Search This Blog

Monday, October 24, 2022

NYUMBA ILIYOJAA DHAMBI - 1

 









    IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI



    *********************************************************************************



    Chombezo : Nyumba Iliyojaa Dhambi

    Sehemu Ya Kwanza (1)



     Ukimya ulitawala ndani ya Jiji la Dar es Salaam, yale magari yaliyokuwa yakipita kwa kasi katika barabara nyingi jiji humu yalikata kabisa. Watu wengi waliokuwa wakienda huku na kule hawakuwa wakionekana kama nyakati za mchana.

    Kila kitu kilibadilika usiku huo, katika mitaa mingi ya Kariakoo hakukuwa na watu kabisa, ilikuwa ni vigumu kuamini kama nyakati za mchana kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakipita huku na kule.

    Katika muda huo, nilikuwa katika Mtaa wa Kongo. Hapo, ndipo kulipokuwa na maisha yangu, niliyaendesha humo, si kama mfanyabiashara bali nilifanya kazi hapo katika kusafisha barabara kila siku usiku.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa jina ninaitwa Edward Francis. Nimeamua kukusimulia maisha yangu yalivyokuwa, najua kuna watu wanamuona mtu fulani amefanikiwa halafu wakahisi kabisa alitoka kwenye familia ya kitajiri, leo watu wanavyoniona nina nyumba kubwa, magari ya kifahari na hata biashara nyingi wanadhani kwamba nilizaliwa kwenye familia ya kitajiri, ndugu yangu, nilizaliwa kwenye familia ya kimasikini tena inawezekana zaidi ya hiyo yako, nilihangaika mno mpaka kufika hapa nilipo.

    Maisha yangu ni simulizi nzuri kwako, kuna mambo mengi mazuri niliyoyafanya, ila kumbuka kwamba kuna mengi mabaya ambayo niliyafanya pia. Mabilionea wengi wa leo wakikusimulia maisha yao, watachambua, watakwambia yale mazuri lakini mabaya yatabaki moyoni mwao.

    Ninaamua kuyafungukia maisha yangu leo, nitakwambia kila kitu, najua kuna watu wengi watajifunza kupitia maisha yangu. Kuna mafunzo machache sana yanapatikana katika yale mambo mazuri uliyowahi kuyafanya ila kuna mafunzo makubwa yanayopatikana kwenye magumu na dhambi nyingi ulizopitia.

    Mishemishe zangu zilikuwa Kariakoo, sikuwa na mahali pa kuishi, wazazi wangu walifariki miaka mingi iliyopita, sikuwahi kuziona sura zao, walifananaje? Walikuwa wembambamba ama wanene? Weusi ama weupe? Kwa kweli sijui kitu chochote kile kuhusu wao.

    Hapo Kariakoo nilikuwa mkimya, sikuwa muongeaji sana, nilijua kufanya kazi zangu nyingine kama kawaida. Nakumbuka kila siku nilipokea kiasi cha shilingi elfu tano kila nilipokuwa nikimaliza kufanya usafi.

    Ilikuwa kazi ngumu, barabara ilikuwa ikichafuka mno, na nilipokuwa nikianza kusafisha nilichoka sana. Kuna wakati nilitamani kuacha kazi hiyo, sikuipenda lakini sikuwa na cha kufanya zaidi ya kuendelea kuifanya zaidi na zaidi.

    Kila siku katika maisha yangu nilitamani kuwa na pesa, demu mkali, nyumba nzuri lakini kwa jinsi nilivyokuwa nikiishi kipindi hicho niliamini kwamba maisha yangu yangeendelea kuwa hivyohivyo.

    Hapo Kariakoo nyakati za asubuhi, mchana na jioni kulikuwa na watu wengi, wanawake wazuri ambao kila nilipowaangalia, niliwapenda. Nilifikiria sana wanawake, katika maisha yangu nimekuwa nikiwapenda mno lakini nilishindwa kuwa nao kwa sababu tu sikuwa na pesa.

    Niliamini katika pesa, sikuamini kama ningekuwa na msichana ambaye angekubali kuwa nami na wakati sikuwa na lolote mfukoni, ili niwe na mwanamke mzuri basi ilikuwa ni lazima nitafute pesa kwanza, halafu hao wazuri wangekuja wao wenyewe.

    Kila siku kazi yangu ilikuwa ni kuwasalimia wanawake na kuwasifia kwamba walipendeza, ningefanya nini sasa? Sikuwa na cha kufanya zaidi ya hicho. Kulikuwa na wanawake wanene, waliojaa, wale mamodo, wembamba, vifua vya kuvutia na walitembea kama twiga awapo mbugani.

    Walinichanganya sana lakini tatizo lilikuwa pesa tu, haikuwa kazi nyepesi kuwapata kwa sababu sikuwa na kitu, yaani hata kama msichana akikubali, aniambie twende tukale raha, tutakulaje raha na wakati nina elfu tano mfukoni? Yaani kwa kifupi sikuwa na meno hivyo nisingeweza kutafuna hata nyama laini.

    “Dada mambo!” nilimsalimia msichana mmoja, alikuwa mrembo sana, alipendeza mno, nilimuona siku ya kwanza, sikumjua, alikuwa akitembea huku akiangalia vitu vya kununua. Si unajua mtaa wa Kongo unayokuwa na watu wengi?

    Msichana huyo akageuka na kuniangalia, jicho lake tu lilionyesha ni kwa jinsi gani alionekana kuchukizwa na mimi, sikuwa mzuri sana, mavazi yangu yalionyesha kile nilichokuwanacho maishani mwangu.

    “Umependezaaaa...” nilimwambia huku nikijitahidi kutoa tabasamu pana lakini wapi! Hakunichangamkia hata kidogo.

    Huyo hakuwa wa kwanza wala wa mwisho, nilikuwa mzee wa shobo sana, kila msichana ambaye nilimuona na kuvutiwa naye, cha kwanza ilikuwa salamu, cha pili kikawa ni kumsifia. Wapo wengine waliitikia lakini hawakutaka stori zaidi, hao waliondoka zao.

    “Dada umependeza kama shangazi yangu,” nilimwambia msichana mwingine, alipendeza mno.

    “Ahsante sana kaka yangu!”

    “Unakwenda wapi? Huogopi kupotea?” nilimuuliza huku nikitoa tabasamu pana ambalo niliamini kwamba lilikuwa na ushawishi mkubwa mno.

    “Hahaha! Nipotee Dar? Basi makubwa!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa jinsi alivyokuwa akinijibu moyo wangu ukafarijika. Nilijiona kuwa na thamani sana, yaani masikini mimi, ambaye kila siku sikuwa na pesa na nilidharauliwa na mademu eti leo huyu mwanamke alikuwa akijibu huku tukipiga stori za hapa na pale.

    “Nichukue namba yake ya simu?” nilijiuliza lakini sikuwa na simu kwa maana hiyo hata kama ningechukua namba yake ingekuwa kazi bure tu.

    Alikuwa akitembea kwenda kule kulipokuwa na nguo za wanawake, sikujua alikuwa akienda kununua nini, kitendo cha mimi kuwa naye, kupiga stori kilinifanya niridhike na kujiona mtu mwenye thamani kubwa kuliko wote katika dunia hii.

    “Ila umependeza sana, unajua siwezi kuvumilia kusema ukweli,” nilimwambia huku nikimwangalia.

    “Mara ya pili unaniambia hivyo!”

    “Ni kwa sababu umependeza kweli, halafu mzuri! Uzuri huo umeridhi wapi?” nilimuuliza.

    “Kwa mama! Mama yangu Mzigua!”

    “Ooh! Mtoto wa Kitanga. Mzuri hasa na hata nikiangalia nyuma, mtoto mashallah!” nilisema huku nikiyapeleka macho mgongoni kwake, akageuka.

    “Ooh! Usifanye hivyo bhana!” aliniambia huku akitabasamu.

    “Usijali!”

    Tulifika alipokuwa akienda, akanunua dela na kuondoka, nilichokifanya ni kuchukua namba ya simu yake na kuiandika kwenye kikaratasi halafu akaingia kwenye daladala.

    Niliuchukia sana umasikini, uliniuma kwa sababu pale alipoingia ndani ya gari, kulikuwa na wanaume waliokuwa wakimwangalia kimatamanio, na hata kwenye siti aliyokwenda kukaa, kulikuwa na mwanaume mmoja ambaye bila aibu, hata kabla gari halijaondoka, akamsalimia na kuanza kupiga naye stori.

    Iliniuma mno kwani niliamini kwa safari ya kutoka hapo Kariakoo mpaka kwao Mabibo, yule msela angechukua namba ya simu na kuanza kuwasiliana na mwisho wa siku kulala naye kitanda kimoja.

    Hiyo ilikuwa sababu ya kwanza kuuchukua umasikini. Msichana yule hakutakiwa kupanda daladala, yaani ilifaa kuingia ndani ya gari langu na kumpeleka mpaka kwao ila kwa sababu nilikuwa kapuku, sikuwa na jinsi. Nikarudi kule Mtaa wa Kongo na kuendelea na mishe zangu kama kawaida.

    Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu, nilipenda sana wanawake lakini sikuwa na makali yoyote yale. Kazi yangu kubwa ilikuwa ni kuwasalimia, wakati mwingine walinitukana, walinichunia lakini sikutaka kujali hilo, niliendelea kufanya hivyohivyo kama kawaida.

    “Issa! Naomba simu yako mara moja,” nilimwambia rafiki yangu Issa, huyu jamaa alikuwa akiuza duka moja hapo Kariakoo, ni duka la familia kwani alikuwa na dada zake wawili, Halima na Shamila ambao walipokezana, walikuwa wazuri lakini kwa jinsi umasikini ulivyonipa uoga na hali ya kujiamini, hata kuomba namba zao za simu sikuwahi.

    “Ya nini?”

    “Kuna demu nataka nimpigie! Niongee naye,” nilimwambia.

    Issa alikuwa mshikaji wangu sana, ishu ndogo kama simu asingeweza kuninyima hata kidogo, akanipa, nikachukua kile kikaratasi ambacho nilipewa jana yake na yule msichana na kumpigia.

    Simu ikaanza kuita na baada ya sekunde chache ikapokelewa na msichana huyo. Nikaanza kuzungumza naye, nilijitambulisha, alionekana kufurahi mno. Tuliongea kana kwamba tulifahamiana miaka mingi iliyopita.

    “Leo sijakuona, nimekumisi sana,” nilimwambia.

    “Nimekumiss pia ila nipo bizebize, nikipata nafasi nitakuja!”

    “Kweli?”

    “Niamini baby boy!”

    “Sawa haina shida.”

    Niliongea naye kwa dakika kadhaa na kumrudishia simu Issa na kumshukuru kwani bila kutumia urafiki wetu na ukaribu mkubwa asingeweza kukubali.

    “Nani? Mama au?”

    “Hapana! Kuna demu nilikutana naye jana. Mnene, mweupe, kajaajaa, kama Kajala!” nilimwambia na kuanza kucheka.

    “Acha masihara!”

    “Ooh! Ni shida mzee baba! Halafu mzuri, sura ya kitoto, sijui nikwambiaje!” nilimwambia Issa.

    Nilimsifia sana mwanamke yule pasipo kujua kama nilikuwa nikikaribisha maumivu moyoni mwangu. Nilitaka Issa anione kama nilikuwa na bahati kumbe ndiyo nilikuwa nikimpa demu wa kuenjoi naye.

    Kila siku ilikuwa kazi yangu kumwambia Issa nimpigie simu mwanamke huyo kumbe upande wa pili naye akaanza kujitengenezea mazingira na kuanza kumtongoza, na sijui msichana huyo alidanganyika na nini, akamkubalia na kukubaliana kulala pamoja, na hilo likatokea.

    Sikuwa nikifahamu kipindi hicho, nilimuona Issa kama mshikaji wangu kumbe alikuwa akinizunguka tu. Sikujua kama alikuwa na uhusiano na mwanamke huyo, sikujua kama walionana mpaka kufanya mapenzi.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya wiki moja akarudi tena. Sikufichi, mpaka muda huo sikujua hata jina lake, ila siku hiyo akaniambia kwamba aliitwa Aisha, nilifurahi sana lakini wakati alipokuja nilipokuwa, nilishangaa sana akimchangamkia mno Issa kuliko hata mimi.

    Hilo likaipa wasiwasi, niliumia sana lakini nikapiga moyo konde pasipo kugundua kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia. Nilipoona wanazungumza wao tu, nikamchukua Aisha na kuondoka naye.

    Alikwenda kulekule kwa siku ile, nilivimba moyoni, wivu ulinijaa, nilitamani nimuulize zaidi kuhusu Issa lakini nikaamua tu kutulia.

    “Aisha! Unajua nakupenda sana,” nilimwambia, nilifanya hivyo kwa kuwa nilijua tu kama ningechelewa, Issa angeniwahi.

    “Unanipenda mimi?”

    “Ndiyo! Ninakupenda Aisha,” nilimwambia!”

    “Huniwezi Edward!”

    “Kwa nini! Unadhani kwa gitaa dogo siwezi kutumbuiza uwanja wa taifa?” nilimuuliza kwa utani huku nikicheka.

    “Utanilisha nini?” aliniuliza swali dogo sana ambalo lilikuwa na maana kubwa.

    Nilibaki kimya nikimwangalia, sikutarajia kupata swali kama hilo kutoka kwake. Ni kweli alikuwa na uhuru wa kuuliza kuhusu majukumu yangu kama mwanaume kwake.

    Alikuwa akipendeza sana, hii ilimaanisha kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakifanya kazi hiyo, yaani kulikuwa na mwanaume aliyekuwa akishughulika na mavazi tu, mwingine nauli za usafiri mwingine viatu na mwingine make up, sasa mimi ningeshughulika na nini? Hata kama angeniambia nishughulike na vocha tu nisingeweza kutokana na kiasi cha pesa kilichokuwa kikihitajika.

    “Kwani wewe unataka nini?” nilimuuliza ili nijue.

    “Matunzo! Mtoto mzuri kama mimi nitunzwe, nitolewe out, niletewe baga, pizza, ice cream, uninunulie pafyumu, ninukie, au hutai demu wako ninukie vizuri?” aliniuliza.

    “Nataka! Tena napenda sana.”

    “Sasa je! Utaweza kunitunza?” aliniuliza.

    Mtu mzima sikujua nimjibu nini, hilo swali lilikuwa kubwa kuliko uwezo wangu. Nilimwangalia tu, kwa kawaida hata kama huwezi, kwa mwanaume ni MARUFUKU kusema neno siwezi, ni lazima useme unaweza halafu umkimbie.

    “Kwa nini nisiweze? Tena umenikumbusha, nataka siku nikuchukue tukale pizza,” nilimwambia.

    “Waooo! Lini bebi?”

    “Tufanye Ijumaa!” nilimwambia, siku hiyo ilikuwa Jumatatu.

    Sikia! Mimi nilikuwa nasikia sana kuhusu pizza ila kiukweli sikuwahi kula hata siku moja. Nilitamani vyakula vinono lakini sikuwa na pesa. Hebu fikiria, kwa siku napokea elfu tano, halafu hapo pizza inauzwa elfu kumi na mbili mpaka nyingine elfu hamsini, hivi ningeweza kumgharamia yote hiyo? Kwangu ilikuwa vigumu, ila nilimwambia kwamba ningemtoa out kwa sababu tu nilitaka kujitia ubabe mfukoni.

    “Basi naisubiri hiyo siku! Zimebaki siku nne, nitakutafuta bebi nikale pizza,” aliniambia kwa tabasamu na kisha kuagana huku moyo wangu ukijisikia burudani sana kwa kuamini kwamba nimeshinda vita kumbe ndiyo kwanza nilikuwa nikiingia kwenye vita na watu waliokuwa na nguvu kuliko mimi.





    Nilichanganyikiwa, sikujua ni kitu gani nilitakiwa kufanya ili niingize pesa kabla ya siku husika kufika. Niliumiza kichwa changu kwani kiasi cha shilingi elfu tano kwa siku kilikuwa kidogo sana kiasi kwamba kisingeweza kunisaidia kwa lolote lile.

    Wakati nikifikiria sana ndipo nikakumbuka kwamba hapo katika Mtaa wa Kongo kulikuwa na uhaba wa walinzi wa kulinda eneo hilo, wale wachache waliokuwa wakilinda walilipwa kiasi cha shilingi elfu kumi kila siku asubuhi.

    Nakumbuka niliwahi kuulizwa kama niliitaka kazi hiyo kipindi cha nyuma, niliikataa kwa kuwa niliamini ningekuwa nachoka sana, ila kwa sababu huyo Aisha nilimwambia Ijumaa ilikuwa ni siku ya kuonana na kwenda kula pizza, basi niliona hiyo kazi ilinifaa sana.

    Nikaelekea katika ofisi moja iliyokuwa hapohapo ambayo ilikuwa chini ya mzee Juma, nilizungumza naye na kumwambia kwamba niliitaka kazi hiyo. Kuipata haikuwa kazi kwani alinifahamu, nilikuwa mtu wa hapohapo hivyo akanipa nafasi hiyo na kuniambia nianze siku hiyo.

    Moyo wangu ukafarijika, na mpango wa kwanza kabisa kabla ya kupanga maisha ilikuwa ni kwenda mtoko huo na Aisha, ilikuwa ni lazima nimuonyeshe kwamba nilikuwa na uwezo mkubwa wa kumchukua msichana na kwenda naye sehemu.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku zilikwenda taratibu sana, kwa kuanzia Jumatatu mpaka Alhamisi ilimaanisha kwamba ningepata kama shilingi elfu arobaini kupitia kazi ya ulinzi lakini pia ningepata shilingi elfu ishirini kwa kazi ya usafi, kwa maana hiyo mpaka Ijumaa nilitegemea kuwa na shilingi elfu sitini mfukoni.

    Kwa mwaka huo wa 2016 zilikuwa pesa nyingi kutokana na hali ya uchumi, maisha kubana hivyo niliamini kwamba siku hiyo ningefaidi sana na Aisha na kubwa zaidi ni kwamba ningeonekana kwamba nilikuwa na pesa na hakukuwa na chochote cha kunibabaisha.

    Wakati nikifikiria kuhusu Aisha, kichwa changu kilikuwa kinaniuma mno kila nilipofikiria kuhusu Issa, niliamini kwamba alinizunguka na kutembea na msichana huyo kwani lisingekuwa jambo jepesi kumuona akichangamkiana naye na wakati niliamini hawakuwa wameonana kabla.

    Hilo sikutakiwa kuhofu sana kwa kuwa niliamini kabisa kwamba mara baada ya kuwa naye faragha basi huyo Issa asingemfikiria kabisa kwa sababu nilijiamini kupita kawaida.

    “Ila subiri! Cha msingi ni kumuonyeshea mapenzi makubwa,” nilijisemea.

    Wakati hayo yote yakiendelea bado sikuacha shobo zangu kwa wanawake wengine waliokuwa wakija hapo Kariakoo kufanya manunuzi yao mbalimbali, nadhani nilikuwa mtu niliyeongoza kusalimia kuliko watu wengine Tanzania. Macho yangu yalikuwa magumu kuvumilia kila nilipokuwa nikiwaona wanawake wazuri ilikuwa ni lazima niwafuate na kuanza kuongea nao kidogo.

    Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu kabla ya kufanikiwa. Mpaka leo ninapokaa na kukumbuka miaka miwili nyuma, maisha yalivyobadilika na kuwa hivi yalivyo, huwa ninaamini kabisa Watanzania tunabaki masikini kwa sababu tu hatuna mitaji, hatuna pesa za kuanzia biashara na ndiyo maana tupo hivi.

    Sikuacha kumfuata Issa na kumuomba simu yake kuzungumza na Aisha, alinipa na kuongea naye sana na hata siku ya Ijumaa ilipofika, akaja palepale alipokuwa akinikuta, nilimchukua na kuondoka naye.

    Njiani nilikuwa nikiongea naye, mfukoni nilikuwa na shilingi elfu arobaini kwani nyingine nilitumia kwenye matumizi yangu mengine.

    Hatukuchukua muda mrefu tukafika sehemu ya kununulia pizza na kununua kisha kuondoka, tulikula huku tukitembea, siku hiyo nilijiamini kuliko siku nyingine na nilichokihitaji kilikuwa kulala na Aisha tu.

    Kwa Kariakoo nisingeweza kupata chumba kwa kuwa ilikuwa ni gharama sana hivyo kama kweli nilihitaji kufanya naye basi haikuwa na jinsi kuondoka kuelekea Magomeni au Manzese.

    Sikutaka kujificha, mwili wangu ulikuwa ni kama umewaka na hakukuwa na kitu cha kunizuia kufanya mambo yangu, nilimwambia ukweli kwamba network ilikuwa ikisoma na nilichohitaji ni kulala naye.

    Aisha alinizoea sana, akaniambia kwamba hakuna tatizo, kama nilikuwa na hela ya kumtoa basi hakukuwa na shida. Hapo nilipata swali moja, huyu Aisha alikuwa akijiuza ama kwa sababu kwa msichana wa kawaida angeniacha mimi nifanye naye halafu mambo ya kupeana pesa yangekuja baadaye.

    “Kiasi gani unataka?” nilimuuliza huku nikimwangalia usoni.

    “Yoyote ile, isiwe elfu kumi, isiwe chini ya elfu kumi,” aliniambia huku akitoa tabasamu lililonimaliza kabisa.

    Mfukoni nilikuwa na shilingi elfu ishirini na tano hivyo hakukuwa na tatizo, nikamchukua na kwenda Mburahati ambapo kulikuwa na nyumba ya wageni ya bei rahisi na kumalizia mambo yetu humo.

    Wanawake wa mjini wanapenda pesa, kama hauna pesa, huwezi kumpata msichana yeyote yule. Hebu fikiria, mwanamke kama Aisha nilitumia kiasi cha pesa ambacho kwangu kilikuwa kikubwa mno, hii inamaana kwamba unapokuwa na pesa basi una uwezo wa kufanya mapenzi na msichana yeyote uliyekuwa ukimtaka.

    Hilo likanifanya kuendelea kuuchukia umasikini, sikuamini kwenye kufanya kazi kwa bidii ndipo ufanikiwe, siku zote niliamini kwamba utajiri ni bahati tu, mtu anaweza leo akawa masikini na kesho akaamka na kuwa tajiri mkubwa.

    Niliamini kwamba kuna siku ningetajirika sikujua ni siku gani lakini niliamini kwamba kuna siku tu ingetokea ningefanikiwa na kuwa tajiri mkubwa.

    Niliporudi Kariakoo nikaanza kumwambia Issa kwamba nilifanikiwa kumalizana na Aisha, kwa jinsi alivyoonekana tu niliamini kwamba hakuwa mtu mzuri, hakuitikia kwa furaha, alionekana kama kuchomwa na kitu chenye ncha kali moyoni mwake.

    Hilo likanipa uhakika kwamba Issa alitembea na Aisha, nilikasirika sana, kwa jinsi tulivyokuwa marafiki sikuamini kama angeweza kufanya kitu kama hicho.

    Aliniumiza, wakati yeye akicheka, moyoni mwangu kulikuwa na majonzi makubwa, sikutaka kukubali, kama yeye alitembea na msichana ambaye alijua kwamba alikuwa wangu, akaniumiza basi na mimi ilikuwa ni lazima nimuumize.

    “Nitamuumiza, kuna siku nitatembea na dada zake wawili, halafu nitatembea na demu wake,” nilijisemea.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Urafiki wetu ukaendelea lakini haukuwa kama kipindi cha nyuma, yaani siku ambayo nilikwenda kulala na Aisha ndiyo ilikuwa siku iliyobadilisha kila kitu.

    Niliendelea kufanya kazi, sikuwasiliana tena na Aisha kwa sababu hata simu Issa hakutaka kunipa kwa kuniambia kwamba alikuwa bize nayo. Kwani simu shilingi ngapi bhana? Nilijidunduliza na kununua yangu, tena ilikuwa ile ya kupangusa.

    Huko, nikafanikiwa kuwasiliana na Aisha kwa WhatsApp, tulikuwa tunaongea mengi, aliniambia kuhusu Issa kwamba alikuwa akimfuatilia sana kiasi kwamba mpaka ikawa kero.

    “Ikawaje?” nilimuuliza.

    “Ikawa hivyohivyo...yaani alikuwa kero,” aliniambia.

    “Ikawaje? Yaani namaanisha baada ya kero zake, nini kilifuata?” nilimuuliza.

    “Nilifanya naye mapenzi, alinishawishi sana, aliniambia kwamba wewe ni masikini, huna pa kulala, unalala kwenye maduka, unapenda kujipendekeza kwa kila mtu ili upate pesa,” aliniambia.

    “Yaani Issa alikwambia yote hayo?”

    “Ndiyo! Nadhani hiyo ilikuwa sababu ya kulala naye. Naomba unisamehe,” aliniambia, nilishikwa na hasira mno lakini sikuwa na la kufanya.

    Sikumlaumu Aisha, alikuwa msichana aliyekuwa akitafuta mwanaume mwenye pesa, mimi sikuwa nazo, nilikuwa masikini hivyo kama kulikuwa na mwanaume alimfuata kwa kisingizio cha pesa niliamini mwanamke yeyote yule angeweza kudanganyika.

    “Ila huyu Issa, ni lazima nitadili naye,” nilijisemea huku nikionekana kuwa na hasira.

    Niliona kama nachelewa kupata mafanikio, mtu wa kwanza ambaye nilitakiwa kufanya mikakati ya kuwa naye alikuwa Shamila. Huyu ndiye yule mdogo wake na Issa ambaye nilimtamani sana kwa kuwa niliamini baada ya Issa kugundua kwamba nimelala naye basi angenichukia maisha yake yote. Hiyo ndiyo ilikuwa maana ya kisasi.

    Nikaanza kupiga ndogondogo, nikaanza kuzungumza naye kila siku kwa furaha, nilichangamka kiasi kwamba mpaka yeye mwenyewe alinishangaa.

    “Mkeka wako umetiki nini?” aliniuliza huku akiniangalia.

    “Kwa nini?”

    “Unaonekana una furaha sana!”

    “We’ acha tu. Ila Shamila wewe mzuri sana,” nilimwambia huku nikimwangalia.

    Alichukia, hiyo ndiyo ilikuwa kawaida yake. Shamila alijua kabisa kwamba nilimpenda tangu zamani ila hakutaka kunikubalia kwa sababu tu alijua sikuwa na pesa, sikuwa na makali yoyote yale ya kumfanya mtoto wa kike anikubali.

    Bila kunificha akaniambia kwamba hanipendi, tena nisifikirie kuwa naye hata kidogo. Unadhani niliumia, walaaa! Shamila alikuwa msichana mrembo, kusema kwamba sikustahili hata kutembea naye kwangu mimi ilimaanisha kuwa nitafute pesa, nikipata nimtafute.

    Kulipa kisasi kwa Issa ilihitaji nguvu kubwa, haikuwa kirahisi kama ilivyokuwa ikionekana, ilikuwa ni lazima nipambane kuhakikisha napata maisha mazuri kama watu wengine, halafu ndiyo nimfuate.

    Wanawake waliendelea kufurika Kariakoo, walikuwa wengi mno tena waliokuwa wakipendeza kupit kawaida. Sikuacha kuwasalimia, kila siku niliamini kwamba ili uwapate wanawake wazuri basi hukutakiwa kuwahofia hata kidogo.

    Siku ziliendelea kukatika, niliendelea kuwasiliana na Aisha na kuonana naye sana. Alinipenda, si kwamba nilikuwa mzuri ni kwa sababu niliwahi kufanya naye mapenzi.

    Nilimzoea, kikafika kipindi akayajua maisha yangu, hata alipokuwa akija na kumwambia kwamba sina pesa, hakuwa akilalamika kwani nilimwambia kila kitu na akatokea kunikubali kwa maisha niliyokuwanayo.

    Mishemishe zangu za kumtafuta Shamila hazikukoma, kila siku nilimwambia maneno yale yale kwamba nilimpenda lakini hakutaka kunielewa hata kidogo.

    Nilipoona nimeshindwa, nikasema si kesi kama nikiamua kumfuatilia mdogo wake Halima ambaye alikuwa akifika hapo mara chache sana.

    Nilijipanga na kusema kwamba ni lazima nimfuate msichana huyo kama tu angekuja Kariakoo kutembea kama alivyofanya. Nikawa mzee wa kucheza karibu, sikutoka maeneo husika kwa kuwa niliamini muda wowote ule Halima angeweza kufika mahali hapo.

    Baada ya wiki ndiyo akafika, nilimsalimia na kuendelea na mambo yangu. Sikuwa na presha, nilijua ningemkamatia wapi hivyo nikaanza kupiga misele lakini macho yangu yalikuwa pale dukani.

    Ilipofika majira ya saa nane mchana nikamuona akitoka, sikutaka kumfuata moja kwa moja, alikuwa akienda kwenye kituo cha daladala za Kimara hivyo nikapitia kule Big Bon na kwenda kumsubiri kwa mbele.

    Nilimuona akija, nikasimama sehemu wanapouza magazeti na kutulia hapo, alipopita tu nikamsogelea na kumshika mkono, alishtuka, akageuka na kuniangalia.

    “Edward...” aliniita huku akiachia tabasamu.

    “Pole kwa kukushtua jamaniiii!” nilimwambia huku nami nikiachia tabasamu.

    “Usijali!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Leo mbona mapema?”

    “Nawahi chuo, nimeanza jana na ndiyo maana naondoka mapema!”

    “Ooh! Msomi wangu! Ningependa nikusindikize!” nilimjaribu.

    “Wapi?”

    “Chuo! Au sisi ambao hatujasoma hatutakiwi kuingia huko?” nilimuuliza kimatani.

    “Hahaha! Acha utani! Nashukuru Edward!” aliniambia.

    “Kushukuru kwako kunamaanisha nini? Kwamba naruhusiwa?” nilimuuliza.

    “Noooo! Hauruhusiwi! Shemeji yako atakuona!”

    “Kwani mimi si joka la kibisa, ananiogopea nini?” nilimuuliza.

    “Hahaha! Una maneno wewe!”

    “Basi sawa. Nashukuru kwa kuniruhusu kukuleta mpaka hapa kituoni, uwe na masomo mema,” nilimwambia.

    “Nashukuru!”

    Akaingia ndani ya daladala na kuondoka zake. Alionekana kufurahia pasipo kujua kwamba kwenye zile hatua kumi za kumuumiza Issa hiyo ilikuwa hatua ya kwanza. Nikarudi kuendelea na ishu zangu kama kawaida.

    ***

    “Paaa! Paaa! Paaa...” nilisikia milio ya bunduki kutoka mbali kidogo na mahali nilipokuwa.

    Ilikuwa ni majira ya saa kumi alfajiri, kila mlinz aliyekuwa mahali hapo alikuwa akiogopa, milio ile ya risasi ilionekana kabisa kuwa bunduki nzito, japokuwa tulitakiwa kulinda mahali hapo, walinzi wakaanza kukimbia.

    Mimi sikukimbia, haimaanishi kwamba nilikuwa na nguvu, hapa, ni kwa sababu sehemu ambayo nilikuwa ilionekana kuwa salama zaidi.

    Wote walikimbia na kubaki peke yangu na kilrungu changu. Kwa mbali nikaanza kumuona mzee fulani akikimbia, alivalia kanzu huku mkononi akiwa na mfuko wa nailoni.

    Niliogopa, kwa jinsi alivyokuwa akikimbia ilionekana kama mtu aliyekuwa akiogopa kitu fulani na nyuma yake kulikuwa na watu waliokuwa wakimfuatilia.

    Nilitoka nilipokuwa na kusogea kule alipokuwa. Mara milio ya risasi ikaanza kusikika tena, mzee yule akaanguka na kutulia.

    Nilitetemeka, sikujua kilichokuwa kikiendelea. Ghafla nikawaona wanaume wawili, sikuweza kuaona vizuri usoni kwa sababu ilikuwa usiku na hata hivyo walivalia vinyago usoni ambavyo niliviona baada ya kupita sehemu iliyokuwa na taa.

    Wakamsogelea yule mzee ambaye alikuwa akiugulia maumivu pale chini, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuuchukua mfuko wake alioushika lakini cha pili kilikuwa ni kutaka kumpiga risasi.

    “Wewe simamemi hapohapo,” nilisema kwa sauti kubwa.

    Sikujua niliupata wapi ujasiri wangu, saut ile ambayo niliitumia kusema maneno hayo ilikuwa na utisho mkubwa na kuwafanya wale vijana kuogopa, hivyo kuanza kukimbia na ule mfuko huku wakimwacha mzee huyo akiwa chini akilia.

    Nikamsogelea, mzee huyo alikuwa ni wa Kihindi, ilikuwa ni lazima niyaokoe maisha yake. Niliogopa kwani sikutaka kujiaminisha kwamba wale watu waliondoka moja kwa moja, niliamini kwamba wanaweza kurudi tena kumalizia kazi yao.

    Mzee yule alikuwa akilia kwa maumivu makali, alipoteza damu nyingi, pale chini alipokuwa hakuwa na msaada mwingine zaidi yangu. Roho yangu iliniuma sana kiasi cha kusema kwamba ni lazima nimsaidie kwa nguvu zote.

    “Nisaidieee....nakufaaaa....nakufaaaa....” aliniambia mzee huyo huku akilia.

    Nikambeba na kumpeleka pembeni, nilipofika kwenye kibaraza kimoja, nikalishika shati lake kwa lengo la kulichana ili nimfunge kwenye kidonda kilichokuwa kimesababishwa na risasi.

    Wakati nimemvua shati hilo na kulichana, nikasikia kitu kimetokea kwenye mfuko wa shati na kuanguka. Sikujua ni nini, nilikichukua harakaharaka na kukiweka kwenye mfuko wangu wa suruali na kuendelea kumfunga.

    Baada kama ya dakika ishirini ndipo walinzi wenzangu wakafika hapo ambapo tukambeba na kumpeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

    “Nyie ni akina nani?” alituuliza nesi mmoja huku akiniangalia hasa mimi ambaye nguo zangu zilikuwa na damu nyingi.

    “Wasamaria wema dada!”

    “Mmemuokota wapi huyu?”

    “Sisi ni walinzi, tulisikia milio ya risasi, kuna watu wakataka kumuua, tukamsaidia!”

    “Sawa. Muacheni, njooni asubuhi tena mkiwa mmetoa taarifa kituo cha polisi,” alituambia na sisi kuondoka.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tuliondoka huku tukisimuliana kile kilichotokea, kila mmoja alinishangaa, nilionekana kuwa mtu wa ajabu sana, iliwezekanaje niende kumsaidia yule mzee na wakati nilisikia milio ya risasi?

    Sikuwa na jibu la kuwapa zaidi ya kuwaambia kwamba mimi mwenyewe nilishangaa. Tulilinda siku hiyo kwa kujificha sana, nakumbuka tulikuwa kama wanne hivi.

    Ilipofika asubuhi, nikaondoka na kuelekea kwenye kichumba changu nilichopewa kwa ajili ya kukaa huko na kujilaza kitandani, siku hiyo nilichoka kupita kawaida.

    Wakati nikiwa nimevua suruali na kubaki na boksa ndipo nikakumbua kuhusu kile kitu nilichokiokota na kukiweka mfukoni.

    Haraka sana nikaichukua surualia yangu, nilipokitoa kitu hicho, nilipigwa na mshangao baada ya macho yangu kugongana na almasi iliyokuwa na ukubwa kama mfuniko wa kisoda.

    “Hii nini? Almasi au kipande cha chupa?” nilijiuliza na kukiangalia vizuri, ni baada ya sekunde kadhaa nikapata jibu kwamba kile kilikuwa ni kipande cha almasi, mapigo yangu ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu, sikuamini kile nilichokuwa nikikiona. Hii ilimaanisha umasikini ndiyo basi tena ama nini? Kila nilichojiuliza, nikakosa jibu.





    ITAENDELEA





0 comments:

Post a Comment

Blog