juliet. Hapa umenisaidia sana. Sijui niseme nini kuonyesha shukrani
kwako.
JULIET: Usijali. Yote ninafanya haya kama
shukrani.
Siku hiyo tuliongea mengi kama marafiki
wa kawaida, akili yangu ilikuwa tofauti na jinsi nilivyokuwa nikifikiria kabla
kwa kuona kwamba Juliet angeniambia maneno mengi kuhusiana na mapenzi, alikuwa
tofauti kabisa. Hakuonekana kutaka kuongea kuhusiana na mahusiano hata kidogo,
alikuwa akiongea kirafiki sana kiasi ambacho nilizidi kushangaa zaidi na zaidi
moyoni mwangu. Mpaka katika kipindi ambacho anaondoka chumbani pale, nilikuwa
siamini kama kweli aliweza kuondoka huku akiwa hajazungumza kitu chochote kile
kuhusiana na mapenzi.
Urafiki wangu na Juliet
ukazidi kuongezeka zaidi na zaidi lakini haukunifanya niache kuchati na kipenzi
changu, barafu wa moyo wangu, Dorcas ambaye katika kipindi hicho alionekana
kuchanganyikiwa kwenye mapenzi yangu. Maisha yangu kwa wakati huo yalikuwa ya
raha kupita kawaida, kulia nilikuwa na rafiki ambaye alikuwa akinijali sana,
Juliet huku kushoto nikiwa na mpenzi ambaye alikuwa akinipenda na kunithamini
sana, Dorcas.
Nikajiona mimi ndio mimi, nilikuwa
nikihitaji nini tena cha zaidi katika maisha yangu? Hakukuwa na cha zaidi.
Ukaribu wangu na Juliet ulizidi kuongezeka zaidi na zaidi mpaka kufika kipindi
ambacho nikaanza kwenda kwao, akanitambulisha kwa wazazi wake kwamba mimi
nilikuwa rafiki bora katika maisha yake. Juliet hakuishia hapo, akawaambia
kwamba nilikuwa nikiandika hadithi katika mtandao wa facebook kitu ambacho
kiliwashtua sana. Baba yake, mzee Lyimo akaanza kuniangalia kwa
mshangao.
MZEE LYIMO:
Unaandika hadithi? (Aliuliza huku akionekana kushtuka)
MIMI: Ndio
mzee.
MZEE LYIMO: Huwa unaandika hadithi za namna
gani?
MIMI: Za kusisimua na hizi za riwaya (Sikutaka kuzitaja za
chombezo, si unajua ningeweza kuharibu kila kitu)
MZEE LYIMO: Safi
sana. Nataka kukupa kazi moja.
MIMI: Kazi gani?
MZEE LYIMO:
Kwanza huwa ukiandika hadithi unategemea kupata kiasi gani?
MIMI: Huwa
siandiki kwenye magazeti. Ila kwenye magazeti unaweza kupata hata milioni tatu
mpaka hadithi yako inakwisha.
MZEE LYIMO: Na kama umeandika
kitabu?
MIMI: Bado sijajua. Ila kama una wateja wengi zaidi ya elfu
kumi, basi unaweza kupata hata milioni sabini.
MZEE LYIMO: Safi sana
Nyemo. Nahitaji unifanyie kitu fulani halafu nitakulipa hiyo milioni sabini. Au
hata milioni mia moja kama utakubali kunifanyia kazi hiyo.
MIMI: (Huku
nikionekana kushtuka) Kazi gani?
MZEE LYIMO: Nitataka uniandikie
kitabu cha maisha yangu yaliyopita mpaka sasa hivi, utatakiwa kuunganisha stori
ya mke wangu Susan pamoja na yangu. Nitakuhadithia, kazi yako itakuwa ni
kuandika tu.
MIMI: Sawa. Nitafanya hivyo.
MZEE LYIMO: Ila
hizo milioni mia moja zitakutosha au nikuongeze?
MIMI: Zitanitosha
sana.
MZEE LYIMO: Sema bwana usije ukatangaza kuwa
nimekunyonya.
MIMI: Zitanitosha
sana.
Unajua wakati mwingine nilikuwa nikijiona
kama naota ndoto moja nzuri na ya kufurahisha sana kiasi ambacho sikutaka
kuamka, ila ukweli ni kwamba hapo sikuwa naota bali kilikuwa ni kitu halisi
ambacho kilikuwa kikitokea katika maisha yangu. Baba yake Juliet, mzee Lyimo
alikuwa akitaka niandike stori ya maisha yake pamoja na mkewe, niziunganishe na
hatimae kiwe kitu kimoja. Hilo lilionekana kuwa dili kubwa ambalo sikutarajia
kulipata katika maisha yangu.
Sikukaa sana
nyumbani hapo, mara baada ya kuongea vya kutosha, nikaaga na kisha kuondoka
nyumbani hapo huku Juliet akinisindikiza na gari lake. Hakutaka nielekee moja
kwa moja nyumbani, tukapitia kwenye mashine ya ATM, akatoa kiasi cha shilingi
milioni moja na nusu na kisha kunigawia shilingi milioni moja, nilishangaa
sana.
MIMI: Juliet.....!
JULIET:
Usishtuke. Twende kwenye ule mghahawa tukale
kwanza.
Tukaanza kuelekea kwenye mghahawa ule na
kisha kutakiwa kuagiza chakula. Nikapewa menu na kuanza kuiangalia. Kulikuwa na
aina ya vyakula zaidi ya sabini ila vyakula ambavyo nilikuwa nikivijua ni viwili
tu, rice na chips, vingine sikuwa nikivijua
kabisa.
JULIET: Unataka nini?
MIMI: Mix
Grill (Nilimwambia Juliet huku hata chakula hicho sikukijua
kinafafanaje).
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mhudumu akaitwa na
kisha kuambiwa kuleta vyakula ambavyo tulikuwa tumeagiza. Ndani ya dakika kumi,
vyakula vilikuwa mezani, tukala na kisha kuanza kuangaliana huku kila mmoja
akionekana kuwa na shauku ya kutaka kumwambia mwenzake jambo
fulani.
JULIET: Unajua kwamba baba naye ana
akaunti facebook?
MIMI: Hapana.
JULIET: Anayo. Nilimfungulia
mwaka jana, ila hatumii jina lake.
MIMI: Kwa nini
sasa?
JULIET: Hataki tu. Ila pamoja na hayo, yeye ndiye aliyenifanya
nipende kusoma stori zako.
MIMI: Kivipi?
JULIET: Mara nyingi
baba alikuwa yupo bize sana na mtandao wa facebook kiasi ambacho hadi mama
alikuwa akikasirika sana. Kila alipokuwa akimuuliza kwa sababu gani, alikuwa
akijibu kwamba hadithi zako ndizo ambazo zilikuwa zinamfanya kuwa bize. Basi na
mimi nikamuomba aniambie kuhusu page yako, akaniambia kwamba ni NYEMO THE
PRINCE, nika-like na kisha kuanza kupata burudani. Huwezi amini Nyemo, kwa sasa
wewe ni rafiki wa familia nzima, ila pale baba hakutaka kujionyesha kwamba naye
ni mmoja wa fans wako.
MIMI: Dah!
JULIET: Ndio hivyo, hadi
mama naye akafungua akaunti ya facebook na kisha kuanza kusoma stori zako.
Unaposema kwamba itaendelea, tunakuwa na mzuka wa kutaka kujua itaendelea vipi.
Unapokaa kimya na kutokutoa kwa siku, tunaonekana kama kuumwa siku
hiyo.
MIMI: Poleni sana.
JULIET: Asante. Baba anakukubali
sana na ndio maana ameamua kutaka kukupa shavu hili la kumwandikia kitabu cha
maisha yake.
MIMI: Asijali. Nitaifanya kazi hiyo.
JULIET:
Unakumbuka kuna kipindi ulilalamika kuhusu tatizo la kompyuta yako kuungua
chaja?
MIMI: Nakumbuka.
JULIET: Basi hali hiyo ikamfanya
kukununulia laptop nchini Marekani kwani alikuwa huko kipindi hicho. Alipokuja,
akanipa na kutaka nikuletee ila nisikwambie kwamba ni yeye ndiye aliyenipa
nikupe.
MIMI: Hahaha! Sasa kwa nini umeniambia?
JULIET: Basi
tu. Hata hizi fedha aliniambia nikupe zikusaidie kwa kuweka vifurushi ili
usiache kutoa hadithi hata siku moja.
MIMI: Duuh!
JULIET:
Ndio hivyo.
Kwa wakati huo nikajiona kupata zali
kubwa sana ambalo wala sikuwa nimelitegemea katika maisha yangu, kukutana na
familia ambayo ilikuwa na utajiri mkubwa ilinifanya kujiona kwamba na mimi
nilikuwa nakwenda kuwa tajiri muda wowote ule. Juliet hakutaka kunificha,
alikuwa akinielezea kila kitu ambacho sikuwa nikikifahamu. Hapo ndipo nilipojua
kwamba baba yake, mzee Lyimo alikuwa tajiri mkubwa na mfanyabiashara ambaye
alikuwa akijulikana sana. Alikuwa na biashara nyingi kubwa ambazo kwa siku
zilikuwa zikimuingizia zaidi ya milioni themanini kwa
mwezi.
Kwangu hata kabla sijakiandika kitabu cha
maisha yake nikajiona kuridhika, fedha hazikuwa mikononi mwangu lakini tayari
nilikuwa nimekwishazipangia bajeti na kilikuwa kimebakia kiasi cha shilingi
milioni arobaini tu, milioni sitini zilikuwa zimekwishakwisha. Maisha
yaliendelea zaidi mpaka siku ile ambayo mzee Lyimo akaniita na kisha kukaa
katika maktaba ndogo ambayo ilikuwepo ndani ya nyumba yake na kisha kuanza
kunielezea historia ya maisha yake.
Usikivu wangu
ulikuwa mkubwa sana, nilikuwa nikimsikiliza kwa makini kabisa. Historia ya
maisha yake ilikuwa ni ya kusikitisha iliyojaa umasikini mkubwa kiasi ambacho
wakati mwingine niliona kama alikuwa akinidanganya. Kila alipokuwa akielezea,
muda mwingi nilikuwa nikishusha pumzi nzito na kisha kumsikiliza zaidi. Alitumia
muda wa masaa mawili, historia ikawa imekamilika na hivyo kumuita mke wake
ambaye nae akaanza kunielezea yake.
Najua kuna
watu ambao walikuwa wamepitia katika umasikini ila kwa watu hawa wawili nadhani
walikuwa wamezidi zaidi ya watu wote. Historia zao kwa pamoja kwangu mimi
zilionekana kuwa kama filamu fulani ya Kitanzania ambayo iliandikwa na mwandishi
mahili kwa sasa nchini Tanzania, mwandishi ambaye anaonekana kuibadilisha jamii,
Andrew Carlos
Mara baada ya kusikiliza historia
zao kwa pamoja, hapo ndipo nilipotakiwa kuanza kazi yangu. Nikaitoa laptop
kutoka katika begi ambalo nilikuja nalo na kisha kumtaka mzee Lyimo achukue muda
wa dakika ishirini kuniambia historia ya maisha yake, akaanza kunihadithia,
alipomaliza, nikavipeleka vidole vyangu katika keyboard ya kompyuta ile,
nilipoyainua macho yangu, nilikuwa nimeandika zaidi ya kurasa thelathini na
kisha kumuonyeshea kwanza aisome kabla
hatujaendelea.
MZEE LYIMO: Kweli wewe mtu
umezaliwa kwa ajili ya kuandika tu, umeandika vizuri zaidi ya nilivyokuwa
nikifikiria.
MIMI: Usijali mzee. Kazi yangu mimi ni kuandika tu, sina
kazi nyingine niliyopewa, sina kipaji kingine maishani mwangu. Uandishi ndio
kazi yangu na ndio kipaji changu.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mzee Lyimo
akaendelea zaidi na zaidi kunihadithia huku nami nikiandika kama kawaida yangu.
Siku hiyo nilitumia masaa manne kuandika historia ya maisha yake na ndipo
nikaondoka huku hata nusu ikiwa haijafika. Katika wiki nzima nilikuwa nikiifanya
kazi yake hiyo, kuandika historia ya maisha ya mtu haikuwa kazi ndogo, ilikuwa
ni aina ya hadithi ya kweli ambayo iliwahi kutokea, hivyo haukutakiwa kuongeza
neno lolote wala kupunguza kutoka
kwake.
Mzee
Lyimo alikuwa akitambua utu, kila nilipokuwa nikienda kwake na kurudi nyumbani,
alikuwa akinikabidhi kiasi cha shilingi elfu hamsini kama pole ya kazi kubwa
ambayo nilikuwa nikiifanya siku hiyo. Uandishi wa simulizi ya maisha yake
nilitumia siku sitini na ndipo ikakamilika huku katika siku zote akiwa
amenigawia elfu hamsini kama pole, kwa hiyo ndani ya miezi miwili nilikuwa
nimekwishachukua milioni tatu nje ya malipo yangu ya milioni mia
moja,
Baada ya historia yake kuisha, hapo ndipo nikaanza na historia
ya mke wake, Bi Susan ambaye naye alikuwa na historia ambayo ilikuwa
ikinishangaza sana. Kama kawaida, malipo ya siku yalikuwa yale yale huku nikila
pale pale nyumbani kwao. Kwa Bi Susan wala sikuchukua muda mrefu, ndani ya mwezi
mmoja na nusu nikawa nimekwishamaliza kuandika historia yake na kisha kuwagawia
na kuanza kuzisoma. Uandishi wangu uliwafurahisha
sana.
Baada ya siku mbili, nikazionganisha
historia zile pamoja na kitabu kukamilika na kisha kwenda kukichapisha huku jina
la kitabu hicho likiitwa MY WIFE AND I. Nilimuuliza juu ya jina la kitabu kuwa
la Kingereza ila aliniambia kwamba alipenda iwe hivyo kwani alikuwa akitaka
kukiuza kitabu hicho katika nchi mbalimbali kwa ajili ya wale watu ambao
walikuwa wamekata tamaa ya maisha waweze kufarijika na kujiona kwamba walikuwa
na nafasi ya kufanya mambo fulani katika maisha
yao.
MZEE LYIMO: Kitabu hiki kitauzwa dunia nzima,
ningependa niongee na maisha ya watu kupitia maisha yetu yaliyopita.
Kitatafsiriwa kwa lugha nne, Kiswahili, Kifaransa, Kingereza na
Kihispania
MIMI: Hapo itakuwa vizuri sana. Kupitia maisha yenu
kumeonekana kunibadilisha hata mimi.
MZEE LYIMO: Umejifunza nini
kupitia maisha yetu?
MIMI: Nimejifunza kwamba hakuna kukata tamaa
katika maisha na pia hatutakiwi kuuogopa umasikini zaidi ya kupambana nao kama
ambavyo mlivyofanya.
MZEE LYIMO: Kuna kingine
ulichojifunza?
MIMI: Labda niseme kwamba mnapokuwa watu wawili,
upambanaji wenu hauwi mgumu sana kama ambavyo utakuwa peke yako.
MZEE
LYIMO: Na hiyo ndio pointi yenyewe. Bila mke wangu, nadhani nisingeweza kufika
hapa nilipokuwa kwa sasa, yeye ameonekana kuwa msingi mkubwa wa maisha yangu,
yeye ameonekana kuwa mafanikio yangu makubwa sana katika maisha yangu. Amekuwa
mwanamke mwerevu sana, naweza kusema ni mwerevu zaidi ya wanawake wote katika
dunia hii.
MIMI: Ningetamani kuwa na mke mwenye hali ya kujituma kama
mke wako, mwanamke ambaye atakuwa akinifariji na kunitia nguvu katika maisha
yangu bila kujali ni maisha gani ya shida tunayopitia.
MZEE LYIMO:
Juliet yupo, amechukua tabia kama za mama yake, ana damu ya mama yake, japo si
mkubwa sana lakini tayari nimeona kuna mengi amerithi kwa mama
yake.
MIMI: Anaonekana kuwa msichana mwerevu sana ambaye anajali na
kusikiliza. Nimeufurahia urafiki wangu pamoja nae.
MZEE LYIMO:
Unakiona kitabu hiki ulichokiandika?
MIMI: Ndio.
MZEE LYIMO:
Mpaka sasa hivi watu walioweka oda ni watu elfu sitini duniani na bado wengine
wanazidi kumiminika kwa wastani wa watu elfu kumi kwa wiki. Nitakwenda kuingiza
fedha nyingi sana, zaidi ya bilioni tano duniani.
MIMI: Duh! Kumbe
uliangalia mbali.
MZEE LYIMO: Sana. Nitaingiza zaidi ya bilioni tano,
halafu wewe nikulipe milioni mia moja, hauoni kwamba huo ni
unyonyaji?
MIMI: Ila nimeridhika na malipo yangu.
MZEE
LYIMO: Hapana Nyemo. Ni lazima nifanye kitu fulani kwa ajili yako, ninataka
kubadilisha maisha yako kabisa, yaani yabadilike kwa asilimia mia moja. Kwa
kutumia fedha hizo, nitakujengea nyumba ya thamani na kukununulia gari la
thamani sana pamoja na kukufungulia biashara kubwa ambazo zitakuwa zako, una
kingine unachokihitaji?
MIMI: Hapana. Nafikiri vinatosha na
nitashukuru sana.
MZEE LYIMO: Okey! Au unamtaka nikuongezee na binti
yangu?
MIMI: Hapana. Bado mapema mno.
MZEE LYIMO: Sawa.
Usijali. Nashukuru sana. Nadhani ungeniachia namba ya akaunti yako ya benki ili
nikuingizie fedha hizo.
Hapo nikamuandikia namba
ya akaunti yangu na kisha kuondoka mahali hapo. Ndani ya gari nilikuwa
nikionekana kuwa mwingi wa furaha kwani kwa wakati huo nilijiona kuwa tajiri
mkubwa sana japokuwa kiasi ambacho nilitakiwa kukipata ni milioni mia moja tu.
Kwa jinsi ambavyo furaha ilivyokuwa moyoni mwangu, nilitamani nipae angani na
kisha kuitangazia dunia kwamba nilikuwa nimeingiza kiasi cha shilingi milioni
mia moja kwa wakati huo.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilipofika nyumbani
pamoja na Juliet, tukateremka kutoka garini na kisha kuanza kuelekea kilipokuwa
chumba changu. Njiani nikakutana na rafiki yangu, Thomas Lyaruu ambaye
akanifuata huku uso wake ukionekana kuwa na
majonzi.
MIMI: Vipi tena?
THOMAS: Kuna
taarifa mbaya.
MIMI: Kuhusu nini?
THOMAS: Kumbe Dorcas
alifariki.
MIMI: Alifariki? Lini?
THOMAS: Toka mwaka jana
alipokuwa shuleni nchini Uganda.
MIMI: Dorcas alifariki toka mwaka
jana alipokuwa nchini Uganda! Kivipi tena? Mbona hata juzi nilikuwa
nae?
THOMAS: Acha utani. Ulikuwa naye juzi juzi?
MIMI: Tena
hata namba yake ya simu ninayo hapa.
THOMAS: Hebu
mpigie.
Nikachukua simu yangu kutoka mfukoni na
kisha kuanza kuitafuta namba ya Dorcas ambaye nilikuwa katika mahusiano pamoja
naye. Katika kipindi hicho nilionekana kushtuka sana, ilikuwaje Dorcas awe
amefariki toka mwaka jana na wakati nilikuwa nikiwasiliana naye huku mara nyingi
akija nyumbani pale. Kwa kiasi fulani nilikuwa nimechanganyikiwa. Juliet alibaki
kimya huku akiniangalia, niliangalia namba ile katika simu yangu, sikuiona
japokuwa nilikuwa nimeisave.
THOMAS: Ipo
wapi?
MIMI: Eti siioni na wakati niliisave.
THOMAS: Hebu
acha utani Nyemo, iweje namba uisave halafu usiione?
MIMI: Hata mimi
nashangaa.
THOMAS: Kwa hiyo unasema kwamba ulikuwa ukionana na
Dorcas?
MIMI: Ndio. Tena hata juzi alikuja hapa
nyumbani.
THOMAS: Alikuja muda gani? Mbona sikumuona?
MIMI:
Huwa anakuja usiku.
THOMAS: Mimi ni rafiki yako wa karibu, sasa kwa
nini hukuniambia nije nionane naye?
MIMI: Nilitaka kufanya hivyo ila
alikuwa akikataa kabisa.
THOMAS: Kwa nini alikuwa
akikataa?
MIMI: Sijui.
THOMAS: Alipokuwa akiondoka ulikuwa
ukimsindikiza?
MIMI: Hapana.
THOMAS: Kwa
nini?
MIMI: Alikuwa akikataa pia.
THOMAS: Kuna
kitu.
MIMI: Kitu gani?
THOMAS: Umekwishawahi kukisoma kitabu
cha A Beautiful Girl from Hell kilichoandikwa na Padwer Simpson?
MIMI:
Hapana.
THOMAS: Huyo hakuwa Dorcas.
MIMI: Hakuwa Dorcas?
Sasa alikuwa nani?
THOMAS: Alikuwa jini.
MIMI:
Whaaaaaaat?
Dizaini kama sikuwa nimemuelewa Thomas
Lyaruu ila kwa wakati huo ilinipasa nimuamini. Huyu ni rafiki yangu mkubwa, ni
rafiki yangu mkubwa kuliko marafiki wote duniani kwa sasa, hakuwahi kunitania
katika jambo kama hili japokuwa mara nyingi sana huwa tunafanya utani katika
mambo mengine. Nilimwangalia Thomas huku macho yangu yakionekana dhahiri
kutokuamini kile ambacho nilikuwa nikikisikia masikioni mwangu. Nikayageuza
macho yangu na kumwangalia Juliet.
Macho ya Juliet
yalikuwa yakionyesha hofu kubwa, alionekana kuogopa kile ambacho alikuwa
amekisikia kwa wakati huo. Hapo ndipo picha fulani ikaanza kunijia kichwani
mwangu. Kwa kukukumbusha nafikiri unajua kwamba Dorcas alikuwa mpenzi wangu,
alikuwa akinipenda kama ambavyo nilikuwa nampenda katika kipindi hicho. Kwa
sababu alikuwa mpenzi wangu, hivyo alikuwa akisikia wivu kama ambavyo nilikuwa
nikisikia wivu katika moyo wangu.
Ninachokihisi
katika kipindi ambacho nilikuwa nawasiliana na Juliet alikuwa akihisi wivu sana
na ndio maana hata katika kile kipindi ambacho nilikuwa nimesafisha chumba
changu na kisha kwenda kumpokea Juliet, nilikikuta chumba kikiwa
shaghalabaghala. Jibu juu ya kile kitu ndicho ambacho kilinijia kichwani mwangu
kwa wakati huo.
MIMI: Jini!
THOMAS: Ndio
maana yake.
MIMI: Inawezekana vipi lakini?
THOMAS: Ngoja
nikuulize swali Nyemo.
MIMI: Uliza.
THOMAS : Unasema kwamba
Dorcas alikuwa mpenzi wako, si ndio?
MIMI: Ndio.
THOMAS: Na
ulisema alikwishawahi kuja chumbani kwako mara nyingi, si ndio
hivyo?
MIMI: Ndiyo.
THOMAS: Mlikwishawahi kufanya
mapenzi?
MIMI: Hapana. Alikuwa akikataa katakata.
THOMAS:
Hukuwahi kuota ndoto za kufanya naye mapenzi?
MIMI: Niliwahi. Nilikuwa
naota sana ndoto za namna hiyo. Nilikuwa nikifanya naye mapenzi sana
ndotoni.
THOMAS: Hivyo ndivyo majini yalivyo, mara nyingi huwezi
kufanya nao mapenzi hivi hivi, hukufuata ndotoni kama ambavyo Padwer Simpson
alivyoeleza katika kitabu chake cha Beautiful Girl From hell.
MIMI:
Sawa. Nimekubali, ila nataka kuamini zaidi.
THOMAS: Unataka kuamini
nini tena?
MIMI: Ngoja niende nyumbani kwao.
THOMAS: Sio
uende, twende wote, si unapajua?
MIMI: Ndiyo. Nilikwishawahi
kufika.
THOMAS: Uliwahi kuingia ndani ya nyumba yao?
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MIMI: Hapana.
Alinionyeshea tu na kisha kuondoka.
THOMAS: Basi sawa.
Twende.
JULIET: Na mimi nataka kwenda. Ni wapi?
MIMI:
Magomeni.
Hatukutaka kuchelewa mahali hapo,
tulichokifanya ni kuanza kulifuata gari la Juliet na kisha kuondoka mahali hapo.
Nilionekana kuwa kama mtu ambaye nilichanganyikiwa kwa wakati huo, maneno ya
Thomas ambayo aliniambia kwamba Dorcas alikuwa jini yalionekana kunichanganya
kupita kawaida.
Kutoka nyumbani Tandale mpaka
magomeni wala hapakuwa mbali sana hivyo kwa kutumia gari tulitumia muda wa
dakika tano tukawa tumekwishafika na kisha kuelekea mapipa ambapo alikuwa
akiishi Dorcas. Njia nilikuwa nikizikumbuka sana, nilikuwa nikielekeza mpaka
pale ambapo nilijua fika kwamba ndipo alipokuwa amenionyeshea kwamba ndio
palikuwa kwao.
MIMI: Mhhh!
THOMAS: Vipi
tena?
MIMI: Mbona kuna mbuyu?
THOMAS: Wapi?
MIMI:
Hapa ndipo kulipokuwa nyumba yao, nashangaa kuna mbuyu.
THOMAS:
Unamaanisha kwamba hapa ndipo alipokuonyeshea kwamba kuna nyumba
yao?
MIMI: Ndio hapa. Nashangaa kuna mbuyu.
THOMAS: Una
uhakika kwamba ni hapa?
MIMI: Ndio. Ni hapa tena hadi ndani niliingia
kila nilipokuja kumtembelea.
THOMAS: nadhani unanitania
Nyemo.
MIMI: Kweli tena Thomas. Siwezi kukutania katika
hili.
Wakati mwingine nilikuwa naongea kama utani
lakini ndivyo nilikuwa nikimaanisha, nilionekana kushangaza kupita kawaida,
sehemu ambayo Dorcas alikuwa amenionyesha kwamba kulikuwa na nyumba yao kwa
wakati huo kulikuwa na mbuyu mmoja mkubwa ambao ulikuwa ukisifika sana Magomeni
kwa mambo ya kishirikina kutoka na kila siku watu kuujaribu kuukata mbuyu huo
lakini haukuwa ukikatika kabisa.
Nilipojaribu
kumtafuta Dorcas hata katika mtandao wa marafiki zangu Facebook, sikuweza
kumuona, sikuweza kuziona tena meseji zake ambazo alikuwa akinitumia, jina la
akaunti yake likapotea kabisa katika mtandao wa facebook. Masikini Dorcas,
msichana ambaye nilikuwa nikimpenda ndio alikuwa amekufa nchini Uganda toka
mwaka jana katika mapigano ya kisiasa nchini humo katika kipindi cha uchaguzi
alipokuwa chuoni. Kuanzia siku hiyo, sikuweza kumuona tena Dorcas mpaka katika
kipindi hiki, hakurudi tena katika maisha yangu hadi pale nilipomuoa Juliet,
hakuwa amerudi.
Kwa sasa, nimefanikiwa katika
maisha yangu, Juliet ndiye msichana ambaye nimemuoa na hatimae kunipatia mtoto
mdogo wa kume aitwaye Henry mwenye miaka 4. Hiyo ilikuwa historia fupi ambayo
nimejaribu kukupa katika kipindi ambacho nilianzisha uhusiano na msichana jini
ambaye nilikuwa nimezoeana nae na nilikuwa nikimpenda sana katika kipindi cha
nyuma.
Umasikini ambao nilikuwa nao,
nilikwishauaga na kwa sasa nipo huku katika visiwa vya Hawaii nchini Marekani
kwa ajili ya kula maisha na mke wangu mpendwa Juliet pamoja na mtoto wetu,
Henry. Kuandika hadithi kwangu facebook ndio kulinipa utajiri nilionao kwa sasa
hasa mara baada ya kukutana na baba mkwe, mzee Lyimo ambaye alibadilisha sana
maisha yangu.
Napenda sana kuyazungumzia maisha
yangu ya nyuma katika kipindi ambacho nilikuwa masikini wa kutupwa. Leo hii
ukisema ni kitu gani ambacho ninakichukia katika maisha yangu, nitakwambia
umasikini. Najua wapo wengi ambao wanaandika hadithi facebook ila ningependa
kuwaambia kitu kimoja tu, usimdharau mtu yeyote katika mtandao huu kwani mtu
huyo anaweza kubadilisha maisha yako katika staili ambayo wala hautoweza
kutegemea.
Kwa sababu sikuwa nikimdharau mtu, hata
nilipoonyeshewa jina analolitumia mzee Lyimo, nilishangaa sana. Alikuwa akitumia
picha ya mtu mwingine, alikuwa akipenda sana kuLIKE na kuCOMMENT post zangu
pamoja na hadithi mbalimbali. Alikuwa akinirekebisha sana na kunikosoa pale
nilipokuwa nafanya makosa, kuna watu kiukweli walikuwa wakimdharau bila kumjua
ila kwangu alikuwa mmoja wa watu muhimu sana. Mara nyingi nilikuwa nikijiuliza
kwamba kama ningeweza kumdharau leo ningekuwa wapi? Natumaini nisingekuwa katika
visiwa hivi, nafikiri nisigeweza kupata milioni mia moja, nyumba ya kifahari,
magari ya kifahari pamoja na miladi mingi.
Kwa
kumalizia tu, bado naendelea kusisitiza kwamba si kila msichana au mvulana
unayemuona ndani ya mtandao wa facebook ni binadamu, kuna wengine huwa majini,
majini ambayo yamekuwa yakihangaika huku na kule kutafuta damu za watu. Kwa
Dorcas, alikuja kwangu kama mwili wake na nilikuwa nikimfahamu, ila kiukweli
kama nisingekuwa namfahamu, tayari angekuwa
amekwishanimaliza.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa kumalizia
naomba ujue kwamba hii ni hadithi ya kutunga tu ambayo nilipewa wazo na huyu
rafiki yangu Thomas Lyaruu Jnr. Aliponipa wazo la kuandika kijistori hiki
kifupi, nilikipuuzia kwa muda wa mwezi mzima, ila nilipokiandika, kiukweli
kimeonekana kueleweka sana.
MWISHO WA SEASON 2,
ENDELEA NA SEASON 3
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment