Search This Blog

Monday, October 24, 2022

KAHABA - 5

 





    Chombezo : Kahaba

    Sehemu Ya Tano (5)



    ILIPOISHIA



    “Mh! Haya bwana. Waswahili walisema mtu chake. Tutaona hiyo jioni kama hizo sifa unazompamba kweli anazo?”. Mama Careen aliongea.



    SASA ENDELEA



    “Hodi humu ndani!”. Nilipiga hodi mara baada ya kufika nyumbani na kubaini kwamba mlango ulikuwa umefungwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa upande wa wakati ilikuwa ni majira ya mchana. Nilikuwa nimerudi nyumbani mapema ili nipate kujiandaa kwa ajili ya safari yangu na Jasmine kwenda kwa dada yake kwa ajili ya kunitambulisha.



    Sikutaka kabisa kumwangusha mpenzi wangu Jasmine.



    Mlango ulifunguliwa na mama Careen ambaye leo alinishangaza sana. Uso wake ulikuwa na furaha kubwa sana tofauti na siku zote katika maisha yetu ya ndoa. Hakika sijawahi kumshuhudia mke wangu akiwa katika hali hii ya furaha katika maisha yetu ya ndoa.



    Furaha ile iliufanya uso wake uchanue na kuuruhusu uzuri wake uonekane dhahiri. Hakika mke wangu alikuwa ni mwanamke mzuri sana ila uzuri wake siku zote ulikuwa ukifunikwa na ukali wake.



    Roho yangu sasa ilianza kuniuma. Nikaanza kujilaumu ni kwa nini nilikuwa nikimsaliti mwanamke huyu ambaye mwenyezi Mungu alikuwa amenipatia.



    Ikafika kipindi mpaka nikataka nighairi safari yangu ya kwenda kwa Jasmine lakini nikaamua kukaza kwamba kwani nilimfahamu sana huyu mwanamke. Aliku-wa ni mwanamke ambaye alikuwa hatabiriki.



    “Leo tuna mgeni mume wangu”. Mama Careen aliongea kwa furaha.



    “Mgeni?”. Niliuliza kwa staajabu.



    “Ndiyo mume wangu”. Mama Careen alijibu.



    “Mgeni gani?”. Name nikauliza.



    “Mdogo wangu, yule ambaye nilikuwa nikikupa habari zake kila siku”. Mama Careen akaongea.



    “Anhaaaaaa! Basi hamna tatizo”. Nilimjibu mama Careen mara baada ya kukumbuka kwamba amekuwa akinieleza mara kwa mara kwamba ana mdogo wake ambaye anaishi katika jiji hili la Kano.



    Mama Careen akatangulia mbele kuelekea sebuleni akaniacha mimi pale mlangoni huku nikijiweka sawa mavazi yangu kwa lengo la kwenda kukutana na mgeni ambaye nilikuwa sijawahi kukutana naye hata siku moja.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilipoingia ndani moyo wangu ulitaka kupasuka kwa mshutuko mkubwa sana ambao uliupata. Macho yangu hayakuamini kile ambacho yalikuwa yakikishuhudia. Ubongo wangu ndiyo uligoma kabisa kukubaliana na picha nzima ambayo ilikuwa ikionekana pale sebuleni.



    “He! Mayanja vipi? Umekujuaje huku?”. Jasmine aliuliza swali ambalo lilileta utata kwa mama Careen.



    Mimi nikaiona hali ya hewa imeanza kuchafuka kabisa pale sebuleni. Nikakosa kabisa nmana ya kuweza kulinusuru lile balaa ambalo harufu yake ilianza kusikika.



    “Vipi Jasmine, kwani mnafahamiana?”. Mama Careen aliuliza kwa mshangao.



    “Huyu ndiye yule mchumba wangu ambaye nilikuwa nikikueleza hivi punde kwamba anataraji kunioa. Mayanja huyu ni dada yangu mpendwa anaitwa mama Careen”.



    Masikini Jasmine alikuwa akiyaongea haya yote asijue ni siri gani ilikuwa nyuma ya pazia. Hakujua kabisa kwamba aliyekuwa akimkaribisha alikuwa ni mwenyeji wa nyumba ile na ndiye ambaye alipaswa kumkaribisha yeye.



    Mama Careen hakukiamini kile ambacho alikuwa akikisikia. Alibaki amesimama akiwa ameduwaa huku macho akiwa ameyatoa mithili ya mjusi ambaye alikuwa amebanwa na mlango.



    Ghafla mama Careen alianguka chini na kuzimia. Kitendo kile kilizua tafrani kubwa mle sebuleni na kufanya kila mtu ataharuki.



    “Kwani ni nini kinaendelea Mayanja? Mbona sielewi?”. Jasmine alihoji wakati huo mimi nikiwa ninampepea mama Careen.



    “Fanya utaratibu tumuwahishe hospitali Jasmine. Huyu ndiye mke wangu niliyekuwa nakueleza siku zote”. Nilimweleza Jasmine.



    “Oooooooh! Mamaaaaaaa! Jamani Mayanja. Ni kwa nini umenitenda hivi. Mbona umenitia aibu ambayo nitashindwa kuibeba. Nitaiweka wapi sura yangu jamani?”. Jasmine naye alikaa chini na kuanza kulia.



    Mimi nikaona hapa nikifanya uzembe nitampoteza mama Careen. Nikachomoka mbio kutoka mle sebuleni na kuelekea nje ambako nilitafuta taksi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tulimpakia mama Careen na kumuwahisha hospitali. Na kwa wakati wote huo Jasmine alikuwa amempakata Careen huku akilia kwa uchungu.



    Tulipofika hospitali, tulimshusha mama Careen na manesi wakampokea na kumpeleka kwa lengo la kupatiwa huduma. Hali yake haikuwa nzuri hata kidogo.



    Mimi na Jasimine tulikaa katika dawati la kupumzikia huku tukimwomba mwenyezi Mungu atende muujiza wa kuyanusuru maisha ya mama Careen.



    Baada ya dakika kama ishirini hivi kupita, daktari alitoka na kutujia pale ambapo tulikuwa tumekaa.



    “Ok, wewe ndiye mume wa mgonjwa?”. Daktari aliuliza hilo kwa kuzingatia maelekezo ambayo tulikuwa tumeyaandikisha kwa nesi awali pindi tukimfikisha mgonjwa pale hospitalini.



    “Ndiyo dokta. Mgonjwa wangu anaendeleaje?”. Nilimwuliza daktari kwa bashasha ya kutaka kujua hali ya mama Careen.



    Daktari hakunijibu bali alinivuta na kunisogeza mbali kidogo na Jasmine. Moyo wangu ulikuwa una hofu kubwa sana kwa wakati ule.



    “Wewe ni mwanaume hivyo unapaswa kujikaza kiume kwa taarifa hii nitakayokupa”. Dakatari alianza kuongea huku akinigongagonga bega.



    “Unataka kusema nini dokta?’ Nilimwuliza daktari huku nikiwa nimemtolea macho.



    “Kwa bahati mbaya, mkeo tumempoteza. Amefariki dunia”. Maneno yale yaligota katika ubongo wangu na kuniletea kizunguzungu ambacho kinilinifanya nile mweleka na kuanguka chini.



    Baada ya hapo nikazirai.



    **********



    Mazishi ya mama Careen yalifanyika nyumbani kijijini kwetu. Ulikuwa ni msiba mkubwa sana ambao ulinipa uchungu mkubwa. Msiba huu ulikuwa umekitikisa kijiji chetu kutokana na umaarufu wangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jasmine kwa wakati wote huo alikuwa akilia asijue ni nini cha kufanya. Kifo cha dada yake kilikuwa kimemchanganya kabisa.



    Baada ya mazishi ya mama Careen tulikaa matanga.



    Msiba ulipokwisha, mimi na Jasmine tulirejea jijini Kano huku Careen tukiwa tumemwacha kijijini na bibi yake.



    Maisha yetu jijini Kano hayakuwa ya furaha hata kidogo. Ile furaha ambayo mimi na Jasmine tulikuwa nayo ilikuwa sasa imeyeyuka.



    Baada ya wiki mbili toka mimi na Jasmine tutoke kijijini, kuna tukio moja kubwa sana lilitokea. Tukio hili lilizidisha ule uchungu ambao mimi nilikuwa nao.



    Jasmine alikutwa akiwa amekufa kwa kunywa sumu huku akiwa ameacha ujumbe wa kunituhumu mimi kuwa ndiye msababishaji wa madhila hayo yote.



    Polisi walinikamata na kunifungulia mashtaka ya kusababisha vifo vya watu wawili ambao ni mama Careen na Jasmine. Kesi hii ilikuwa nzito na ililalia upande wangu.



    Hatimaye nikapatikana na hatia na nikahukumiwa kifungo cha miaka ishirini gerezani.



    MWISHO



    FUNZO

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Katika mahusiano ya ndoa yatupasa tuepuke tamaa. Turidhike na ndoa zetu. Siku zote tuishi katika kuzijenga ndoa zetu na si kuzibomoa. Tuepuke kufanya maamuzi ambayo baadaye huja kutugharimu sana.

0 comments:

Post a Comment

Blog