Search This Blog

Monday, October 24, 2022

JICHO LA KAMORE - 2

 





    Chombezo : Jicho La Kamore

    Sehemu Ya Pili (2)



    *****

    SUZANA alizaliwa miaka 20 iliyopita huko Kondoa mkoani Dodoma. Elimu ya msingi aliipata katika shule ya Jamhuri kabla ya kuikwaa elimu ya sekondari katika Shule ya Wasichana ya Tabora. Baada ya kuimaliza miaka minne hapo Tabora na kuambulia alama zisizoridhisha katika matokeo ya mtihani wa mwisho, akaamua kulivaa jiji la Dar es Salaam ambako alifikia kwa dada yake. Mwezi mmoja baadaye, kwa jitihada za huyo dada yake, alipata ajira katika kampuni moja iliyouza vifaa mbalimbali vya ofisi na shule. Na miezi minne baada ya kuanza kazi, alihama kwa dada yake, Sinza Kwa Remmy na kwenda kuishi Magomeni.



    Suzana alikuwa kivutio kikubwa mtaani alikoishi. Wanaume wakware walimtazama mara mbili-mbili, baadhi yao wakimbembeleza mithili ya waombao ajira. Kuna ambao baada ya kumsumbua sana, wakitumia hata pesa kwa wingi, kwa kuwaonea huruma aliwapa 'zawadi' waliyoihitaji. Pia, walikuwepo ambao pamoja na kutumia mbinu hiyo bado walijikuta wakiambulia patupu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kamore alikuwa ni miongoni mwa waliovutiwa na umbo pamoja na sura ya Suzana. Alimtamani, akamhitaji. Na kufuatia taarifa alizopewa na vijana wa vijiweni, akaona hatapata shida kumnasa. Alichofanya ni kumvizia katika baa aliyopendelea kwenda kunywa bia. Hazikupita siku tatu, akamwona akiingia katika baa moja iliyotulia. Akamfuata. Akaketi meza moja pamoja naye, akiwa ni kama wateja wengine wa kawaida walioingia katika baa hiyo.



    Nusu saa baadaye walikuwa wamezoeana kufuatia mazungumzo ya kawaida yaliyovitawala vinywa vyao. Na ndipo Kamore alipoamua kurusha ndoana kwa mzunguko wa mbali akihitaji kupata miadi ya kuonana tena kesho yake.



    “Kesho?” Suzana alionekana kushangazwa na kauli ya Kamore.



    “Yeah, kesho.”



    “Huwa sina kawaida ya kuingia baa kila siku.”



    “Siyo lazima kukutana baa,” Kamore alisema. “Tunaweza kukutana popote pale, tukaongea kwa kirefu.”



    Suzana aliguna, akauliza, “Lakini ni maongezi gani hayo ambayo hatuwezi kuongea leo na muda huu?”



    “Ni maongezi ya kawaida tu, dada'ngu,” Kamore alijibu huku akitokwa na tabasamu pevu, tabasamu la kujiamini sanjari na kumtazama kwa macho ya kirafiki, zaidi ya urafiki wa kawaida. “Hauonekani kuwa ni mtu wa kushangazwa na ombi langu,” aliongeza. “Vaa yako, sura yako, tembea yako na umbo lako vinaonesha bayana kuwa uko katika dunia ya kisasa. Vipi, uwe na wasiwasi? Nilitegemea utoe tamko la ama hutaki kuongea na mimi, ama una nafasi finyu ya kuzungumza na mnyonge mimi, ama lini, wapi na muda gani tukutane na kuzungumza.”



    Suzana alitabasamu. Lilikuwa ni lile tabasamu lake ambalo mara nyingi huwaroga wanaume kiasi cha kumwona kuwa ni mwanamke zaidi ya wanawake. Mara tabasamu hilo lilikatika. Akaitazama saa yake ya mkononi. Sasa hakukiona kipingamizi cha kumfanya asikubaliane na ombi la Kamore. Akakubali bila ya hiyana, bila ya kulijua lengo kamili la Kamore. Kwa ujumla alikuwa mtu wa kupenda kuzungumza na kubadilishana mawazo na watu. Na maongezi ya jioni hii na Kamore yalikuwa ya kawaida, yasiyohusisha mapenzi, na hakukuwa na dalili yoyote ya Kamore kumtaka kimapenzi. Hivyo hakuwa na wasiwasi wowote.



    “Tufanye saa ngapi?” Kamore alimwuliza.



    “Natoka kazini saa kumi na moja. Labda tufanye saa moja.”



    Kamore alifikiri kidogo. Suzana alishamwambia kuwa hana tabia ya kuingia baa kila siku. Sasa watakutana wapi? Apendekeze kukutana nyumbani kwake Kamore? Hapana. Hilo nalo akaona ni wazo ambalo linaweza kukumbana na kipingamizi. Bado walikuwa wabichi sana katika uhusiano. Wamekutana leo, na leo hiihii wakubaliane kukutana nyumbani kwa mmojawao?



    Akilini mwa Kamore hakuona kuwa hilo linaweza kuwa tatizo lakini aliamini kuwa Suzana asingekubaliana naye kwa kuhisi kuwa anaweza kuonekana ni 'maharage ya Mbeya.' Rahisi mithili ya changudoa. Na alitambua fika kuwa kama atamtupia mpira Suzana kwa kumwuliza ni wapi panapostahili kukutana, kwa vyovyote vile Suzana atakwepa; atajibu, “Sijui.” Hivyo, mwanamume akaamua 'kukaza buti.'

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akamwambia, “Japo unasema si kawaida yako kuingia baa kila siku, lakini nadhani hautakuwa umevunja sheria kwa kudiriki kuja tena kesho kwa minajili ya kukutana. Haitakuwa vibaya, Suzy. Unasemaje?”



    Suzana alionekana kuzama mawazoni. Akamtazama kidogo Kamore na kuhamishia macho kaunta haraka. Kisha akashusha pumzi ndefu. “Okay, tufanye hivyo,” hatimaye alisema.



    “Nashukuru sana,” Kamore alifurahishwa na kauli ya Suzana. Akaongeza, “Muda kama wa leo si unafaa?”



    Suzana alitikisa kichwa akiashiria kukubali.



    *****



    ILIKUWA ni kama walivyokubaliana. Bia zikatua mezani. Na ndipo Kamore, baada ya kupata bia mbili, tatu hatimaye aliamua kuliondoa dukuduku lake. Akamshushia Suzana 'mashairi' ya mapenzi, 'mashairi' ambayo yalishakinai moyoni na masikioni mwa Suzana. Si mara moja au mbili alishaimbiwa sana 'mashairi' hayo na wanaume tofauti, baadhi yao wakiwa ni wale ambao kwa marika yao na kwa jinsi alivyowaheshimu, hakutegemea kuwa wangediriki kufumbua vinywa vyao na kumtamkia yale waliyomtamkia.



    Kwa uzoefu wake wa kuzisikiliza kauli za wanaume waliompenda na wale waliomhitaji, hakuwa mbumbumbu wa kutotambua kuwa nani anatamka kutoka moyoni na maneno ya nani yanatoka kinywani tu. Kwa ujumla aliweza kujua nani ni mkweli na nani ni mwongo.



    Kwa takriban dakika kumi alizokuwa akimsikiliza Kamore, alijenga imani kuwa kuna asilimia tisini na tano za ukweli katika maneno yake. Aliyaamini maneno yake! Lakini, pia kwa muda mfupi tu waliokuwa hapo, Suzana alishangazwa na matumizi yaliyodhihirisha kuwa Kamore hakuwa na uhaba wa fedha.



    Aliwanunulia watu sita bia mbili- mbili kila mmoja, alilipa shilingi 30,000 za rafikize waliokunywa bia jana yake, na alimpatia shilingi 20,000 jamaa yake mmoja aliyekuja pale kumwomba msaada wa kifamilia. Almradi alitumia pesa kiajabu-ajabu akionekana kutokuwa na wasiwasi wowote. Zaidi, uso wake ulionekana kuitangaza fahari kwa matumizi hayo. Ndiyo, alijisikia huru, na alikuwa huru kustarehe kwa kiwango alichotaka.



    Kuna wakati alichomoa pochi yake na kutoa noti moja kwa minajili ya kumlipa mhudumu. Ni wakati huo ndipo macho ya Suzana yaliposhuhudia wingi wa noti za shilingi 10,000 zikiwa zimebanana ndani ya pochi hiyo. Alishangaa, lakini hakushangazwa na wingi wa pesa hizo, alishangazwa na mfumo wa matumizi. Na pia hakutaka Kamore ajue kuwa anashangaa.



    Alijiuliza, kama kwa kipindi hiki kifupi ametumia pesa nyingi kiasi hiki, na bado anazo nyingi ndani ya pochi, je, ni kiasi gani alichotumia jana na juzi? Ni kiasi gani alichokiacha nyumbani? Na kama anajali kuweka pesa benki, ni kiasi gani alichokihifadhi katika akaunti yake?



    Kwamba Kamore ana kisima cha pesa, ni wazo lililomjia Suzana kichwani wakati huo na kupata imani zaidi pale Kamore alipomkabidhi noti tano zenye thamani ya shilingi 50,000 akidai kuwa ni za supu.



    Shilingi 50,000 eti ni pesa za supu! Suzana alishangaa. Ndio, alishangaa, na mshangao huo ulikuwa ni maradufu ya ule mshangao wa mfumo wa matumizi ya Kamore. Lakini alijitahidi kutouweka bayana mshangao huo kiasi cha kubainika machoni na akilini mwa Kamore. Na zaidi, alistahimili hata pale bia zikiwa zimekwishatambaa katika mishipa ya fahamu za Kamore, alidiriki kumkumbatia na kumbusu bila ya kuyaogopa macho ya watu.

    Muda ulizidi kwenda, bia zikinyweka, nyama-choma zikilika. Hatimaye bia ziliwakinai, nyama zikawashibisha. Wakaamua kuondoka. Wakati huo ilikwishatimu saa 5 usiku. Njiani, Kamore akatoa pendekezo la kuumaliza usiku huo wakiwa pamoja.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mara hii?” Suzana alishangaa. “Mbona mapema hivyo? Sidhani kama kuna haja ya kuharakisha kiasi hicho.”



    Kamore hakukubali. Alikuwa king'ang'anizi. Akapanga maneno katika kumbembeleza Suzana. Akasema hili na lile, akibembeleza na kusihi. Lakini pamoja na kuzungumza kwa utulivu sana, akipanga maneno yake kitaalamu, bado Suzana alihisi kuna jambo moja, kwamba Kamore anampenda, lakini kiwango cha mapenzi hayo ni kidogo sana tofauti na jinsi anavyomtamani. Kwamba, huenda wapo wanawake wengi waliokwishaambiwa maneno kama hayo aliyoambiwa yeye, wapo waliomruhusu awakumbatie, awabusu na hata kuwatomasa kipupa-pupa, na wapo pia waliodiriki kumchojolea nguo kwa hiari au kwa ushawishi wa pesa zake.



    Fikra hizo zilimfanya ajisikie kumwona Kamore kama kiumbe asiyetofautiana na funza wa chooni. Ile huruma ya kumchojolea nguo, huruma iliyoanza kumjia dakika chache zilizopita, sasa iliyeyuka ghafla. Badala yake akajiwa na wazo jipya, wazo la kumtumia. Amtumie kwa nguvu mpya, ari mpya na kasi mpya. Ndiyo, amtumie ili anufaike. Ni dhamira hiyo iliyompa mori wa kutoa tamko, tamko alilodhamiria kuwa liwe ni ahadi ya kudumu.



    “Vuta subira, mpenzi,” alimwambia kwa mnong'ono. “Nipe siku mbili, tatu hivi. Usiwe na haraka. Usiwe na pupa. Mimi ni wako. Kama huniamini...”



    “Nakuamini,” Kamore alimkata kauli. “Sina shaka yoyote. Najua wewe siyo mhuni. Huwezi kunidanganya. Kama hutaki si ungesema tu?”



    Kitendo cha Kamore kumkata kauli Suzana, kilikuwa nafuu ya Suzana. Alitaka kumpa namba yake ya simu japo kwa shingo upande. Lakini sasa akajisahihisha. Akaamua kukaa kimya. Isitoshe hata simu yenyewe alikuwa kaizima tangu walipokutana. Na alifanya hivyo kwa makusudi ya kutoombwa namba yake. Hata hivyo Kamore alikumbuka kuhusu suala la simu. Akasema, “Suzy, naomba namba yako ya simu.”

    “Sina simu,” alijibiwa.



    “Huna simu?” Kamore alishangaa.



    “Ndiyo.”



    “Kwa nini? Mrembo wa aina yako unakuwa huna simu?”



    Suzana alicheka, kisha akasema, “Siyo ajabu. Lakini kwa kweli simu yangu ni mbovu. Iko kwa fundi, na fundi mwenyewe kafiwa. Yuko kwao huku Kisarawe. Atarudi baada ya siku tatu hivi.”



    Ulikuwa ni uongo uliokuwa ukweli akilini mwa Kamore. Hakudadisi tena. Na Suzana hakutarajia kumpatia namba yake ya simu mapema kiasi hicho. Alihitaji muda wa kumjua vizuri Kamore kabla hajaamua kumpa namba ya simu. ‘Ipo siku nitampa, siyo leo.’



    Siku zilikuja, siku zikaenda, bado Kamore alikuwa hajapata kile alichokihitaji. Hata hivyo alijipa matumaini kwa kufuata ule usemi wa “subira yavuta heri.” Naye Suzana akitaka kumtumia vilivyo Kamore, alihakikisha anamweka karibu zaidi. Alimpa uhuru wa kumkumbatia na kumtomasa sehemu yoyote ya mwili wake. Ilifikia hatua ya kuchezeana kimahaba kwa kiwango ambacho ni nadra sana kwa mwanadamu mwenye ukamilifu wa kila kiungo kuweza kustahimili kutofanya ngono.



    Suzana aliweza kustahimili. Japo alimhurumia sana Kamore kwa jinsi alivyotaabika, hata hivyo ile dhamira yake ya kumtumia kwanza ilizidi kujenga himaya katika nafsi yake. Kwa Kamore, japo Suzana alikuwa hajampa kibali rasmi cha kupenya katikati ya miguu yake kwa starehe rasmi ya mapenzi, hata hivyo aliona fahari kuonekana mitaani wakiwa pamoja.



    Na katika kuhakikisha kuwa Suzana hamtelekezi, Kamore alijijengea kinga aliyoamini kuwa ni madhubuti. Alitoa huduma nyingi na kubwa kwa Suzana. Kwa kipindi kifupi tu Suzana akawa na samani nyingi na za thamani kubwa. chumba kilifurika samani zenye mvuto. Wala si kwamba Kamore aligharimia vitu hivyo tu, bali pia alimpatia pesa zisizo haba mara kwa mara. Hazikupita siku tatu bila ya kumpatia pesa kati ya shilingi 50,000 na 200,000. Tayari Suzana alikuwa na akaunti yenye shilingi 1,500,000 katika benki moja jijini Dar es Salaam.



    Uonevu Suzana aliwaza. Mwanamume wa watu kajitolea kumhudumia kwa kiwango kikubwa hivi, halafu bado anamzungusha! Kama siyo uonevu, ni nini? Kama siyo wizi, ni nini? Kama siyo dhuluma ni nini? Kama siyo unyanyasaji ni nini? “Dhambi!” alinong'ona. Sasa huruma ikamwingia, huruma ya kujitoa mzima kwa Kamore. Ndio, amwachie mwili wake wote, autumie apendavyo, auchezee atakavyo. Aliamua hivyo. Lakini siyo leo, siyo kesho. Alitarajia kuitoa zawadi hiyo baada ya kuwasiliana na dada yake, Martha. Asubuhi moja ya siku ya Jumamosi akaamkia kwa Martha.



    Akamkuta.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    *****



    “JIHADHARI na wanaume wa siku hizi, Suzy,” lilikuwa ni onyo la Martha baada ya kusikiliza maelezo ya Suzana kwa muda. Akaendelea, “Inabidi uwasome sana wanaume wa siku hizi. Wengi wao ni mafataki. Mwanamume anaweza kukufanyia mambo mengi mazuri, lakini akiwa na dhamira moja tu; kuuchezea mwili wako.



    “Na huwezi kujua, labda huyo jamaa ni mfanyabiashara wa dawa za kulevya. Mtu wa ‘unga’ ni hatari sana. Huwa yuko tayari kufanya lolote kwa gharama yoyote ili afanikishe analolitaka. Na mtu mwingine wa kuogopa yule mwenye madaraka serikalini au bosi wa shirika Fulani. Mtu mwenye wadhifa wa juu serikalini au katika shirika anaweza kutumia wadhifa wake huo kulihujumu taifa kwa kuchota mamilioni ya fedha bila taabu yoyote. Yaani kwa jina jingine watu wa aina hiyo siku hizi wanaitwa MAFISADI. Fisadi yeyote, kuhonga milioni moja kwake siyo tatizo. Hana uchungu nazo, na hakuzipata kwa kuvuja jasho bali amezichota kwa wavuja jasho!



    “Tatizo ni kwamba, labda siyo wewe peke yako, mko wengi tu mnaopewa huduma hizo, na labda wengine wanapewa vingi zaidi yako. Ni pale atakapokutema ghafla ndipo utakapojikuta ukihangaika kumtafuta wa kukuoa. Na huenda wakati huo umri wako umeshakwenda, na pia hujui kama jamaa huyo alikuwa mzima, asije akawa amekuzawadia tiketi ya kifo!”



    “UKIMWI?!”



    “Nd'o maana a'ke,”Martha alisisitiza.



    “Dadaa!” Suzana aliziba kinywa kwa kiganja cha mkono wa kushoto.



    “Yeah, hilo pia ni muhimu kulizingatia,” Martha alisema. “Kwa ujumla baada ya kutemwa na huyo jamaa, hata wale ambao walikuwa wanakutaka zamani huenda wakakuangalia kama uchafu fulani usiotazamika na unaochefua.”



    Akasita kidogo akimtazama Suzana kwa macho makali. “Chunga sana, Suzy,” aliendelea. “Cha muhimu ni kwamba, badala ya kuendelea kudanganyana kwa uhusiano wa aina hiyo, jaribu kumpa pendekezo la kufunga ndoa. Yeye ni Mkristo au Mwislamu?”



    “Mkristo.”



    “Kumbe shwari tu. Mshinikize kufunga ndoa. Hata ka' yeye s'o Mkatoliki mwenzako, hilo lisikukondeshe; fuata madhehebu yake. Mwambie hautaki kuchezewa, kama kweli anakupenda basi afike kwa wazazi kujitambulisha kuwa ndiye mchumba wako, na baada au kabla ya kufika kwa wazazi, hakikisha mnakwenda kupima. Dunia ya sasa imekwisha, mdogo wangu. Kupima HIV ni muhimu.”



    “Nimekuelewa dada,” Suzana alisema. Kisha kwa unyonge aliongeza, “Lakini dada, mtu mwenyewe yule...mara nyingi huwa anasumbua...”



    “Anasumbua?” Martha hakumwelewa. “Anasumbua...anasumbua kivipi?”



    Suzana alicheka kidogo. Sasa Martha alielewa.



    “Umewahi kufuatilia nyendo zake kwa makini?” Martha alimwuliza.



    “Ndio,” Suzana alijibu huku akijua fika kuwa anajibu uongo. Ukweli ni kwamba hakuwahi kuzifuatilia nyendo za Kamore hata mara moja. Ya nini kumfuatilia ilhali hata moyoni mwake hakuwamo?



    “Na unamwonaje, sio mhuni? Hana tabia za kifataki-fataki?”



    “Kwa hilo sina jibu la uhakika. Lakini kwa kweli sijawahi kusikia au kumwona na mwanamke.”



    “Hiyo si hoja,” Martha alitikisa kichwa kwa masikitiko. “ Unapaswa kuzijua nyendo za bwana'ako ambaye hujadiriki kumvulia nguo, Suzy. Hilo ni muhimu sana hasa katika kipindi hiki cha magonjwa yasiyotibika! Zaidi, ukiwa tayari kustarehe naye, kondomu ipewe kipaumbele.”



    Kicheko kikali kilimtoka Suzana. “Na mwanzo wa kuvaa kondomu nd'o mwanzo pia wa kuja kuachana nayo siku moja, na kucheza peku,” alisema. Akaongeza, “Dada, kubali usikubali, siyo rahisi kumvalia kondomu mpenzio mara kumi mtakazokutana. Huo nd'o ukweli. Kondomu itavaliwa mara tatu, nne, basi. Kitakachofuata ni kujisikia kuaminiana, na hapo ndipo kosa litakapofanyika, kama kweli ni kosa.”



    “Hiyo ni kweli,” Martha alikiri. “Basi kwa kifupi, cheza unavyojua. Ulishamgeuza bwege, mchune kiasi chako, shosti. Lakini kama kweli unampenda...”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Simpendi!” Suzana aliwaka.



    “Humpendi?”



    “Ndio, simpendi!”



    “Hata kidogo?”



    “Hata kikubwa!” Suzana alibwata. “Nazijali huduma zake tu. Kama ningekuwa nampenda nisingekuwa namchezeachezea tu kisha namwacha akitaabika huku mimi moto ukiniwakia.”



    Martha aliguna. Akamkazia Suzana macho makali. “Suzy, ya kweli hayo?” hatimaye alimwuliza kwa sauti ya chini.



    “Sikutanii da' Martha. Nimekueleza ishu hii kwa kuwa huruma imeniingia. Tafadhali unielewe, ni huruma siyo mapenzi!”



    “Huruma?!” Martha alimshangaa. “Huruma ya nini tena?”



    “Ya kumchuna. Kwa kweli ni'shamchuna kishenzi. Nilikuwa nafikiria kuwa sasa nimruhusu japo mara moja.”



    “Umruhusu?” Martha alicheka.



    “Usicheke da'Mratha,” Suzana alisema kwa huruma.



    “Kha! Nisicheke kwa nini?” Martha alifyatuka. “Nilie kwani tuko msibani? Akha babu! Kwa kweli unanichekesha, na kwa nini nisicheke? Eti unamwonea huruma! Huruma ya kumchuna?!”



    Mara akakikata kicheko na kukohoa kidogo. Akaendelea kumtazama Suzana, safari hii tabasamu pekee ndilo likiwa limeutawala usowe. “Lakini kwa kweli mdogo wangu una bahati ya mtende,” hatimaye alisema. “Huyo bwana anaonyesha dhahiri kuwa ana kisima cha pesa. Kisima kisichokauka. Au ni fisadi wa EPA?”



    Kwa mara nyingine vicheko vikatawala chumbani humo, safari hii wote wakiangua kwa mkupuo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog