Search This Blog

Monday, October 24, 2022

UTAMU WA ZEGE - 1

 





    IMEANDIKWA NA : HASSAN S. KAJIA



    *********************************************************************************



    Chombezo : Utamu Wa Zege

    Sehemu Ya Kwanza (1)


    MLIO wa simu yake ndiyo uliozindua kutoka katika njozi yake ambayo hakuimalizia vizuri. Hakuwa na jinsi zaidi ya kutii amri ya simu yake. Alijiwekea alamu tayari kwa kumwamsha kila siku. 
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    Alizitumia kama dakika tano kujiweka sawa kabla ya kutoka kitandani. Usingizi haukumweka tena kitandani. Alijivuta hadi kushika simu yake na kuiangalia. Hakukuta chochote zaidi ya nambari zilizoonyesha muda wa kuamka baada ya ile alamu kuisha. 


    Saa kumi na moja na nusu asubuhi ni muda ambao siku zote alikijuta yuko macho. Wakati mwingine aliiwahi alamu ya simu yake kabla haikulia. Hapo alijua labda ililia na hakuisikia na hivyo amechelewa. 


    Wakati mwingine hakuipenda kwani ingemaliza hamu yake ya kulala wakati bado hivyo alijua siku za kuiweka na siku za kuitoa. Ni endapo angechelewa kulala sana. Asingeiweka na siku hiyo angeamka muda wowote na kwenda kazini.


    Kama kawaida yake. Kioo kilikuwa ni kitu cha pili baada ya kuiwasha taa yake iliyokuwa karibu na kitanda. Taa inayowekwa mezani kwa ajili ya dharura. Mwanga hafifu uliomwangazia ulimtosha kujiangalia usoni peke yake. Alitaka kila siku aone mabadiliko yaliyotokea wakati akiwa amelala. Kama angeona utofauti, hakusita kwenda kwa mtaalamu ili amsaidie. Lakini leo hakuona lolote. Alijiona vilevile kama alivyolala jana yake saa tano na nusu usiku.


    Kati ya mambo ambayo Jane aliyahusudu sana ni jinsi alivyo. Aliamka sasa na kukifuata kioo kikubwa alichokuwa amekiegemeza ukutani. Vyumba vyake viwili na maliwato iliyokuwa ndani ilimfanya ajisikie huru kama aishiye katika hekalu. Yote aliyafanya ndani. Alifurahia maisha yake. Alifanya alichokitaka.


    Kioo chake hakukitumia vibaya. Sasa ilikuwa zamu ya umbo lake. Alikifuata kioo na kukisimamisha vizuri. Sasa alijiona wote. Alitoa shuka ambalo alikuwa amejifunika. Alilirusha hadi kitandani kama vile alisahau bahati mbaya akashuka nalo. Alisahau kwamba lilitakiwa limsitiri. Habari hiyo hakuitaka. Alisimama wima. Tabasamu lilianza kuchanua taratibu. 


    Alijitazama na kuliangaza umbo lake lililoimarika vizuri. Alijitamani. Alishika kiuno chake kwa staili ifanywayo na walimbende wawapo katika mashindano. Kisha akatembea hatua mbili mbele. Alicheka. Alijikubali. Alitamani apige kelele kumshukuru aliyemleta duniani.


    Alirudi tena hatua mbili nyuma. Sasa aligeuka kuangalia umbile lake kwa nyuma. Aliguna akimaanisha muumba hakumkosea. Taratibu akawa anaelekea bafuni akiwa hajaridhika. 
    Alilifuata bafu huku macho yake yakiwa nyuma kumalizia kujitazama tena na tena kama hatatoka tena alikokwenda. 


    Dakika kumi zilimtosha kujimwagia maji. Alirudi tena kiooni. Sasa ilikuwa ni kujikausha kwa taulo lake jeupe na safi. Alifanya hivyo akilipitisha katika kila kiungo chake. Matiti, shingoni, mapajani na miguuni huku akimalizia mgongoni kwa kulibenua nyuma na kulitembeza sehemu yote ya mgongo. Aliridhika. 


    Alilifuata kabati lake na kutoa nguo. Kioo hakikuwa mbali. Alikifuata na kucheza nacho tena kama pacha wake. Alicheka mwenyewe. 


    Alijiona amependeza. Alitembea kwenda mbele na kurudi nyuma. Mwishowe alijiona mjinga. Alikimbilia simu yake na kuzima taa tayari kufunga mlango na kuelekea ofisini.
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    *****
    Jane alikuwa msichana anayejithamini sana. Hakujali watu wasemavyo juu yake wala hakutaka kujisahau na kwenda kinyume na matarajio yake kwa siku nyingi. Kujiamini ndio kitu alichokijua anacho. Hakuwaogopa wanaume wakware waliomtamani na alilijua hilo. Utitiri wa wakware hao ulimfanya ajione mlimbwende zaidi ya alivyosifiwa. Kwa upande wa wanawake aliwajua pia. Hakuwajali wanawake waliokaa vibarazani na kumsema. Alijua alipotokea na alilolifanya. Ziada ingekuja baada ya kugundua jipya. Alilolipanga usiku asubuhi na kutwa nzima angelitekeleza. Hakuamini kama kuna kushindwa wala kukata tamaa. “eti maisha magumu.”


    Hayo maneno aliishia tu kuyasikia kwa watu lakini kwake hakuyaruhusu. “Mwanamke kupambana” ni maneno aliyosimama nayo na aliyoyaheshimu katika fikra zake na ndoto zake za kujiinua kimaisha.


    Alikuwa wa namna ya pekee. Uzuri wake haukuwachosha wanaume wakare kumtazama. Machoni ukimtazama utatamani umweke ndani. Wanaume wengi walimtamani na hilo alilijua. Mvuto wake ni karibisho tosha kwa yeyote anayehisi maumivu ya moyo. Lakini utamwanzaje. Wengi wao walijiuliza bila ya kuwa na majibu kwani hakuna aliyekaribia kumpata Jane.


    “Anatembea na wazungu na wanaume matajiri tu yule.”


    “Inawezekana ana ngoma hataki tujue. Mbona hata hashindi nyumbani.”


    “Haeleweki, kila siku anafuatwa na magari ya kifahari na kurudishwa. Ni Malaya yule dada, achene tu.”


    “Na ndo maana haeleweki, pengine mgonjwa na anasambaza kwa wakware wenye kumtamani.”
    Hizo ni kauli za wanawake kwa wanaume walivyomfikiria Jane.




    *****
    Ni James tu aliyekuwa na mazoea na binti huyu. James alikuwa ni mfanyabiashara. Mfanyabiashara aliyejituma na kuifanya kazi yake vizuri. Alikuwa na kibanda chake cha kukaanga chipsi maeneo ya Magomeni Mapipa ambacho alikitegemea kusogeza siku.


    Alimfahamu Jane kwa kuwa alikuwa mteja wake mkubwa sana. Walitaniana sana japo James hakufika kwa utani wa Jane. Jame alikuwa mwongeaji zaidi ya James. Jane alitumia mwanya huo kukopa hata chipsi na kulipa baadaye. Kwa James hilo halikuwa tatizo kwani Jane hakuwahi kumdhulumu kamwe. Alimwamini zaidi ya wateja wake wote. Na siku zote lazima angeonana na Jane kabla au pindi arudipo kutoka kazini kwake Kariakoo.


    “Dada Jane, habari za asubuhi,” James alimsalimia Jane.


    “Nzuri James umeamkaje,” Jane aliitikia salamu ya James. Kwa nusu dakika James alikuwa amehisi baya kwa Jane. Hakuwa kawaida. Alionekana kachoka sana hali iliyomfanya James aache alilokuwa akifanya na kumuuliza.


    “Kulikoni dada Jane leo nakuona tofauti, vipi mgonjwa au?” Jane hakuwa Jane aliyekuwa akicheka mwenyewe na kioo chake. Alibadilika. Ni baada tu ya kutoka nje ndipo alipokumbuka yaliyomsibu.
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    “Acha tu James,” Jane hakumwambia James juu ya kinachomsumbua. James aliendelea na kazi yake ya kukusanya masalia ya mbao kwa ajili ya kuwashia moto ili aanze shughuli yake ya kupika chipsi. Siku hiyo Jane aliondoka pasipo kumsemesha James. Haikuwa kawaida kwa wawili hao.




    *****
    Saa tano usiku Jane alirudi na kupitia kibandani kwa James kwa lengo la kuchukua chipsi. Alikuwa amebadilika tofauti na asubuhi. James alimshangaa sana, alifurahi kumwona.


    “Ooh! Mamaaa, karibu. Kama kawa nini? Maana na we kwa zege sikutoi, leo badilisha basi, kula kavu?” James alimtania Jane ambaye siku zote alikuwa akinunua chipsi mayai kibandani kwa James. James alimzoesha Jane kwa jina la zege akimaanisha Chipsi mayai.


    “James hutaki hela eeh? Mi siwezi kavu napenda zege.”


    "Eeh, ndo maana mtoto unaimarika tu kila kukicha kwa sababu ya James," James alitania huku akicheka.


    “James, spendi hivyo, sipendi tena useme huo ujinga wako. Mi nlikuambia nlinenepea kwetu,” Jane alikuwa mkali lakini mwishowe na yeye alicheka. Alifurahi kusikia kauli ya James iliyojaa utani.


    “We nishukuru mimi, ulikuja hapa mwembambaa ka umetengenezwa, James kakunenepesha, waangalie wadada ambao hawali chipsi kwa James wote wembamba,” James aliendelea kumtania Jane huku akicheka sana. Jane alibadilika sura na kuanza kununa. Mwishowe alicheka kwa nguvu kwa kushindwa kujizuia kuonyesha hisia zake za furaha.


    “Kwa hiyo unataka kuniambia we ndo uliyeniwezesha.”


    “Sasa je, mwanamke akiwezeshwa anaweza. Mi nakucheki tu tangu umekuja hapa, afu ulikuwa mpolee, zege la James limekuchangamsha.”


    “Bana, n'fungie mi niende nshachoka kucheka na utani wako,” James alimfungia Jane chipsi mayai na kumkabidhi mfuko. Jane aliondoka kwa madoido na kumgeukia James. James alikuwa akimwangalia Jane alivyochangamka siku hiyo.


    “We James, aliita Jane. “Mbona huweki soda hapa karibu mpaka kila siku niende mbali kuchukua.”


    “Dah, mama, mtaji wa kuweka hapa na eneo lenyewe si unaliona. Wengi wakija wanakuja kabisa na soda zao au naenda kuwachukulia. Niambie unakunywa soda gani nitakuwa nakuwekea kwangu ukija nakupa dada."


    “Soda n’nayokunywa mimi huwezi kuiweka, usiku mwema,” Jane aligeuka na kuanza kuondoka tena.


    ”Dada Jane, samahani kwanza,” James alimwita na kuanza kumfuata.


    “Samahani, nlikuona asubuhi uko tofauti sana. Vipi kuna nini dada'angu?”


    “Aaah, James ni maisha tu, kuna mambo yanan’sumbua sana na nashindwa nifanyaje.”


    “Sema tu dada'angu mi n'tajaribu kukusaidia japo hata ushauri.”
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    “Usijali James n'takuelezea kesho, nakuahidi.”


    “Sawa dada Jane,” James aliitikia kauli ya Jane. Jane alielekea katika mlango wa chuma chake. Chumba chake ambacho kilikuwa kipo karibu na geti la kutokea nje. Aligeuka na kumwona James ameshikilia geti.


    “Usiku mwema Jane.”


    “Usiku mwema James.” Kisha aliingia ndani.




    *****
    JANE Amos aliondoka nyumbani kwao ambako alikuwa akiishi na mama yake wa kambo baada ya baba yake kuoa mke mwingine. Mama'ake aliyemzaa, Janeth, alifariki dunia wakati Jane akiwa bado mdogo sana. 
    Malaria kali iliyomsumbua kwa kipindi kifupi wakati akimnyonyesha Jane yalimfanya aache huduma hiyo ya kumnyonyesha na kuanza matibabu. Hakuna aliyemtegemea zaidi ya Amosi. 
    Amos aliacha kwenda safari na kumhudumia mke wake. Ni mwezi mmoja tu ulitosha kutaabika kabla ya kufariki dunia na kumwacha Jane akiwa mdogo sana. Amos hakujua la kufanya. Baadhi ya ndugu walifika mara kwa mara kumsaidia Amos kumlea Jane. Mwishowe rafiki na ndugu walimshauri Amosi aoe. Alifanya kama alivyoshauriwa kwa ajili ya mtoto wake. Alimpenda sana Jane kama ilivyokuwa kwa mke wake Janeth.
    Alikumbuka siku ya kwanza alipokutana na Janeth. Pambano la kati ya Yanga na Polisi Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma. Janeth alikuwa anafanya kazi ya kuuza maji. 
    Amos alikuwa ni mmoja wa walionunua maji ya Janeth. Wakati Janeth anashusha ndoo yake ili kuwapa maji wateja wake. Simu yake aliyokuwa ameiweka kifuani ilidondoka. Aliwahi kuiokota lakin Amosi alikuwa tayari ameiokota kwa vile alikuwa ameketi akiangalia mechi.
    Janeth alimwangali Amos kwa aibu baada ya kugundua kwamba wakati anainama aliona sehemu ya kifua chake.
    Amosi alitabasamu. Alisita kumpa ile simu Janeth. 
    “Naomba simu yangu,” Janeth alilalamika akiomba Amos ampe simu yake.
    “Aaah, dada. Embu kaa kwanza hapa. Unawaziba watu wasione mechi.”
    “Huoni niko kwenye biashara, siwezi kukaa mimi. Naomba hiyo simu.”
    Baadhi ya mashabiki walianza kufoka baada ya kuona Janeth akiwakinga kuona uwanja.
    “We dada kaa na maji yako,” sauti ya moja wa mashabiki waliokuwawakifatilia kwa makini mechi ilimshtua Janeth. Alikaa haraka kuhofia matusi zaidi. 
    “Unaona sasa. Mi nawajua hawa mashabiki.”
    “Nipe simu yangu nimesema. Si umeshachukua maji.” Subiri chenchi yako.”
    “Mbona wewe unayo chenchi yangu mi silalamiki.”
    “Haya chukua, nipe simu mi niende,” Janeth alikuwa mkali.
    “Basi utakachokikuta huko usishangae.”
    “Nini.”
    “Ndiyo dada,” Amos alimpa simu Janeth na kumruhusu aondoke. Janeth aliendelea na kazi yake.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    *****
    Baada ya mechi, macho ya Amos yalikuwa yakimtafuta Janeth. Alimtafuta kila mahali. Aliamua kutoka na kwenda mbele ya lango kuu la kuingilia uwanjani. Alijua tu Janeth atakuwa yuko ndani akimalizia kuuza maji kwani wengi walinunua maji muda huo.
    “Majiii,” aliita kwa nguvu.
    Mmoja wa wauzaji aligeuka. Hapo Amos aligundua si yeye aliyemwita. Lakini yule dada alikuja na kumsikiliza Amos. 
    “Mia mbili,” yule dada alisema.
    “Naomba moja,” Amosi alitoa shilingi mia mbili na kumkabidhi yule dada. Alitamani simu ya Janeth ingekuwa na salio kwani baada ya kuandika namba zake kwenye simu ya Janeth, alijaribu kubipu simu lakini haikuwa na salio.
    Hakukata tama, aliendelea kusubiri. Alikaa chini ya mti na kununua sigara moja. Aliiteketeza yote. Watu walikuwa bado wakitoka. Alinunua nyingine ikawa vilevile. 
    Akiwa ameegemea mti. Alimwona Jane akitoka na ndoo yake ya maji kichwani. Tena akija upande ambao alikuwepo.
    “Majiii,” Amosi aliita tena. Safari hii alikuwa ni Janeth. Aliyawahisha kwa Amos.
    “Unanikumbuka?” Amos alianza kumwambia Janeth.
    “Ndiyo, usizoee tena simu yangu,” Janeth alisema huku akicheka.
    “Sihitaji maji kwa sasa, nahitaji kuzungumza na wewe.” Amos alimdokeza Janeth.
    “Hapana niko na biashara zangu,” Janeth alionyesha kukataa.
    “Shusha ndoo chini tafadhali,” Amosi aliishika ndoo na kuishusha kutoka katika kichwa cha Jane. Aliifungua na kuangalia maji yaliyokuwa ndani. Zilikuwa zimebaki chumba ndogo kama tano. Kwa hesabu za harakaharaka Amos aliona kama zote zingegharimu shilingi elfu mbili.
    Alitoa noti ya elfu mbili na kumkabidhi Janeth.
    “We kaka, si umesema huitaji maji, hela ya nini sasa?” Janeth alifoka huku akiinua ndoo yake na kujitwisha.
    “Hapana, usifanye hivyo. Naomba uipokee. Nafanya hivi kwa sababu nataka kuongea na wewe. Nimehesabu chupa za maji ndani ya ndoo nikakadiria. Ili nisiwe nimepoteza muda wako nikaona nizilipie zote hata ukimaliza maongezi na mimi utaendelea kuuza.”
    “Sawa, haya ongea.”
    “kwanza nilikuwa naomba kujua jina lako dada.”
    “Naitwa Janeth,” Janeth alijibu kwa kujiamini.
    “Na unakaa wapi hapa Dodoma?” swali hilo halikumwingia vizuri Janeth. Hakujua alijibu vipi. Aliamua kumdanganya Amos. 
    “Naishi Kikuyu.”
    “Sawa, mimi naitwa Amosi. Naishi Kizota. Sio mbali sana kutoka hapa tulipo.”
    “Nimekupa namba yangu. Nadhani umeona namba yangu mpya katika simu yako.”
    “Nimeiona.”
    “Sawa, kabla ya kulala naomba unibipu nitakupigia.
    “Sawa, nitakupigia.” 
    Janeth alipatwa na aibu. Alimwangalia Amosi kwa macho ya kuibia. Ile hali ya kujibu kwa ukali haikuja na wala hakuifikiria. Upole ulemvaa na kusahau kuhusu maji.




    *****
    Saa nne na robo usiku, simu ya Amos ilianza kuita. Hakuwa na haraka nayo kwani alijua ni Janeth anabipu. Alimalizia kumimina chai yake tayari kwa kuinywa. Alipiga funda mbili na kuichukua simu yake. Alikuta ni Janeth aliyebipu. Alitabasamu kidigo na kujiweka sawa.
    “Halow, “ Amos alianza kumwita Janeth.
    “Ehh, mambo,” Janeth aliitikia na kumsalimia Amos.
    “Poa, nimefurahi ulivyonibipu.”
    “Ndio, ulikuwa unasemaje kwani.” Sauti ya Janeth ilikuwa ya woga. Ilitetema kama mtu aliyehojiwa kwa mara ya kwanza na polisi kwa kosa la kusingiziwa.
    “Janeth, ni kama bahati leo nimekutana na wewe. Haikuwa mara ya kwanza kukuona. Ila kwa uzuri wako na jinsi ulivyo umenivutia sana. kwa kifupi tu. Napenda tuwe wote.”
    “Haloow,” Amos aliita. Janeth alikuwa amenyamaza kimya akimsikiliza Amos. Aliona kama bahati ikija mbele.
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    JANE ANAMPOTEZA MAMA YAKE AKIWA BADO MDOGO. AMOS ANAKUMBUKA UHUSIANO WAKE NA JANETH. JANETH ANAKUWA MPOLE KILA ANAPOSIKIA SAUTI YA AMOS. ANAHISI KUNA KITU KINAKUJA MBELE.
    NI KITU GANI ANATEGEMEA JANETH…


    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog