Chombezo : Jamani Dada Martha... Looo!
Sehemu Ya Tano (5)
“Mungu wangu, atakuwa nani amejitoa ufahamu mpaka kuamua kugonga geti langu?” alijihoji Roi akiwa anatafuta namna ya kutoka kwa mama Anna.
JIACHIE MWENYEWE SASA...
Roi alijitoa, akavaa bukta na kwenda sebuleni. Lakini akili ikamwambia kwamba amalizane na mama Anna kwanza, atoke kisha yeye amfungulie Martha wayaongee na kuyamaliza...
“Atanielewa tu,” alisema moyoni Roi.
Alirudi chumbani, kweli alimalizana na mama Anna na akamtoa huku mwanamke huyo akiamini kwamba, Roi hatamudu kukutana kimwili tena na Martha labda mpaka waende kwake au kama watalala hapohapo, basi usiku sana.
Wakati Roi anamtoa mama Anna, alimuahidi kwamba, atampa pesa kwa ajili ya kupanga chumba Sinza kama walivyokubaliana.
“Poa baby,” alikubali mama Anna akiwa anatoka geti la uani ambalo lipo ubavuni mwa nyumba hiyo na kutokomea upande wa pili kwa nyuma.
Roi alirudi chumbani na kumpigia simu Martha.
Martha akiwa bado dukani baada ya kugonga sana geti, alishangaa kuona simu ya Roi, akaipokea haraka sana huku akisema moyoni...
“Utadhani alikufa sasa amefufuka. Ngoja nimsikilize. Si ajabu anajua mimi nipo nyumbani, hajui kama nipo getini kwake...”
“Haloo...”alipokea Martha...
“Ee, nilikuwa sebuleni, simu ilikuwa kwenye chaja chumbani. Si unajua sijabeba chaja kuja nayo huko...”
“Roi,” aliita Martha...
“Sema...”
“Una uhakika upo sebuleni?”
“Kha! Sasa nipo wapi kama si sebuleni? Au wewe upo sebuleni kwangu?”
“Mimi nipo nje kwako hapa. Na nimeambiwa mengi sana kuhusu wewe.”
“Mengi kama?”
“Wewe unajijua. Unajua uko wapi na nani! Kama kweli upo sebuleni toka unifungulie geti.”
“Poa,” alijibu Roi na kukata simu huku moyoni akisema...
“Haya ndiyo mambo nisiyoyataka. Anaanzaje kunikontroo wakati anajua mimi si mume wake?”
Martha, alikwenda getini na kupiga kambi hapo akisubiri kufunguliwa. Yeye alijua Roi hawezi kufungua na kama atafungua kweli basi atakuwa ameongozana na mama Anna.
Alishangaa geti limefunguliwa, Roi akiwa ndani ya bukta tu, tena akionesha hana wasiwasi wowote ule...
“Unajua nikiwa hapa nyumbani sipendagi kuacha geti wazi. Si unajua naishi mwenyewe?” alisema Roi akimbusu Martha ambaye alikuwa mbali sana kimawazo...
“Ina maana maneno ya muuza duka si ya kweli?” alijiuliza Martha akiwa hajui akubali au akatae.
Walizama mpaka sebuleni, Roi akakaa hapo kisha akamwambia Martha kama amefika kufanya usafi, aanze na chumbani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Martha alisimama, akaenda chumbani. Lakini akashika mlango wa chumba cha kwanza, akaufungua, hakuona mtu, akashika mlango wa chumba cha pili, hakuona mtu, akaenda jikoni, hola. Akaenda stoo, hakuna kitu, akaenda chooni na bafuni hakukuwa na dalili ya kuwepo mtu...
“Mh! Basi yule kijana ni mwongo mkubwa. Afadhali hata ningemwona mwanamke, hata kama si mama Anna kuliko kutokuwa na mtu yeyote yule,” alisema moyoni Martha akiingia chumbani.
Sebuleni, Roi alikuwa kwenye kompyuta mpakato akibofyabofya huku akijivunia ushindi wake kwa mama Anna.
Martha alifanya usafi sehemu mbalimbali za nyumba hiyo hadi akafika sebuleni, kisha uani.
Alipofika uani, kwa mara ya kwanza alibaini kuwepo kwa mlango mdogo ambao mtu anaweza kutoka nje. Lakini ulikuwa umetiwa kufuli...
“Aa...aaaaa! mama Anna alikuwepo, ametokea mlango huu. Sasa nimejua,” alisema moyoni Martha huku hasira za wivu zikimpanda kama mwanamke.
Ili aujue ukweli alimfuata Roi sebuleni na kumwambia ampe funguo za mlango huo ili akatupe taka nje...
Kwa kujikaza sana, Martha alisema...
“Baby, naomba funguo za mlango wa uani. Nataka kutupa takataka.”
Roi naye alijua kimenuka au kitanuka, kwamba Martha atajua nini kiliendelea...
“Ooh! Baby, ule mlango tangu nimehamia nyumba hii haujawahi kufunguliwa na wala sijawahi kuona funguo yake. Pia kwa sababu ni uchochoroni sijawahi kutaka kuufungua,” alisema Roi kwa macho makavu kabisa.
Martha alikubaliana na utetezi wa Roi, moyo wake ukarejea katika hali yake ya kawaida.
***
Mama Anna alipotoka hapo, moja kwa moja alikwenda nyumbani na kuwasimulia wale mashoga zake, wapangaji wenzake kilichojiri nyumbani kwa Roi. Walicheka sana na kumshauri...
“Wewe usiwe mjinga. Pesa za kupanga za nini? Usipokee. Unachotakiwa kufanya wewe ni kung’ang’ania kuishi kule kwake. Mwambie wewe utakuwa unaishi kule yeye na Martha waishi hapa. Kwa hiyo akitoka kazini anakufuata kule. Mnajirusha halafu midamida anakuja huku,” alisema mmoja wa wanawake hao.
Mama Anna alikubaliana na ushauri huo kwani kwake aliuona kama ni wa kuweza kumfikuisha kwenye ndoa kabisa na kumpiku Martha.
***
Martha na Roi waliwasili nyumbani hapo, usiku wa saa tatu. Waliwakuta wapangaji wapo nje bado wakipiga domo licha ya kibaridi cha mbali.
Macho ya Martha yalitua kwenye sura ya mama Anna, akakasirika kwa mbali. Kilichomshtua zaidi Martha na gauni alilovaa mama Anna muda huo ndiyo lilelile ambalo aliambiwa na muuza duka kwamba, mwanamke aliyeingia na Roi ndani alikuwa amevaa...
“Inawezekana kweli mama Anna alikuwa amekwenda kula kwa Roi lakini labda hakukaa sana akatoka ila yule kijana wa dukani hakumwona ndiyo maana alijua bado yupo,” alisema moyoni Martha...
“Jamani za leo?” alisalimia Roi akiwa nyuma ya Martha wakiingia ndani...
“Nzuri tu za kwako shemeji?”
“Salama za kazi shemeji?”
“Salama za kazi honey,” alijibu mama Anna kwa sauti ya chini...
“Wewe usiwe mjinga. Pesa za kupanga za nini? Usipokee. Unachotakiwa kufanya wewe ni kung’ang’ania kuishi kule kwake. Mwambie wewe utakuwa unaishi kule yeye na Martha waishi hapa. Kwa hiyo akitoka kazini anakufuata kule. Mnajirusha halafu midamida anakuja huku,” alisema mmoja wa wanawake hao.
SASA ENDELEA MWENYEWE...
Mama Anna alikubaliana na ushauri huo kwani kwake aliuona kama ni wa kuweza kumfikisha kwenye ndoa kabisa na kumpiku Martha.
***
Martha na Roi waliwasili nyumbani hapo, usiku wa saa tatu. Waliwakuta wapangaji wapo nje bado wakipiga domo licha ya kibaridi cha mbali.
Macho ya Martha yalitua kwenye sura ya mama Anna, akakasirika kwa mbali. Kilichomshtua zaidi Martha ni gauni alilovaa mama Anna muda huo ndiyo lilelile ambalo aliambiwa na muuza duka kwamba, mwanamke aliyeingia na Roi ndani alikuwa amevaa...
“Inawezekana kweli mama Anna alikuwa amekwenda kule kwa Roi lakini labda hakukaa sana akatoka ila yule kijana wa dukani hakumwona ndiyo maana alijua bado yupo,” alisema moyoni Martha...
“Jamani za leo?” alisalimia Roi akiwa nyuma ya Martha wakiingia ndani...
“Nzuri tu za kwako shemeji?”
“Salama za kazi shemeji?”
“Salama za kazi honey?” alijibu mama Anna kwa sauti ya chini kiasi kwamba, Martha alijua amezungumza kitu kwa sauti ya chini ambayo hakuisikia hali iliyompa dukuduku kubwa sana...
“Baby,” Martha alimuita Roi wakiwa wameshazama ndani kwao...
“Yes! Niambie...”
“Mimi nahisi huyu mwanamke huyu...mama Anna ana jambo na wewe lakini sijalijua. Ila nalifanyia kazi.”
“Jambo kama lipi?”
“Kuna jambo. Mfano, hapo wakati tunaingia wenzake wamekusalimia. Hata yeye amekusalimia, lakini kuna maneno f’lani ameyasema naamini siyo salamu na ameyasema kwa sauti ya chini sana.”
“Mh! Mimi sijui kwa kweli. Labda ana mambo yake mwenyewe,” alijibu Roi huku moyoni akiujua ukweli.
***CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa saa nne usiku, Martha akiwa anapiga pasi sebuleni, Roi yuko chumbani. Nje, usawa wa dirisha la sebuleni kwa Martha, alikaa mama Anna peke yake. Alikuwa akichati na Roi kule chumbani.
Alichokishangaa Martha, simu ya Roi ilipotoa mlio wa meseji, baada ya dakika kadhaa, simu ya mama Anna kule nje nayo ilitoa mlio wa meseji.
Martha alishtuka, hasa baada ya kubaini kuwa, milio hiyo ya meseji ilikuwa ikipokezana kusikika. Kwamba, unapolia wa simu ya Roi, baada ya muda unadakia wa simu ya mama Anna...
“Mh!” aliguna Martha, akaacha kupiga pasi, akasimama kusikilizia kwa umakini zaidi...
“Titiri...titiri...” huo ulikuwa mlio wa simu ya Roi...
“Titiiiti...” huo ulikuwa mlio wa simu ya mama Anna.
Martha aliingia chumbani, akampiga jicho moja Roi, akamwona akiweka simu juu ya dressing table...
“Baby, nataka kumpigia simu bro, lakini kumbe simu yangu sijaweka salio, niazime ya kwako nimpigie,” alisema Martha...
“Mh! Hata yangu haina salio, chukua elfu mbili hii ukanunue vocha,” aliwahi kusema Roi, Martha akaanza kushtuka. Aliamini Roi alikuwa akichati na mama Anna nje.
Alikwenda dukani kununua vocha, wakati anarudi alisimama chini ya mti wenye giza na kumwangalia mama Anna anavyoongea na simu huku akicheka...
“Teh! Teh! Mimi ni mashine baby...tena nakwambiaje? Siku akijua naamini patachimbika. Lakini mimi wala simuogopi,” alisema mama Anna huku akicheka.
Akaendelea...
“Duu! Baby, mfano pale kwako. Mimi miguu yote ilinyong’onyea, nikajua tumekwisha! Loo!”
Martha alipojitokeza, mama Anna alishtuka, akapunguza sauti huku akisema...
“Basi tufanye kesho baby wangu, usiku mwema.”
Martha alipita bila kusema kitu kwa mama Anna, akazama ndani na kumpa Roi vocha ya buku, akabaki na ya buku kuingiza kwenye simu yake.
***
Ilikuwa saa saba usiku, Martha alichelewa kupata usingizi kwa mawazo kuhusu kutaka uhakika wa kuwepo kwa mawasiliano kati ya mama Anna na jamaa yake, Roi...
“Hivi kama ni kweli nichukue hatua gani?” alijiuliza moyoni Martha...
“Na yale mazungumzo ya kwenye simu ya mama Anna muda ule mbona ni kama alikuwa akiwasiliana na Roi?”
Ghafla alipata wazo, alitoka kitandani huku macho yake yakitua kwa Roi. Alipobaini anauchapa usingizi mzito, aliifuata simu yake, akaichukua na kwenda nayo sebuleni.
Aliikuta simu hiyo haina ‘password’ kwa hiyo akaingia ndani moja kwa moja kwenye kiboksi cha meseji...
“Baby, unajua wakati tunaongea ghafla akatokea demu wako, ndiyo maana nikakuaga.”
Meseji hiyo ilitoka kwa mama Anna kwenda kwa Roi. Martha aliishiwa nguvu, nusura aanguke. Akaendelea kusoma nyingine...
“Basi usiku mwema baby. Nimekumisije jamani!”
Roi naye akajibu...
“Mimi je? Natamani kesho ifike haraka tukutane unikate kiu yangu. Lala salama mpenzi wangu nikupendaye.”
Martha alisimama, akamwomba Mungu kwanza kisha akajipa moyo na ujasiri wa hali ya juu. Akatuma meseji kwa mama Anna...
“Baby...”
Ingawa ilikuwa usiku sana, Martha akaamini atajibiwa, lakini hakujibiwa, akatuma nyingine...
“Jamani baby, naomba nije kwako basi, nimekumisi kweli mwenzio.”
Dakika zilikatika, hakupata jibu. Akazifuta meseji zake hizo mbili na kuamua kurudi chumbani kulala. Alitamani sana kumwamsha Roi ili ambane kuhusu meseji hizo lakini akajivumilia. Aliirudisha simu mahali alipoichukua na kulala.
***
Kulikucha, Martha aliamka na kuanza kufanya kazi za ndani lakini siku hiyo hakumwamsha Roi mpaka alipoamka mwenyewe.
Roi, kabla hajatoka kitandani, aliichukua simu na kuangalia meseji, akakutana na meseji ya mama Anna ikiomba radhi...
“Baby samahani, ulipotuma meseji usiku nilikuwa nimelala fofofo mwenzako. Halafu uliposema umenimisi unataka kuja ulikuwa unamaanisha au utani tu? Bibiye ungemwachaje kitandani peke yake?”
Roi alishtuka sana. Akaangalia kama alituma meseji amesahau, hakuona meseji yoyote. Akahisi huenda meseji hiyo ya mama Anna ilimfikia yeye kwa bahati mbaya tu, akamuuliza…
“Sweet, meseji hii ya nani?”
Akajibiwa…
“Ya nani kwani darling. We unadhani inaweza kuwa ya nani zaidi yako jamani? Au unanituhumu kwamba nina mchepuko?”
“Mh!” Roi aliguna kwanza. Akakaa kitandani na kufikicha macho. Bado aliamini mama Anna anajitetea tu…
“Mimi nilikutumia meseji wewe ya kukutaka nije kwako?”
“Ndiyo. Kwani si imekuja kwa namba yako baby! Acha hizo bwana.”
Roi alitoka kitandani, akasimama na kujishika kichwa. Mapigo ya moyo yakamwenda kwa kasi ya ajabu.
Aliizima simu, akaenda kuoga. Aliporudi alivaa kisha akamuaga Martha kwamba anaondoka…
“Baadaye baby.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Poa sweetheart,” Martha alimjibu kama hakuna lolote jambo ambalo lilizidi kumchanganya Roi.
Hatua kumi hazikufika baada ya kutoka na gari, Roi alimtumia meseji mama Anna akimtaka akae sehemu nzuri anataka kumpigia simu…
“Piga tu baby, niko chumbani bado nimelala. Kwani we umeshatoka kwenda kazini?”
Roi hakujibu meseji ya kuulizwa kama ameshatoka kwenda kazini. Alichofanya yeye alimvutia uzi moja kwa moja…
“Yes baby, niambie,” alipokea mama Anna kwa sauti iliyojaa kudeka kimahaba…
“Hivi ulichosema ni kweli au utani?” aliuliza Roi…
“Kwamba?”
“Kwamba nilikutumia meseji ya kutaka nije kwako?”
“Khaa! Jamani! Sasa …kwanza nikuulize baby, kwani jana ulilewa?”
“Sikulewa. Hata wewe unajua sikulewa.”
“Sasa kwa nini usijue kama ulinitumia meseji mimi mke wako?”
“Sijatuma meseji ya hivyo kwako. Imeingia saa ngapi?”
“Mh! Hujatuma? Ilikuwa usiku kama saa saba hivi.”
“Kweli?”
“Kweli baby.”
“Meseji ngapi?”
“Mbili.”
“Zilisemaje?”
“Ya kwanza uliita baby…ya pili ukasema jamani baby, naomba nije kwako basi, nimekumisi kweli mwenzio.”
Roi alikosa nguvu, kidogo aiingize gari kwenye mtaro. Ni Mungu tu alimsaidia…
“Mimi siamini mpaka nizione hizo meseji kama kweli zimetoka kwenye namba yangu ya simu.”
“Ina maana huamini?”
“Siamini.”
“Nije ofisini kwako muda huu?”
“Itakuwa vizuri aisee. Njoo,” alisema Roi.
Roi alimwelekeza mama Anna ofisini kwake akimsisitizia kwamba aende na Bajaj, yeye atalipa.
***
Mama Anna naye alianza kuingiwa na wasiwasi. Alijua kama Roi hakutuma meseji zile basi aliyetuma ni Martha. Alitungua taulo, akavaa, akatoka kwenda uani kwa sababu mbili. Kwanza akamwone Martha anafananaje! Sura yake inasema kwamba kuna donge moyoni au kawaida. Pia, akaoge tayari kwa kwenda mjini kazini kwa Roi.
Hakumwona Martha zaidi ya wale wapangaji wenzake wawili…
“Jamani kimenuka,” alisema Martha.
“Ki nini?”
“Martha alichukua simu ya jamaa yake usiku akanitumia meseji mimi.”
Wale walishtuka sana…
“Kwa hiyo wewe ukajibu nini?”
“Sikujibu, nilikuwa nimelala.”
“Loo! Sasa?”
“Hata sijui, naoga nakwenda kazini kwake muda huuhuu.”
Mama Anna mpaka anaondoka, hakuonana na Martha. Alifuata maelekezo mpaka akafika ofisini kwa Roi.
Kitu cha kwanza, Roi aliomba simu ya mama Anna na kuangalia meseji. Kweli zilitoka kwenye simu yake…
“Daa! Hatari. Hizi alituma Martha kweli. Na kama alituma yeye ina maana kwamba aliziona meseji zote za awali ambazo mimi nilikutumia,” alisema Roi akiwa tayari na macho mekundu.
“Sasa itakuaje?” alihoji mama Anna…
“Hamna jinsi.”
“Jinsi ipo.”
“Ipi?”
“Akikuuliza mwambie mimi ni dada yako.”
“Ah! Kwa zile meseji halafu niseme wewe ni dada yangu, inakuja kweli?”
“Inakuja. Huna utetezi mwingine kwa siku ya leo. Lakini pia si ulisema unataka kumwacha Martha uwe na mimi tu, yameishia wapi mpaka unakuwa mwoga?” aliuliza mama Anna kwa sauti iliyojaa ujasiri wa hali ya juu.
“Ni kweli, lakini si katika mtindo wa kukuta meseji zako kwenye simu yangu. Nilitaka iwe amani tu.”
“Ameshakuta sasa, itakuaje?”
“Hata sijui.”
“Ndiyo ujue sasa. Mimi nakushauri jambo moja mpenzi wangu.”
“Lipi hilo baby?”
“Mimi na Martha wajina wangu, nani unampenda zaidi?”
“Martha wewe.”
“Basi mtumie meseji kwamba umeamua kuwa na mimi, hivyo jioni utakwenda kuchukua nguo zako tu.”
“Mh! Atakuibulia ugomvi wewe.”
“Mimi nipo tayari.”
Wakati wakizungumza hayo, mara Martha akaingia…
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Anhaaa! Mungu kweli mkubwa. Leo nimeamini. Kumbe hii ndiyo biashara yenu siyo?” aliuliza Martha kwa sauti yenye kujiamini...
“Hebu kaa kwanza hapo,” alisema Roi huku akitetemeka. Mama Anna alitetemeka lakini si sana.
Martha alivuta kiti, akakaa na kusema...
“Unasemaje wewe mwanaume mwenye majina mengi. Maana nimesikia una majina kama matatu hivi wewe peke yako. Kila mtu mtaani anakufahamu kwa jina lake.”
Roi alishtuka kusikia hivyo. Kwani ni kweli mtaani ana majina mengi...
“Mh!” aliguna Roi huku akimtumbulia macho ya aibu Martha. Lakini hakujibu hoja ya kuwa na majina mengi.
“Sikia nikwambie baby wangu Martha. Huyu si mpenzi wangu, ni sista‘angu ila sijawahi kukwambia,” alianza kusema Roi...
“Mimi dada yako mimi?” mama Anna alikuja juu kumuuliza Roi...
“Aaa! Jamani dada Martha...looo! yaani unanikataa kaka yako hivihivi naona jamani?”
“We wajina...sikia, mimi si dada yake wala yeye si kaka yangu. Mipango yetu ni kufunga ndoa. Huyu si wa kumtegemea wewe kwani mapenzi yake ameyahamishia kwangu...we ulie tu,” alisema mama Anna kwa macho yaliyokosa aibu.
Martha alidondoka palepale, akapoteza fahamu, hali ikawa tete. Roi huku akiogopa, alimtupia lawama mama Anna...
“Unaona sasa? Kwani kulikuwa na ulazima gani wa kumwambia wewe. Si ningemwambia mimi mwenyewe...
“Na haikuwa lazima kumwambia sasa hivi, hata nyumbani ningemwambia...”
“Baby, mimi tatizo langu sipendi kukatishakatisha. Niko moja kwa moja sana. Nisamehe kwa hilo. Ndiyo maana nilikuuliza awali unampenda nani. Mtu akifiwa hakuna haja ya kufichaficha, ni kumwambia tu ili kama kulia alie,” alisema mama Anna.
Roi na mama Anna walimzoa Martha na kumkimbiza hospitali ambako alilazwa. Mama Anna aliwapa taarifa wale wapangaji wengine kuhusu kuugua ghafla kwa mwenzao huyo.
***
Ilikuwa saa kumi na mbili jioni, Martha alikuwa kwake baada ya kutoka hospitali. Wapangaji wenzake waliingia kumpa pole kasoro mama Anna tu ambaye muda huo alikuwa nyumbani kwa Roi...
“Pole mwaya! Yaani tuliposikia umelazwa tukashangaa sana. Da! Sasa tatizo lilikuwa wapi Martha?” mpangaji mmoja alimuuliza...
“Jamani ni hadithi ndefu sana. lakini kifupi nilikuwa sijui kama jamaa yangu anatoka na mama Anna. Nilihisi wakati f’lani nikafuatilia, jana usiku nikanasa meseji zao za mahaba.
“Leo asubuhi nikasema niende kazini kwake kufika namkuta mama Anna ndani. Yeye jamaa yangu akasema mama ni dada yake, japo nilijua ni uongo, lakini mama Anna mwenyewe akanipasulia kwamba wao si ndugu bali ni wachumba na wanatarajia kufunga ndoa hivi karibuni,” alitiririka Martha...
***
Kule nyumbani kwa Roi, mama Anna alimtaka Roi amruhusu awaite wale wapangaji wenzake wawili ili awatambulishe rasmi kwake...
“Aaaa...eeee...oke, waite basi,” alisema Roi ambapo awali alianza kwa kutaka kukataa.
“Mbona baby kama unasita? Au mipango yetu imekufa nini?” aliuliza mama Anna...
“Aaa! Noo...iko palepale. Basi waite.”
Mama Anna alimpigia simu mmoja wa wapangaji wenzake, akampa maelekezo ya namna ya kufika hapo.
Wakati wanaondoka, wakamuaga Martha...
“Basi twendeni wote na mimi nataka kupeleka nguo za Roi.”
Wale ilibidi wamjulishe mama Anna kwanza ambapo naye alikubali bila kumuuliza Roi...
“Aje tu, hakikisheni amebeba hizo nguo za Roi ili asije kupata kisingizio kingine baadaye,” alisema mama Anna.
Wakati anazungumza hivyo, Roi ndiyo akasikia na kuhoji ni nini, mama Anna akamwambia, Roi akatingisha kichwa tu kukubaliana naye.
Kutoka moyoni mwake, Martha alishakubaliana na hali iliyotokea, akajilaumu sana kwa uamuzi wake wa kung’ang’ania yeye na Roi wasiwe kaka na dada na badala yake wawe wapenzi...
“Ningeusikiliza moyo siku zile haya maumivu yalikuwa yanakwepeka,” alisema moyoni wakiwa wanakaribia nyumbani kwa Roi yeye akiwa kiongozi maana alishafika.
Waliingia ndani watatu, wale wapangaji wawili na Martha.
Mama Anna aliwakaribisha kwa mbwembwe akijifanya mama mwenye nyumba huku Roi akionekana kukosa amani...
Karibuni jamani...karibuni sana,” alikaribisha mama Anna kwa sauti ya ‘mimi ndiye mmiliki halali wa mwanaume huyu’, yaani Roi sasa.
“Tunashukuru sana,” waliitikia wale wapangaji wawili kasoro Martha ambaye yeye alifikia kuweka begi chini kisha akamwambia Roi...
“Ungeangalia kama nguo zako zote zipo maana nimehakikisha siachi nguo yako hata moja.”
“Naamini zote zipo bila hata ya kuhakikisha,” alisema Roi kwa sauti iliyojaa dharau, mkono mmoja ulipita kiunoni kwa mama Anna huku mkono mwingine ukishughulika na rimoti ya televisheni.
Bila kukaa, Martha akageuza kutoka lakini kabla hajafika mlangoni, ikasikika hodi...
“Hodi,” hodi hiyo ilipigwa huku aliyepiga akisukuma mlango kuingia sebuleni.
Roi alishtuka sana, akatumbua macho huku akisimama na kusema...
“Mama Neema...mbona umekuja bila taarifa mke wangu? Umeona sasa umenikuta katika mazingira tata. Lakini kifupi hapa hakuna mwanamke wangu mama Neema.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kauli ya Roi ilimshtua sana mama Anna, Martha mwenyewe na wale wapangaji wawili…
“Ha! Mpenzi wangu, kumbe wewe una mke?” aliuliza mama Anna kwa sauti yenye mshtuko…
“Wewe. Mimi ni mpenzi wako tangu lini? Acha uzushi? Eti Martha, huyu mama Anna ni mpenzi wangu?” Roi aliomba huruma ya Martha ili kuokoa ndoa yake.
Mama Neema ni mke wa Roi. Alikwenda masomoni Uingereza kwa mwaka mmoja na muda huo ndiyo alikuwa amerudi rasmi. Neema alipelekwa kusoma kwa babu yake.
“Mi mwenyewe nimeshangaa. Kwani we mama Anna, Roi ni mpenzi wako?” aliuliza Martha huku akianza kujisikia furaha kwa anguko la mwanamke huyo aliyempindua yeye.
Mama Neema alifika kukaa kwenye kochi kubwa huku akimshangaa mume wake na ugeni ule. Alitaka kujua…
“Baba Neema hawa wote ni akina nani na wamefuata nini hapa nyumbani?”
“Mama Neema wewe ndiyo kwanza umefika. Ungetulia kwanza basi. Umekuja na begi hilo moja tu?”
“Nina mizigo mingi ipo kwenye gari nje,” alijibu mama Neema kwa sauti iliyojaa hasira.
Roi alisimama na kutoka nje. Alishusha shehena ya mizigo huku moyo ukiwa kasi. Alijua kimenuka…
“Eti nyie ni akina nani?” mama Neema aliwauliza kwa mpigo huku akimwangalia mmoja mmoja.
“Mimi naitwa Martha. Ni rafiki wa Roi,” alisema Martha huku akiogopa. Mama Neema akamwangalia mama Anna kama anayesema ‘na wewe?’
“Mimi naitwa mama Anna. Roi nii…niii…mimi sikujua kama Roi ana mke.”
“Nimekuuliza wewe nani, siyo Roi ana mke au hana,” alikuja juu mama Neema huku akionekana kutaka kusimama kumfuata mama Anna…
“Mimi pia ni rafiki yake wa karibu tu,” alijibu haraka mama Anna.
Wale wapangaji wengine walijitambulisha kwa haraka huku wakisimama kutaka kuondoka. Mizigo iliingia ndani, Roi alisaidiwa na vijana wa mtaani.
Mama Neema aliwazuia wote kutoka mpaka Roi arudi na kuzungumza naye kuhusu wao. Walikaa kinyonge.
Baada ya utulivu, Roi alirejea na kukaa…
“Baba Neema naomba utambulisho wa hawa watu wote humu ndani,” alisema mama Neema kwa sauti yenye hasira…
“Wote ni marafiki zangu. Wametoka kumoja na wataondoka pamoja.”
“Kwa nini huyu alikaa jirani na wewe kiasi kile?”
“Nani, huyu? Huyu aliamua tu.”
“Lakini mwenyewe si alisema we ni mpenzi wake?” alihoji mama Neema.
Roi alitulia akiashiria hana cha kujibu…
“Nyie malaya, nawaomba muondoke sasa hivi la sivyo nitampiga mtu risasi,” alisema mama Neema.
Akina Martha walitoka mbio, mlangoni waliminyana kila mmoja akitaka kuwa wa kwanza kutoka nje.
Wakiwa nje ya geti kuu, mama Anna alimuomba msamaha Martha…
“Martha ndugu yangu. Mi naomba nisamehe sana. Ni kweli nilikuingilia kwenye penzi lako. Sikujua kama Roi yuko vile. Nisamehe sana ndugu yangu. Nimejifunza kwamba, kila binadamu na riziki yake. Roi alikuwa riziki yako. Mimi nikaingilia kati,” alisema mama Anna huku akimwangalia Martha…
“Mh! Yaani wewe unamwomba samahani mwenzako kwa sababu kule kumeharibika siyo? Kwa nini usingemwomba sahamani jana au juzi?” mmoja wa wale wapangaji aliingilia kati…
“Eti!” mwenzake alidakia.
Walimnanga mama Anna kama si wao waliokuwa wakimuunga mkono na kumficha Martha kwamba wanajua.
“Sikiliza mama Anna. Kwanza sipokei msamaha wako. Pili, uache unafiki wako. Kilichokufanya uniombe msamaha ni baada ya kujua Roi kumbe ana mke. Usingejua je? Yaani we mwanamke mimi nimekushangaa sana. Umekuwa ukinila hivihivi najiona,” alisema kwa ukali Martha…
“Siyo hivyo Martha. Jamani msinielewe vibaya. Mambo mengine yanafanyika ili mtu ujifunze. Naamini hata kilichotokea nyumbani kwa Roi kimekuwa cha makusudi ili mimi nijifunze. Please nisamehe sana Martha,” alisema mama Anna kwa sauti ya unyonge huku akimtangulia mbele na kuonesha ishara ya kutaka kupiga magoti huku akifunga mikono…
“Oke, sawa. Sasa niambie ukweli…”
“Niko tayari Martha,” alisema mama Anna…
“Wewe na Roi mmeanzia wapi na lini mpaka mkawa wapenzi?”
Japokuwa mama Anna alikuwa tayari kujibu maswali kama alivyosema mwenyewe, lakini swali hilo lilikuwa gumu sana kwake. Ikabidi adanganye…
“Sikia Martha. Mimi na Roi tunajuana zamani sana. Tena sana. Kwa hiyo alipokuja kwako ikawa kama tunakumbushia tu,” alisema mama Anna…
“Muongo huyu Martha. Alichukua namba za simu palepale nyumbani. Siku ile wakati shemeji anatoka kuoga ndiyo akachukua, wakaanza mawasiliano. Na alisema nia yake mpaka akupindue,” alisema mmoja wa wale wapangaji.
“Sawa jamani. Martha ni kweli walichosema hawa. Mimi nilijua nikikwambia hivyo utazidi kuumia wakati mtu mwenyewe haunaye tena. Nisamehe sana.”
Martha aliamua kumsamehe mama Anna huku akimwonya kutorudia tabia hiyo kwa watu wengine kwani si njema…CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Yaani kama utakuja kumfanyia hivi mtu mwingine yeyote yule, ujue maisha yako yatakuwa mabaya sana mama Anna. Nakwambia mimi,” alisema Martha.
Wale wapangaji wengine pia wakamzodoa mama Anna na kumwambia ana tabia mbaya. Hata wao wamejifunza kuwa naye mbali. Hata hivyo, mama Anna aliahidi kubadilika kanzia siku hiyo.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment